WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, September 24, 2012

BASATA NA MMOMONYOKO WA MAADILI YA WASANII TANZANIA


JE BARAZA LA SANAA TANZANIA  (BASATA) LIMESHINDWA KUWAELIMISHA WASANII KUFANYA KAZI ZAO KWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI ZAO ZA SANAA?


Mwandishi mmoja alishawahi sema huku nyuma kuwa “Msanii ni mtu muhimu na ana nafasi kubwa katika jamii. Ni vema wasanii mkatambua kuwa mna jukumu kubwa katika jamii kuelimisha na si kupotosha”


Afande Sele naye aliwahi kuimba huko nyuma kuwa, “mimi ni msanii, mimi ni kioo cha jamii”.

Sanaa katika nchi na jamii mbali mbali imeendelea kutumika kama dhana ya kusaidia jamii kujikosoa na wakati huu huu kupata burudani ambayo ni sehemu muhimu sana katika maisha ya jamii yeyote ile.


Sanaa katika Jamii au taifa lolote lile ni sawa na kiumbe hai, ambacho kinaendelea kukua na kujifunza kulingana na wakati na kufanyia mabadiliko sanaa yake ambayo ni kielelezo cha utamaduni wa taifa hilo. Sanaa pamoja na wasanii ni nguzo muhimu katika kuelimisha jamii hasa pale jamii inapojitahidi  kukopi mambo bila kujua uzuri au ubaya wa jambo husika; hivyo sanaa ikitumika vizuri inaweza kusaidia kuondoa tatizo hili kwa jamii ambayo pengine imekosa elimu, au teknolojia mpya, na hata kushindwa kujifunza kwa sababu ya utofauti mkubwa wa mazingira na maendeleo.

Katika kufaninikisha malengo ya kuielimisha jamii, serikali huunda chombo cha kusimamia na kuratibu shughuli za sanaa ili ziweze kuendana kusimamii shughuli za wasanii kulingana na maadili ya Taifa; katika  taifa letu la Tanzania tunachombo ambacho kinaitwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Chombo hiki kinatakiwa kiwe ndio kiranja mkuu wa kusimamia  kazi za wasanii ili ziweze kuchezwa au kuonyeshwa  kulingana na maadili ya Taifa letu, “pengine”.


Nimetumia neno pengine kutokana na ukweli kuwa chombo hiki kinayumba na katika kusimamia maadili ya kazi za wasanii kwani  wasanii sasa wamekuwa na nguvu ya kuleta mmomonyoko wa maadili katika ndani ya taifa letu huku, kikishindwa kabisa kuwawajibisha wale wachache wanaoharibu sifa nzuri ya kazi ya sanaa kwa masilahi yao au tu kwa huluka zao binafsi; uthibitisho mdogo tu wa kauli yangu ni pale BASATA ilipoagiza kuwa “ baraza hilo limevitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti kazi za Sanaa zisizo na maadili kabla ya kwenda hewani ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii”. Kwa uelewa wangu ilitakiwa chombo hiki kiwe na sheria ambayo inavikataza vyombo vya habari kutokurusha hewani kazi zote ambazo zinaharibu maadili kwa taifa;


Taifa letu lina wananchi wa rika mbali mbali lazima kuwe na utaratibu kama ilivyo katika nchi za wenzetu  muvi ambazo zinaonyeshwa katika vyombo vyetu vya habari  ‘television” zionyeshe ni Rika gani wanatakiwa kuona kwa mfano ikionyesha kuwa muvi hii ni “ p13” hivyo inamaanisha kuwa ni wale wote wenye rika ya miaka kumi na tatu na kwenda mbele; hivyo wale ambao hawajefiki umri huu sio busara kuona muvi  hiyo; hivyo sheria  au utaratibu wa namna hii ukieleweka, jamii nayo sasa inaanza kuwajibika kwa kuwaelimisha/kuwakemea  kwamba hawastahili kuangalia muvi hiyo.

Kama alivyowahi kuandika mwandishi JENNIFER ULLEMBO alishauri kuwa  katika taifa letu katika siku za karibuni kumekuwa na malalamiko sana ya wananchi dhidi ya wasanii “KERO, tumechoka kuona nguo zenu za ndani ninyi waigizaji wa filamu hapa nchini. Mnatuchosha sana jamani hivi karibuni tumeona picha za ajabu ajabu za waigizaji wetu, ambao wameongozana na wasanii waliopita katika mikoa mingi kufanya shoo za Fiesta”.




Aliendelea kusema kuwa “Waigizaji wetu mmekuwa mkikubalika sana na mashabiki wengi je? Kwa haya mnayoyafanya mnadhani jamii iwakifikirie vipi. Badala ya kuwa kioo cha jamii mumegeuka kuwa giza, ambalo halionyeshi na hugubikwa na mambo ya ajabu wakati wa usiku. Kwanini lakini mnapenda kufanya mambo ya ajabu kiasi hicho, hamjui kama mnapoteza thamani kama muigizaji. Imekuwa ikishangaza sana waigizaji wetu mnavyofanya vitu vya ajabu, kuanzia katika tabia zenu hadi mavazi mnayo vaa. Vaeni hayo mavazi yenu wakati mnaigiza tu na kisha mnapojumuika katika jamii nyingine mvae kiheshima”.

Alimaliza maelezo yake kwa kuuliza swali ambalo hata mimi naendelea kujiuliza kuwa  “Sijui Baraza letu la Sanaa nchini BASATA, linachukua hatua gani, kwa wasanii wetu kuonyesha nguo za ndani. Naomba Basata iangalie kwa umakini suala hili, maana tunapoelekea siyo pazuri kabisa.”
  • ninafikiri kama wadau wengi walivyowahi sema kuwa wakati Baraza letu la sanaa linatakiwa kuanza kuchuaka hatua kali ya kudhibiti hali hiyo.

  • Baraza linatakiwa kuendelea kuwaelimisha wasanii wetu kufanya kazi na maonyesho yao  na sio kusingizia Pombe kuwa ndio iliyofanya mambo haya yote.
Shabani Matutu aliwahi andika kuwa  “UVAAJI wa wachezaji wa filamu za sasa unanifanya kukumbuka namna ambavyo hapo zamani kulivyokuwa kukirushwa filamu kwenye majumba mbalimbali ya sinema ambayo yalikuwa yakichambua nzuri za kurushwa na rika. Kwani halikuwa jambo la kawaida kuwahusisha watoto kutazama mapenzi ambayo yalikuwa maalumu kutazamwa na watu wazima kwani walizuiliwa watoto kuingia kuzitazama”.


BASATA lazima ikubaliane wadau wengi ambao wanakerwa na hali hii kuwa:

  • Lifanye utaratibu wa kudhibiti wimbi kubwa la filamu ambazo zikikiuka maadili na husababisha mmommonyoko wa maadili kwa kwa vijana wetu ambao wengi wamekuwa wapenzi wa kuzitazama


  • Kazi za wasanii wetu kwa ujumla hazioneshi umri wa kuzitazama kwa hiyo kwa mfano muvi ya Opral ya Marehemu Kanumba inatazamwa mtu wa rika yeyoteile wakiwamo watoto pamoja kuwa kuna matukio ambayo watoto hawashauriwi kuona wakiwa wananagalia pamoja na wazazi wao hata peke yao.
  • Matukio ambayo yameripotiwa hivi karibuni katika “ fiesta” ambapo wasanii wa kike wamekuwa wakicheza au kuvaa kinyume na maadili; kwa wasanii wahusika ni jambo la kawaida kuacha wazi baadhi ya maeneo yao wakidhani ndiyo kujitangaza kisanii lakini binafsi siamini hilo . Ni jambo la aibu kwa msanii ambaye ameolewa au anategemea kuolewa kufanya vituko kama hivyo.



BASATA tunaomba iangalia upya  tatizo hili la  la mmomonyoko wa maadili. Kuna mambo mengi yanaikabili jamii na wasanii wana jukumu la kuielimisha jamii badala ya kuipotosha kwa kuvaa nusu uchi. Huo si utamaduni wetu, tukizingatia kuwa msanii ni kioo cha jamii na ana nafasi kubwa kufikisha ujumbe kwa jamii, lakini kwa baadhi ya wasanii wetu wamekuwa wakikitumia kioo hicho kwa masilahi binafsi ya kuonekana tu! Bila kujali jamii inayowatazama na nini inanufaika na kile inachokitazama.

Tujaribu kuliepusha taifa letu na matendo haya ambayo hayakubaliki ya wasanii ya kuharibu vijana wetu kwa kuwaiga hizo tabia zao chafu; tunaomba BASATA iyumie msumeno wake katika kurekebisha uchafu huu, BASATA inatakiwa kuwa na kifimbo cheza msanii anapofanya kazi yake nje ya maadili achapwe kwa msingi wa sheria mara moja na sio kusubiri kwa muda mrefu tunapunguza ukali wa sheria.

Tatizo la mmomonyoko wa maadili ni la muda mrefu. Mmomonyoko huu huu umekuwa  ukiendelea  kuichafua jamii kutokana na  ukimya  wa  serikari (BASATA) . Hali hii inapelekea tasnia kudharaulika kutokana na kazi chafu za wasanii wachache.
Nikiwageukia wasanii wenyewe nafikiri tatizo nyingine la wasanii wetu ni kulewa sifa, sifa ambazo wanapewa wanaona kama vile wamefika mwisho; na swala la maadili haliwagusi na fikiri hili ni tatizo sugu, bado nasisitiza kuwa wasanii wetu wanahitaji elimu na busara ya kumpapanua nini waonyeshe, nini wavae, namna gani wacheze; na pombe kama ni lazima itumike, itumike wapi na kwa kiasi gani.

Nitajisikia vibaya kama mwanajamii wa kitanzania ambaye ninawapenda wasanii na kazi zao za sanaa, kama tuna wasanii ambao  kwa hayo wanayoendelea kuyafanya au kuonyesha kuwa wamefika mwisho wa upeo wao wa kujua majukumu yao kwa jamii; hapo dhana ya msanii kioo cha jamii itakuwa haina maana yeyote kuendelea kutumika;



Tunawashukuru wasanii wale ambao wamekuwa msatari wa mbele kuonyesha kuwa msanii ni kioo cha jamii ana jamii inamwitaji sana kwa maendeleo na mabadiliko; wasanii kama marehemu Kanumba, Hoyce Temu, Pastor Myamba kwa wakati tofauti wameweza kuwakilisha jamii katika nafasi kama balozi wa jambo fulani  au hata kuanzisha chuo ambacho kinasaidia kuwaelimisha wasanii katika kukuza maadili yao kupitia elimu.


Naungana na mwanazuoni aliyewahi kuandika kuwa:

  • “Ninacho amini mimi ni kuwa Msanii ni kioo cha jamii, Je hiki ndio jamii inastahili kukiona na kujifuza?”  Wewe kama msanii utajibu nini hapo?

  • “Uigizaji ni kazi,Muziki ni kazi, na kila siku wasanii wanataka umoja na ushirikiano na wanaitaji sapoti kutoka kwa serikali, je kwa mambo haya itawezekana?”

  • “Inabidi uonyeshe heshima ili upate heshima, na mafanikio huja kwa kujituma, nina aminii wasanii wakiwa wamoja sanaa yetu itafika mbali na tutaeleweka,sanaa ni wito yataka moyo”


Wasanii ambao wameguswa na makala hii wakiwa ni viongozi wa mmomonyoko wa maadili nafikiri kuteleza sio kuanguka na hamjechelewa mnaweza kubadilika na kuwa kioo ambacho jamii inataka kukitumia katika kuleta mabadiliko;


MUNGU IBARIKI SANAA NA WASANII WA TANZANIA.

3 comments:

  1. ni kweli taifa letu kupitia serikali yetu linatakiwa kuamka na kupinga kwa nguvu moja uchafu huu wa wasanii; wanawafundisha watoto wetu nini? hatutaki kuwa taifa la watoto wenye maadili mabaya toka wakiwa wadogo. tuungane pamoja katika kukemea uozo huu

    ReplyDelete
  2. mbona wakivaa nguo zao za heshima wanapendeza sana; inaelekea walipigwa stop kuvaa kiaina walivyokwenda kumwona msheshimiwa Rais; sometimes naona ni kama ulimbukeni hivi; wasanii mjiheshimu na taifa litawaheshimu

    ReplyDelete
  3. du inatisha kila siku wasanii wanaendelea kutonyesha mambo ya ajabu kuhusu maungo ya miili yao, tatizo hasani nini, nafikiri wamesahau ule usemi usemao chema kinajiuza kibaya kinajitembeza; wanafanya madudu na wanafurahia na kujitangaza wazi na kufurahia uchafu wao; hebu serikali leteni hiyo sheria upesi kama alivyosema Muhogo Mchungu akihojiwa na mkasi tv. tunawahofeha sana watoto wetu kwa hizi tabia mbaya za baadhi ya wasanii.

    ReplyDelete