WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 27, 2013

Wabunge CCM wavuana nguo


 


 *Lugora, Filikunjombe washambuliwa mbele ya Pinda
*Wajibu mapigo, Lugora asema acheni unafiki
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana waliumbuana na kushutumiana wazi mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao chao katika ukumbi wa Msekwa mjini hapa ambako waliumbuana na kushutumiana waziwazi.
Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kilifanyika baada Spika wa Bunge, Anne Makinda kuahirisha mjadala wa makadirio ya mtumizi ya fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Spika aliahirisha mjadala wa makadirio hiyo uliokuwa uhitimishwe jana, baada ya wabunge wengi kuonyesha nia ya kuyakwamisha kutokana na kutoridhishwa na jitihada za Serikali za kukabiliana na kero ya maji nchini.

Chanzo chetu kilichokuwa katika kikao hicho kilisema mjadala ulipoanza, Pinda aliizungumzia kwa kifupi Wizara ya Maji na kuonyesha jinsi Serikali ilivyokubali kwa dhati kurekebisha makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara hiyo.

Baada ya hoja hiyo, chanzo hicho kilisema Waziri Mkuu aliwasilisha hoja nyingine iliyowataka wabunge wa CCM kuchangia posho zao za siku moja kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

“Hoja hiyo ilipopita, Nyoka wa Shaba (Kangi Lugora, Mbunge wa Mwibara), alisimama na kuhoji ni kwa nini chama kimekubali kusaidia uchaguzi wa madiwani wakati huwa hakisaidii kesi za uchaguzi za wabunge.

“Si unajua Nyoka wa Shaba naye ana kesi mahakamani, sasa ndiyo maana akaamua kuhoji iweje yeye hasaidiwi na chama wakati huo huo anaambiwa asaidie uchaguzi wa madiwani.

“Alipomaliza kusema hivyo, akasimama Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba. Aliposimama aliwashutumu moja kwa moja Lugora na Filikunjombe (Deo, Mbunge wa Ludewa).

“Akasema wabunge hao badala ya kuisaidia Serikali wanapokuwa bungeni, wao wamekuwa wakiishambulia jambo ambalo halileti picha nzuri kwa wananchi.

“Akasema kitendo cha Filikunjombe kusema bungeni kwamba Serikali ina miwani ya mbao hakikuwa kizuri… akasema ‘hawa wenzetu hatuko nao na kwa kuwa mwezi ujao tutaonana na Mwenyekiti wa Chama (Rais Jakaya Kikwete) nitasema mengi’.

“Alipomaliza kusema hayo akasimama Kibajaji (Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera). Kibajaji akaungana na Nkumba, akawashambulia Lugora na Filikunjombe kwamba wanaiua Serikali kutokana na maneno yao bungeni.

“Akasema kama Lugora ana kesi mahakamani ni bora akakabiliana nayo mwenyewe kwa sababu inaonekana hayuko pamoja na chama,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Baadaye alisimama Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima ambaye alimshutumu Lugora kwamba kitendo chake cha kuliambia Bunge kuwa kuna baadhi ya mawaziri wanajihusisha na dawa za kulevya, kinawaweka njia panda wananchi kwa kuwa wanahisi wabunge wao ambao ni mawaziri, nao wamo kwenye orodha hiyo ikizingatiwa kuwa hakuwataja majina.

“Pia, akahoji kama wabunge wana kero zao ni kwa nini wasiwafuate mawaziri na kuzungumza nao badala ya kuwasema bungeni.

“Kisha, alisimama Mangungu (Mbunge wa Kilwa Kaskazini) ambaye alionyesha wasiwasi juu ya majaji wanaosikiliza kesi za uchaguzi.

“Yeye akasema kesi nyingi za uchaguzi ambazo CCM inashindwa ni kwa sababu majaji wengi wanaichukia CCM na wanaipenda Chadema.

“Baadaye aliungwa mkono na Dk. Chami (Dk. Cyril Chami, Mbunge wa Moshi Vijijini) ambaye alidiriki kumtaja jaji mmoja kwa jina kwamba ana upendeleo wa wazi wazi kwa Chadema.

“Kisha, alisimama Mbunge wa Karagwe (Gosbert Blandes) na akatoa ushauri kwamba kuna haja chama kusaidia majimbo ya uchaguzi na wakati huo huo, viongozi wakuu wa chama waende kwa wananchi kama wanavyofanya viongozi wa Chadema.”

Mbali na hao, chanzo hicho kilimtaja Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia kwamba alimshutumu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kwamba hakusaidia wakati wa vurugu zilizotokea hivi karibuni mjini Mtwara.

“Ghasia alianza kwa kusema kwamba, siku hizi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, anafanya ziara za mara kwa mara jimboni kwake Mtwara Vijijini lakini CCM haijali.

“Pia akamlalamikia Waziri Nchimbi kwamba wakati wa vurugu za wananchi mkoani Mtwara alimpigia simu lakini hakupokea na hata alipomtumia ujumbe mfupi wa simu hakumjibu.

“Akahoji pia kwamba iweje wakati wa vurugu zote Mtwara, nyumba zinazochomwa ni za wabunge wa CCM wanawake na nyumba za wabunge wanaume hazichomwi, akahoji kuna kitu gani hapo,” kilisema chanzo hicho.

source Mjengwa Blog

Miaka 49 Ya Muungano Uwanja wa Uhuru

 


 Sehemu ya wananchi waliojitokeza kushuhudia sherehe hizo.
 Rais Jakaya Kikwete, akiingia uwanja wa Uhuru akiwa ndani ya gai la wazi wakati alipowasili uwanjani hapo kwa ajili ya kuwaongoza wananchi katika shambra shambra za sherehe za miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kushoto ni Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange. Katika kuadhimisha sherehe hizo, Rais Kikwete, ametoa msamaha kwa wafungwa wapatao 4180 kwa nchi nzima, huku msamaha huo ukiwa hauwahusu, Wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha, Kifungo cha ubakaji, wezi wa magari, Rushwa, Matumizi mabaya ya Madaraka na Kunyongwa.

 Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete akikagua gwaride la heshima wakati wa sherehe za miaka 49 ya Muungano kwenye Uweanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana
Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume (kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa
 Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idii (kulia) akisalimiana na Jaji Mkuu wa Zanzibar Othmani Makungu
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (kulia), Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shalif Hamad wa pili kutoka (kulia), Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Othmani Ramadhani Makungu wakiwa katika maadhimisho   hayo.
 Rais Jakaya, akisalimiana na baadhi ya viongozi baada ya kuwasili uwanjani hapo.pichani akisalimia na makamu wa Rais Dr Gharib Bilal
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bila, Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Mama Karume na baadhi ya viongozi wakisimama kumpokea Rais Kikwete wakati akiwasili uwanjani hapo.
 
 Viongozi wa kiatifa wakimba wimbo wa Taifa. Kutoka kushoto, Rais mstaafu, Ali Hassani Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na  Mama Fatma Karume.
 Askari wa Jeshi la Magereza wakipita mbele ya jukwaa kuu kwa mwendo wa haraka na kutoa heshima. 


   Jeshi la Wanamaji (Nevy)

 Kiapo cha Utii kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete jana.Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais na Issa Michuzi-IKULU

Wednesday, April 24, 2013

Kuwang’oa mafisadi ni kuua CCM

WAKATI Tanzania imetimiza zaidi ya miaka 20 tangu yatokee mageuzi ya kisiasa yaliyosababisha kuruhusiwa kwa siasa za vyama vingi, kuna haja ya kufanya tathmini japo fupi kwa minajili ya kuyafanya mageuzi hayo yawe na manufaa kwa nchi yetu.

Miongoni mwa machapisho mbalimbali yanayozungumzia suala la mageuzi ya kisiasa barani Afrika ni kitabu maridhawa kilichohaririwa na Profesa Adebayo Olukushi, kinachoitwa The Politics of Opposition in Contemporary Africa (yaani, Siasa za upinzani katika Afrika ya sasa).

Katika tafiti zilizofanyika kwenye nchi saba za Afrika (na ambazo zimejadiliwa katika kitabu hicho) masuala kadhaa ‘yasiyopendeza’ yalibainika. Masuala hayo ni pamoja na

Mosi, tawala zilizokuwa madarakani (wakati wa mageuzi) kuridhia kwa ‘shingo upande’ mageuzi hayo, na matokeo yake tawala hizo zimeendelea kuyakwaza, kunyanyasa wapinzani sambamba na kuwadhoofisha na ‘kuwafitini.’

Pili, uungaji mkono wa taasisi mbalimbali (za umma na za binafsi) uliondolewa kwa kila aliyeonekana kuwa karibu au kuwaunga mkono wapinzani, na hii imeathiri uwezo wa kiuchumi wa vyama vya upinzani hususan kwa wafanyabiashara kuchelea ‘hasira za watawala’ pindi wakitambulika kuwa wanawasaidia wapinzani.

Tatu, vyama tawala kupata upendeleo zaidi ya vyama vya upinzani katika maeneo mbalimbali, hususan kutoka kwa vyombo vya habari vya umma na taasisi za usalama (ambavyo licha ya kushiriki ‘kuchakachua’ matokeo ya chaguzi mbalimbali pia vimekuwa vikiwanyanyasa na kuwaonea wapinzani).

Nne, mfumo wa uchaguzi wa ‘mshindi kuchukua vyote’ (winner takes all) umekuwa kikwazo kwa wapinzani ambapo idadi ya viti wanavyoshinda kwenye chaguzi havilingani na mgawanyo wa kura.

Tano, katika kukimbilia kwao kushiriki kwenye chaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi, vyama vya upinzani vilijinyima fursa muhimu ya kudai mabadiliko ya Katiba ambayo yangesaidia uendeshaji wa shughuli za kisiasa wakati na baada ya chaguzi.

Sita, harakati za kisiasa za vyama vya upinzani kutegemea mno misaada au uungwaji mkono kutoka nje yao.

Japo kitabu hicho kilichapishwa miaka 15 iliyopita, tafiti husika zilifanywa nchini Kenya, Zimbabwe, Niger, Nigeria, Senegal, Afrika ya Kusini na Uganda, takriban vipengele vyote nilivyotaja hapo juu vinaakisi hali ilivyo huko nyumbani.

Wakati chaguzi mbalimbali zilizofanyika huko Kenya, Nigeria na Afrika Kusini zinaweza kutoa picha tofauti kiasi na inayobainishwa kwenye kitabu hicho, yayumkinika kuhitimisha kuwa kwa Tanzania yetu hali inaelekea kubaya zaidi. Nitafafanua.

Tuweke kando tawala za Awamu ya Kwanza na ya Pili (angalau kwa minajili ya mjadala huu), Awamu zilizofuatia (ya Rais Benjamin Mkapa na ya sasa ya Rais Jakaya Kikwete) kwa kiasi kikubwa zimetawaliwa na harakati na mikakati ya makusudi si tu ya kudhoofisha siasa za upinzani bali pia kuutokomeza kabisa upinzani.

Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa zama za Mkapa ambaye wapinzani wataendelea kukumbuka kwa hotuba zake kali dhidi yao, sambamba na ‘kuwaponda’ mara kwa mara, ni nadra kwa Kikwete ‘kuwapiga vijembe’ wapinzani, na hata anapofanya ni rahisi kumtoa lawamani kwa hoja kuwa “huwezi kuwa kiongozi kamili wa kitaifa wa CCM pasipo angalau ‘kuwapiga madongo’ wapinzani.” Ni kama anatekeleza tu wajibu wake kwani hata ‘tone’ yake huwa sio ya mwanasiasa mwenye chuki au uadui dhidi ya wapinzani.

Lakini kama kuna zama ambazo nchi yetu imeshuhudia siasa hatari kabisa basi ni hiyo ya Mwenyekiti ‘mpole’ wa CCM Taifa, yaani Kikwete. Sasa kama Kikwete ana ‘sura mbili’ (ya upole hadharani lakini mwenye hasira anapokuwa na wasaidizi wake ndani ya CCM na serikali), au amezungukwa na watu wenye chuki kubwa dhidi ya wapinzani, ni vigumu kuhitimisha hilo kwa dhati.

Naomba nisiume maneno. Kuna wanasiasa watatu ambao wote ni wasaidizi wa karibu wa Kikwete huko CCM, wamekuwa sio tu wakijitahidi kufanya kila wawezalo kuteketeza vyama vya upinzani-hususan Chadema bali pia wanaweza kabisa kuliingiza taifa letu matatizoni kutokana na siasa zao za chuki. Hao ni Steven Wassira, Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba.
Wassira, maarufu kama Tyson, amekuwa ‘asset’ muhimu kwa CCM dhidi ya wapinzani, pengine kwa vile alikuwa huko kabla ya kurejea CCM. Nafasi niliyonayo katika makala hii haitoshi kuorodhesha matendo kadhaa ya mwanasiasa huyo dhidi ya vyama vya upinzani, lakini kubwa, na pengine la msingi zaidi, ni kauli yake hatari kuwa Chadema itakufa kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Ikumbukwe kuwa Wassira si mnajimu wala hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa ana uwezo wa kupiga ramli kubashiri uhai au vifo vya vyama vya siasa. Kauli hiyo ya Wassira ina uzito mkubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa nafasi yake serikalini inaweza kusukuma vyombo vya dola kufanikisha utabiri wake huo (ambao kimsingi ni fyongo lakini unaoweza kutimia kwa ‘nguvu za giza.’)

Nape ni mwanasiasa ambaye binafsi ninamwona kama disappointment of the century. Kabla ya kuingia kwenye siasa za ngazi za juu, mwanasiasa huyu kijana alijipambanua kama mtu mwenye maono, ujasiri na msimamo usioyumba. Pasi kuchelea matokeo, alimudu kukosoa vikwazo kwa maendeleo na ustawi wa taifa letu na kupingana waziwazi na wanasiasa wenye mitizamo fyongo ndani ya chama chake.

Kijana huyo 'alilipa gharama’ kubwa ya msimamo wake usioyumba (wakati huo) na akakumbwa na zahma kubwa ya kisiasa. Pengine kwa kutambua kuwa kosa pekee la Nape ni msimamo wake makini, Rais Kikwete ‘alimzawadia’ ukuu wa wilaya (ambapo wachambuzi wa siasa walitafsiri hatua hiyo kama sapoti ya Rais kwa mwanasiasa huyo).

Alipoteuliwa kushika nyadhifa ya juu ndani ya CCM, Nape alikuja na nuru mpya ndani ya chama kilichokuwa kikionekana machoni mwa wengi kuwa kimezama kwenye himaya ya mafisadi, akatangaza dhamira ya kihistoria ya ‘CCM kujivua magamba,’ yaani chama hicho tawala ‘kuwakalia kooni’ viongozi na wanasiasa wake wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi. Kwa nyakati kadhaa, Mwenyekiti wake wa CCM Taifa, Rais Kikwete alionyesha kumuunga mkono Nape.

Nikiri kuwa nami ni miongoni mwa ‘tuliongizwa mkenge’ (kughilibiwa) na suala hilo la CCM kujivua magamba. Pengine kilichoniaminisha zaidi kuhusu suala hilo ni kauli za Nape na ukweli kwamba historia yake huko nyuma ilipaswa kumwaminisha yeyote anayemfahamu vema kuwa hakuwa ‘anapiga  politiki’ bali alikusudia kwa dhati kukisafisha chama chake.

Pamoja na ‘hasira’ za Nape kutonifuatilia (unfollow) kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kumwandama kwa maswali ya/hoja za kichokozi (lengo likiwa kumhamasisha arejee kwenye mstari sahihi), bado ninaamini kwa asilimia 100 kuwa mwanasiasa huyo alikuwa na dhamira ya dhati kuivua CCM magamba, na kilichomkwaza si unafiki bali ukweli kuwa ‘tofauti na nyoka ambaye uhai wake hutegemea kujivua gamba, ukimvua gamba kobe utamuuwa.’

CCM si kama kobe bali ni kama nyoka ambaye kujivua gamba ni sehemu muhimu ya uhai wake. Jitihada zozote za kukitenganisha chama hicho na mafisadi kitakuwa na matokeo ya aina moja tu: kukidhoofisha na hatimaye kukiuwa.

source: Raia Mwema

Wagombea binafsi watokane na vyama

 
CHARLES Montesque ni mwanafalsafa mkongwe aliyezaliwa mwaka 1689 nchini Ufaransa. Ndiye  aliyejenga hoja ya kuwa na dola yenye mihimili mitatu huru.

Kwa mujibu wa Montesque, Dola haina budi kutenganisha mamlaka ya taasisi hizi tatu. Ni muhimu kwa mihimili hii mitatu kuwa huru. Ifanye kazi kwa kujitegemea. Kuwepo pia na mazingira ya mikono yote mitatu kudhibitiana.

Mihimilimitatu ya dola ni; Utungaji sheria (Bunge) Utawala (Serikali) na Hukumu (Mahakama). Kuna wenye hoja ya kwamba mikono hii mitatu iwe na ushirikiano wa karibu.

Montesque anapingana na hoja hiyo, anaamini kutenganisha mamlaka ya mihimili hii mitatu ya dola kunaipa  uhuru kamili wa kufanya kazi zake bila kuingiliana. Hilo ni muhimu ili kuwepo na utawala bora uliojengeka katika misingi ya haki.

Katika nchi zetu hizi tunahitaji rais (serikali) yenye nguvu za kikatiba, bunge lenye nguvu za kikatiba na mahakama huru yenye nguvu za kikatiba. Mahakama zenye majaji wasioteuliwa na rais. Kwamba mikono hii mitatu iwe huru na yenye majukumu ya kudhibitiana kwa maslahi ya nchi. Tuandae katiba yenye kulipa bunge  uwezo zaidi wa kufanya maamuzi ya kikatiba. Bunge ndilo mwakilishi wa wananchi.

Tuwe na Mahakama Kuu Huru ya Katiba. Mahakama yenye jukumu la kutafsiri sheria na maamuzi yote yaliyofikiwa na Bunge. Mahakama ya Katiba iwe ni chombo cha juu kitakachoshughulikia mashauri ya ukiukaji wa sheria na maamuzi ya Bunge. Iwe na uwezo wa kisheria wa kupitisha hukumu kwa kuzingatia sheria za nchi bila kuathiriwa na Serikali au Bunge.

Kwa mujibu wa Montesque, kama bunge halitakuwa na nguvu, kuna hatari ya bunge hilo kuchukua nafasi ya serikali na kwa maana hiyo utaratibu mzima wa mgawanyo wa madaraka ya dola kwa mihimili hii mitatu utakufa.

Montesque anabainisha pia; kuwa endapo mawaziri ambao ni watekelezaji wa maamuzi ya bunge watatoka miongoni mwa wabunge, basi, hakutakuwa tena na uhuru, kwani serikali yenye mamlaka ya utekelezaji itakuwa imechanganyika na bunge.

Rais apewe madaraka ya kuchagua mawaziri, lakini, watoke nje ya bunge. Hata kama rais atamteua waziri ambaye pia ni mbunge, basi, mbunge alazimike kuachia kiti chake cha ubunge na atafutwe mwakilishi mwingine wa wananchi. Haiwezekani kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.

Na kuna hoja hii ya kuwapo ama kutokuwapo kwa wagombea binafsikatika chaguzi zetu.  Tunapaswa kujiuliza;je, ni wakati sasa wa kuwa na wagombea binafsi? Swali hilo linatutaka kuumiza zaidi vichwa vyetu. Maana, maamuzi yatokanayo na vifungu vya sheria ya vitabuni ni jambo moja, lakini hali halisi katika jamii tunayoishi ni jambo jingine kabisa.

Kwa kuziangalia jamii nyingine na kulinganisha na hapa kwetu, mimi nadhani,kuwa nchi yetu haijawa tayari kuruhusu wagombea binafsi katika utaratibu usiotokana na vyama vya siasa.

Nasema hivi kwa kuzingatia kuwa nchi yetubado ni changakidemokrasia. Demokrasia hukua kulingana na hali halisi ya nchi.Ni vema na ni busara kwawagombea binafsi wakatokana na vyama na waruhusiwe tu katika nafasi ya udiwani, ubunge na useneta, na si katika nafasi ya urais. 

Kwa kuweka msisitizo; kusiwe na mgombea binafsi katika nafasi ya urais. Mgombea urais kikatiba atokane na chama cha siasa. Apitishwe na idadi ya wanachama itakayokubalika, mathalan, awe ni Mtanzania aliyepigiwa kura na kupitishwa na wanachama wa chama chake wasiopungua 1,000.

Tusiruhusu mazingira ya Mtanzania aamke tu Kamachumu au Masaki na amwambie mkewe au mumewe kuwa; “ Naenda kuchukua fomu ya kugombea urais!”.Katika mazingira ya nchi zetu hizi, huko ni kukaribisha uwendawazimu, na mwishowe ikulu zetu zitakaliwa na wendawazimu au watu wasio hata na uwezo wa kuongoza klabu ya soka lakiniwana pesa, umaarufu na mbinu za kufika ikulu.

Hivyo basi, Katiba ijayo ingewekautaratibu wa kuruhusumgombea binafsi anayetokana na chama cha siasa katika ngazi ya udiwani, ubunge na useneta, si urais.

Katika utaribu huu wanaonawania ubunge katika jimbo X watapigiwa kura na wanachama wenzao katika idadi ya wanachama itakayokubalika. Atakayeongoza katika kura atakuwa ni mgombea ubunge kuwakilisha chama chake.Huyo atapewa pia msaada wa kukampeni na chama chake ikiwamo fedha za kampeni.

Mgombea ubunge huyo atatambuliwa rasmi na chama chake. Lakini wagombea wengine walioshindwa katika kura wana hiari ya kusimama wenyewe kama wagombea binafsi. Wajinadi wenyewe na kwa gharama zao na bila kupigiwa debe na chama chao. Wakibahatikakuchaguliwa na wananchi na kuingia bungeni, basi, wataingia bungeni kama wagombea binafsi lakini wakiwakilisha itikadi na sera za vyama vyao.

Utaratibu wa wagombea binafsi wanaotokana na vyamautasaidia pia kuimarisha vyama vya siasa. Tumeamua kuingia katika mfumo wa vyama vingi na si mfumo wa wagombea wengi binafsi. Chama ni wanachama na vikao vya chama. Ni itikadi na sera.

Kuruhusu mgombeabinafsi asiyetokana na chama ni kuhujumuna kupoteza maana nzima ya uwapo wa siasa za vyama vingi. Na swali ni je, hatuoni kuwa umefika wakati wa kuondokana na uchaguzi wa rais na badala yake rais atokane na chama kilichopata kura nyingi? Hili nalo linajadilika.

source: Raia Mwema :Maggid





 

Shein: Siiongozi Z'bar kwa shinikizo la mtu

 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema hatoongoza serikali yake kwa shikinikizo la mtu au kiongozi yeyote.
Aidha, amewashangaa wanaohoji sababu za yeye kutowateua wakuu wa wilaya na mikoa wapya tangu achaguliwe kuwa Rais mwaka 2010.
 
Rais Shein aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika Amani Mkoa wa Mji Unguja.
 
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, yeye ndiye Rais baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na ndiye aliyewateua Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais kuwa wasaidizi na washauri wake.
 
Aidha, alisema kutokana na nguvu za kikatiba na kisheria alizonazo, anaweza kumuondoa yeyote katika uteuzi wake bila ya kuvunja na kikuika sheria ikiwa hataridhishwa na utendaji wa kiongozi aliyemteua.
 
Kauli ya Dk. Shein, ilionekana ni kama kumpiga `kijembe' Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye aliwahi kutamka katika mkutano wa hadhara Fuoni katika uwanja wa Magirisi kuwa hawezi kufukuzwa kazi na Rais.
 
“Mimi ndiye mshindi wa urais wa Zanzibar mwaka 2010, nimeunda serikali na kuteua Makamu wa Kwanza na wa Pili ili kunisaidia kazi na kunipa ushauri, nimetengeneza wizara na kuteua mawaziri na naibu mawaziri bila ya kupangiwa na mtu na wakati wowote naweza kumuondoa yeyote,” alisisitiza.
 
Tangu kuchaguliwa kwake, Dk. Shein ameendelea kubakia na wakuu wa mikoa na wilaya wale wale aliowateua Rais wa awamu ya sita, Amani Abeid Karume na kufanya mabadiliko madogo katika Wilaya ya Kati na Kaskazini `B’ kati ya wilaya 10 za Unguja na Pemba.
 
Kutowateua wakuu wa wilaya na mikoa, kumewahi kuhojiwa mara kadhaa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa nyakati tofauti wakiwa kwenye vikao vya Baraza. Rais Dk. Shein alisema ana uzoefu na maarifa ya kutosha katika masuala ya uongozi na anapenda kuheshimu Katiba na kufuata sheria na hapendi kukurupuka au kusema kutokana na watu wanavyosema mitaani na kwenye majukwaa ya kisiasa.
 
CHANZO: NIPASHE

Msigwa: Kigogo wa CCM anauza pembe za ndovu




Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa.  
 Mbunge wa Mbeya mjini- Joseph mbilinyi aka Sugu akiunguruma kwenye mkutano mkubwa  wa hadhara wa chadema kwenye viwanja vya  Uwanja wa Mwembetogwa iringa jana
  Mbunge wa jimbo la Ubungo John Mnyika akihutubia mamia yawatu waliofurika katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika vinwaj vya Mwembetogwa mjini Iringa
 Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilbrod Slaa Akiunguruma mbele ya mamia ya wafuasi wa chadema kwenye mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya Uwanja wa Mwembetogwa iringa jana
 Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilbrod Slaa Kushoto akipitia katiba kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliyofanyika iringa jana kulia kwake ni mbunge wa jimbo la ubungo Mh John Mnyika
 Sehemu ya mamia ya wafuasi wa chadema wakisiliza hotuba mbalimbali kutoka kwa viongozi mbalimbali wa chama hicho viwanja vya Uwanja wa Mwembetogwa iringa jana. Picha Zote na Chadema na Said Ng’amilo


Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa. Picha na Said Ng’amilo 

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amemlipua kigogo mmoja wa juu wa CCM (jina tunalihifadhi kwa kuwa hakupatikana kujibu tuhuma hizo), kuwa ndiye kinara wa biashara haramu ya pembe za ndovu na utoroshaji wa wanyama nchi za nje.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa jana, Mchungaji Msigwa alisema anashangaa Serikali ya CCM kushindwa kumchukulia hatua.
Mchungaji Msigwa alidai kuwa tembo wapatao 75 wamekuwa wanauawa kila siku kutokana na tatizo hilo kufumbiwa macho na Serikali.
Alidai kuwa pamoja na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kujiuzulu mwaka jana kutokana na kashfa ya kutorosha twiga, Serikali ilitakiwa kuwafuatilia wahusika wote.
“Kinara wa biashara haramu ya uuzaji wa pembe za ndovu anajulikana, sasa inakuwaje Serikali inashindwa kumkamata?” alisema Msigwa na kuahidi kulipua mabomu zaidi atakaporudi bungeni kwa maelezo kuwa anao ushahidi wa suala hilo.

Huo ulikuwa mkutano wa mwendelezo wa wabunge wa Chadema waliosimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kuwapasha wananchi sababu ya kuchukuliwa hatua hiyo.
Wabunge hao walisimamishwa na Naibu Spika, Job Ndugai kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuwazuia askari wa Bunge kumtoa nje ya ukumbi, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu. Wabunge waliosimamishwa pamoja na Lissu ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Ezekiah Wenje (Mwanza Mjini) na Msigwa.

Hata hivyo, Lema na Lissu hawakuwapo katika mkutano huo wa jana ambao pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.

Mnyika kutoa hoja binafsi
Katika mkutano huo, Mnyika aligawa fomu kwa wananchi kuomba aungwe mkono wakati atakapotoa hoja binafsi bungeni juu ya mfumuko wa bei na umaskini nchini.
Mbunge huyo alisema wananchi wanakabiliwa na maisha magumu kutokana na hali mbaya ya uchumi.

“Napata uchungu ninavyoona Watanzania wakiishi maisha magumu kwa hiyo naandaa hoja binafsi ya kuwasilisha bungeni ili umma uelewe umuhimu wa suala hili,” alisema Mnyika na kuongeza kwamba atagawa fomu hizo kila atakapohutubia mikutano ya hadhara.

Dk Slaa na Usalama wa Taifa
Katika mkutano huo, Dk Slaa alidai kuwa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wamegawanyika kutokana na makundi ya wanaotaka kuwania Urais mwaka 2015 kupitia CCM.

Dk Slaa alisema mgawanyiko huo ndiyo chanzo cha siri nyingi za idara hiyo kuvuja.
Aliwatuhumu baadhi ya wanachama wa CCM akidai kuwa wamekuwa wakiwavuta baadhi ya maofisa katika idara yao ili kuwasaidia kwenye harakati zao.
 
source: mwananchi

Rais Kikwete, watawajibika kwa mdomo au vitendo?

NI Jumatano nyingine tunakutana tena katika safu ya ya Jicho la Mtanzania. Wiki iliyopita, tulijadili suala la afya ya mama na mtoto, mada ambayo nilipokea michango mingi kwa njia ya simu na barua pepe.
Napenda kuwashukuru wasomaji wote walioguswa na mada hiyo. Jumatano ya leo nitazungumzia mpango maalumu wa kutathmini utendaji kazi wa viongozi wa Serikali, uliozinduliwa wiki iliyopita na Rais Jakaya Kikwete.

Ni jambo lililo wazi kuwa nchi yetu pamoja na kuwa na rasilimali nyingi ukilinganisha na nchi nyingine za Kiafrika kama jirani zetu Rwanda, bado imekuwa nyuma kimaendeleo. Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa uchumi wa nchi yetu, umekuwa lakini wananchi wake wanaishi kwenye umaskini mkubwa.

Moja kati ya sababu zinazotolewa na wachambuzi wa mambo kuhusu Tanzania kuwa maskini, wakati ikiwa na rasilimali nyingi ni usimamizi mbaya wa rasilimali za nchi. Viongozi wetu hawajaweza kuwajibika ipasavyo kusimamia rasilimali zetu na hii inakwenda mpaka kwenye sekta ya huduma.

Wiki iliyopita, naweza kusema kuwa nchi yetu iliandika historia mpya ya kujaribu kuweka utaratibu ambao utawafanya viongozi wa umma, wajenge tabia ya kufanya kazi kwa malengo na ufanisi, baada ya kuzinduliwa kwa mpango maalumu wa kutathimini utendaji kazi wa viongozi.

Tukio hili la kupongezwa ni matokeo ya ziara ya Rais Kikwete nchini Malaysia aliyoifanya mwaka 2011, ambako alikwenda pamoja na mambo mengine, kuhudhuria mkutano wa kibiashara ulioitwa mkutano wa Lankavi.

Akizungumzia mpango huo, Rais Kikwete alisema ni busara kwa nchi kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa kimaendeleo kama Uingereza, Vietnam na Malaysia ambazo zinatekeleza mpango huo.

“Nchini Malaysia, mpango huu unafanya vizuri zaidi, waziri akishindwa kutekeleza miradi aliyopangiwa, akaitwa kwa Waziri Mkuu, ina maana ameshindwa kazi na hawezi kuendelea tena kuwa waziri,” alisema Kikwete.

Alisema kuwa mpango huo mpya una lengo la kutoa majukumu kwa kiongozi mmoja mmoja, ili aweze kutoa matokeo mazuri ya kazi zake na kwamba hilo ndilo litakalomfanya aendelee na wadhifa wake.

Kwa kuanzia, wizara zitakazoanza kutekeleza mpango huo ni Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Chakula, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Maji.

Katika tukio hilo, mawaziri wa wizara zilizo katika mpango huo, walisimama na kuahidi kutekeleza majukumu yao chini ya mpango huo na kwamba hivi sasa watendaji mbalimbali wa wizara hizo wako kwenye mafunzo maalumu kuhusu mpango huo.

Mpango huu umekuwa na faida kubwa kwa nchi ambazo zimekuwa zikiutumia na leo nitajaribu kueleza namna ambavyo umeweza kuleta mabadiliko kwa jirani zetu, Rwanda.

Miaka 18 iliyopita, Rwanda ilikuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe na zaidi ya watu 800,000 waliuawa kutokana na vita hivyo, huku wengine wengi wakikimbia nchi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani ikiwamo Tanzania.

Lakini leo, Rwanda chini ya Rais Paul Kagame, imeweza kuujenga uchumi wake ulioharibiwa vibaya na vita na kuwa moja kati ya nchi chache za Kiafrika, ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.

Pato la ndani la Rwanda limekuwa kwa asilimia nane katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Rwanda haina madini, mafuta wala gesi kama ilivyo nchi yetu. Lakini kupitia rasilimali chache na vivutio vichache vya utalii pamoja na kilimo imeweza kuushangaza ulimwengu. Hii ni kwa sababu ya usimamizi mzuri wa rasilimali ambao pia ni matokea ya utaratibu kama ambao umezinduliwa hapa kwetu Tanzania.

Miundombinu Rwanda imekuwa kwa kasi ya ajabu, watu waliounganishwa kwenye gridi ya taifa, wameongezeka kutoka watu 91,000 mwaka 2006 hadi 215,000 mwaka 2011. Upatikanaji wa elimu umeimarika ambapo asilimia ya watoto wanaomaliza darasa la saba ni 79 kufikia mwaka 2011 juu ya malengo ya asilimia 58 ambayo ilijiwekea.

Tanzania tumesherehekea miaka 51 ya Uhuru, huku tukiwa hatuna Shirika la Ndege la Taifa lililo imara. Wenzetu Rwanda shirika lao limeanza mwishoni mwa mwaka 2002, lakini leo hii limekuwa na linasafirisha abiria zaidi ya nchi 15 duniani.

Rais Kagame aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akisema kuwa maendeleo ya kweli ya nchi yake, hayatatokana na misaada ya wafadhili bali katika uwekezaji wa kuwajengea uwezo watu wake.

Mwaka 1995 bajeti ya Rwanda ilikuwa ikitegemea wafadhili kwa asilimia 100, lakini mwaka 2011 ilishuka mpaka asilimia 40. Bajeti yetu ni tegemezi kwa wahisani kwa asilimia 40 kama Rwanda wakati tukisherehekea miaka 51 ya Uhuru.

Kusajili biashara Rwanda kama unakila kinachohitajika, itakuchukua siyo zaidi ya siku tatu. Karibu kila kitu kinafanyika kwa njia ya kompyuta na kumekuwa na ufanisi mkubwa.

Haya yanayotokea Rwanda siyo miujiza. Ni matokeo ya utaratibu wa kuwajibika unaokwenda na malengo ambayo viongozi huwekewa na kutakiwa kuyatimiza pasipo kuwa na visingizio na usimamizi thabiti wa utaratibu huo.

Katika nchi ya Rwanda ambayo mpango huo unatekelezwa, kiongozi wa umma anaposhindwa kufikia malengo yaliyowekwa katika wizara ama idara yake, anahesabika kuwa ameshindwa kazi na anatakiwa kuachia ngazi na kumpisha mtu mwingine.

Nafasi ya uwaziri Rwanda siyo lelemama kama hapa kwetu, ambapo mtu akiteuliwa waziri anafanya sherehe ya kujipongeza. Mawaziri wa Rwanda wanawekewa malengo ambayo wanaposhindwa kuyafikia wanatakiwa kuachia ngazi na Kagame hana msamaha na hilo.

Tanzania ni hodari wa kuwa na mipango. Mipango yetu ni mizuri kiasi kwamba hata majirani zetu wamekuwa wakiiga. Tatizo kubwa ni utekelezaji wake na ndiyo maana nimekuwa na wasiwasi kama kweli pamoja na uzuri wa mpango huu, utekelezaji wake utafanikiwa.

Fedha za walipa kodi masikini wa Tanzania, zimetumika kufanikisha mpango huu kutekelezwa hapa nchini na kwa hiyo ni matumaini ya Watanzania wengi kuona mabadiliko katika utendaji wa Serikali.

Ni wazi kuwa kama kutakuwa na ufuatiliaji wa kutosha katika utekelezaji wake, viongozi wazembe watajikuta wakijifukuzwa kazi wenyewe na kuwaacha wachapa kazi wakiendelea.

Rwanda ni mfano mzuri wa kuwa na uongozi imara wanaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika nchi. Kwa kipindi kifupi pamoja na uchache wa rasilimali, imeweza kupiga hatua kubwa ya kiuchumi, kiasi cha kuwashangaza magwiji wa kiuchumi duniani. Kwa nini isiwe sisi Tanzania?

Moja kati ya mambo yanayotufanya tusisonge mbele kimaendeleo, ni kulindana hasa inapotokea kiongozi ameboronga. Ni mara nyingi tumesikia na kuona watendaji wa Serikali wakiboronga katika utendaji kazi wao bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi yao.

Nakubaliana na nia nzuri ya Rais Kikwete ya kuanzisha utaratibu huu, ila ni muhimu sana kuwepo na ufuatiliaji wa karibu na viongozi wanaoshindwa kufikia malengo yaliyowekwa wasionewe huruma wala haya. Mungu ibariki Tanzania!

source:  Mtanzania; Justin Damian