“
Mamlaka zote msingi wake ni imani, tunawajibika katika kuyatekeleza
yaliyo kwenye mamlaka zetu, na kwamba, mamlaka yatatokana na watu, kwa
ajili ya watu, na chemchem zote za fikra ziachwe hai”- Benjamin Disraeli.
Katika nchi, ustawi wa demokrasia na maendeleo ya kiuchumi
huimarika zaidi kwa kuwapo na uhuru wa kifikra. Kwamba kuwapo kwa
tofauti za kifikra si jambo baya, bali ni jema na la muhimu kwa
maendeleo ya nchi, kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kwamba siku zote,
mawazo na mahitaji ya wananchi yatangulizwe.
Hivyo basi, ustawi wa demokrasia na maendeleo ya kiuchumi huchangiwa
pia na kuwapo kwa wananchi wenye uwezo wa kutathmini michango
itokanayo na wengine katika jamii husika.
Ni muhimu pia kukawapo wanasiasa wenye uwezo wa kutathmini mambo na
kuja na hoja zenye mashiko kwa maslahi ya nchi, badala ya hoja zenye
kulenga kuibakisha nchi kwenye hali ya kugota kisiasa na kimaendeleo ya
kiuchumi.
Kuwapo kwa siasa za vyama vingi ni jambo jema kwa nchi, lakini,
kukosekana kwa umakini katika kuendesha siasa za vyama vingi hupelekea
kupunguza ladha na maana ya kuwa na siasa za vyama vingi. Maana, vyama
vingi ina maana pia ya kuwapo kwa fikra nyingi zenye kutofautiana na
hata kufanana, lakini, ni vema zikawa ni zenye kujenga.
Nahofia, kuwa katika wakati tulio nao sasa, pamoja na hoja za msingi
zinazoibuliwa kwenye jamii, bado nchi yetu imekumbwa na balaa la
kuwapo kwa siasa za reja reja ( retail politics). Ni siasa zisizo na
maslahi kwa nchi.
Ningependa hapa nitoe mfano wa siasa za rejareja zenye kupunguza
ladha ya siasa za ushindani wa vyama vingi. Hivi karibuni Katibu Mkuu
wa sasa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana amekuwa akizungumzwa
kuhusishwa na kashfa ya kusafirisha pembe za ndovu.
Hakika, haya ya Kinana ni mfano wa siasa zetu za reja reja. Binafsi
niliyasoma zamani sana maelezo ya Kinana mwenyewe juu ya asivyohusika
na kashfa hiyo, ingawa ni kweli kuwa pembe hizo za ndovu zilikamatwa
zikiwa zimepakiwa kwenye meli ambayo Kinana ana hisa nayo kwenye
umiliki.
Inavyoeleweka, si kwa Kinana tu, hata kwa yeyote mwenye kutaka
kujua. Kwamba kwenye taratibu za usafirishaji wa majini kuna Wakala wa
Meli ( Shiping Agency) na wenye kuhusika na taratibu za kupakia mizigo
kwenye meli kabla haijasafirishwa, (Clearing and Fowarders).
Hivyo basi, mmiliki wa meli ni mtu mmoja na wenye kukagua na
kuipitisha mizigo ni wengine. Mmiliki wa meli anaweza kabisa asijue
kilicho ndani ya shehena kwenye meli yake mbali ya kile kilichoandikwa
kwenye nyaraka alizokabidhiwa na wahusika wa zoezi la ukaguaji na
upakiaji wa shehena ndani ya meli. Na katika hili, Kinana mwenyewe
ameshaweka wazi, kuwa yeye si mtendaji wa shughuli za kila siku za
kampuni hiyo ya meli ambayo ana hisa nayo kwenye umiliki.
Hivyo basi, kwa akili ya kawaida tu, binafsi sioni ni kwa namna gani
Kinana ahusishwe na kashfa hii. Isitoshe, shauri lenyewe
lilishafikishwa mahakamani. Hivyo, hili si shauri jipya. Vinginevyo,
kuwepo ushahidi wa moja kwa moja wenye kumhusisha Kinana na kadhia ili
kulifanya kuwa ni shauri jipya.
Kwa sasa hakuna kitu kama hicho. Badala yake, siasa hizi za reja
reja ndizo zinazofanya Abdulrahman Kinana pasipo kutendewa haki,
ahukumiwe mitaani.
Ndio, katika hili Abdulrahman Kinana ni mhanga wa siasa za reja reja
ambapo, upinzani wa kisiasa, kwa kutumia hoja dhaifu kama hizi au
zinazofanana nazo, badala ya kumboboa Kinana kisiasa, itakuwa ni
kudhihirisha kiwango cha chini cha ujengaji wa hoja mbele ya watu
makini wenye kuchambua mambo kwa mtazamo usiokuwa na upendeleo wala
ubaguzi. Na watu hao makini siku hizi ni wengi, hata miongoni mwa watu
wa kawaida vijijini.
Na hakika inasikitisha, kuwa jamii yetu imekumbwa na wimbi hili la
siasa za reja reja ambazo wenye kuzifanya, yumkini huwa na malengo ya
kuwachafua wahusika na hata kuwavunjia hadhi na heshima katika jamii.
Si siasa za kistaarabu. Tukiacha haya yakaendelea kushamiri bila
kukemewa, basi, ni wengi watakuwa wahanga wa siasa hizi.
Hivyo, ni vema na ni busara, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi,
na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa kwanza, sote tukashiriki kupiga
vita siasa hizi za reja reja ambazo, kimsingi, zinachangia kufifisha
maana nzima ya ushindani wa kisiasa wenye maana.
Kwamba tuhakikishe kuwa roho ya upinzani na ushindani wa kisiasa
haipotei. Maana, ushindani wa kisiasa ni chachu ya kuongeza kasi ya
ustawi wa jamii, kisiasa, kiuchumi na kimaadili. Nahitimisha
source: Raia Mwema Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment