Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
(email the author)
Mchakato wa kuandika Katiba Mpya
umepamba moto, huku Tume ikielekea kwenye hatua ya Mabaraza ya Katiba,
baadhi wadau wakidai mabaraza hayo yana kasoro, yamechaguliwa
kiitikadi.
Hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitishia kujitoa katika mchakato wa Katiba iwapo madai yake mbalimbali yasingesikilizwa hadi Aprili 30, 2013.
Katika msimamo huo uliokuwa umetolewa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akijadili hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, chama hicho kilitaka:
Mosi, kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe hao wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na Mkutano wa Maendeleo ya Kata (WDC);
Pili, walitaka Serikali ilete mbele ya Bunge Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kufanya marekebisho ya vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kuweka wazi namna wawakilishi wa taasisi hizo watakavyopatikana kutoka kila taasisi na idadi yao kwa kila taasisi;
Pia walitaka vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara, ili kuhakikisha kwamba wajumbe wa Zanzibar ambao hawatakuwa pungufu ya theluthi moja ya wajumbe wote watashiriki katika mijadala inayohusu mambo ya Muungano tu na siyo mambo ya Tanzania Bara yasiyokuwa ya Muungano;
Katika sheria hiyo, pia Chadema walitaka vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge Maalumu la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni viondolewe ili kumwondolea Rais uwezo wa kubadilisha uamuzi uliopitishwa na Bunge Maalumu;
Walitaka pia vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura ya maoni ili kurekebisha hali ya sasa ambayo Katiba na Sheria za Uchaguzi hazitambui uwepo wa kura za maoni na utaratibu wa namna ya kuiratibu, kuisimamia na kuiendesha;
Hata hivyo, madai hayo hayakutekelezwa hadi ilipofika siku ya mwisho ya tishio, hali iliyokilazimu chama hicho kubadili msomamo kupitia maoni ya kambi hiyo kuhusu bajeti ya
Wizara ya Sheria na Katiba iliyowasilishwa na msemaji wake, Tundu Lissu.
“Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hayajatimizwa hadi tunatoa maoni haya. Mwenyekiti wa Tume (ya Katiba), Jaji Joseph Warioba amesema kwamba uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ambayo Tume inakiri ulivurugwa na mivutano ya kisiasa na kidini, hautarudiwa na Mabaraza hayo yataendelea,” anasema Lissu.
Hata hivyo, kwa upande wa Serikali, Waziri Mkuu aliahidi wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.
Ahadi hiyo ya Waziri Mkuu inaelezwa kuwa ndiyo imewalainisha Chadema hadi wakaacha kujitoa katika mchakato huo.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetafakari sana
ahadi hii ya Waziri Mkuu. Pamoja na kwamba ni ahadi ya maneno tu, kama
ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete kwamba
marekebisho yote yanayohitajika katika Sheria hiyo yatakamilika hadi
kufikia Novemba 2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona ni vyema
iipe muda Serikali wa kuleta marekebisho tajwa ndani ya Mkutano huu wa
Bunge la Bajeti,” anasema Lissu
Hata hivyo, Lissu anatoa sharti jipya: “Endapo hadi kufikia
mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa
marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi
matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, basi
Chadema itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima,
pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania
wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha Watanzania kuikataa
Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni”.
Lissu ambaye ni mwanasheria anaonya kwa kutumia
mifano ya Kenya na Zimbabwe ambako rasimu za katiba zilikataliwa na
uchaguzi zilizofuata zikafanyika chini ya Katiba za zamani, hali
iliyozua machafuko.
“...Kenya, kwanza Serikali ya KANU chini ya Rais Daniel arap Moi, na baadaye Serikali ya NARC chini ya Rais Mwai Kibaki, zilijaribu kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya ya Kenya kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ambayo ilipopelekwa kwenye kura ya maoni mwaka 2005 ilikataliwa na wananchi wa Kenya...baadaye Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 2007 kwa mujibu wa Katiba ya zamani ya Kenya ya mwaka 1969. Matokeo ya uchaguzi huo chini ya Katiba ya zamani yaliingiza Kenya katika machafuko.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment