Na Gustav Chahe, Iringa
RAIS wa Baraza la Maakofu Tanzania
(TEC) Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa amewataka waamini wakristo
kutokuwa na moyo wa kuhamaki kutokana na kitendo kilipuliwa Kanisa
Katoliki huko Arusha.
Amesema kama ilivyoutamaduni wa
Kikristo, yanapotukia matukio ya kusikitisha kama hayo silaha iliyo
kubwa ni sala kumuomba Mungu atoe jibu kwa wanaohusika na mateso kama
hayo.
“Kasi ya sala iendelee, ili Mungu wetu wa Amani ajenge fikira za upendo na haki katika mioyo yetu” alisema.
Amesema waamini wasikate tamaa na
kuacha kusali kwa kuwa Mungu ndiye mwenye jibu na atatoa majibu kadiri
atakavyo kwa wale wote wanaowatesa wenzao kwa sababu zao binafsi.
Hata hivyo alisema licha ya kuwa
kila mtu amepokea kwa mshituko na maumivu makubwa, roho za watu
zinazoteswa na wengine Mungu atazifariji na kuziponya lakini mtesaji
atapata majibu yake.
Alisema waliopoteza maisha katika mlipuko huo Mungu atawarehemu na kuwafariji majeruhi wote.
“Waliopoteza maisha wapokee Rehema ya Mungu na waliojeruhiwa wafarijiwe na uwezo wa Mungu” alisema.
Hali kadhalika amesema upendo na haki ni zawadi kutoka kwa Mungu na hivyo, anayedhurumu wengine zawadi hiyo atapata pigo kubwa.
Aidha amesema wakati uliopo sasa ni
wakutafakari na kumkabidhi Mungu yale yote yanayowasumbua wanadamu na
kuongeza nguvu ya sala ili majibu ya Mungu yapatikane kwao.
“Tulieni na kufanya tafakari kasha
mwambie Mungu hayo yote ayafanyie kazi kwa uweza wake. Sisi binadamu
tunategemea nguvu kutoka kwake” alisema
No comments:
Post a Comment