THE
CIVIC UNITED FRONT- (CUF – Chama Cha Wananchi)
GHASIA ZA MTWARA
The Civic United
Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimesikitishwa sana na vurugu zilizotokea
Mtwara tarehe 22 Mei 2013 na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na
polisi tarehe 23 Mei 2013. Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na
Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi zaka za miradi ya
kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha
kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya
taifa.
CUF inalaani
vikali vitendo vya kihalifu vya kuchomea nyumba ya mwandishi wa habari wa
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo, na nyumba za baadhi ya
viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani vikali vitendo vya kuhujumu miundombinu
muhimu likiwemo daraja la Mikindani linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya
Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
CUF
imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya askari wanne wa JWTZ kwa ajali ya
gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao wakisafirishwa toka Nachingwea
kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti vurugu.Tumepeleka salamu za pole kwa CDF Jenerali
Mwamunyange na kupitia kwake kwa familia za marehemu. Tunawapa pole askari wote
waliojeruhiwa na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na waweze kurejea
katika ulinzi wa taifa letu.
Vilevile
tumesikitishwa na kifo cha raia wawili kwa kupigwa risasi akiwemo mama mjamzito
na raia wengi kujeruhiwa. Tunawapa pole familia za marehemu na kuwaombea wote
waloumia wapone haraka na waendelee na shughuli zao.
Taarifa za
vyombo vya habari vinaeleza kuwa ghasia hizi zilianza baada ya hotuba ya bajeti
ya Waziri wa Nishati na Madini iliyosomwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kusisitiza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara
kwenda Dar es Salaam.
Taarifa
tulizozipata toka Mtwara zinaeleza kuwa jana kuanzia asubuhi, wakati Waziri Nchimbi
akisoma tamko la serikali bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu kuwa hali ya Mtwara
sasa ni shwari askari wa Jeshi la Polisi walifanya vitendo vya kinyama kwa raia
wasio na hatia. Polisi walipita katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana,
kuwapiga na kuwachukua kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi
za moto zilipigwa hovyo hovyo. Aidha katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo
waliwapiga wake zao, watoto wadogo na hata wazee kwa madai kwamba vijana wao
wanasumbua. Binti mjamzito aitwae Fatuma alipigwa risasi na kufariki. Katika
eneo la Mkana Read, Polisi walichoma moto soko la wananchi, nyumba nyingi za
raia zimechomwa moto na polisi wamepora mali za watu zikiwemo za maduka ya
wafanyabiashara. Wananchi wengi wakiwemo wanawake wamelazimika kukimbia nyumba
zao. Taarifa tulizopata zinaeleza vitendo vya kinyama vya polisi vilisita baada
ya maafisa wa juu wa Jeshi la Polisi kufika Mtwara.
Vurugu
zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei hazihalalishi Jeshi la Polisi kupiga watu,
kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda vya biashara na kupora mali za watu wasio
na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora mali na kuchoma vibanda vilitokea
Tandahimba mwaka jana. Weledi ndani ya Jeshi la Polisi uko chini sana.
Tunalaani vikali vitendo vya Jeshi la Polisi la kupiga watu, kuchoma nyumba na
kupora. Uongozi wa Jeshi la Polisi uchukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi
ya polisi waliohusika na vitendo hivyo. Tunatoa wito kwa asasi za haki za
binadamu na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia wahanga wa Mtwara kudai
haki zao.
Pamoja na
kulaani vitendo hivi vya kihalifu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale
waliohusika na vitendo hivyo, Serikali itafanya makosa makubwa na kuingiza nchi
katika mgogoro wa muda mrefu na wananchi wa mikoa ya kusini ikiwa itafumbia
macho chimbuko la mgogoro huu na kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni
matokeo ya uchochezi wa wanasiasa wachache wanaojitafutia umaarufu. Narudia
Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa
serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi
Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na
kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa. Mradi mwingine ni
kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi kama malighafi kama
ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki visima vya gesi ya Mnazi
Bay na Msimbati. Kama miradi hii ingeanza kutekelezwa nina uhakika wananchi
wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga gesi ya ziada kusafirishwa Dar es Salaam.
Kauli ya Waziri
Nchimbi Bungeni kuwa serikali itawasaka waasisi wa vurugu hizi ndani na nje ya
Mtwara ni juhudi za kutafuta mchawi badala ya kutathmini kwa nini wananchi wa
Mtwara hawaiamini kabisa serikali ya CCM. Tumepata taarifa kuwa pana mpango
kabambe wa kuwakamata viongozi mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa
wanaohusika na kuchochea, kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na
wafuasi wa CUF. Serikali ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito watu
wasiokuwa na hatia. CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la gesi
tumejenga hoja za kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu
utekelezaji wa miradi ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza.
Viongozi wa CUF hawajachochea vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara
na maandamano ya amani kujenga hoja za kimsingi.
Mimi binafsi
nilienda Mtwara mwaka jana nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara Mtwara mjini
kwa madai kuwa hali siyo shwari wilaya ya Tandahimba. Wananchi wa Mtwara
walitaka nifanye mkutano huo pamoja na kuwa umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye
hivyo na wakakubali. Tarehe 14 Aprili 2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya
mkutano wa hadhara sikukaidi nikafanya mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu
Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya
mkoa wa Mtwara akaambiwa hana ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara mkoa wa
Mtwara na hivyo akasitisha ziara yake.
Kuwakamata
viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na Lindi na wa kitaifa hakutamaliza mgogoro
kati ya serikali na wananchi wa Mtwara ikiwa serikali itaendelea kuwabeza,
kuwadharau na kutowasikiliza. Badala yake itaongeza chuki dhidi ya serikali.
Wakati wananchi
wa Mtwara wamepoteza imani kwa uongozi wa CCM na serikali yake, Serikali
imezuia vyama vingine vya siasa na asasi za kiraia kufanya shughuli za
kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa hiyo kuunyima umma miongozo ya kisiasa
za demokrasia. Umma uliokata tamaa na unaoamini unabezwa, kudharauliwa na
kudanganywa na watawala unaweza kuchukua hatua zenye madhara hata kwa maslahi
yao wenyewe.
Serikali imekuwa
inapotosha kwa makusudi madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara ambayo ni kuwa
serikali itekeleze miradi ya gesi iliyoahidi wananchi wa Mtwara. Badala yake
wananchi wa mikoa mingine wanalishwa sumu kuwa Wananchi wa Mtwara hawataki
raslimali ya gesi iwanufaishe Watanzania wengine. Umeme ukifuliwa Mtwara na
kuunganishwa katika gridi ya taifa utatumiwa na wote waliounganishwa na gridi
ya taifa. Kiwanda cha mbolea cha Mtwara kitazalisha mbolea itakayotumiwa nchi
nzima. Wananchi wa Mtwara hawajasema Watanzania wengine hawana haki ya kwenda
Mtwara kupata ajira au kufanya shughuli za kibiashara. Wanaobomoa umoja na
mshikamano wa kitaifa ni wale wanaowabeza, kuwadharau na kuendelea kuwadanganya
wananchi wa Mtwara na kupandikiza sumu kwa Watanzania wengine kwa kupotosha
madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara na kushindwa kwa serikali kuwajibika
kisiasa kwa ahadi ambazo viongozi akiwemo Rais alizitoa kwa wananchi wa Mtwara.
Wananchi wa
Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka sahihi na kupeleka ombi (petition) kupitia
Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni kujadili kutekelezwa kwa miradi ya gesi
ya Mtwara. Spika Anna Makinda kazuwia ombi hilo kujadiliwa.
Bunge
limeshindwa kuisimamia serikali na kuhoji kwa nini mradi wa kufua umeme MW 300
ambao katika mwaka wa bajeti wa 2011/12 ulitengewa na kutumia shilingi 540
milioni umesitishwa. Mpaka hivi sasa hakuna kamati ya Bunge iliyoenda
kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala yake Spika amekuwa mstari wa
mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala ya kuhakikisha kuwa Bunge
linaisisimamia serikali.
Katika hotuba ya
bajeti ya mwaka huu, Waziri kaeleza serikali kupitia TANESCO kwa kwa
kushirikiana na kampuni ya Symbion itajenga kituo cha kufua umeme cha MW 400 na
kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa kupitia Songea. Hata hivyo bajeti ya
maendeleo haijautaja mradi huu wala kutenga hata shilingi 1 kwenye mradi.
Wananchi wa Mtwara wanaona wanaendelea kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo,
majigambo na kauli za kejeli za Waziri wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa
wananchi wa Mtwara katika masuala ya gesi zinazidi kuongeza chuki na jazba za
wananchi. Mpaka hivi sasa serikali imekataa kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa bomba
na upembuzi yakinifu wa mradi huu. Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati
haielezi kama Wentworth Resources wanaoendesha visima vya gesi wataweza
kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda
Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya kutumia gesi mkoani Mtwara.
Linalonistusha
na kunitisha ni kwa nini viongozi wa juu wa serikali hawataki kuwa wawazi
kuhusu mradi huu na wako tayari kupotosha, kuwagawa wananchi na kudanganya
alimuradi mradi huu utekelezwe na usihojiwe?
Gesi ya Mnazi
Bay, Mtwara iligunduliwa toka mwaka 1982 lakini mpaka hivi sasa haijatumiwa
kikamilifu. Kampuni ya Artumas ilianza utaratibu wa kuichimba gesi mwaka 2006
na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18. Tarehe 17 Oktoba 2007 kampuni ya
Artumas ilitoa taarifa ya mpango wake wa kujenga kituo cha kufua umeme wa MW
300. Mpango huu ulitarajiwa kugharamiwa toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi -
Netherlands Development Finance Company. Gharama za mradi wa kufua umeme
zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 225. Kampuni maalum ya kuendesha mradi huu
ya Tanzania Generation Company Ltd (TANGEN) ilisajiliwa ili kujenga na
kuendesha mradi huu. Kampuni hii ingekopa dola milioni 160 na dola milioni 65
zingechangiwa kama hisa na kampuni nyingine zikiwemo mifuko ya pensheni ya Tanzania
na kampuni ya madini ya Barrick International.
Kampuni nyingine
maalum ilitarajiwa kuanzishwa ili ijenge msongo wa umeme (nguzo za nyaya za
kusambaza umeme) na kuunganisha umeme wa Mnazi Bay kwenye gridi ya taifa. Mradi
huu ungegharimu dola milioni 400. Mradi huu ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko
ya pensheni ya Tanzania na wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu
ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua
na kusambaza umeme (National Power Development Master Plan). Mradi huu wa kufua
umeme MW 300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco
inaueleza mpango huu kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali iliukabali
mradi huu baada ya kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.
Mtikisiko wa sekta
ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka 2008 uliathiri kampuni ya Artumas. Thamani
ya hisa moja ya Artumas iliporomoka toka dola za Marekani 10.80 mwezi wa Aprili
2008 na kufikia dola 0.12 mwezi wa Machi 2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa
ya ukata na ilibidi serikali iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na
ufuaji wa umeme wa MW 18 Mtwara. Barrick International ilijitoa katika mradi wa
TANGEN. Katika kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha
jina lake na kuwa Wentworth Resources Limited na kuteua menejimenti mpya.
Tarehe 10 Juni
2009 Rais Kikwete alipokuwa anawahutubia Wabunge na Wananchi katika Ukumbi wa
Kilimani Dodoma kuhusu athari za mtikisiko wa uchumi duniani alieleza “Kwa
sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua.
Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. Matokeo
yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa
mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na ajira. Kwa mfano: Mradi wa umeme wa
MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake
haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium smelter,
Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji
na mbolea Mtwara.” Kwa kauli ya Rais ambayo wananchi wa Mtwara na Watanzania
kwa ujumla waliisikia kwani hotuba hii ilirushwa live na Shirika la Utangazaji
la Tanzania – Radio na Televisheni na vyombo vingine vya habari. Miradi ya
kutumia gesi ni pamoja na kufua umeme MW 300, kutengeneza mbolea inayotumia
gesi kama malighafi, aluminium smelter inayohitaji umeme mwingi, na kiwanda cha
saruji ambacho kinatumia umeme na kinu chake kinaweza kutumia gesi. Wananchi
wakamuamini Rais wetu na wakaelewa kuwa miradi hii imekwama kwa sababu ya
mtikisiko wa uchumi na kwamba serikali inajitahidi kutafuta njia mbadala ya
kujikwamua ili miradi hiyo iendelee.
Wakati wa
kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais Kikwete aliwaeleza wananchi wa Mtwara
akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara itakayotumia gesi ya Mnazi Bay.
Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa 2010, ibara ya 63 kifungu (j) Kuzalisha
umeme (300MW) kutokana na gesi asili ya Mnazi Bay (k) Kupanua mitambo ya
kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es
Salaam. Mitambo ya kufua umeme ya Dar es Salaam ilitegemewa itumie gesi ya
Songosongo kwani bomba la kutoka Songosongo hadi Somanga mpaka Dar es Salaam
lingepanuliwa. Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq- Songas ilijiandaa
kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka Songosongo – Somanga
– Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya kufua umeme Dar es
Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi. Serikali iliisitisha kampuni hiyo
isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa umekamilika na kuongeza uwezo
wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau MW 200.
Rais Kikwete
alipoenda Mtwara kuhudhuria sherehe ya Mashujaa tarehe 25 Julai 2011
alizungumza na wananchi wa Mtwara na kueleza miradi ya maendeleo
itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay ikiwemo ufuaji wa umeme wa MW
300 na kupanua bandari ya Mtwara.
Tarehe 12 Oktoba
2011, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa “Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba
12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango
Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa
yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo. Rais Kikwete amepokea ripoti
hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery&Equipment
Import&Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo
kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na
gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha
umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huo mkubwa wa umeme
wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na
utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV
High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka
Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.”
Mikoa sita
ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa,
Kigoma na Kagera. Mradi huu pamoja na kufua umeme wa MW 300 Mtwara ungekamilisha
kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye gridi ya taifa. Taarifa iliendelea
kueleza “Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja
ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia
maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo
itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.”
Maelezo haya
yametolewa na Ikulu na vyombo vya habari vikayatangaza na wananchi wa Mtwara
wakasikia. Kutekeleza mradi wa kufua umeme kutaifanya Mtwara iwe na umeme wa
kutosha kushawishi kampuni kuanzisha viwanda hasa ukizingatia ahadi ya Rais
Kikwete ya kupanua bandari ya Mtwara. Mwaka wa fedha wa 2011/12 serikali
ilitenga na kutumia shilingi 540 milioni fedha za maendeleo za mradi wa Mnazi
Bay 300MW Development Project. Baada ya hapo mradi huu haukutengewa fedha tena.
Badala ya mradi huu kuendelezwa kama Rais alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na
Watanzania kwa ujumla badala yake wanasikia serikali imezindua mradi wa kujenga
bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Kwa taarifa ya
Ikulu gharama za mradi wa kufua umeme wa MW 300 Mtwara na kuiunganisha mikoa
sita katika gridi ya taifa gharama yake ni dola milioni 684. Mradi wa kutandaza
bomba la gesi unagharimiwa na mkopo wa dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export
Import Bank ya China. Ni wazi gharama za kufua umeme Mtwara na kuunganisha
mikoa sita kwenye gridi ya taifa ni ndogo zaidi kuliko gharama za kutandaza
bomba la gesi.
Msongo wa umeme
za kV 400 unajengwa kuunganisha Iringa – Dodoma – Singida na Shinyanga. Mradi
huu unatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Nyaraka ya mradi unaonyesha
gharama za kujenga umeme za kV 400 ni dola za Marekani 600,000 kwa kilomita 1. Gharama za kujenga
bomba la gesi lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola 1,309,636 kwa kilomita
1. Kwa madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga bomba la gesi ni zaidi ya
mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es Salaam. Isitoshe unaweza
kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusambaza kwa msongo huo huo.
Ujenzi wa bomba
la Dar es Salaam Mtwara umeanza bila kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa
kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha hadi Dar es Salaam. Bomba hili
litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya
Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango
unaoeleweka wa kupata futi za ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze
kutumiwa kikamilifu.
Mpaka hivi sasa
gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33.7 imegunduliwa katika bahari yenye
kina kirefu. Uchimbaji wa gesi hii bado haujaanza. Inaweza kuchukukua miaka 7 –
10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa gesi kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi
bahari kuu bado hazijafanya uamuzi wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha
gesi hadi nchi kavu. Kwa kuwa gharama za kujenga bomba la gesi chini ya bahari
ni za juu sana, kampuni hizi zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu
kwenye eneo lililo fupi kuliko yote. Statoil imegundua gesi nyingi eneo la
Zafarani bahari kuu eneo la mkoa wa Lindi. Hivi sasa wanatazama maeneo ya Kilwa
kuweza kuweka kituo cha nchi kavu. Bandari ya Lushungu kata ya Limalyao, wilaya
ya Kilwa ambayo ina kina kirefu cha bahari yaelekea kuwavutia. Kwa hivi sasa
hakuna uhakika gesi iliyogunduliwa bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa
kujenga bomba kubwa umefanywa haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida
zake kiuchumi. Jambo la kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na kuacha
kutekeleza mradi wa kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi, kijamii na
uwajibikaji wa kisiasa?
Wentworth
Resources wamefanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kubaini kwamba
njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi
bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mbolea na kemikali nyingine
Mtwara. Kiwanda cha mbolea chenye faida kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa
hata kama akiba ya gesi iliyogunduliwa siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay.
Mradi wa kujenga kiwanda unaweza kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea
kiwanda kitazalisha methanol yenye soko kubwa duniani. Kiwanda kitatumia hewa
ukaa (carbondioxide) na kwa hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha mazingira.
Uongozi wa Wentworth Resources una uzoefu wa miaka mingi katika miradi ya
kutumia gesi. Wanajua wanalolieleza. Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka
gesi watakayozalisha kwenye bomba la gesi la kwenda Dar es Salaam.
Serikali
imeanzisha mgogoro wa gesi kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kutandaza
bomba la mafuta na kuacha miradi yenye manufaa makubwa kiuchumi na kijamii kwa
taifa letu. Uchunguzi huru na wa kina ufanyike kubaini sababu za serikali
kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara na kukumbatia mradi wa kutandaza bomba.
Ripoti aliyopewa Rais ya mradi wa kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6
katika gridi ya taifa itolewe ili Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi
huu. Mkataba wa mkopo na utekelezaji wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe
wazi. Serikali iruhusu kampuni ya Wentworth resources kuendelea na mradi wa
kiwanda cha mbolea. Rais aende Mtwara kuwaeleza wananchi kuwa ahadi alizoeleza
za kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.
Vyama vya siasa
na asasi za kiraia viruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara kueleza njia za
kidemokrasia za kudai haki za kiuchumi za wananchi wa Mtwara. Bunge liunde
kamati teule ya kuchunguza kwa nini Mradi wa Kufua umeme MW 300 umesitishwa na
serikali, upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi na mikataba yote
inayohusiana na mradi huu.
Sakata hili la
gesi ya Mtwara linaonyesha wazi kuwa hatuna sera muafaka na mkakati wa
kuendeleza sekta ya gesi kwa manufaa ya taifa letu na Wananchi wa kawaida. Badala
ya gesi kuwa neema inaelekea kuwa itakuwa balaa na laana. Sera ya gesi inapaswa
kuweka taratibu zitakazohakikisha kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta
hii na utakaolinufaisha taifa letu bila kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye
teknolojia ya kutafuta na kuchimba gesi. Wananchi wa Mtwara wanahitaji
kushirikishwa. Serikali iwe wazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi ya gesi.
Prof. Ibrahim
Haruna Lipumba,
Mwenyekiti
wa Taifa, Mei 24 2013
source Haki Ngowi
No comments:
Post a Comment