Bunge jana kwa kauli moja lilitoa azimio la
kuitaka Serikali na vyombo vyake vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi
ya viashiria vya aina zote za uvunjifu wa amani unaojitokeza nchini.
Hatua
hiyo ya Bunge inafuatia matukio kadhaa yaliyotokea katika siku za hivi
karibuni na kutishia amani kwa misingi ya dini kama kushambuliwa na
kuuawa kwa viongozi wa dini, kuchomwa moto nyumba za ibada na chokochoko
za watu wachache zinazopandikiza chuki miongoni mwa wafuasi wa
madhehebu mbalimbali ya dini.
Jumapili iliyopita mtu asiyejulikana
alirusha bomu wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la Kanisa la
Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi ya Olasiti, jijini Arusha na kuua
mtu mmoja na kujeruhi wengine zaidi ya 60. Hadi sasa watu waliokufa ni
watatu baada ya majeruhi wawili kufariki hospitalini.
Tukio hilo la
Arusha limelitikisa taifa, huku Serikali ikionekana kushindwa kupata
jibu kuhusu lengo la watu waliofanya kitendo hicho cha kigaidi. Fadhaa
hiyo ya Serikali inaeleweka, hasa tukitilia maanani kwamba wakati bomu
hilo likilipuka, alikuwapo Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu
Francisco Montecillo Padilla ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe
hizo akiwa na mwenyeji wake, Askofu Josephat Lebulu wa Jimbo Katoliki la
Arusha.
Hivyo, Serikali ingekuwa katika wakati mgumu iwapo viongozi
hao wa Kanisa Katoliki wangedhurika au kuuawa katika shambulio hilo. Pia
taswira ya nchi yetu mbele ya jumuiya ya kimataifa ingechafuka. Taarifa
zisizo rasmi zinasema Balozi huyo wa Vatican ndiye aliyekuwa mlengwa wa
shambulio hilo, ingawa sio viongozi wa Serikali wala Kanisa Katoliki
waliokuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Ndio maana Bunge
limetafakari hali hiyo na kuona umuhimu wa kutoa azimio la kuitaka
Serikali kuchukua hatua za haraka. Pamoja na kwamba sio jukumu la Bunge
kuiambia Serikali hatua za kuchukua, azimio lake lililotolewa jana mjini
Dodoma halikuacha shaka yoyote kwamba Serikali lazima ianze utekelezaji
wake haraka kadri inavyowezekana.
Bunge limetaka uchunguzi wa kina
ufanyike na kuwatia nguvuni wahusika wote wa tukio hilo na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria ili kuwapa wananchi matumaini ya kujumuika na
kuabudu kwa uhuru pasipo kuwa na hofu ya usalama wao. Tunaambiwa kwamba
tayari baadhi ya watu wamekamatwa.
Hata hivyo, tungependa kutoa
tahadhari kwa Serikali kuhusu utekelezaji wa Azimio la Bunge, kwani
kutokana na mazingira tuliyomo hivi sasa inawezekana kabisa Azimio la
Bunge likapotoshwa makusudi na kupewa tafsiri ya kisiasa. Lazima
Serikali na vyombo vya dola vitambue kwamba azimio hilo la Bunge halina
maana ya kutangaza hali ya hatari wala kufuta Katiba ya nchi, kwa maana
ya kuondoa haki za kiraia, kufuta shughuli za kisiasa na kuendesha nchi
kwa amri na udikteta.
Kwa maana hiyo, shughuli za kisiasa lazima
ziendelee bungeni na nje ya Bunge kwa vyama vya siasa kushindana kwa
hoja na vyama vya upinzani vikiendeleza mikakati ya kukiondoa chama
tawala madarakani. Hizo ndizo siasa za ushindani na Serikali lazima
iikubali hali hiyo. Hata hivyo, vitendo vya kugawa wananchi kwa misingi
ya dini, siasa na kabila vipigwe vita na kamwe visivumiliwe. Hayo ndio
madhumuni ya Azimio la Bunge lililotolewa jana.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment