Ndugu zangu,
” Maisha yetu huanza kuisha siku tunapoanza kunyamaza kwenye mambo yenye maana”- Martin Luther King Jr.
Leo Mei 3
ni Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari Duniani. Hapa Afrika Mashariki,
siku hii inaazimishwa kule Arusha kwa Kongamano lililoandaliwa na Mfuko
wa Ruzuku kwa Vyombo Vya Habari ( TMF). Macho na masikio yetu
yanaelekezwa Arusha. Maana, kule Arusha kunatarajiwa kuzinduliwa kwa
Itifaki ya Vyombo Vya habari. Ndio, kuna Azimio la Arusha linakuja,
lakini hili linawahusu Wanahabari. Na kauli mbiu ya Siku hii ya Vyombo
Vya Habari ni ” Mazingira Mazuri na Salama ya Kufanyia Kazi Kwa
Wanahabari wa Afrika Mashariki”.Ni ukweli, kuwa mwanahabari hawezi kuwa
huru
kwenye mazingira mabaya na yasiyo salama ya kufanyia kazi. Lakini, kuna
maswali ya kujiuliza na kutafakari kwa kina. Ni natumaini yetu walio
kule Arusha wataifanya kazi hii ya kufikiri. Wafanye hivyo ili Azimio
watakalotoka nalo Arusha liwe lenye maana kwa wanahabari na umma
unaowatumikia.
Na mwanahabari anapokuwa hana uhuru wa kiuchumi kimsingi anawekwa kwenye mazingira mabaya na yasiyo salama ya kufanyia kazi.
Hakika,
Media ni mhimili muhimu sana katika nchi yeyote inayotaka kupiga hatua
za kweli za maendeleo. Hata hivyo, katika nchi zetu hizi, media
imefanywa kuwa adui wa watawala na hivyo basi, wakati mwingine kumekuwa
na mahusiano ya uhasama, kuviziana na kuwindana.
Na kwa
umma, media nayo ina sehemu yake ya lawama pale inaposhiriki kubomoa
badala ya kujenga misingi ya Utaifa na Ujenzi wa Taifa Huru lenye nguvu
za kiuchumi. Ni pale, inaponyamaza kwenye mambo ya maana na kushabikia
yasiyo na maana, yenye kupotosha na kusababisha chuki na migongano
katika jamii. Mathalan, udini, ukabila na mambo ya abrakadabra kama
vile ndoto za Babu wa Loliondo na Kikombe chake.
Na hakika
hili huchagizwa pale Media inapoingiliwa na wanasiasa, wafanyabiashara
na hata baadhi ya viongozi wa dini. Ni matokeo ya Media kukosa uhuru wa
kiuchumi. Ni wakati sasa wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla
wake, kudai haki za kuwa na trade unions zake zenye meno. Kudai pia haki
ya kupewa ruzuku na Serikali inayotokana na kodi za wananchi ili vyombo
hivyo viweze kujijengea uwezo zaidi katika kuitumikia jamii. Media ya
nchi haiwezi kuishi kwa kutegemea ruzuku inayotokana na walipa kodi wa
Ulaya na Marekani. Ni fedheha pia.
Ndugu zangu,
Mengine
tunayoyashuhudia siku hizi ni kwa baadhi ya vyombo vya habari
kushabikia mambo yasiyo na maana na kunyamazia yale ya msingi. Hii ni
hatari kwa mustakabali wa nchi zetu hizi.Na tusije kusahau kuwa umma
bado una imani kubwa kwa media. Hivyo, kuna umuhimu wa kuzingatia
maadili. Inahusu virtue, kwa maana ya maadili na kutenda yalo ya haki.
Kutenda yalo mema. Mtu mwenye maadili mema utamwamini, ndivyo pia
wasemavyo Waingereza; a virtuous person is someone you can trust.
Mzazi anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kisiasa anapaswa kuwa a
virtuous person, kiongozi wa kidini anapaswa kuwa a virtuous person,
Mwandishi wa habari anapaswa kuwa a virtuous person. Vivyo hivyo kwa
mwalimu.
Ndugu zangu,
Wanahabari
wa Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wao uliopita wameonyesha kuwa
inawezekana, kwa Media kutanguliza maadili, kuachana na yasiyo na maana
na kujielekeza kwenye yaliyo ya msingi na yenye kulinda Umoja na Utaifa
wao.
Na katika
haya ya kushabikia yasiyo na maana, kuna wakati Julius Nyerere alitua
Jomo Kenyatta Airport. Hapo aliongea na wanahabari. Ni miaka ile ya
mwanzoni mwa Uongozi wa Rais Mwinyi baada ya Nyerere kung’atuka. Enzi za
Mwinyi kuna mambo yaliyoonekana yana nafuu zaidi. Kukawa na minong’ono,
kuwa eti Julius Nyerere anamwonea wivu Mwinyi na ana mipango ya
kumwondoa madarakani.
Pale Jomo
Kenyatta mwanahabari wa Kenya akamwuliza Nyerere: ” Mwalimu tunasikia
unapanga njama za kumwondoa Mwinyi madarakani na hata Rais Moi wa hapa
Kenya!”
Julius Nyerere alijibu, ” Hivi wewe ukiambiwa mimi natembea na mama yako, utakimbilia kwenda kuandika habari hiyo?!”
Naam, tunajifunza nini kwenye jibu hilo la Julius Nyerere?
Kwamba
kwenye falsafa tunaambiwa, kuwa unapoletewa jambo kuna matatu ya
kuyaangalia na kuyazingatia: Udadisi wa uhalisia wa jambo lenyewe
(Reasoning), Mantiki ( Logic) na Ulinganishi wa nadharia ( Metafisiki)
Hivyo
basi, unapokutana na mtu akakuambia kuwa alipokuwa akitembea jana
usiku, njiani alimwona mbwa akimtafuna mbwa mwenzake, basi, unachopaswa
kufanya ni kutulia na kutafakari.
Yumkini
usiku huo mtu huyo alikuwa akitoka kwenye kilabu cha pombe, na kwenye
ulevi wake, paka aliyemwona akigombana na paka mwenzake, kwake ilikuwa
ni mbwa anayemtafuna mbwa mwenzake!
Happy Media Day!
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
No comments:
Post a Comment