Ndugu zangu,
Naiona hatari kubwa nyingine inakuja
mbele yetu. Ni haya makundi mawili; MaBodaboda na MaMachinga. Hofu
yangu kuna wanasiasa wachache wanaowaona vijana hawa, katika matatizo
yao ya kiuchumi, kuwa ni mtaji wa kisiasa. Na kimsingi wanawageuza kuwa '
Shuka za Kisiasa'. Na hapa ni wanasiasa wa vyama vyote.
Hatari yake?
Viongozi wasipokuwa makini, wakaacha
kutanguliza busara na hekima kwenye kauli zao, basi, hofu ya kauli
kupelekea machafuko na kuvunjika kwa amani itabaki kuwepo.
Maana, hawa MaBodadoba na
MaMachinga, pamoja na kuwa wengi wao ni vijana wema kabisa, na ambao,
kwenye mahangaiko yao, kama wagonjwa, wanamsikiliza kila anayekuja na
kauli za kuwapa matumaini, hata kama ni ya muda mfupi, na hata kama ni
kwa kuvunja sheria.
Na kwa vile Elimu ya Uraia iko chini
sana katika jamii yetu, hata kwa miongoni mwa viongozi wetu, basi, ndio
maana naiona hatari hii kubwa inayokuja mbele yetu. Kwamba MaBodaboda
na MaMachinga wakiendelea kutumiwa kama ' Shuka za Wanasiasa', basi,
yumkini, huko tuendako Watanzania tujiandae na kazi ya kuchimbiana
makaburi. Maana, siku zote, maovu huzaa maovu. MBodaboda au Mmachinga
mmoja akiuawa, kuna mia watakaokuja kutaka kulipiza kisasi. Na Polisi
mmoja akiuawa, kuna operesheni ya kipolisi itakayofuata. Na polisi wetu
hawa ni vijana hawa hawa ambao wengine wameponea chupuchupu kuwamo
kwenye makundi haya ya MaBodaboda na MaMachinga, lakini sasa, tumewapa
pia silaha za moto wabebe.
Naam, tukichoka kuhubiri Amani, Upendo Na Mshikamano, basi, tujiandae na kazi ya kuchimbiana makaburi.
Maggid
Iringa,
0754 678 252
No comments:
Post a Comment