NI
vigumu kuamini mambo tunayoyashuhudia kwa kuyaona na kuyasikia. Binafsi
najiuliza ni nini kimetusibu hadi tunafanya mambo yakitoto kiasi hiki?
Na ni kwa nini tunaonyesha kila dalili za jamii ya watu waliokata tama
kabisa na sasa wanajifanyia kila linalokuja akilini mwao… alimradi.
Siendi mbali, na wala tusiende mbali kwa sababu siku hizi huhitaji
kwenda mbali kukutana na uthibitisho wa kile ambacho nimekuwa nikikisema
muda wote huu, nacho ni kwamba hatuna muda wa kufanya jambo lolote kwa
kulitafakari kwa makini kwa sababu tuko “transit” tukienda
nisikokujua.
Tusiende mbali kwa sababu hatuhitaji kielelezo zaidi kuliko jinsi
ambavyo serikali yetu iko “bize” inafanya madudu, ikihaha huku na kule
ili kueleza jambo ambalo yenyewe haijalielewa. Ni dhahiri kwamba maelezo
ya asiyeelewa hayawezi kumwelewesha mweleweshwaji na akaelewa.
Ni kweli kwamba tarakimu na asilimia za viwango vya watoto wetu
kufeli katika mtihani wa kidato cha nne ni za kutisha kwa baadhi ya
watu. Lakini hazishangazi, kwa sababu hali ya elimu tunayowapa watoto
wetu ni ya kutisha. Kwa hiyo, ingawaje ni halali kwa yeyote kutishika
kutokana na takwimu za mwaka jana, lakini si halali kushangaa.
Labda nijieleze kidogo. Ukiwa unatembea katika mbuga ambayo
inajulikana kuwa na nyoka wengi, na ukagongwa na nyoka, utatishika bila
shaka, lakini hutakiwi kushangaa kwa sababu unajua fika kwamba mbuga
hiyo ni maskani ya nyoka na wewe umewaingilia katika maskani yao.
Lakini ukikodi chumba katika hoteli ya nyota tano, kama Serena kwa
mfano, kisha wakati umelala kitandani ukajikuta umemlalia nyoka, hata
asipokugonga, utatishika na kushangaa kwa mara moja.
Utatishika kwa sababu ile ile ya yule aliyetembea mbugani na
akagongwa na nyoka, kwa sababu kuna hatari ya kweli ya kifo, lakini
katika hoteli kama Serena utashangaa ni jinsi gani hoteli kama ile
imeruhusu nyoka kitandani. Kwa kweli utakuwa na haki hata ya kushuku
kwamba “wabaya” wako, kama unao, wamepanga wafanyakazi wa Serena
wakutegeshee mdudu huyo hatari kama mwenza wako wa usiku.
Sasa, kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha nne, tunashangaa nini? Au
tunataka kusema kwamba hatukujua kwamba hali ni mbaya katika shule zetu
na kwamba elimu tunayowapa watoto wetu haifai hata kuwafanya wapagazi
wa watu wa mataifa mengine?
Au ni kwamba tunajua fika kwamba mambo ni mabaya sana katika shule
zetu, kwamba mfumo wa elimu ulikwishakusambaratika kitambo na kwamba
watoto wengi wanahitimu na kutoka shuleni wakiwa mbumbumbu kama
walivyoingia, lakini tunaamini papo hapo kwamba kwa kudra za nguvu
fulani watafanya vizuri.
Najua kuna misemo mingi inayoeleza mtazamo kama huu, kama vile
“kuvuna usichopanda” na kadhalika. Lakini kwangu ni kukosa uaminifu kwa
nafsi zetu, na tunajidanganya sisi wenyewe iwapo tutaamini kwamba
tutazembea kufanya wajibu wetu na bado tufanikiwe.
Hii pia ni aina ya ufisadi, kwa maana ya neno la Kiingereza
“corruption.” Ni ufisadi kuwaona wenzako wanafanya kazi kwa nguvu,
bidii na maarifa wakati wewe umelala ama unalewa na kisha utaraji
kuvuna sawa na wao wanavyovuna.
Aidha ni aina ya ushirikina, kama ambavyo nilikwishakueleza katika
safu hii huko nyuma. Siwezi kushangaa nikiambiwa kwamba wazazi na watoto
wa nchi hii wanaamndamana kwenda Mlingotini kutafuta “fundi’ wakufanya
mambo ili watoto wapate kufaulu katika mitihani.
Kwa jinsi hii haiwezi kunishangaza kwamba tumetambuliwa barani
Afrika kama vinara wa waumini wa uchawi. Ungedhani kwamba taarifa kama
hizi zingewasumbua watawala wetu, na tungesikia ni nini wanapendekeza
tufanya kuondoa picha hii. Kusema kweli ni picha inayolidhalilisha
Taifa letu.
Kama unataka kutishika zaidi, fikiria kwamba watoto wenye ulemavu wa
ngozi, albino, wamo hatarini hapa nchini kila wanakokua kwa sababu ule
ujuha tulioulea kwa miongo kadhaa sasa umekomaa na umerudi kututesa kwa
maumivu makubwa na aibu kubwa kwetu sote. Haipendezi kutembea duniani
ukijulikana kwamba unatoka nchi ya wachinjaji wa albino kwa imani
kwamba viungo vya masikini hawa vinaweza kuleta bahati na mafanikio
yasiyotokana na kazi ya mhusika.
Sasa najiuliza, ni watoto wangapi mazuzu ambao nao wana wazazi wao
mazuzu vivyo hivyo, ambao wanaweza kuwaambia wazazi wao wawafanyie
mpango wapate viungo vya albino ili waweze kufaulu katika mtihani ujao?
Labda viungo vya albino wanaosoma nao katika darasa moja au shule
moja, au shule ya jirani? Nasema tutafakari.
Nchi ikiishakujiachia ikatawaliwa na ushirikina wa aina mbalimbali,
(na washirikina wengi hawajijui kuwa ni washiriki na kwa sababu ushiriki
na wako ndiyo imani ya mwenzio) inakuwa imepotea na hakuna njia yoyote
kwa nchi kama hiyo kuendelea.
Anayebisha na anionyeshe nchi moja tu ambayo watu wake walio wengi
ni washirikina wasiotaka kujua (ila kuamini tu) na ambayo imepiga hatua
za maendeleo endelevu, hata kama inazo rasilimali kubwa.
Ushirikina hauhitaji kuwa na sanamu za mizimu chumba kwako au
kucheza uchi na madogoli (alama za dini za mababu zetu), bali unaweza
pia kupatikana katika kuamini katika mizungu, mambo yasiyokuwa na
mashiko. Kwa maneno mengine ni kushindwa kutafakari kwa kina matatizo
yetu na badala yake tukakimbilia majibu rahisi kwa maswali magumu.
Watoto wamefeli vibaya, na sisi tunasema jibu lake ni nini? Moja,
wachape viboko. Pili, kwa kweli ukiangalia vyema hawajafeli bali
mitihani yao ilisahihishwa vibaya na alama zao hazikupangwa sawa sawa.
Kwa hiyo? Badilisha alama zao ili wengi wapasi. Ushirikina.
source: Raia Mwema : Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment