BAADHI ya raia wa Ethiopia wamekuwa wakiishi kwa kuzingatia msemo
mashuhuri ambao kwa namna fulani umebeba mantiki ya kifalsafa ndani
yake.
Wanasema; “When spider webs unite they can entangle a lion.” Kwamba
utando wa buibui unapounganishwa basi huweza kumnasa hata Simba.”
Buibui ni mdudu mdogo na kimsingi, utando wake si imara ikilinganishwa
na nguvu za mnyama Simba, lakini bado Waethiopia wanasema utando huo
unapotanda vizuri, basi huweza kumnasa huyo Simba. Kwa maana nyingine,
unaweza kusema jambo dogo linaweza kusababisha maafa makubwa.
Ni katika muktadha huo huo, tunaweza kuanza kulitazama Bunge hili la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama chombo kinachoashiria au
kuthibitisha kupungua kwa kiwango cha kuvumiliana miongoni mwa
Watanzania na hata kupungua kwa ustaarabu na staha, miongoni mwa
Watanzania. Kwa mfano, tumemsikia bungeni, Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi akitamka kuwa Baraza la Mawaziri limejaa wapumbavu!
Si kwamba Mbilinyi ambaye aliwahi kuwa mwanamuziki wa bongoflava
alitamka hayo maneno wakati akiimba mashairi au mistari ya bongo flava
la hasha, alizungumza akiwa bungeni katika mjadala wa hotuba ya Bajeti
ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Sugu anajitetea ya kwamba maneno upumbavu si matusi lakini hata kama
si matusi, ni lazima kila mahali kuna hadhi ya lugha au matamshi yake.
Kwa mfano, lugha inayotumika katika vijiwe vya watumiaji wa dawa za
kulevya na mihadarati mingine hata kama si matusi, haiwezi kutumika
ndani ya Bunge.
Lugha inayotumika kwenye vijiwe mbalimbali vya mitaani (hata kama si
lugha za matusi) nazo zina nafasi yake katika maeneo hayo husika.
Lugha ya kuitana wapumbavu, kwa watu walioko katika ngazi ya uongozi
wa kitaifa ni sawa na lugha ya kihuni, na pengine inaakisi kiwango cha
hadhi ya mtamkaji wa maneno hayo.
Kwa viongozi wa kitaifa kuitana au kutambulishana mbele ya umma (tena
kupitia Bunge linalorushwa hewani moja kwa moja nchi nzima), kama ni
wapumbavu (hata kama upumbavu si tusi) ni kuashiria shari. Ni kuashiria
kutoweka kwa ustaarabu kati ya viongozi husika.
Katika mfumo wa demokrasia ambao bila shaka vyama vyote vya siasa
nchini vinautumikia hata kama si kwa dhati, kura za wananchi ndizo, kwa
kawaida, huamua nani aongoze nchi. Na waliopewa mamlaka ya kuongoza
nchi, ni lazima waunde serikali. Na kwa hiyo basi, mfumo wa dekomrasia
kwa wanaouamini kwa dhati katika mfumo huo hawana budi, hasa katika
vyombo vya uwakilishi kama Bunge, kushindanisha hoja zao kwa kuzingatia
nguvu za hoja husika na si nguvu ya misamiati ya kukera wengine,
misamiati au maneno yanayoashiria shari na kimsingi, yanayoweza
kusababisha wadogo wakapuuza kuheshimu wakubwa.
Kwa bahati mbaya, Mbunge Mbilinyi hakuwa tayari kuomba radhi bungeni
na hata kufuta kauli yake kwa kuwa tu, neno pumbavu au mpumbavu lipo
katika biblia.
Kwa kawaida, madhara ya matumizi ya maneno fulani hutegemea sana
mazingira maneno hayo yanapotamkwa na msukumo wa utamkaji wa maneno
husika.
Inawezekana, tunao mawaziri ambao hawafanyi kazi yao vizuri na kwa
kweli nami nakubaliana na hali hii ya kwamba kuna mawaziri ni mzigo tu
kwa nchi, ni kama hawapo na hata ukitathmini utendaji wao wa kazi,
huoni mabadiliko yoyote katika sekta wanazosimamia.
Lakini hata kama kuna viongozi wa namna hii, haikuwa sahihi kwa mbunge
kuwaita wapumbavu, kwa kuzingatia mazingira ya kibunge. Pengine,
kuwaita hivyo inawezekana katika vijiwe vya kuvutia bangi na
kwingineko, lakini kwenye chombo rasmi cha uwakilishi wa umma ni kuvuka
mipaka.
Tutafakari, inawezekana kabisa katika maisha yake Joseph Mbilinyi
amewahi kushuhudia wazazi wake wakiwa wametenda makosa ya hapa na pale,
makubwa au madogo kwa sababu mbalimbali, za msingi au zisizo za msingi.
Je, mbunge huyo atakuwa tayari kuwatamkia wazazi wake kuwa ni
wapumbavu? Je, anaweza kutamka hivyo kuwa wazazi wake au mzazi wake ni
mpumbavu kwa sababu tu neno pumbavu si tusi?
Bila shaka, jibu ni rahisi tu kwamba hawezi kuwatamkia hivyo licha ya
udhaifu fulani ambao anaweza akawa ameubaini. Kwa nini hawezi? Hawezi
kwa sababu neno hilo ingawa si tusi, lakini halibebi ustaarabu kati ya
mwana na wazazi wake.
Tutambue ya kuwa, mawaziri ambao wameitwa wapumbavu ni watu wenye
familia zao na miongoni mwao ni wachapakazi ingawa pia wapo ambao ni
butu katika utendaji kazi.
Lakini si Joseph Mbilinyi pekee, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia
naye alitamka bungeni akimweleza mbunge mwenzake kuwa; yeye (Nkamia)
hazungumzi na mbwa bali anazungumza na mwenye mbwa.
Bahati nzuri, Nkamia alitambua makosa yake katika kutamka maneno hayo
ndani ya ukumbi wa Bunge, akaomba radhi. Inawezekana kwa mfano, kama
mtu fulani akatamka maneno hayo kwenye vijiwe vya kuvuta bangi au
maeneo mengine yasiyo ya kistaarabu, asingelazimika kuomba radhi na
tena kila mmoja katika eneo hilo asingebaini kama ni tatizo kutamka
hivyo.Sasa kwa kuzingatia msemo wa Waethiopia, utando wa buibui unaweza
kumnasa Simba na kwa hiyo, kauli zenu hizi wabunge wetu zinaweza
kuashiria machungu mbele ya safari zenu za kisiasa na hasa katika
majukwaa ya kuomba kura siku zijazo.
Tunaweza kutamka maneno ambayo yanaweza kufurahisha baadhi ya
mashabiki wetu lakini gharama zake zinaweza kuwa kubwa zaidi ya furaha
hiyo ya muda mfupi kutoka kwa mashabiki.
Tusiitane wapumbavu wala mbwa bungeni, jiulizeni, watoto wenu wanaweza kujifunza nini kutokana na kauli zenu hizo?
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
source: Raia Mwema: Godfrey Dilunga
Chukulia suala la wagombea ubunge wa CCM kutoroka midahalo wakati wa kampeni ule mwaka 2010. Sina sababu ya kuminya maneno: huu ulikuwa ni upumbavu. Wakati huu wanatamba Bungeni, lakini mimi sijasahau upumbavu waliofanya.
ReplyDeleteHivi kweli, tunawafundisha nini watoto wetu, endapo hatujihusishi na mijadala na midahalo, ambayo ni njia moja ya kuelimishana? Ilichofanya CCM ni kuwafundisha watoto wetu upumbavu.