Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Akizindua rasmi Tawi la
Chuo cha Mwalim Nyerere lililopo Bububu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
ameitaka Bodi na Menejiment ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
kuendelea na jitihada za kukiimarisha Chuo hicho ili kutoa Elimu bora
yenye viwango vya kitaifa na kimataifa.
Rais Shein ameyasema hayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Tawi la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalim Nyerere lililipo Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Rais Shein ameyasema hayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa Tawi la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalim Nyerere lililipo Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Amesema njia nzuri ya kupelekea kiwango cha ubora wa elimu chuoni hapo ni kuhakikisha Wanafunzi wanaojiunga wanakuwa na sifa zinazotakiwa pamoja na kupata Walimu wenye ujuzi.
Ameongeza kuwa ubora wa Elimu unaotolewa Chuoni hapo utawafanya Wahitimu kukabiliana na ushindani wa Soko la Ajira jambo ambalo litaweka heshima ya Chuo hicho.
Aidha Dkt. Shein ameitaka Bodi ya Chuo kuandaa mikakati ya kuliwezesha Tawi la Chuo hicho kuwa Chuo kamili kinachojitegemea badala ya kubakia kuwa Tawi.
Amesema Utaratibu wa aina hiyo ndio unaofuatwa Duniani kote ambapo Matawi ya Vyuo vya Elimu ya Juu huwa yanaendelezwa na kuwa Vyuo kamili vinavyojitegemea.
Dkt. Shein amewataka Wanafunzi wa Chuo hicho kuitumia fursa waliyoipata ya kuwepo Chuoni hapo kwa kujikita zaidi katika masomo bila ya kujiingiza katika mambo yanayowapelekea katika malumbano.
Amewasihi Wanafunzi wa Chuo hicho kuendeleza maadili mema sambamba na kufuata Mila na silka zinazoendana na utamaduni wa kitanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere Dkt. John Magotti alielezea mafanikio ya Chuo hicho kuwa ni pamoja na kukamilika kwa Jengo hilo ambalo lina uwezo wa kuwahudumuia wanafunzi katika ngazi za Cheti, Stashahada na Shahada.
Aidha alielezea changamoto zinazokikabili Chuo hicho kuwa ni pamoja na upungufu wa Mabweni ya kulalia Wanafunzi na Idadi ndogo ya Wanafunzi wanaojiunga na Chuo hicho.
Amewataka Wanafunzi wenye sifa kujiunga na Chuo hicho na kuwataka Wazanzibari wenye ujunzi kuomba nafasi za ajira ikiwemo ufundishaji ili kukifanya Chuo hicho kuwa na sura ya kitaifa.
Awali akimkaribisha Dkt. Shein Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Dkt. Salim Ahmed Salim amewataka Vijana kuithamini Elimu wanayoipata Chuoni hapo ili iweze kuwa Mkombozi wa maisha yao.
Jengo la Tawi la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere lililopo Bububu limegharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 3.6 ambazo zimegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kwa sasa Tawi hilo ni kwa ajili ya Wanafunzi wa ngazi ya Cheti.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
Mkuu wa Chuo cha Mwalim Nyerere
John Magotti akimuonyesha moja ya madarasa ya Chuo hicho, Rais wa
Zanzibar Dr. Ali Muhamed Shein mara baada ya uzinduzi huo.
Mwalimu pekee wa I .T. Chuoni
hapo Julius akimfahamisha Rais wa wa Zanzibar Dr. Ali Muhamed Shein
jinsi anavyokabiliana na majukumu yake ya kila siku Chuoni hapo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Mwalim Nyerere Salim Ahmed Salim akitoa nasaha kwa wanafunzi wa Chuo hicho.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed shein akiwahutubia wanafunzi na
walim, huko Tawi la Chuo cha Mwalim Nyerere Bububu nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar
No comments:
Post a Comment