KATI
ya taarifa kubwa za kimataifa kuhusu Bara la Afrika, zilizotolewa wiki
iliyopita ni ziara ya pili ya Rais Baraka Hussein Obama wa Marekani
katika nchi za Tanzania, Rwanda, Afrika Kusini na labda Nigeria
ikitegemea hali ya usalama nchini humo.
Ziara hii, inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwezi ujao wa Juni, ni
ya pili kwa Afrika kwa Obama akiwa Rais ikitanguliwa na ile aliyoifanya
Julai mwaka 2009, Ghana.
Obama
mtoto, ambaye marehemu baba yake, naye pia anaitwa Baraka Hussein
Obama (18 Juni 1936 - 24 Novemba1982) ni Mwafrika mzaliwa wa Kenya
akitokea eneo la Rachuonyo kandokando ya Ziwa Victoria, alikulia kijiji
cha Nyang’oma Kogelo eneo la Nyanza nchini Kenya.
Hapa Tanzania wakati tukisubiri ziara ya kiongozi wa taifa kubwa
kiuchumi duniani, kuna maswali kadhaa tunapaswa kujiuliza. Kwa nini
anakuja? Au, anakuja kufanya nini? Kwa nini sasa?
Labda, kabla ya majibu ya maswali haya, tukumbushane kuwa marais wa
Marekani wa karibuni, wote wametembelea Tanzania. Bill Clinton amekuja
mara kadhaa ikiwa ni pamoja na mwaka 1998 wakati Rais George Bush
alitutembelea mwaka 2008.
Ni ishara njema kutembelewa na wageni hususan pale wanapokutembelea
ukiwa salama, hakuna vita wala ugomvi. Wanafika kukusalimu,
kubadilishana mawazo na kukupa ushauri wa hapa na pale.
Kwa msingi huu, ugeni huu si kama ule wa wanajeshi wa Tanzania
waliokwenda Mashariki wa Congo hivi karibuni kusimamia amani. Lakini,
nini hasa kinamleta Obama (51) Tanzania na Afrika?
Hali ya usalama Afrika
Jambo la kwanza tunalopaswa kukubaliana ni kwamba maslahi ya
kiusalama, kiuchumi na kijamii yametapakaa duniani kote. Wamarekani na
kampuni zao wapo kila kona ya dunia wakifanyabiashara na shughuli
mbalimbali za kijamii na hivyo wanahitaji ulinzi.
Bila shaka, Afrika pia wamo na tunawaona na ndiyo maana kuna chombo
kiitwacho USARAF (United States Africa Army) na AFRICOM (United States
Africa Command). Kimsingi, kwa mujibu wa Marekani, lengo la vyombo
hivi, pamoja na kusimamia maslahi ya Marekani barani Afrika, pia ni
kusisimua na kuhamasisha mabadiliko chanya katika Bara la Afrika kwa
kuzima vikundi vyenye misimamo mikali (violent extremist organisations) na hivyo kutengeneza mazingira salama kwa biashara na ukuaji wa demokrasia.
Bila shaka, katika hili nchi zote zilizotajwa kuwa Obama
atazitembelea zina nafasi kubwa ya kuyasimamia haya. Tanzania
inafahamika, tangu miaka ya uhuru na hadi sasa, kama kinara wa masuala
ya kuimarisha usalama barani Afrika. Uthibitisho wa karibuni kabisa ni
jitihada za kurudisha amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),
Madagascar na hata Zimbabwe.
Rwanda, kwa upande wake inatajwa kama kiungo muhimu cha amani katika
eneo tete la Mashariki ya DRC. Inawezekana pia ziara hii ya Obama ni
kuzitia moyo Tanzania na Afrika Kusini ambazo zimewatoa askari na
maofisa wake kwenda DRC kuimarisha amani. Hii pia inaweza kuikumbusha
Rwanda kujitahidi kuondoa hisia katika anga za kimataifa kuwa nchi hiyo
inahusika na vita hiyo isiyoisha Mashariki mwa DRC na kusini mwa
Rwanda.
Lakini Rwanda ina nafasi nyingine zaidi. Pamoja na kutokuwa na
bandari na historia ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, Rwanda ni miongoni
mwa nchi za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi ya wastani wa
asilimia 7 kwa mujibu wa Benki Kuu ya nchi hiyo, kasi kubwa kuliko ile
ya asilimia 4.8 ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa mujibu wa
tathmini ya Benki ya Dunia (Africa’s Pulse, 2012).
Kwa sababu hii, Rwanda imekuwa ikipigiwa mfano na wakubwa ikiwemo
Marekani si katika uchumi tu, bali hata katika kusimamia masuala
mtambuka ya kimataifa kama usawa wa kijinsia. Na ni ukweli ulio wazi
kwamba, nchi hizi tatu (Tanzania, Rwanda na Afrika Kusini) ni miongoni
mwa nchi zilizopiga hatua katika kuongeza idadi ya wanawake katika
vyombo muhimu vya uamuzi, zote zimepita asilimia 30 iliyowekwa na Umoja
wa Mataifa (UN).
Kwa hiyo, itakuwa sahihi kusema kuwa kiongozi yeyote mkubwa duniani,
kama Obama, angependa kuitembelea Rwanda na hizi nyingine ili
kuwaamsha wengine kuiiga.
Nigeria na Afrika Kusini ni mataifa makubwa kiuchumi kwa Afrika. Kwa
taifa kubwa kama Marekani, hizi ni nchi ambazo inabidi ikae nazo meza
moja na kuzungumza namna bora ya kufanya biashara hususan wakati huu
ambao taifa jingine kubwa kama China linawekeza kwa kasi Afrika. Na
hili linaweza kutupa hoja ya nyingine ya ziara ya Rais wa China Africa,
mapema mwaka huu.
Kufuta nyayo za Rais wa China
Itakumbukwa kuwa ni Rais wa China Xi Jinping, aliyechaguliwa Machi
14, mwaka huu alifanya ziara ya siku sita Afrika kuanzia Machi 24 mwaka
huu.
Ziara hii ilimwezesha kutembelea nchi za Tanzania, DRC na Afrika
Kusini. Kati ya hizi, tunaambiwa kuwa Obama atazuru Tanzania na Afrika
Kusini.
Katika ziara hii, Jinping alitia saini mikataba mikubwa na nchi hizi
ikiwemo aliyosaini na Tanzania iliyolenga kuimarisha miundombinu kama
ujenzi wa bandari kubwa na ya kisasa Bagamoyo na uimarishaji wa reli.
Kwa ufupi, akiwa Tanzania alisaini mikataba 17 ukiwamo ule wa miaka
mitatu wa ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi wenye thamani Sh trilioni
1.8 (Dola za Marekani milioni 800).
Itakumbukwa pia kuwa China ni taifa la pili kwa ukubwa kiuchumi
duniani, nyuma ya Marekani. Bila shaka, hata ningekuwa mimi, nisingekaa
kimya nikikodolea macho hali hii bila nami kuchukua hatua.
Nadhani, Obama atapenda pia kufuta zile nyayo za Jinping ambazo
baadhi ya wadau wanaamini zimekwishajikita na itabidi kutumia nguvu za
ziada kuzifuta kwa sababu zina historia ndefu tangu enzi za Mwalimu
Nyerere. Kwa vyovyote vile, nchi za kiafrika, ikiwemo Tanzania,
tuwaache wakitukimbilia ili ule msemo, Mgeni Njoo, Mwenyeji Apone,
utimie.
Kenya na ICC
Tunafamu kuwa viongozi wakuu wa majirani zetu Kenya, Rais Uhuru
Kenyatta na Makamu wake William Rutto wanakabiliwa na tuhuma za kupanga
na kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi nchini mwao mwaka 2008.
Viongozi hawa wawili, pamoja na tuhuma hizo, walipewa ridhaa na
kuongoza Kenya na wananchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia tena chini
ya Katiba Mpya inayopigiwa mfano na wadau wengi ndani na nje ya Afrika.
Hali hii, inaelekea haijawahi kuwafurahisha wakubwa hata kidogo.
Kuna baadhi yao walitishia, kabla ya uchaguzi, kuwa wangesitisha
ushirikiano na Kenya iwapo wawili hao wangechaguliwa kuiongoza nchi
hiyo yenye uchumi mkubwa katika Afrika Mashariki.
Kwamba Kenya haimo katika ratiba ya ziara ya Obama kwa Afrika
halipaswi kuwa jambo geni kwa wanaofuatilia masuala ya Marekani na
Kenya. Obama, pamoja na kuwa baba yake mzazi alitokea nchini humo,
hajawahi kuitembelea nchi hiyo akiwa Rais ukiondoa ile ziara yake ya
mwaka 2006 akijiandaa kugombea urais nchini Marekani.
Kama anavyowahi kusema Kwaku Osei, mchambuzi wa masuala ya siasa na
mzaliwa wa Ghana, suala la Kenya na ICC ni kati ya mambo yanayoiumiza
kichwa Marekani na ICC, Mahakama ambayo inalalamikiwa na baadhi ya
waafrika kuwa inaliandama bara hili.
Kwa hiyo, pamoja na sababu nyingine nyingi za Obama kutarajiwa
kutembelea nchi mbili (Tanzania na Rwanda) kati tano zinaunda Jumuiya
ya Afrika Mashariki (Kenya ikiwemo), tunaweza kutaja sababu nyingine ni
kuwatia wivu ndugu zetu wa Kenya. Ni kama kuwaambia, ‘pamoja na kuwa
nina damu ya Kenya, kwa sasa sitafika huko hadi haya mambo ya ICC
yaishe.’
Lakini wakati Obama akisema haya, tunaweza kusema angependa kujenga
uhusiano mzuri na majirani wa Kenya hiyo hiyo ambao inaelekea wanaiunga
mkono Kenya katika jitihada zake za kuanza ukurasa mpya wa kuijenga
nchi yao na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hili linathibitishwa na ushiriki wa viongozi wa nchi wanachama
katika sherehe za kuwaapisha Kenyatta na Rutto pale katika uwanja wa
Kasarani jijini Nairobi siku ile ya Aprili 9, mwaka huu.
Mchakato wa Katiba Tanzania
Ukweli kwamba Watanzania wapo katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya
itakayotoa mustakabali wa mambo kadhaa ya nchi yao, linaweza kumvutia
kiongozi mkubwa kama yeye.
Kwa namna mchakato unavyoendelea, ni imani ya wengi kuwa mchakato
huu wa kuandika Katiba Mpya utakwisha salama. Labda kinachoweza
kumvutia Obama ni hatma ya Muungano, hususan baada ya maoni
yanayokinzana kutoka kwa baadhi ya wadau – mengine yakiashiria
uimarishwe na mengine, kwa kweli yakiashiria kuuvunja nguvu au kuubomoa
kabisa.
Ukweli ni kuwa maoni yanayoashiria kuubomoa hayakubaliki na wengi
wetu kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kiusalama katika
Pwani ya Bahari ya Hindi. Na bila shaka hili halikubaliki na hata
marafiki zetu na wadau wengine ikiwemo Marekani.
Kwa kuwa taarifa zinaeleza anaweza kuzuru nchini mwishoni mwa Juni,
muda ambao tunaamini rasimu ya Katiba yetu (mpya) itakuwa imetolewa na
Tume ya Jaji warioba, basi tutumaini kuwa wakati huo suala hili la
Muungano litakuwa limefikia pazuri. Tusubiri.
Utamaduni wa kupokezana vijiti
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na mgeni wake, Barack Obama wote
wapo katika vipindi vya pili na vya mwisho vya uongozi katika nchi zao.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, unaweza kujiuliza swali je, nini
watafanya baada ya kustaafu? Inawezekana, nalo hili wanaweza kuulizana
(JK na Obama) wakikutana hapo mwishoni mwa mwezi ujao.
Lakini, katika hili kuna kubwa zaidi. Umuhimu wa kupeana vijiti
katika uongozi. Nchi zote anazotarajia kutembelea Obama, isipokuwa
Rwanda, zimekuwa na utaratibu (uliokwishawahi kutumika kwa miongo
kadhaa) wa kikatiba wa ukomo wa madaraka ya urais na umekuwa
ukiheshimiwa.
Tangu enzi za Mwalimu Nyerere Tanzania tumeheshimiwa kukabidhiana
madaraka kwa amani. Mwalimu alimkabidhi Mzee Ali Hassan Mwinyi mwaka
1985 naye kukabidhi kwa Benjamin Mkapa (1995) na baadae kwa JK mwaka
2005.
Hili pia linatokea Marekani, Afrika Kusini na Nigeria. Unaweza
kusema, Obama atataka kuwaambia wengine, ikiwezekana majirani zetu,
kuwa hili linawezekana na wafanye hivyo.
Kwa kumalizia, kwa vyovyote vile, kama ilivyokuwa kwa ziara ya Rais
wa China, ni matarajio ya wengi kuwa ziara hii italeta tija kwa pande
zote mbili.
source: raia mwema: Simon Mwalwimle
No comments:
Post a Comment