MAJUZI
hapa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha,
alitoa kauli yenye hekima na busara nyingi juu ya umuhimu wa viongozi
kuchunga kauli zao.
Nahodha alialikwa kwenye kusanyiko la viongozi wa kidini
lilioandaliwa na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kujadili, pamoja na
mambo mengine, juu ya hali inayojitokeza sasa kwenye jamii yetu. Hali
ya misuguano ya kidini.
Waziri Nahodha alisema kwamba yanayotamkwa na viongozi, hayaishii
pale yanaposemwa tu. Hutafsiriwa kwa maana iliyokusudiwa au hata ile
ambayo haikukusudiwa. Hivyo, umuhimu wa kuchunga kauli. Na hakika, hapa
duniani kuna mifano ya viongozi, ambao kupitia kauli zao, ama
zimewajenga au zimewabomoa kisiasa.
Siku zote, historia ni mwalimu mzuri. Ili tuweze kutafsiri na
kuyaelewa yanayotokea sasa na kuyaelewa yatakayotokea kesho, tuna
lazima ya kuangalia na kutafsiri kilichotokea jana. Na hii ni moja ya
maana ya kusoma na kutafsiri alama za nyakati.
Katika hili la kauli, hapa kwetu Tanzania kuna kisa cha Uchaguzi
Mkuu wa Rais na Wabunge wa Mwaka 1985. Mzee John Malecela alikuwa bado
na ujana wa kisiasa. John Malecela, katika uchaguzi ule wa mwaka 1985,
ndiye alikuwa waziri pekee katika baraza la mawaziri lililovunjwa
ambaye hakurudi bungeni. Alikataliwa na wapiga kura wake. Hakurudi
bungeni. Kwanini?
Kwa mujibu wa maandiko ya wasomi watafiti, ma-Bwana Mvungi na Amos
Mhina (Searching for a people M. P?), anguko la John Malecela lilitokana
na kukosa uzoefu na mahusiano mazuri na wapiga kura katika ngazi za
chini. Huyu alikuwa John Malecela ambaye ndugu yake Job Lusinde ndiye
alikuwa mbunge aliyemtangulia jimbo la Dodoma Mjini. Malecela alibwagwa
na Injinia asiye na uzoefu wa kisiasa, aliitwa Mazengo Yohana.
Hata hivyo, katika hili la mahusiano na watu, watafiti wale katika
maandiko yao kwenye kitabu kiitwacho: Tanzania, Democracy In Transition,
kwa mtazamo wangu, wameshindwa kubainisha sababu nyingine iliyochangia
kuharakisha anguko la John Malecela wa wakati huo. Hili linahusiana
pia na mahusiano kati ya John Malecela wa wakati huo na wapiga kura
wake.
Na hapa inahusu kauli ya John Malecela wakati huo akiwa Waziri wa
Mawasiliano na Uchukuzi. Katikati ya kilio cha watumiaji wa njia ya reli
ya kati (TRC) juu ya huduma mbaya za Shirika la Reli miaka ile ya
1980, Mzee huyu alipata kukaririwa akitamka kuwa hakukuwa na tatizo la
huduma mbaya, na kwamba wenye kufikiri hivyo, “they can go to hell!.”
Kwamba wanaoliona tatizo, wanaweza kwenda kuzimu.
Katika sanaa ya mawasiliano, tunaamini kuwa sentesi moja inayotamkwa
na mwanasiasa, yaweza kumjenga au kumbomoa kabisa kisiasa. Kwa John
Malecela, kauli yake ile ataishi asiisahau, maana, pamoja na kuwa
tulikuwa katika mfumo wa chama kimoja, redio moja ya taifa na magazeti
matatu, bado wananchi waliweza kufikisha shutuma zao kwa Malecela juu
ya kauli yake ile.
Na kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliofuata wa mwaka 1985, ilikuwa
ni kwa wapiga kura wa Dodoma Mjini kushindilia msumari wa mwisho
kwenye jeneza la kisiasa la John Malecela. Walifanya hivyo kwa niaba ya
Watanzania wengine, na hususan watumiaji wa reli ya kati. Malecela
aliangushwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Hakupata ubunge
na hivyo hakuweza kuwa Waziri.
Na hakika, Malecela alijifunza, na hata aliporudi tena kwenye ulingo
wa kisiasa, John Malecela, hata hii leo, amekuwa ni makini sana katika
kuchagua maneno anapowasiliana na umma.
Nahofia, kwa hali tunayokwenda nayo sasa, kuwa yaliyomkuta Mzee wetu
John Malecela miaka zaidi ya 20 iliyopita, huenda yatakuja kuwafika
baadhi ya wanasiasa wetu wa sasa, na wengine ni mawaziri wenye dhamana.
Yatakuja pia kuwafika baadhi ya wabunge, ambao, wakiwa bungeni,
kauli zao zisizo makini, wanajisahau kuwa kuna wengi wenye
kuwasikiliza.
Kwanini? Wapiga kura wa leo ni wenye uelewa zaidi kuliko wale wa
1985. Wapiga kura wa leo si tu wanakumbuka na kufuatilia matendo ya
wabunge wao, na hususan ahadi walizotoa ambazo hazikutimizwa, bali
wanakumbuka, na wataendelea kuzikumbuka pia, baadhi ya kauli za kejeli
kwa wapiga kura kutoka kwa baadhi ya wabunge na mawaziri.
Na mara nyingi kuna kosa kubwa linalofanywa na wanaotafiti hali ya
kisiasa, na hasa kuelekea uchaguzi mkuu. Wengi wa watafiti wanalenga
zaidi katika kuchambua mienendo ya wagombea na kampeni zao. Watafiti
hawa wamesahau kutafiti mienendo ya wapiga kura ambao kimsingi ndio
wenye uchaguzi na maamuzi ya nani awe kiongozi wao.
Moja ya hulka za mpiga kura, ni kujaribu kukumbuka kauli za nyuma za
wagombea. Hivyo, kama alivyobainisha Waziri Vuai Shamsi Nahodha kwamba
upo umuhimu mkubwa kwa viongozi kuwa makini kwenye kauli zao!
Nahitimisha.
source: Raia Mwema: Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment