WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 16, 2013

Tume ya Kidato cha IV yatoa mapendekezo 130

Profesa Sifuni Mchome 
Na Fredy Azzah,

Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012, imetoa mapendekezo 130, mojawapo ikitaka kupitiwa upya kwa mitalaa ya elimu nchini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema likitaka mitalaa ya shule za msingi hadi vyuo vya ualimu itazamwe upya.

Tume hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari 23, mwaka huu kuchunguza chanzo cha asilimia 65.5 ya wanafunzi kupata daraja la sifuri kwenye mtihani wa mwaka 2012.

Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu baada ya Tume kumaliza kazi yake Juni 15 mwaka huu.

“Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea,” alisema Profesa Mchome.

Alisema kwa kawaida mtalaa unabadilishwa baada ya kumaliza mzunguko wake mmoja, hivyo tume hiyo imependekeza kupitiwa upya kwa mitalaa yote ambayo imemaliza mzunguko. Mzunguko huu ni miaka saba kwa elimu ya msingi, minne kwa sekondari na miwili kwa kidato cha tano na sita.

“Mtalaa wa sekondari unaweza kupitiwa upya baada ya miaka minne tangu kuanza kutumika kwake, huu wa Sekondari wa ‘based competence’ (kuangalia ubora) ulianza kutumika 2006, mpaka sasa tayari umemaliza mzunguko wake na haya matokeo yametokana na mtalaa huu.

Tume imependekeza mitalaa yote itazamwe upya kuanzia ile ya shule za msingi mpaka vyuo vya ualimu,” alisema.

Kuhusu vitabu, Tume imependekeza kuangaliwa kwa njia rahisi ya kutumia teknolojia kuhakikisha vinapatikana badala ya kusubiri mpaka vichapishwe na kisha kupelekwa kwa wanafunzi.

“Unaweza ukaongea na makampuni ya simu kuwa waweke vitabu kwenye system (mfumo) yao na wakaanza mashindano kuwa mwanafunzi atakayesoma sana atapata zawadi,” alisema na kuongeza.

“Unaweza pia kuongea na kampuni ya magazeti kama Mwananchi ukawaambia watoe ukurasa wachapishe kitabu fulani kwa mwezi mzima na shule ziambiwe zinunue nakala moja ambayo kwa mwezi itakuwa Sh30,000 kwa kila shule na tatizo la vitabu litakwisha.”
Pendekezo jingine alisema ni kuangaliwa upya kwa sheria mbalimbali za elimu jinsi zilivyo na utekelezwaji wake pamoja na kuhakikisha madaraka yanapelekwa kwenye ngazi za Serikali za Mitaa.

Kufutwa kwa Matokeo

Akizungumzia kufutwa kwa matokeo hayo, Profesa Mchome alisema katika uchunguzi wake, tume hiyo haikuwa na shida yoyote juu ya utungaji na usahihishaji wa mitihani.

“Ndiyo maana tukapendekeza kupangwa upya kwa madaraja, kitakachofanyika ni kubadilishwa tu kwa kanuni iliyotumika mwaka jana na kutumia ile ya miaka ya nyuma,” alisema.

Alisema kwa miaka ya nyuma upangaji wa madaraja ulikuwa unazingatia matokeo ya mitihani jinsi yalivyo na kisha kuyafananisha na miaka ya nyuma.

“Ukiona kuwa mwaka uliopita somo fulani matokeo yake yalikuwa hivi, basi unaangalia na ufaulu wa mwaka huu kisha mnaamua kuwa daraja A lianzie alama fulani, hicho ndiyo kilichopendekezwa.”

“Kilichofanyika mwaka jana, masomo yote yaliwekwa kwenye daraja fulani bila kuzingatia jinsi ufaulu ulivyokuwa. Kwa hiyo sisi tukaona kwa kuwa wanafunzi hawa wamesoma kwenye mazingira sawa na yale ya miaka ya nyuma, hakuna sababu ya kuwabadilishia kanuni.”

source: mwanachi

  • MiNasemaHivi  
    Mapendekezo 130!!!! Are you kidding me? Mapendekezo ni matatu tu. Serikali itimize wajibu wake. Mbili walimu wafanye kazi kwa wito. Kwani uongo jamani? . Tatu wanafunzi waache 'ujinga'. Hayo mengine ni kujaza makabati tu. I'm serious. 

  • Henry Kifwambele  
    Kama mapendekezo ya kamati hiyo iliyoundwa ndio haina mashiko hivo, hakukuwa na sababu ya kuweza kuunda kamati yenye mapendekezo finyu hivo, vitab na mitandao ya simu wapi na wapi? au kuchapisha kitabu kwenye gazeti? Hawa watu wameangalia familia masikini ya mtanzania ambae anaishi kwa shilling 200 kwa siku ataweza kununua gazeti kweli? au mtu atakuwa na simu na kanuni za shule na sharia zinazuia mtu kutumia simu? Kama maabara hamna, leo hii ufaulu huo utatoka wapi? Hebu watafakari vizuri kabla hawajatuletea hayo madudu.

  • BENSON KASALILE  

    Ningeshauri pia Tume itoe mapendekezo yake juu ya lugha ya kutumika kufundishia, na mikakati ya kuboresha ufundishaji au matumizi ya lugha hiyo, kwa wote, Waalimu na Wanafunzi, kwani lugha imekuwa kikwazo kikubwa cha kufanikisha uelewa wa Wanafunzi, kiasi cha kuwafanya washindwe hata kujieleza kiufasaha. Pamoja na hayo, niipongeze Tume hii, kwani kwa kiasi fulani, kinachofanyika kinaonekana, na siyo kama matokeo ya Tume nyingine yanayoishia makabatini.

  • Cyril Njau
    Kupanga upya madaraja ya kufaulu kweli haitakuwa na maslahi yeyote kwa umma, la msingi wale ambao walionekana kufanya vizuri kidogo basi wapate nafasi ya kwenda kidato cha tano, kupoteza fedha ya serikali kwa kazi ilikwisha fanyika ni danganya toto. Je kushusha kiwango cha kufaulu huoni ndiyo kuanguka kiwango cha elimu? Tuwe na viwango vya elimu yetu au tutatengeneza taifa la watu mbumbu. Tatizo siyo wanafunzi tu bali hata mazingira ya walimu ya kufanyia kazi ndiyo kikwazo kikubwa. tuboreshe vitendea kazi kwa shule zote, tuinue hali ya walimu na wazazi wapewe changamoto kuhimiza watoto wao kusoma kwa bidii, na hapa shida inakwisha.

  • Pashal Ngeleja  
     
    Nanyi tume kuweni wakweli na muache siasa katika mambo ya Kitaifa........mapendekezo 130 nani atayafanyia kazi? Ni vizuri mkachambua mapendekezo muhimu matano (5 strong recommendations) ndo yakaleta manufaa Tanzania.Watanzania tunataka mabadiliko katika elimu

  • paul ndomba  
    kwa mfugaji wa ng'ombe ili ng'ombe wake atoe maziwa ya kutosha ni lazima amuwezeshe mchungaji wa ng'ombe hao kwa namna yoyote ili kumfanya atumie uwezo wake wote wa kuchunga ng'ombe hao bila hivyo, atawapeleka sehemu ambayo haina majani, saa ya kunywa maji hatawapeleka kisimani, unadhani nini kitatokea kama si kuwa fanya ng'ombe hao wakonde, sasa je! utarajie kupata maziwa hapo?, hayo mapendekezo kipao mbele ni kipi maana kuyatekeleza yote ni kama muda utakuwa umeshapita sana na taifa litaendelea kuangamia.
    hapa walimu wakipewa kipaao mbele watoto watafaulu tu hata kwa kufundishiwa chini ya kimvuli cha mwarobaini.
     

    chukueni hatua, tupunguze muda wa kuongea km watasema walimu ni wengi hakuta kuwa na pesa nyigi kuwaongezea mishara basi katiba mpya itaje viwango sawa kwa waajiriwa wote wa serikali kwa kuangalia viwango vyao vya elimu pesa zitatosha tu ili watofautiane kwenye maposho ,kuliko ilivyo sasa wote ni graduates lakini mwl aliyepangwa kufundisha shule ya ufundi 533,000/=, aliyepata kazi TRA 3,5000,000, alipata tanroad naye zaidi ya 2,000,000 hujazungumzia maposho. unadhani nini kitatokea kama si kuwafanya wengine wasihamasike kwa kazi zao.

  • Richard Kilonzo
    Watanzania tunataka tutajiwe hayo mapendekezo 130 acheni kuandikia mate na wino upo. Mikataba ya uwekezaji siri na mapendekezo ya elimu ya watoto wetu pia siri. Wekeni mambo yanayohusu watoto wetu hadharani msifanye mchezo na warithi wetu. Hayo mengine ficheni wakiingia wakorofi yatafichuka tu na hiyo haituhusu sisi ambao hatujui Siasa tunajua kupiga kura tu kwa mtu anayekufaa.

  • RushaRoho
    Kweli hapa Tanzania kuna vichekesho, kama mzunguko wa mitaala ya sekondari imeisha toka mwaka 2010, na sasa tuko 2013 na wanafunzi wamefanya mtihani kutumia mitaala ilionza 2006, hii inaonyesha wazi kwamba hakuna coordination kati ya wizara, wadau wa kurudia mitaala na NECTA na wadau wengine. Mbatia aliposema hatuna mitaala ya elimu, wabunge wafata bendera kama upepo na waziri wa elimu na naibu wake alyegushi vyeti walimwona kachanyikiwa. Sasa tume ya pinda inarudia yale yale aliyoyasema Mbatia. Masuala ya elimu, maji, umeme, afya, barabara na mengine ya muhimu kwa maendeleo ya nchi, hayahitaji siasa au usanii bali uongozi bora unaojali maslahi ya umma. Tuwe more objective kwenye mambo haya jamani hii ni aibu.

    Hii tume haina jipya. Matatizo ya elimu yanajulika na yapo wazi. Wewe umeona wapi watu waliopata madaraja ya chini form four na six ndio waendao vyuo vya elimu kusomea ualimu na kupelekwa mashuleni ili wafundishe mtoto afaulu? Utasikia watu wakisema mtaani, "yaani hata nafasi ya ualimu au unesi umekosa?.Huu mfumo haufai hata kidogo. Walimu walipwe vizuri na mazingira yao ya kazi yaboreshwe ili wale waliofaulu zaidi wavutiwe kuwa walimu. Sio kupeleka failures kwenda vyuo vya ualimu. Then, textbook jamani. Kuandika notes kumepitwa na wakati. Kila mwanafunzi awe na kitabu cha kila somo na wafundishwe kusoma na kufikiria zaidi badala ya kuandika notes kibao ambazo upelekea kukariri badala ya kuelewa.

    Matatizo yapo debe, ila mapendekezo 130 ya tume ni kiini macho. Ni hayo tu. Ee mungu, tupe viongozi wenye uchungu na maslahi ya mwananchi sio hawa wanaojali matumbo yao wenyewe na familia zao.

No comments:

Post a Comment