WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 2, 2013

Pengo: Viongozi msilewe madaraka

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Askofu Mkuu wa Kanisa  Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, amewataka viongozi wanaopata madaraka wasijisahau na kubweteka kwa kuacha kuwahudumia wananchi kwa kufanya mambo tofauti na yaliyowaweka madarakani.
Aidha, Kardinali Pengo, amesema viongozi hao wakitekeleza majukumu yao kikamilifu kwa wananchi wao watapata nafasi kubwa zaidi ya hizo walizonazo kwa ustawi wa nchi na jamii kwa ujumla.

Aliyasema hayo jana katika ibada maalum ya kumuwekea Wakfu Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Askofu Titus Joseph Mdoe, iliyofanyika katika Kanisa la Msimbazi, jijini Dar es Salaam jana.

“Nawasihi viongozi wanapopata madaraka wasijisahau kutenda yale yanayotakiwa kwa kuwatumikia wananchi, wengi wamekuwa wanyenyekevu wanapoomba nafasi, lakini baada ya kuzipata wamekuwa wakibweteka na kufanya mambo kwa maslahi binafsi, jambo ambalo ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu,”alisema Kardinali Pengo.

Alisema Askofu Mdoe ni zawadi kutoka kwa Papa Mstaafu Benedict (XVI), alipomuomba kumpa msaidizi wake, baada ya kumhamisha Askofu Saltarius Libena, ambaye kwa sasa anaongoza Jimbo la Ifakara mkoani Morogoro na kuwataka waumini na viongozi wengine wa dini kumpa ushirikiano wakati akitekeleza majukumu yake.

Kardinali Pengo alitumia fursa hiyo kugawa majukumu kwa maaskofu wake wasaidizi kwa kusema kuwa Askofu Mdoe atashughulikia masuala ya uchungaji, vijana, litrujia, vyama vya kitume, mawasiliano, afya, katumeni  na majadiliano ya kidini huku Askofu Eusebius Nzigilwa, akipangwa kushughulikia fedha za jimbo, miito, elimu, katekisi na ardhi.

Kardinali Pengo alisema yeye atakuwa akishughulikia masuala ya mapadre, watawa, wawata, utatu mtakatifu na mahakama ya Kanisa.

Akizungumza katika hafla hiyo mgeni rasmi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete, alisema Tanzania na dunia kwa ujumla, inapitia katika changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kiutawala, hivyo ni jukumu la kila mmoja wakiwamo viongozi wa dini kuhimiza moyo wa upendo, busara na hekima. Waziri Mkuu Pinda aliongeza kuwa nchi ina zoezi la mchakato wa maandalizi ya Katiba mpya na kwamba ni jukumu kubwa kuweka nchi katika hali ya amani na utulivu wakati huu wa kuelekea katika chaguzi mbalimbali zitakazoanza mwakani.

“Sisi tukiwa viongozi wa serikali na wa madhehebu ya dini, tunalo jukumu la kuwaweka wananchi na waumini wetu katika imani zao zenye maadili mema na kusisitiza suala la amani na utulivu,” alisema Pinda.

Akizungumza baada ya kusimikwa, Askofu Mdoe alisema atafanya kazi kwa kuwa muwazi na kwa haki kama ilivyo kwa Askofu Pengo ambaye alisema alikuwa mwalimu wake katika Seminari ya Segerea na kuwa kila mara alikuwa akiwasisitizia kuwa na moyo mkuu.

Askofu Mdoe alisema alipopata taarifa kutoka kwa mwakilishi wa Baba Mtakatifu hapa nchini kuwa ameteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alifadhaika, lakini alijipa moyo na kutiwa moyo ndipo alipokubali uteuzi huo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa pamoja na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa.

Kwa upande wa viongozi wa serikali ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi James Mbatia pia alihudhuria.
 
CHANZO: Na Jimmy Mfuru:  NIPASHE

No comments:

Post a Comment