WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 9, 2013

Udhaifu wa uongozi wa Bunge unachangia matendo ya hovyo


YAMEANDIKWA mambo mengi mno kuhusu utovu wa nidhamu wa baadhi ya wabunge ndani ya vikao vya Bunge, hususan lugha ya matusi inayotumika na baadhi ya hawa “waheshimiwa.”

Katika makala ya wiki jana nilijaribu kueleza baadhi ya sababu za hali hii inayowaonyesha baadhi ya wabunge kama wasiostahili kuwa ndani ya jingo lile kwa sababu hawaelewi dhima waliyonayo kwa wananchi waliowachagua na kwa Taifa letu kwa ujumla.

Binafsi nachelea kwamba kadri tunavyokaribia uchaguzi wa miaka miwili ijayo ndivyo hali itakavyozidi kuwa ya hovyo iwapo uongozi wa Bunge hautajinasua kutoka kile ninachokiona kama kutokuwa na mizania katika kufanya uamuzi, kuelekeza, kuasa na kutoa adhabu.

Ili uamuzi wa uongozi huo uheshimike, si tu ndani ya Bunge bali ndani ya jamii kwa ujumla, hakuna budi kuonekana kama wenye mantiki na unaotenda haki kwa wote bila kuegemea upande wowote. Muhimu siyo tu kwamba haki itendeke, bali pia ionekane imetendeka. Katika hili uongozi wa Bunge umeshindwa.

Mantiki ya kutenda haki inataka hivi: Iwapo Hamisi kakamatwa kwa kosa la kuiba kuku, na kosa limethibitika, na Hamisi kapewa adhabu ya kwenda jela kwa siku saba kwa kosa la kuiba kuku inakuwa ni adhabu ya mfano kwa kila aliyena nia ya kuiba kuku, na hakimu ajaye siku za usoni ataongozwa na msingi wa adhabu aliyopata Hamisi.

Inapotokea kwamba wiki chache baada ya adhabu ya Hamisi, Yohane anakamatwa na kosa lile lile (la kuiba kuku) na akahukumiwa kifungo cha miezi mitatu bila maelezo kwa nini adhabu yake imekuwa nzito kuliko ya Hamisi, maswali mengi yataulizwa. Vivyo hivyo iwapo adhabu ya kosa lile lile itakuwa ni ndogo kuliko ile ya awali aliyopewa Hamisi.

Mambo yanakuwa tata zaidi pale ambapo uzito wa makosa unatofautiana, kwa mfano iwapo mmoja kaiba kuku lakini mwingine kaiba ng’ombe, halafu adhabu ya mwizi wa kuku ikawa kubwa kuliko ile ya mwizi wa ng’ombe, au hata pengine mwizi wa ng’ombe wala asifikishwe mahakamani.

Bila maelezo ya ziada kutolewa kuhusu hali kama hiyo, ni lazima kwamba wanajamii watajiuliza maswali mengi. Watasaili sababu za mahakama kutoa adhabu ambazo hazina urari na makosa; watajiuliza juu ya dhamira ya vyombo vya utoaji haki.

Watadodosa uhusiano baina ya Hamisi na hakimu, na uhusiano kati ya Yohane na hakimu; watajiuliza ni nani ni ndugu ya nani, ni nani wa kabila la nani, na ni nani wa madhehebu ya nani. Aidha watajiuliza ni kiasi gani cha mlungula kimelipwa ili kupindisha mkondo wa haki.

Maswali ya aina hii, tunajua, yanaulizwa katika jamii yetu kila shauri linapokwenda mahakamani na halafu zinatolewa hukumu za mizungu. Sasa wanajiuliza juu ya urari na mizania ya wakuu wa Bunge wanapotaka kuelekeza mwenendo wa Bunge.

Kutokana na wanajamii wengi kutoridhishwa na urari huo, sasa nasikia mapendekezo kadhaa yanayotolewa katika muktadha wa maandalizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kwamba Spika wa Bunge asitoke katika chama chochote kwa maelezo kwamba kwa jinsi hiyo hatapendelea chama chochote.

Mimi siamini kwamba hivyo ndivyo tunavyotakiwa kujenga hoja zilizosimama juu ya misingi ya mantiki. Mtu anaposema kwamba Spika asiyekuwa na chama hatapendelea chama chochote, nataka tuamini kwamba ili kupendelea chama chochote unahitaji kuwa na chama, na tunajua bila shaka kwamba hii si kweli.

Zipo sababu nyingi za mtu mwenye madaraka kupendelea upande mmoja katika shauri na si lazima binafsi awe anatokana na kundi analolipendelea. Sababu zinazomfanya mwamuzi kufanya uamuzi wa hovyo ni vingi mno,  tukiacha zile zinazohusiana na uwezo mdogo wa kiufundi au udhaifu katika utambuzi na uchambuzi.

Angalau, katika hali ya sasa, ni rahisi kushuku kwamba uamuzi Fulani umefanyika kwa sababu ya waamuzi kupendelea chama chao; ni sababu iliyobayana. Tutakapokuwa na wakuu wa Bunge wasiokuwa na vyama, halafu wakafanya uamuzi usioeleweka, pamoja na kupendelea chama fulani, tutasema nini? 

Na vyovyote vile, tunajuaje kwamba mtu fulani, kabla hajachaguliwa kama kiongozi wa Bunge, hana chama? Na kutokuwa na chama maana yake ni nini? Kutokuwa na kadi ya chama? Kutoshabikia chama? Kutopendelea falsafa ya chama? Tunajuaje kwamba huyu anayetaka kuwa kiongozi wa Bunge hana ushawishi wa mrengo Fulani wa siasa ambao unakaribiana sana na chama fulani, hata kama hana kadi wala hajaonekana kabeba mabango?

Aidha, katika mazingira yetu, kila mwenye madaraka ni mwamuzi. Iwapo tutasema kila mwamuzi asiwe na chama, itabidi tukubali pia kuwa hata Rais wa Jamuhuri asiwe na chama, achilia mbali kwamba hata refa wa soka asiwe mpenzi wa klabu yoyote. Mantiki inayotumika hapa inaladha ya kukata miti kwa sababu inaficha nyoka.

Hapana, kinachohitajika ndani ya Bunge ni kile kile kinachohitajika ndani ya jamii yetu pana: kutendeana haki, kuheshimiana, kuvumiliana, kusikilizana kupima hoja hata kama zinatolewa na upande usiokuwa wetu, na kuchukua mitazamo ya masafa marefu inayoliangalia Taifa hili miaka angalau mia tano ijayo, mitazamo inayokinzana vijimisimamo hafifu vinavyolenga maslahi binafsi ya vikundi-maslahi vya leo na kesho.

Refa wa soka anayependa kukuza mchezo ataangalia hilo. Rais wa Jamuhuri aliyedhamiria kujenga Taifa kubwa zaidi kuliko tumbo lake na matumbo ya ndugu zake ataliona hilo. Spika wa Bunge aliyedhamiria kujenga asasi hiyo ili itoe mchango wake wa kweli katika maedeleo ya Taifa ataliheshimu hilo, badala ya kujali maslahi ya muda mfupi ya chama ambacho labda hakitakuwapo miaka ishirini ijayo. 

Sote tukiangalia picha kuu, tukiona mbali, tutatendeana haki, na tukitendeana haki hata lugha zetu zitakuwa na murua. La sivyo tutaendelea kuzoza, kama wahuni. 

source: Raia Mwema: Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment