TAALUMA
ya habari inahusiana kwa wanahabari kusema yalo ya ukweli kwa jamii.
Na jambo hili lina changamoto zake katika jamii zetu hizi.
Maana, ukweli una sifa na tabia zake. Ni kwa vile, ukweli nao una
uhai. Ukweli unaishi. Katika kuishi kwake ukweli hupitia hatua tatu;
Kwanza, kukataliwa, kwamba ukweli unapowekwa hadharani mara nyingi
hukataliwa.
Pili; gharama, kwamba ukweli una gharama zake. Kwa anayesema ukweli
awe tayari pia kulipa gharama za kusema ukweli. Na hapa kuna kisa cha
bwana mmoja aliyekuwa na kiu ya kuupata ukweli. Alitembea huku na kule
kuusaka ukweli. Na hamu yake ilikuwa kuupata ukweli mzima.
Siku moja katika pitapita zake, bwana yule akaliona duka limeandikwa nje; “ Hapa tunauza ukweli!|”
Bwana yule akasimama. Akaona dukani kuna bei za ukweli
zilizoandikwa. Kuna bei ya robo kilo ya ukweli. Kulikuwa na bei pia ya
nusu kilo ya ukweli. Lakini, mwenye duka hakuandika bei ya kilo nzima
ya ukweli.
Bwana yule aliyekuwa na kiu ya kuupata ukweli akaulizia bei ya kilo
nzima ya ukweli. Mwenye duka akamwuliza kuthibitisha hitaji lake; “E
bwana ee, unataka kilo nzima ya ukweli?”
“Ndio” Mwenye duka akamwambia aingie ndani dukani. Humo akamnong’oneza; “Bei ya kilo moja ya ukweli ni uhai wako!”
Basi, bwana yule mwenye kiu ya ukweli alitimua mbio na kuacha vumbi nyuma. Ndio, hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli.
Tatu; ukweli udhihiri, kwamba, hata baada ya kukataliwa, kuwa na
gharama, lakini, hatimaye, siku zote, ukweli udhihiri. Yumkini ukweli
ukachelewa kufika, lakini, siku zote hufika. Na uhalali wake huanzia
pale ulipoanza kukataliwa.
Kazi ya uanahabari inatutaka pia kuwa tayari kulipa gharama za
kusema ukweli. Leo ni ukweli, kuwa baadhi ya wanahabari wanatumika
zaidi kisiasa badala ya kuwatumikia watu.
Leo utamkuta mwanasiasa anaongozana kwenye mkutano na wanahabari
wake. Imekuwa kawaida siku hizi kwenye mkutano kusikia wanahabari
wakitambulishwa rasmi kwa majina na vyombo vyao wanakotoka.
Binafsi nimekulia katika nchi hii. Hakika, mambo hayo hayakuwa
yakifanyika huko nyuma. Maana, mwanahabari ni kazi yake kuwa kwenye
mikusanyiko na kufanya kazi yake ya uanahabari. Hana haja ya kualikwa
au kutambulishwa na mwanasiasa. Isitoshe, jambo hilo la kutambulishwa
laweza kumuweka katika mazingira hatarishi katika kazi yake.
Wanahabari tunaojitahidi kusema ukweli tunakabiliwa na changamoto
nyingi. Binafsi, leo naweza kukutana na watu wa upande mmoja wa kisiasa
na nikaambiwa kuwa niko upande mwingine. Na nikikutana na wa upande
mwingine naambiwa niko na wa upande mwingine.
Kuna wanaodhani kuwa haiwezekani kwa mwanahabari kuwa kwenye upande
wa umma. Hivyo basi, kuwa kwenye upande wenye kulinda maslahi ya nchi
na umma kwa ujumla. Na tunaojitahidi kuwa kwenye kundi hili tumo pia
kwenye hatari kubwa kwa watu wenye kutanguliza fikra binafsi na za
kimakundi badala ya za kitaifa, hivyo basi, kwa wasiotanguliza yalo na
manufaa kwa umma.
Ni ukweli, kuna wenye kuona wanavyopenda kuona. Kuna wenye kusikia
wanavyopenda kusikia. Kuna wakati nikiwa Sweden nilizungumza na vijana
wanafunzi wa Kisweden kuhusu mgogoro wa Congo DRC. Haraka vijana wale
walitaka niwaambie ni upande gani wa kushabikia kati ya Rais Kabila na
waasi wanaompinga.
Niliwaambia, kuwa ni muhimu kwanza wakaielewa historia ya Congo
kabla ya kuhitimisha ni nani mbaya na nani mzuri. Ndio, tumekuwa wepesi
wa kukimbilia kushabikia mambo kuliko kutafakari kwanza.
Kuna siku mtoto wangu wa miaka 12 alinifanya nitafakari sana.
Nilimpa asome hoja zangu zilizokuwa zikijibu mashambulizi ya hoja
kutoka kwa walionishambulia kwa hila.
Mwanangu yule alisoma kwa makini. Kisha akaniangalia na kunitamkia;
“Baba, hoja zako zimesimama vema, lakini nikuulize, je, unaweza
kuniambia udhaifu wako katika hoja ulizozijenga?”
Naam, wanadamu mara nyingi tunaona udhaifu wa wenzetu, lakini,
hatufikiri juu ya udhaifu wetu ambao tunaowaita maadui zetu nao
wanaweza kuutumia katika kujenga hoja zao.
Ndugu zangu wanahabari, mna dhamana kubwa katika kuitumikia jamii
yetu. Mjitahidi katika kusimamia kwenye ukweli. Mjitahidi sana pia
katika kusoma vitabu ili muweze kujenga uwezo zaidi katika kazi yenu ya
kuutumikia umma.
source: Raia: mwema Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment