Ndugu zangu,
Leo saa
mbili na nusu asubuhi nilifika Jengo la NSSF nikitokea kufanya jogging
yangu ya asubuhi. Nilifika hapo kuwahi kununua magazeti.
Hali
ilikuwa shwari kama ilivyo kawaida ya Iringa Jumapili asubuhi. Kunako
saa tatu asubuhi nilipokuwa nyumbani nikisoma magazeti, ndipo
niliposikia mlio wa kwanza wa bomu la machozi. Idadi yake ikaanza
kuongezeka.
Nikiwa na
kamera yangu nikajisogeza hadi katikati ya mji kufahamu zaidi
kinachotokea. Nilichokiona ni vurugu kati ya Wamachinga na Jeshi la
Polisi.Tatizo?...
Ni dogo sana, lakini linakuzwa kwa
vile siasa imepelekwa mbele badala ya kutanguliza hekima na busara. Kwa
kufuatilia suala la Wamachinga kufanya biashara eneo la barabarani pale
Mashine tatu naamini kabisa, kuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji
Msigwa angeweza kuepusha hali inayoendelea sasa kwa kuwasihi Wamachinga
watii kwanza amri ya Manispaa, na yeye, kama Mbunge wao, kujiingiza
kwenye mazungumzo ya dhati na wenzake kwenye Halamshauri ya Manispaa ya
Iringa katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili. Na hiyo ndio siasa. Siasa
ina maana ya majidiliano endelevu badala ya kuhamasisha matumizi ya
nguvu au vurugu pale milango ya majadiliano ingali wazi.
Kinachotokea Iringa kwa sasa ni doa
kubwa kwa mji wetu wenye sifa ya muda mrefu ya utulivu. Kina athari
kubwa kiuchumi pia. Pale Iringa mjini nilichokiona leo ni kama mji ulio
katika mapigano ya kivita. Watu ni wachache na wenye hofu.
Biashara nyingi zimesimama. Niliziona
Daladala zikitoka Kituo cha Miyomboni bila hata abiria, watoke wapi?
Wakati kwa sasa walio nje ya mji wameambiwa na jamaa zao walio katikati
ya mji kuwa wasijaribu kufika mjini, kwamba hali imechafuka.
Nimeongea na mwuza nyama ya bucha
aliyeniambia kuwa mgomo wa Daladala wa hivi karibuni ulimfanya apate
hasara kubwa kwenye biashara yake ya nyama kwa vile wateja wake wengi
wanatoka nje ya mji. Na anachokiona leo ni hasara nyingine kwa vile
hakutakuwa na biashara nzuri. Je, ni wafanyabiashara wangapi
watakaoathirika na hali hii ya leo?
Na kwa kuwa mkweli, kisiasa
kinachotokea Iringa kwa sasa kinaweza kuwa na athari hasi kwa Mchungaji
Msigwa badala ya kumjenga kisiasa, kwani, wengi niliozungumza nao
katikati ya mji wanamwona Mchungaji Msigwa kuwa ni mtu ambaye angeweza
kuiepusha hali hii kama asingeyatumia majukwaa ya siasa kuwahamasisha
Wamachinga kuendelea kufanya biashara, na hivyo, kutokutii amri ya
Manispaa.
Mchungaji Msigwa ni rafiki yangu, muda
mfupi uliopita nimempigia simu. Imeita bila majibu. Mmoja wa watu wake
wa karibu ameniambia yuko kwenye Harambee pale Tumaini University.
Kama Mchungaji Msigwa angejibu simu yangu, basi, ningemwambia haya ninayoyaandika hapa.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
(Pichani ni hali ya sintofahamu niliyoikuta wakati nikaribia kwa miguu eneo la Stendi Kuu asubuhi hii.)
chanzo: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment