Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa
ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki
la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo
la kigaidi limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.
Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu
waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu
wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.
Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila huruma. Aidha,
tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina
yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko
lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu. Kamwe hatutakubali kuwaacha
wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa
Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana
na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake
kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana
nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika
tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi
wa taifa.
Rais Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini
wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada
na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
source: Haki Ngowi
No comments:
Post a Comment