Mwenyekiti wa Tume wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
---
Na Mwandishi Wetu
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imesema haimzuii mwananchi, asasi au taasisi
yoyote kufungua kesi Mahakamani kupinga au kuzuia mchakato unaoendelea
wa Katiba Mpya.
Mwenyekiti
wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi huo kwa baadhi ya
waandishi wa habari waliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam
jana(Jumatano, Mei 15, 2013) kutaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali
yaliyotolewa na Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam jana (Jumanne, Mei
14, 2013).
Katika
tamko lake, Jukwaa la Katiba lilieleza nia ya asasi yake kufungua kesi
Mahakama Kuu ya Tanzania ndani ya siku saba ili kusimamisha mchakato wa
katiba Mpya kutokana kile ilichodai ni kasoro zinazojitokeza katika
mchakato wa katiba unaoendelea.
Ruksa kwenda Mahakamani
Hata
hivyo, akiongea na baadhi ya waandishi wa habari waliofika leo ofisini
kwake leo, Jaji Warioba alisema Tume yake haina tatizo na mtu au asasi
kwenda Mahakamani kwa kuwa hiyo ni haki yao ya kikatiba.
“Nimesoma
tamko lao na niseme tu halina jipya. Hii si mara ya kwanza kusikia hili
(la kwenda Mahakamani), na jibu letu lilikuwa waende na ndio jibu letu
hadi sasa,” alisema Jaji Warioba anayeongoza Tume hiyo iliyoanza kazi
Mei 2 mwaka jana.
“Mimi
nasema waende ili tujue Jukwaa haswa ni nani, kwa sababu ninafahamu ni
mkusanyiko wa asasi mbalimbali na baadhi ya asasi hizohizo zimetuletea
maombi ya kuunda Mabaraza ya Katiba ya Taasisi na Asasi… sasa jukwaa
hili ni nani haswa?,” alisema Jaji Warioba.
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
Kuhusu
marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba amesema
kuwa ingawa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sio jukumu la
Tume, wanafahamu kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kurekebisha sheria
hiyo kama ilivyoahidiwa.
“Hili
la marekebisho ya sheria ingawa sio jukumu letu, lakini nalo sio jipya.
Wote tulimsikia Waziri Mkuu hivi karibuni kule Bungeni akisema kuwa
Serikali inaandaa marekebisho ya Sheria hiyo yatakayowasilishwa Bungeni …
sasa hawa wanataka nini?,” alihoji Jaji Warioba.
Tume ina watu wenye weledi na uadilifu mkubwa
Kuhusu,
mchakato wa Katiba kukosa uongozi madhubuti, Mwenyekiti huyo amesema
kuwa Tume yake imeundwa na watu wenye sifa, weledi na uadilifu mkubwa
ambao wametokana na mapendekezo ya wadau mbalimbali yakiwemo makundi,
vyama, asasi mbalimbali za kijamii na kiraia.
“Mimi
najivunia kuongoza Tume yenye watu wenye weledi na uadilifu mkubwa na
wananchi wanalifahamu hili na kwa kweli wanatuunga mkono,” alifafanua
Jaji Warioba.
Muda wa kutolewa Rasimu ya Katiba
Katika
mahojiano hayo, Jaji Warioba pia alifafanua kuhusu muda ambao Tume yake
inatarajia kutoa Rasimu ya Katiba kwa lengo la kujadiliwa na kutolewa
maoni katika Mabaraza ya Katiba.
Kwa
mujibu wa Jaji Warioba, hivi sasa Tume inaendelea kuandaa Rasimu ya
Katiba na wananchi watapata muda wa kutosha kuijadili na kutoa maoni
yao.
“Mpango
wa Tume ni kukamilisha kazi zake ndani ya muda uliopangwa na sheria...
tutatoa Rasimu ya Katiba katika muda ambao utatosha kuwafanya wananchi
na wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuisoma,” alifafanua Jaji Warioba.
Jaji
Warioba pia ameelezea kushangazwa kwake na kauli za wadau mbalimbali
kuhusu utendaji kazi wa Tume na kusisitiza kuwa wananchi na wadau
wengine wasubiri Rasimu ya Katiba itolewe na Tume ndipo watoe maoni.
“Nadhani
itakua ‘fair’(sawa), tukishatoa rasimu ndiyo watu watuhukumu,”
alifafanua Mwenyekiti huyo ambaye pia alishawahi kuwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali.
Tusiwabeze Wananchi
Kuhusu
madai kuwa wananchi waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
ya Wilaya hawana uwezo na waledi wa kujadili na kutoa maoni kuhusu
Rasimu ya Katiba, Jaji Warioba amesema madai hayo hayana msingi na
yanabeza maamuzi ya wananchi.
Mwenyekiti
huyu ameongeza kuwa uamuzi wa Tume kushirikisha wananchi kuanzia ngazi
ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia ulilenga kuwapa wananchi hao fursa
ya kuchaguana na kuongeza kuwa wananchi walitumia fursa hiyo vizuri.
“Wanaosema
haya wanawabeza wananchi waliowachagua hao wajumbe,” alisema Mwenyekiti
huyo na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake imezipata zinaonyesha
kuwa katika wajumbe hao kuna wananchi wasomi na wenye weledi wa kutosha
kujadili rasimu ya katiba.
SOURCE: Haki Ngowi
No comments:
Post a Comment