Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imesema
haizuiwi kwa namna yoyote na uamuzi wa viongozi wa nchi wanachama wa
Muungano wa Afrika (AU) kutaka kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu
inayowahusu viongozi wakuu wa Kenya irudishwe nchini humo.
Mmoja wa wasimamizi wa mahakama hiyo, Maria Kamara alisema juzi kwamba uamuzi huo uliofikiwa Jumatatu ni wa kisiasa zaidi ambao hauwezi kuingilia wala kushawishi mahakama ya ICC kuacha kuendelea na kesi hiyo.
Kesi hiyo inawahusu viongozi wakuu wawili wa Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake, William Ruto, pamoja na mtangazaji wa Redio, Joshua Sang.
“Uamuzi wa viongozi wa AU ni wa kisiasa na ICC ni mahakama inayotambulika katika mfumo wa kimahakama wa kimataifa, ikisimamiwa na Mkataba wa Roma. Hii inamaanisha wazi kwamba hizi ni taasisi mbili zilizoko tofauti kabisa,” alisema Kamara alipozungumza na kituo cha redio cha Easy FM.
“Uamuzi wa kisiasa wa hauwezi kuingilia utendaji wa ICC. Kesi hiyo itaendelea na majaji tayari wameshapangwa. Hakuna uamuzi tofauti na huo. Majaji ndiyo pekee wenye uwezo wa kuamua iwapo kesi hiyo iendelee au la,” aliongeza.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wakuu wa nchi wanachama wa AU walikutana na kujadiliana kuhusu uamuzi wa kuitaka ICC irejeshe kesi hiyo kwenye mahakama za Kenya uliopitishwa awali na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa AU.
Katika msimamo wao, wakuu wa nchi wanachama wa AU waliituhumu Mahakama ya Kimataifa (ICC) kwa kuwaandama Waafrika kwa sababu ya rangi yao.
AU inapinga hatua ya ICC kusisitiza kusikiliza kesi za washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi Kenya mwaka 2007, Rais Kenyatta na Ruto kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn aliyasema hayo akiongeza kuwa watalalamika mbele ya Umoja wa Mataifa kuhusu hilo.
Rais Kenyatta anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Julai kusikiliza mashtaka dhidi yake kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu.
Aidha Kenyatta amekanusha tuhuma hizo zinazotokana na madai ya kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi Kenya mwaka 2007 ambapo maelfu walipoteza maisha yao na wengine kuachwa bila makao.
Alichaguliwa kama Rais katika uchaguzi uliofanyika
mwezi Machi na kumshinda mpinzani wake mkuu, Raila Odinga katika
uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Akihutubia kikao cha marais wa Afrika kwenye mkutano wa AU mjini Addis Ababa, Hailemariam alisema kuwa viongozi wa Afrika wameelezea wasiwasi kuwa asilimia 99 ya wale wanaotakiwa na mahakama ya ICC kwa makosa yoyote yale ni Waafrika.
“Hii ni dalili ya kuwa mambo siyo sawa, mfumo wa ICC una hujuma,” alisema Hailemariam.
“Mahakama ya ICC ilibuniwa ili kuangamiza kile kilichoonekana kuwa viongozi wanaofanya uhalifu bila kujali, lakini sasa mfumo huo umegeuka na kuwa mfumo wa kuwaandama watu kwa misingi ya rangi,” alisema Hailemariam.
“Mahakama ingali inawataka Kenyatta na Ruto licha ya jamii zao zilizokuwa na uhasama katika uchaguzi wa 2007 kuungana na kuwachagua wawili hao kuwa viongozi wa Kenya,’’ aliongeza Hailemariam.
Kenyatta na Ruto walikuwa wapinzani wakuu katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2007 ambapo ulifuatwa na mauaji ya watu 1,000 na wengine laki sita kuachwa bila makao.
Wadadisi wanasema kuwa kesi za ICC ziliwapatanisha wawili hao kushirikiana katika uchaguzi wa 2013, kwani waliamini kuwa jamii ya kimataifa ilikuwa inaingilia maswala ya ndani ya Kenya.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment