Rasilimali ziwaunganishe, kuwaendeleza Watanzania wote na uvivu wa kudiriki ndiyo unaoitesa, kuiharibu sifa ya nchi yetu.
Hivi vilikuwa ni vichwa vya habari ambavyo niliviandika katika safu hii mapema mwaka huu nilipozungumzia suala linalofanana.
Suala hili ni gesi asilia iliyogundulika Mtwara na Lindi na dhamira ya kuifikisha Dar es Salaam ambayo kwa sasa imegeuka kiama, laana kwa nchi badala ya baraka zitokazo kwa Mungu.
Nilisema kuwa mijadala yote inayohusu mustakabali wa nchi tangu kugundulika kwa rasilimali hiyo asilia umebadili mwelekeo na kuiweka majaribuni Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Nikaeleza pia kuwa wapo wanaiona rasilimali hiyo kama baraka, njia ya nchi yetu kutokea, kuelekea kwenye neema na kuuaga umaskini.
Ninakubaliana na maoni ya msomaji wangu aliyewahi kuniandikia kwamba Tanzania kama jamii, lazima iweke msimamo au mfumo wa pamoja wa jinsi ya kutumia vizuri rasilimali hizi ikiwamo gesi asilia, kwa kuzingatia umoja wake.
Ni dhahiri wanasiasa, wanaharakati wote wanaozungumzia mradi huu kwa sasa hawana budi kuongozwa na mtazamo huu.
Hata hivyo, wasisahau kuwa walisoma au kusomeshwa bure, kwa fedha za kahawa, pamba, mkonge na au almasi ya Mwadui kwani hakukuwa na ubaguzi.
Inafaa wakumbuke kuwa wanaposhika bango kuhusu gesi asilia kutosafirishwa kwa bomba kwenda miji kama Dar es Salaam na mingineyo ambako ndiko kuna soko la uhakika, wasijisahau.
Hata wanaposhinikiza kwamba rasilimali hiyo ibakie kusini wasisahau mgawo na mapato ya mazao yetu yaliyouzwa ndani na nje kwa miaka mingi kupitia vyama vya ushirika, wakulima wakanufaika, kiasi kilichobaki kikatengwa kwa shughuli za maendeleo katika maeneo yote ya nchi, pia bila ubaguzi.
Ni kwa mfumo huo wa mazao ya biashara zama hizo, bado naamini kuwa hata gesi asilia badala ya kung’ang’aniwa kuwa ibaki kusini, inafaa iuzwe kokote Tanzania.
Gesi asilia iuzwe, viwanda vijengwe, mitambo ya
kufua umeme ijengwe pia Mtwara au Lindi kulingana na mahitaji, lakini
kiasi kinachotakiwa kufika Dar es Salaam kiachwe kiende.
Kwa ufupi, wananchi kule wajengewe uwezo, waondokane na umaskini na sababu za kuhamia kwingine nchini kwa shughuli za uchuuzi.
Wasaidiwe kubadilika na kuithamini elimu, shule bora , hospitali za kisasa zenye vifaa na watalaam kama ile ambayo tunaambiwa itajengwa Kilwa, mkoani Lindi kupitia Kampuni ya Statoil ya Norway, vyote vifanyike.
Nirudie kusema kuwa wakazi wa kusini wanahitaji
kuwa na shule bora zilizojengwa katika maeneo mengineyo nchini na ambazo
zimekuwa zikifanya vizuri kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha pili,
nne au sita na hivyo kufuta aibu ya maeneo hayo kufanya vibaya kila
mwaka na kushika mkia. Hiki ndicho kitu cha msingi ambacho kinaweza
kufanyika kwa kutumia mgongo wa rasilimali zikiwamo gesi asilia.
Kingine kinachotakiwa kufanyika ni kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi wote kuhusu manufaa ya rasilimali hizi kwao na nchi kwa jumla.
Viongozi wetu wa ngazi zote wasimamie jukumu hili, tena kwa vitendo ili ubabaishaji usipate nafasi na badala yake wananchi wajione kuwa sehemu ya miradi yote inayoanzishwa kule.
Hili nadhani inafaa lifanywe kwa ushirikiano baina ya serikali kuanzia za mitaa, vijiji, kata, wilaya, mkoa hadi serikali kuu kwa maana ya Wizara ya Nishati na Madini, chini ya uongozi wa Profesa Sospeter Muhongo.
Ushauri wangu ni kwa wanaharakati wa aina zote na wananchi kwa ujumla kusini waone manufaa ya gesi asilia kwao, wasubiri kufaidi matunda ya uwekezaji wake.
Hata hivyo, si kwa kufanya vurugu kama ambazo zimetokea wiki hii na kusababisha maafa makubwa ikiwamo vifo vya watu wanne na mali nyingi kuharibiwa.
Lazima kujifunza kutoka Mwanza, Shinyanga ambako wananchi siku zote wameachiwa mahandaki, mashimo makubwa baada ya dhahabu na almasi kwisha.
Rasilimali hii ya gesi inahitaji uwekezaji mkubwa ambao wakati mwingine nchi kama Tanzania haina uwezo, hivyo lazima wageni waingize mtaji, jambo ambalo huenda wanaoshawishi watu wa Mtwara kuandamana hawawaelezi ukweli.
Ninarudia kusema rasilimali hizi ni zetu sote Watanzania, hivyo hazina sababu ya msingi ya kujaribu kutugawa kwa namna yoyote ile, haina sababu ya kuingiza nchi vitani, mizozo ambayo Watanzania hawakuzoea.
Watanzania kwa zaidi ya miaka 51 ua uhuru wao wameishi vizuri, kwa amani, utulivu na mshikamano mkubwa, kiasi cha kuwa kama ndugu wa familia moja, sioni sababu ya kuanza leo kukimbiana kwa sababu ya gesi.
Rasilimali hizo na nyinginezo zinafaa zituunganishe zaidi sisi
Watanzania ili tuzidi kuwa kitu kimoja wakati huu ambao ulimwengu
unafikiria kuwa wenye umoja kama ambao umetokea Ulaya, wanakotumia
sarafu moja.
Msimamo wangu katika hili upo wazi mara zote nimesema kwamba wananchi wa Lindi, Mtwara na kote kwingineko nchini wanahitaji maendeleo, wala hili halina ubishi.
Kama walivyo Watanzania wengine kokote waliko, wananchi hao wanahitaji maji, shule, zahanati, vituo vya afya, hospitali nzuri zenye dawa, madaktari bingwa, barabara, viwanja vya ndege na mambo mengine mengi.
Lakini, huduma hizo na nyinginezo haziwezi kamwe kuwanyeshea kama mvua, hazishuki kama ‘manna’, yaani kile chakula walichoshushiwa wananchi wa Israel kule jangwani zama za Mussa.
Kama Wayahudi walivyoshushiwa manna kwa mahitaji yao wakala, wakashiba, lakini hakuna siku wananchi wa Mtwara, Lindi ambao wao utajiri wa gesi watashushiwa mahitaji yakiwamo maendeleo.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment