- Ni kuhusu tishio la kujitoa mchakato wa Katiba
- Amwambia Dk Slaa nchi kwanza, CHADEMA baadaye
"If I'm told to choose between my party and my country, I will choose my country"
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Profesa Mwesiga Baregu, amekataa kata kata wito wa chama chake wa
kumtaka ajitoe ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku yeye akiweka
msimamo wake wazi kwamba Tanzania ni mhimu zaidi kwake kuliko chama
chake hicho.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa Profesa Baregu, zinasema
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa, alimwita msomi huyo
ambaye ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akimtaka ajitoe ndani
ya Tume hiyo kwa sababu za kisiasa kwa madai kwamba Chama cha Mapinduzi
(CCM) kimeuteka mchakato huo.
Profesa Baregu anaelezwa kumjibu Dk Slaa kwa kutumia maneno ya
Kiingereza, akisema: “If I told to choose between my country and my
party (CHADEMA), I will choose my country,” akiwa na maana kwamba kama
angetakiwa kuchagua kimoja kati ya nchi yake na chama chake cha
CHADEMA, angechagua nchi yake kwanza.
Akizungumza na Raia Mwema juzi Jumatatu jijini Dar es Salaam,
Profesa Baregu amekiri kutoa msimamo huo Katibu Mkuu wake, Dk Slaa,
pamoja na chama chake cha CHADEMA, akisema viongozi wenzake hao
wanapaswa kujishauri mara mbili mbili kabla ya kuchukua uamuzi huo wa
kujitoa ikizingatiwa kwamba tangu mwanzo chama hicho ndicho
kilichoasisi suala zima la Tanzania kuwa na Katiba Mpya tofauti na hii
ya sasa.
Itakumbukwa kwamba CHADEMA, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman
Mbowe, wakati akiwasilisha hotuba mbadala ya kambi rasmi ya upinzani
kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, ilitangaza kujitoa katika mchakato wa
mabadiliko ya Katiba, akitaja sababu kadhaa, zikiwamo za mchakato mzima
huo kutekwa na CCM na lakini pia kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawana
weledi wa kutosha kufanya kazi hiyo.
“Ni kweli, niliitwa na Katibu Mkuu (Dk Slaa), akaniambia Kamati Kuu
ya chama chetu imeazimia kwamba chama hakiridhishwi na mchakato mzima
wa kutunga Katiba mpya, na kwa hiyo akaniambia chama kimeagiza nijitoe
ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Akaniambia Kamati Kuu imeamua
mambo mawili; kwanza kijitoe na pili, kikishakujitoa kianzishe kampeni
ya nchi nzima kuwahamasisha wananchi nao wasusie mchakato huo,” anasema
Profesa Baregu katika mahojiano maalum na Raia Mwema.
Anasema aliomba kujulishwa rasmi maamuzi hayo ya CC kwa maandishi,
ili ajue atachukua uamuzi gani lakini hadi anafanya mahojiano na Raia
Mwema hakuwa amepata majibu, huku akisema kwamba kwa maoni yake kama
kweli yalikua ni mamuzi ya kikao, basi Kamati Kuu itakua ilifanya
makosa kufikia uamuzi wa kujitoa bila kumshirikisha.
“Kwanini? Mimi tangu mwanzo kabisa sikuona kama suala hili la
kuandikwa kwa Katiba mpya ni suala la mapambano kwa sababu kubwa moja
kwamba CHADEMA ndiyo mwasisi wa mabadiliko haya ya Katiba. Mimi
nilikuwa Meneja wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010 na nilishiriki
kuandika Ilani ya uchaguzi, na hili la kutaka Katiba mpya lilikuwemo
ndani ya Ilani yetu.
“Wakati ule wenzetu (CCM) waliweka msimamo wao wakisema hakuna
sababu ya kuwa na Katiba mpya, iliyopo inatosha, lakini baadaye
Serikali ikaona ipo haja ya kuwa na Katiba mpya inayokidhi mahitaji ya
sasa na yajayo. Muswada ukapelekwa bungeni, wabunge wa upinzani
wakasusa na kutoka nje. CHADEMA tukapewa fursa ya kwenda Ikulu kuonana
na Rais kwa siku mbili mfululizo na karibu mapendekezo yetu yote
yakakubaliwa.
“Muswada ukarudishwa bungeni upya, sheria ikafanyiwa marekebisho na
kukubaliwa na wabunge wa kambi ya upinzani. Sasa leo hii, wabunge wale
wale waliokubali, wanataka kukataa mchakato wa Katiba unaoendeshwa kwa
mujibu wa sheria waliyoipitisha wao wenyewe…kwa maoni yangu, hadi sasa
sijaona matatizo ya mchakato, yawe ya maandishi au ya malengo ya
kisheria. Kama ningekuwa nimeona tatizo, nisingekuwamo humu, ningejitoa.
Tunatengeneza Katiba ya Watanzania wote, si Katiba ya chama fulani.
“Lakini pia, CHADEMA tulipokutana na Rais (Jakaya Kikwete),
alitushauri na tukakubaliana naye, twende hatua kwa hatua. Itungwe
sheria yenyewe kwanza, halafu iundwe Tume, baada ya hapo mambo mengine
yaendelee kujadiliwa... tangu wakati huo hadi sasa nadhani sisi kama
Tume tunafanya vizuri ikilinganishwa na wenzetu huko nje walioandika
upya Katiba yao.
“Mchakato unaofuata sasa ni wa kuundwa kwa Bunge Maalumu la Katiba,
hatua hii nayo wananchi wametakiwa wajiandae kutoa maoni yao juu ya
muundo wa Bunge hilo. Ushauri wangu kwa CHADEMA, naomba chama chetu
kikae mkao wa kujenga nchi yetu, na si mkao wa kuibomoa. Kama chama
tukae na Watanzania kujenga Katiba yetu mpya kwa ajili ya Watanzania na
Tanzania yetu hii kwa sababu fursa hii haitakuja tena karibuni labda
baada ya miaka 50 ijayo…kuzira, kujitoa, nasema Watanzania
hawatatuelewa.”
Akifafanua msimamo wake alioutoa kwa Dk Slaa kwamba kama angeambiwa
achague kati ya nchi yake na chama chake, angechagua nchi kwanza,
Profesa Barugu anasema: “Ndiyo, chama kinaundwa na kinapita, lakini
Tanzania kama nchi itaendelea kuwepo daima. Ushauri wangu kwa CHADEMA
ni kwamba kwa kuwa sisi tulishajiweka katika kusimamia mchakato huu wa
kuwa na Katiba mpya, tusijiharibie kwa kuvuruga mchakato huu.”
Akizungumzia kauli ya Mbowe katika hotuba yake bungeni kwamba Tume
ya Mabadiliko ya Katiba haina watu weledi, Profesa Baregu anasema:
“Sisemi katika hili CHADEMA imekurupuka, nasema ijishauri upya. Sijui
ni weledi wa aina gani wanaousema, lakini naamini Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imejaa watu weledi watupu, imejaa watu waadilifu na wasiokuwa
na matope yoyote…ndiyo maana tangu iundwe, hakuna Mtanzania yeyote
ambaye ameiita Tume hii kwamba ni genge jingine la mafisadi.
“Sitaki kuwasemea wajumbe wenzangu juu ya weledi wao, lakini mimi
mwenyewe tu mbali na elimu yangu, lakini pia nimetumika katika Tume ya
Mo Ibrahim inayotathimini utawala bora wa marais wa Afrika kwa muhula
mmoja. Mtu huwezi kuwa katika Tume hiyo kama huna weledi wa kutosha.”
Dk Slaa alipotafutwa jana Jumanne, ili pamoja na mambo mengine,
aelezee hatua hiyo ya Profesa Baregu kukataa kujiuzulu akiweka wazi
kwamba hadi sasa hajaona tatizo lolote kubwa ndani ya Tume hiyo
linaloweza kumshawishi akubaliane na msimamo huo wa chama chake, na
msisitizo wake huo wa kuweka maslahi ya nchi kwanza mbele kuliko ya
chama chake, alisema: “Saa hizi niko kwenye kikao, pole baba!”
Moja ya eneo linalolalamikiwa na CHADEMA katika mchakato huo wa
Mabadiliko ya Katiba hadi kutishia kujitoa katika mchakato mzima huo,
ni pamoja na uundwaji wa mabaraza ya kata, ikielezwa kwamba wajumbe
wengi wa mabaraza hayo ni makada na viongozi wa CCM, na hivyo kuhofu
kuwa Katiba hiyo mpya inaweza kukibeba zaidi chama hicho Tawala.
Hata hivyo, akitoa msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mbele ya
waandishi wa vyombo mbalimbali nchini kuhusiana na mabaraza hayo ya
Katiba ngazi ya kata, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba
alivitupia lawama baadhi ya vyama vya siasa na makundi ya dini
kujifungamanisha na uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza hayo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Warioba alisema Tume yake italazimika
kuyaondoa mawazo yote hasi yanayokinzana na misingi ya kitaifa
yaliyotolewa na wananchi na makundi mengine ya kijamii ili kuhakikisha
kwamba nchi inakuwa na Katiba Mpya inayokidhi maslahi ya wananchi
wenyewe na maslahi ya taifa pia.
source: Raia Mwema : Mayage S. Mayage
No comments:
Post a Comment