WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, May 23, 2013

Muhongo: Lazima bomba lijengwe


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jana aliwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/14, akisema msimamo wa serikali wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam  uko pale pale.
Alisema kukamilika huko kutawaletea wakazi hao na taifa manufaa makubwa.

Alisema ujenzi huo utaongeza fursa za ajira kwa wananchi hususan waishio katika maeneo hayo kwa sababu vitajengwa viwanda, hivyo serikali itapata mapato makubwa.
Kauli hiyo inakuja wakati bado wanananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wakipinga hatua ya serikali ya kujenga bomba hilo wakidai wanataka waone faida wanayopata kutokana na ujenzi huo.

Profesas Muhongo alisema mradi huo uliozinduliwa Novemba 8, mwaka jana na Rais Jakaya Kikwete, unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 552 na kipenyo cha inchi 36.

Alibainisha kuwa, pia mitambo miwili ya kusafisha gesi asilia itajengwa katika maeneo ya Mnazi Bay-Madimba mkoani Mtwara na Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi ambayo itagharimu Sh. trilioni 1.96.

“Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu hii utaleta manufaa makubwa kwa taifa na hadi sasa mikoa ya Lindi na Mtwara imepata manufaa mbalimbali yatokanayo na miradi ya gesi asilia kama tozo asilimia 0.3 ya mauzo, umeme, maji na ufadhili wa mafunzo katika vyuo vya ufundi na sekondari,” alisema.

Aliongeza kuwa, kitajengwa kiwanda cha saruji cha Dangote, mtambo wa kufua umeme wa megawati 400 kupitia Kampuni ya Symbion pamoja na ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 220 na kiwanda cha mbolea mkoani Mtwara.

Kuhusu Songosongo, Profesa Muhongo alisema  gesi asilia ya Songosongo Iligundilika mwaka 1974 na tayari kuna bomba limejengwa la kupeleka gesi jijini Dar es Salaam, lakini hakukuwa na ushabiki kama Mtwara.

Alisema gesi hiyo inasafirishwa na bomba lenye urefu wa kilometa 225 na kipenyo cha inchi 16 kutoka Songosongo hadi jijini Dar es Salaam na asilimia 80 ya gesi hiyo itatumika kufua umeme na kiasi kilichobakia kinatumika kwenye baadhi ya viwanda na taasisi.
 
MAFUTA MABOVU
Alisema Novemba mwaka jana, Kampuni ya Addax Energy SA ya Uswisi, ilishinda zabuni ya kuagiza mafuta kwa pamoja ambapo iliagiza tani 100,000 za dizeli.

Hata hivyo, alisema mafuta hayo yaligundulika kuwa ni chini ya viwango vinavyotakiwa nchini.

Alisema mafuta hayo yalikuwa na thamani ya Sh. bilioni 154.72 na kwamba Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Kampuni ya Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PIC)  ilifanikiwa kuzuia mafuta hayo kuuzwa katika soko la nchini.

Alisema kufuatia tukio hilo, kampuni hiyo ililipa faini ya takribani Sh. bilioni 1.98 na kufungiwa kushiriki katika shughuli za uagizaji mafuta nchini kwa kupindi cha miezi minne.
 
MIGODI ITAKAYOFUNGWA
Alisema migodi ya Golden Pride (Nzega) na Tuwalaka (Biharamulo) inatarajiwa kufungwa rasmi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na maeneo hayo kukabidhiwa serikalini.

Kwa mujibu wa sheria, migodi inayofungwa hurejeshwa serikalini ili ipangiwe matumizi mengine kadri inatakavyoonekana inafaa.

“Hivyo, serikalini imeamua eneo la mgodi wa Tulawaka lichukuliwe na Stamico (Shirika la Madini) ili liendeleze uchimbaji kwa kiwango cha kati kwa kuwa bado yapo mashapo ambayo yanaweza kuchimbwa kwa faida,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha, alisema kuwa mgodi wa Golden Pride utakabidhiwa katika Chuo cha Madini cha Dodoma utumike kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa mafundi mchumo.

Kadhalika, Profesa Muhongo alisema wizara itakamilisha hatua ya pili ya mipango ya ufungaji migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi, Golden Pride, North Mara na Tuwalaka kwa kuhakikisha kuwa migodi hiyo inaweka hatifungani (rehabilitation).

“Wizara itakamilisha mipango ya ufungaji wa migodi ya Geita Gold Mine, Tanzania One na Williamson Diamonds Limited,” alisema.
 
HASARA TANESCO
Profesa Muhongo alisema Shirika la Umeme (Tanesco), katika kipindi cha kati ya Julai mwaka huu hadi Aprili mwaka huu, limepata hasara ya takribani Sh. milioni 966.18 kutokana na wizi na uharibifu wa miundombinu nchini.

MADINI YAKAMATWA

Profesa Muhongo alisema Wakala wa Ukaguzi wa Madini  (TMAA), imekamata madini yenye thamani ya Sh. bilioni 13.12 yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege kinyume cha sheria.

Alisema madini hayo yalikamatwa katika kipindi cha kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Aprili mwaka huu katika viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere, Kilimanjaro na Mwanza.

Aliisifu bajeti yake kwamba ni ya kihistoria pamoja na mambo mengine, asilimia 90 kuelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, alisema kamati yake imesikitishwa kuona sehemu ya mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, hasa mlima wa Kabulo leseni yake yenye namba ya mgodi SML 235/2005 ilihamishwa kinyemela kutoka Tanpower Resources Ltd kwenda Tanzacoal East Africa Mining Ltd Agosti 6 mwaka 2011.

Alisema kamati hiyo inaishauri serikali kuinunua leseni hiyo upya na kuikabidhi Stamico kwa ajili ya kuendeleza mgodi wa Kiwira.

Akizungumza mara baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Mbunge wa Simanjiro (CCM) Ole Sendeka, aliilaumu serikali kwa kuwalaghai wananchi wa Mtwara kwa kuwaahidi kuwa kampuni ya kufua umeme ya Symbion itazalisha umeme mw 400 wakati haijawahi kutangaza tenda ya kampuni hiyo.

Sendeka alisema kuwa huko nyuma serikali iliwahi kumpata mbia ambaye ni kampuni ya China ya Seemek kuzalisha megawati 300, lakini baadaye wizara kupitia kwa watendaji wake iliondoa mpango huo ambao ulikuwa umekamilika.

“Huo mradi wa Kinyerezi ni mradi ambao ulikuwa ujengwe Mtwara na kampuni ya Seemek ya Kichina ambayo ndiyo ingetoa mw 300, badala yake wameuhamishia Kinyerezi na kuwahadaa wananchi kuwa Symbion itawajengea mw 400, huu si ukweli hata kidogo,” alisema Sendeka.

Profesa Muhongo aliliomba Bunge kuiidhinishia jumla ya Sh. 1,102,429,129,000 huku Sh. 110,216,384,000 sawa na asilimia 10 zikiwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. 992,212,745,000  sawa na asilimia 90 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment