Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kijo-Bisimba
UTAWALA bora wa sheria, demokrasia safi, uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji ni nguzo zinazodaiwa kuwa muhimu katika taifa lolote duniani linalohitaji kujenga misingi ya maendeleo katika nyanja zote kupitia mipango, sera na dira iliyojiwekea.
Ili taifa liweze kuwa imara kupitia nguzo hizo, nchi nyingi hususan barani Afrika zimekuwa zikifanya mabadiliko ya mara kwa mara ya Katiba kutokana na upungufu unaokuwa ukijitokeza au kubadili sheria zilizopitwa na wakati kwa lengo la kuhakikisha nchi inapiga hatua ikiwa na amani na utulivu.
Kutokana na vigezo hivyo, Tanzania ikaamua kuwa moja kati ya nchi zinazohitaji mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zinazoikabili ambapo mwezi Aprili mwaka jana Rais Jakaya Kikwete aliteua tume itakayoshughulika na kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi.
Hatua ya kubadilisha Katiba hiyo hapa nchini imejitokeza baada ya Watanzania kubaini baadhi ya upungufu unaoleta mgogoro katika jamii. Inawezekana udhaifu huo ulitokana na utashi wa kundi la watu kuangalia masilahi ya jambo au kitu fulani.
Suala moja linalotajwa kuwa ni udhaifu katika Katiba hiyo ni mamlaka aliyokabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo suala la kumteua mtumishi anayetumikia nafasi ya Serikali Kuu kushiriki katika shughuli za Bunge.
Kipengele kimojawapo cha udhaifu huo kinatoka kwenye ibara ya 36(1) cha Katiba hiyo kinachosema kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Kipengele hicho kinatafsiriwa kuwa, Rais wa Tanzania amekabidhiwa mamlaka ya ‘umungu mtu’ mbali na utambuzi, utashi na hisia alizonazo kama sehemu ya upungufu alionao mwanadamu.
Moja ya viongozi wenye majukumu hayo ni Injinia Stella Manyanya ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Mpangilio huo umezua mjadala hususan katika kipindi hiki cha kuandaa Katiba Mpya ambapo Watanzania wamekuwa wakihoji endapo kumetokea mvutano bungeni kati ya wabunge na Serikali kiongozi huyo anaweza kusimamia upande gani?
Injinia Manyanya aliwahi kuingia kwenye malumbano kisiasa kutokana fuatia sakata la mgomo wa madaktari baada ya kunukuliwa akisema kipigo cha Dk Steven Ulimboka ulikuwa ni mpango wa Mungu kumwepusha asiongoze mgomo huo.
Mgogoro huo ulidaiwa kuwa na sehemu ya uchochezi wa kisiasa kutoka katika chama fulani cha upinzani hapa nchini kwa lengo la kuidhoofisha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na kujitengenezea nafasi ya umaarufu kwa Watanzania.
Injinia Manyanya anasema haoni kama mfumo huo una upungufu wowote katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana na mpangilio uliopo na kwamba mihimili yote inategemeana katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Naweza kutolea mfano wa seti ya kuhifadhia vifaa vya kuandikia, tunafanya kazi kwa mtandao wa kutekelezaji majukumu ya Serikali, jambo muhimu ni kuzingatia tu misingi na kanuni za kazi pale unapokuwa bungeni au mtumishi wa umma,” anasema Manyanya.
Injinia Manyanya anasema mbali na mfumo huo kukubalika kikatiba lakini pia unajenga mtandao madhubuti katika utekelezaji wa ahadi na mipango ya Serikali.
“Sisemi hivyo eti kwa sababu mimi ni mhusika lakini lazima ieleweke hivyo, lakini pia Rais ambaye ni wa chama tawala ndiye anayeteua hao wakuu wa mikoa, mimi ni mbunge wa Viti Maalumu CCM, kwa hiyo bado utaona mfumo ni uleule,” anasema Manyanya.
Injinia Manyanya anawataka Watanzania wasijenge dhana ya siasa wakati wa kutafasili majukumu ya watumishi na wabunge na kwamba kama ni tatizo basi linatokana na Katiba iliyopo.
“Suala la kuonyesha hisia mbona hata baadhi ya waandishi wa habari wanaonyesha hisia zao za kimasilahi, kwani mwandishi wa habari haruhusiwi kuegemea upande wowote,kwa hiyo sidhani kama kuna mtumishi aliyekamilika asilimia mia,” anasema Manyanya.
Katika maoni yake Injinia Manyanya anasema mfumo huo hautofautishi na waziri kuwa mbunge kwa hiyo kinachotakiwa endapo Watanzania wataamua kufanya mabadiliko basi waangalie kama kuna sababu za msingi kuondoa mfumo huo.
Mwanaharakati (LHCR)
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kijo-Bisimba anasema mfumo huo ni tatizo ambalo linatakiwa kufanyiwa marekebisho katika kipindi hiki cha mchakato wa kuandaa Katiba Mpya.
“Haiwezekani mbunge ambaye unasimamia Serikali halafu uwe sehemu ya Serikali, bado tutaendelea kuyazungumzia sana, ni makosa yaliyofanyika hivyo ni lazima kutafakari na kufanyia mabadiliko,” anasema Kijo-Bisimba.
Anaongeza kuwa mfumo huo unasababisha mtumishi wa Serikali apoteze uaminifu kwa jamii katika utekelezaji wake wa majukumu ya kiserikali, hatua ambayo inapoteza utashi kwa mtumishi wa Serikali.
“Lakini pia tatizo hilo nalifananisha na mfumo wa mbunge kuwa waziri, ni jambo ambalo pia linonyesha utata kwa hiyo nadhani huu ndio muda sahihi wa kufanya marekebisho hayo,” anasema Kijo-Bisimba.
Msomi (UDSM)
Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo anasema mfumo huo haukubaliki katika taifa linalofuata misingi ya demokrasia.
Dk Kitila anasema ni makosa yaliyojitokeza katika kipindi cha utawala wa Serikali ya kikoloni ambapo kiongozi wa nchi alitambuliwa kuwa mamlaka makubwa kikatiba katika kupitisha uamuzi kuhudu masuala ya mbalimbali ya kitaifa.
“Mkuu wa mkoa halafu ni mbunge ikitokea Bunge linapinga kupitisha Bajeti ya Serikali, siku hiyo kiongozi huyu atasimama upande gani? Kwa hiyo utaona ni jinsi gani atakavyokuwa kwenye wakati mgumu sana,” anasema Dk Kitila na kuongeza kuwa;
“Mbunge kazi yake kuu ni kusimamia Serikali kuu kutekeleza majukumu yake, kwa tafsiri hiyo kiongozi ambaye ni mtumishi na mbunge kwa wakati mmoja atamsimamia nani? Hayo ni makosa ambayo yako wazi sana.”
Dk Kitila anaongeza kuwa makosa hayo ni sehemu tu ya ubovu wa Katiba iliyopo hivyo Watanzania wanatakiwa kutumia nafasi hii kufanya mabadiliko makubwa yatakayoleta Katiba Mpya kwa maslahi ya taifa.
Mwanasheria
Katika maoni yake Mwanasheria nguli na Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu anasema wabunge kuwa sehemu ya mawaziri au wakuu wa wilaya kuwa sehemu ya Bunge ni madudu ambayo yanatakiwa kufanyiwa mabadiliko katika Katiba.
Kauli hiyo aliitoa katika ukumbi wa mikutano Dodoma mjini Novemba 4, mwaka jana alipokuwa akitoa maoni yake ya Katiba Mpya na kuongeza kuwa matatizo hayo yanatokana na mwingiliano wa mihimili ya Serikali.
“Bunge na Serikali vinatakiwa kujiendesha bila kuingiliana, Bunge linatakiwa kuwa la wabunge, Katiba Mpya inatakiwa kueleza wazi kwamba Rais sio sehemu ya Bunge na asiwe na uwezo wa kuteua wabunge kama ilivyo sasa.” anasema Lissu.
Lissu anasema ndani ya Katiba Mpya kunatakiwa kuwe na mfumo wa Serikali Kuu na Serikali za mikoa utakaoweka utaratibu wa wananchi kuchagua viongozi ngazi ya mkoa ili kuwafanya viongozi hao wawajibike kwa wananchi.
Kutokana na changamoto zilizopo, Lissu anasema Katiba Mpya inatakiwa kupunguza madaraka ya Rais ikiwa ni pamoja kuwapo kwa kipengele kitakachoeleza kuwa Rais sio sehemu ya Bunge ili kulifanya Bunge kuwa na nguvu.
Wanasiasa
Wabunge zaidi ya 36 walishiriki siku ya utoaji wa maoni Dodoma mjini baada ya kufikiwa na wajumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya ambapo baadhi ya mapendekezo yao ilikuwa ni kuondoa kutenganisha mwingiliano wa majukumu ya kazi kwa watumishi wa wabunge.
Akitoa maoni yake, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR- Mageuzi) Mosses Machali anapingana na hatua ya mtumishi wa Serikali kuwa sehemu Bunge jambo ambalo limekuwa na mgongano wa kimasilahi.
“Ni vigumu kwa wabunge kumdhibiti waziri ambaye ni mbunge mwenzao kama ilivyo sasa, kwa hiyo Katiba Mpya itamke wazi kuwa mtumishi yeyote wa Serikali wakiwamo mawaziri wasiwe wabunge ili kuondoa mgongano wa kimasilahi,” anasema Machali.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, anasema Viti Maalumu vya ubunge vifutwe na badala yake wanawake waende katika majimbo kugombea sambamba na wanaume.
“Kuendelea kuwa na wabunge wa Viti Maalumu ni kuwafanya waendelee kujiona wanyonge, wakati hivi sasa kuna wanawake wenye uwezo mkubwa sawa na wanaume, hatua hiyo itasaidia kujenga Bunge imara.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment