“Zanzibar ikijitenga
kutokana na ulevi tu wa kusema Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika, wakumbuke
kuwa Muungano ndiyo unaowafanya wanasema ‘Sisi Wazanzibari na wao
Watanganyika’, nje ya Muungano hawawezi kusema hivyo: Kuna ‘wao Wapemba na wao
Waunguja.”- Julius Kambarage Nyerere!
JUMAMOSI ijayo
Zanzibar inatimiza miaka 49 tangu kufanyika mapinduzi ya Januari 12, 1964
ambayo yaliung’oa utawala wa kisultani ambayo uliingia madarakani Desemba 10,
1963 baada ya kuondoka wakoloni wa Kiingereza.
Mapinduzi hayo yanatokana
na tangazo la Januari 12, 1964 asubuhi, pale sauti ambayo haikuwahi kusikika
katika ukanda wa Tanganyika wala Zanzibar ikitangaza kufanyika kwa mapinduzi
kisiwani humo.
Tangazo hilo
ilikuwa la John Okello, ambaye mpaka mauti yanamfika haikufahamika kama alikuwa
ni raia wa Kenya au Uganda. Okello na msaidizi wake Engine walitoa amri ya
kukamatwa kwa mawaziri wa Serikali ya Sultan na kukataza watu kutembea.
Itakumbukwa kuwa
usiku wa sherehe za Mapinduzi hayo Januari 11, 1964, Hayati Aman Karume alipelekwa
mafichoni jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumwepusha asikamatwe endapo
mapinduzi hayo yasingefanikiwa.
Katika mwendelezo
wa juhudi za kukikomboa kisiwa hicho, mamia ya watu wenye asili ya Oman na
Comoro walifukuzwa Zanzibar ambapo watoto wadogo walipelekwa maeneo ya
bandarini kuonana na baba zao kwa ajili ya safari ya Oman.
Kazi iliyofuata
ilikuwa ni kulinda mapinduzi hayo na hatua zilizofikiriwa ilikuwa ni kuwa na
Muungano utakaohakikisha kuwapo kwa ulinzi wa kuinusuru Zanzibar isirejeshwe
mikononi mwa Sultani baada ya kupinduliwa.
Kupitia waasisi
ambao ni Hayati Julius Nyerere na Abeid Aman Karume kutoka kila upande wa
Aprili 26,1964 wakaamua kuchanganya udongo kama ishara ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar mnamo Aprili 26,1964 na kusaini Hati ya Makubaliano ya
kuunda Tanzania.
Sababu nyingine za
kulinda kisiwa hicho kupitia Muungano ilikuwa ni kujenga umoja wa Wazanzibar
baada ya kuonekana mpasuko uliosababishwa na ubaguzi miongoni mwa Wapemba na
Waunguja ambapo hali inaonyesha bila Muungano, visiwa hivyo vingeweza kutengana
wakati wowote.
Pamoja na kuwapo
Muungano, mpasuko baina ya Uunguja na Upemba umeendelea kuonekana hadi leo na
wakati wa kutoa maoni ya Katiba Mpya, wapo waliosema wazi kuwa ziwepo Serikali
nne, wakimaanisha Serikali ya Unguja, Pemba, Tanganyika na ile itakayokuwa ya
Muungano.
Ieleweke kwamba
hata busara ya makubaliano kati ya Rais msaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume
na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kupitisha kura ya maoni kwa
Wazanzibar na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inatokana na sababu ya
kuimarisha uhusiano kati ya Unguja na Pemba.
Pamoja na kubainika
kwa upungufu mkubwa ukiwamo kutonufaika na Muungano huo, inasemekana kuna
makundi yanayotumiwa sasa kisiasa na Sultani au wafuasi wake, kutaka kuuvunja
Muungano wakati huu wa kuandaa Katiba Mpya, ili kuirejesha Zanzibar mikononi
mwao.
Hata hivyo, umuhimu
wa Muungano huo unazidi kuwapo na kuonekana kama ambavyo hayati Mwalimu alikuwa
akisema mara kwa mara, kuwa mgawanyiko huo ukiruhusiwa Zanzibar haitakuwa
salama.
Mwalimu anasema: “Zanzibar ikijitenga kutokana na ulevi tu wa kusema Sisi Wazanzibari
na wao Watanganyika, wakumbuke kuwa Muungano ndiyo unaowafanya wanasema ‘Sisi
Wazanzibari na wao Watanganyika’, nje ya Muungano hawawezi kusema hivyo: Kuna
‘wao Wapemba na wao Waunguja.”
Pamoja na haki ya
kutoa maoni waliyo nayo wananchi wa Tanzania, sioni kama ni busara kuuvunja
Muungano. Suluhisho pekee ninaloliona ni kuondoa kero zake lakini si
kuuvunja bali kuuimarisha.
Kutokana na umuhimu
wake, ndiyo maana hata kwenye mchakato wa Katiba suala la Muungano halitaguswa
kwa maana ya kuuvunja.
Katika Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba Muungano ni moja ya vipengele nyeti ambavyo
havitagusa Katiba Mpya, lakini mjadala wake unazidi kuwa moto hasa upande
wa Zanzibar.
Kama ni Mtanzania
na unayo mapenzi na Kisiwa cha Zanzibar tafakari sana uamuzi ambao utakuwa
umeufanya, ili usije kuwa mfano wa visiwa mbalimbali vinavyojuta na kuitafuta
amani bila mafanikio.
Chanzo cha Habari: Mwananchi
Kwa maelezo zaidi
kutoka Mwananchi bonyeza hapa: Zanzibar Ni Kwetu
No comments:
Post a Comment