Rais
wa kwanza wa Afrika Kusini,Mzee Nelson Mandela
Imeandikwa na Francis Godwin wa http://francisgodwin.blogspot.com
Leo Jumatano, 18
Julai ni kumbukumbu ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, rais wa kwanza wa Afrika
Kusini ya Kidemokrasia (18.07.1918). Kadri ya kumbukumbu zangu huyu ndiye mtu
pekee ambaye Umoja wa Mataifa umemtengea siku katika mwaka mahususi kwa heshima
yake. Hivi leo anatimiza miaka 93 toka azaliwe; ni mmoja kati ya viongozi
wachache wa Afrika ambao wameishi kwa muda mrefu.
Nelson Mandela ni
mtu anayepewa heshima kubwa duniani kote kwa wanaomfahamu na hata wasiomfahamu.
Watu wengi hasa nje ya Afrika hususani katika jamii zinazopenda kusoma vitabu
wanamfahamu kupitia kitabu chake cha "Long Walk to Freedom". Hiki ni
kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake kwa kina kabisa. Sehemu kubwa ya
kitabu hicho ameandika yeye mwenyewe na tena akiwa gerezani.
Hili ni moja
ya mambo ya kujifunza toka kwa mzee huyu-maktaba kubwa duniani kote. Tujipange
tuandike historia zetu sahihi ili kuiachia jamii na dunia kwa ujumla utajiri wa
mawazo kama alivyofanya mzee Mandela. Wengine tulimfahamu mzee Madiba toka enzi
za utoto; tukiwa shule ya msingi tuliimba nyimbo za kutaka Mandela aachiwe huru
na serikali ya makaburu. Utawala wa makabulu ulitawala Afrika Kusini kwa mabavu
na kwa misingi ya kibaguzi ya rangi za binadamu; ni udhalimu wa aina yake kwa
ustawi wa wanadamu.
Kwanini mzee huyu
ni maarufu?
Kwa hakika sifahamu
yote juu ya mzee huyu anayependwa mno si tu kwake huko Afrika Kusini bali pia
duniani kote kwa ujumla, hilo ladhihirika kwa Umoja wa Mataifa (UM) kumtengea
siku maalum ya kumuenzi.
Mandela, alifungwa
katika magereza tofauti kwa jumla ya miaka 27; umri wa kijana aliyekomaa.
Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa pia Mwanasheria, mwanamichezo na mpigania haki
za watu, alifungwa na serikali ya Makaburu kwa walichokiita uhaini.
Nelson Mandela moja
ya vijana walionzisha madai ya uhuru kwa njia ya mapigano alikuwa na imani kuu
juu ya haki sawa kwa watu wote. Aliamini na anaamini kuwa binadamu wote ni sawa
katika misingi ya ubinadamu- kwa haki na mahitaji yetu. Ni kwa imani na msukumo
huo wa kudai uhuru na haki za watu wote wa Afrika Kusini ndo alikuwa tayari
kudai haki hizo hata kama ingemlazimu kuyatoa maisha yake; funzo kubwa hilo.
Kwa hakika imani
juu ya haki sawa kwa watu wote ni funzo na changamoto kubwa kwa viongozi wote
duniani. Nini imani yako wewe kiongozi juu ya haki sawa kwa wananchi
unaowaongoza? Ni dhahiri kuwa unatambua kuwa wananchi wako wote wanahitaji
chakula cha kutosha, makazi, huduma muhimu za kijamii; afya, elimu, na
kadhalika (nk).
Lakini tunacho
kishuhudia hii leo ni ubinafsi mkubwa wa viongo na hata wananchi wengine wenye
nafasi bila kujali mahitaji ya wengine wenye haja ya vile vitu tu vya msingi.
Wasomi wengi katika nchi zetu zinazoendelea tunahangaika na mahitaji ya ziada
ila hali kuna wenzetu wengi tu wasio na mahitaji yao ya lazima. Tukitaka
kutambulika vyema hapa duniani ni lazima tujifunze kwa mzee Mandela kujisahamu
kwa ajili ya wengine.
Baada ya kuachiwa
huru mwaka 1990 alirejea kwenye harakati za kudai haki za Waafrika Kusini walio
wengi. Mwaka 1991 alichaguliwa rais wa "African National Congress"
ANC Mandela alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya kidemokrasia
mwaka 1994. Alitumikia muhula mmoja tu wa miaka mitano na mwaka 1999 kuacha
mamlaka ya dola kuu kabisa kiuchumi barani Afrika. Utaona kuwa Mzee Madiba
alifanya kinyume kabisa na viongozi wengi wa barani mwetu.
Suala kuu ambalo
dunia imejifunza toka kwa mzee huyu wa miaka 93 sasa ni moyo wa msamaha. Kumbe
hata kwa binadamu msamaha unawezekana. Msamaha huu umeongozwa na busara kuu
bila shaka na neema tele za Mwenyezi Mungu.
Rais Nelson
Mandela angeweza kabisa kulipa kisasi cha Waafrika Kusini weusi wengi
waliopoteza maisha kwenye harakati za kujikomboa, lakini hakufanya hivyo,
alisamehe na badala yake aliwaunganisha wananchi wote wa Afrika Kusini mpya,
ingawa kuna vidonda vingi na makovu watakayoishi nayo daima, na kuanza kuijenga
nchi yao kwa manufaa yao wote.
Hii ni changamoto
kuu kwa wanadamu wote - nadhani ni sababu hii hasa ndo imeulazimu Umoja wa
Mataifa kuanzisha siku mahususi kumuenzi mpigania haki za binadamu Nelson
Mandela Madiba. Kwa hakika Madiba ni mjenga dunia!!!
No comments:
Post a Comment