WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, July 15, 2012

Dalili Ya Mvua Ni Mawingu. Afrika Mvua Hainyeshi Ghafla...!



Na Maggid Mjengwa
DALILI ya mvua ni mawingu. Afrika mvua hainyeshi ghafla Mwenye kutamka kuwa mvua imenyesha ghafla, huyo hajajisumbua kuangalia juu mawinguni. Afrika hata kusanyiko la mawingu ya mvua lina dalili zake. Wazee wetu wa zamani walikuwa na maarifa ya kuona dalili za kusanyiko la mawingu ya mvua. Ninachotaka kusema hapa ni hiki; kila jambo dalili.

Na tunapokumbushana umuhimu wa kusoma alama za nyakati hatuna maana ya kuziangalia saa zetu za mikononi au ukutani. Ni kuyaangalia matendo yetu ya sasa na hivyo basi umuhimu wa kuzisoma dalili za mambo yatakayotokea.
Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Tuna lazima ya kuwa na uchungu wa nchi yetu tuliyozaliwa. Ubinafsi na tamaa ya kujilimbikizia mali kwa baadhi yetu imepelekea dhahma kubwa kwa mamilioi ya watu wa nchi hii.

Miaka 50 baada ya uhuru wetu bado walio wengi wanaishi katika umasikini mkubwa wakati wachache, na si wakoloni, bali Watanzania wenzetu, kwa uchoyo wao na zaidi kwa ubinafsi wao. Wanaishi maisha kama wapo peponi, na hawaoni soni wakati Watanzania wenzao wakitaabika kwa umasikini. Tusisubiri mambo yakaja kuharibika na yakatokea ‘ mafuriko’ ya kijamii, kisha tukatamka; “ Ni ghafla tu!” Yatakuwa ni matokeo ya uvivu wetu wa kuangalia dalili za mvua. Naam, Afrika mvua hainyeshi ghafla.

Sote, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na kiimani, tuna lazima ya kufanya juhudi za makusudi za kujikomboa kutoka kwenye hali hii. Kama taifa, tunahitaji kujikomboa kiuchumi. Tuanze sasa kujenga misingi ya kujitegemea kiuchumi kama taifa. Tuanze sasa kuwaandama wale wote wasio tayari kugawana rasilimali zetu kwa usawa na haki.

Wale wenye kujiona kuwa wanastahili kupata zaidi ya wenzao. Na kamwe hatuwezi, na ni mkakati wa kimakosa, kuliacha jukumu hili la kujikomboa kiuchumi kwa Serikali pekee, au kwa chama na rais aliye madarakani. Ni jukumu letu sote kushiriki vita vya kujikomboa kiuchumi. Tuanze sasa kazi ya kujenga taifa lenye kujitegemea kiuchumi.

Kuna maeneo mengi ya kuyafanyia kazi ili tupate nguvu kazi iliyo bora ya kuweza kushiriki harakati hizi. Eneo muhimu kabisa ni ELIMU. Tuanze sasa na kuufanyia mageuzi na kuuboresha mfumo wetu wa elimu, kuanzia shule za msingi hadi Vyuo Vikuu.

Bila kuuma maneno, elimu yetu ya msingi ambayo ndio msingi wa elimu, iko katika hali mbaya sana. Kuna haja ya kufikiria uwepo wa mfumo utaofanya elimu ya darasa la kwanza hadi kumi na nne iwe ni ya lazima na itolewe bure. Kwamba mzazi awe na uhakika wa mtoto wake kusoma kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne katika shule moja.

Maana, katika hali ya sasa, zaidi ya nusu ya watoto wanaishia darasa la saba wakiwa na miaka kumi na nne, na bila kuwa na uwezekano wa kwenda mbele. Hawa bado ni watoto, kuwaacha wakizurura mitaani wakiuza karanga si kuwatendea haki. Na kama taifa, tunapoteza nguvu kazi ambayo kama ingepewa fursa ya kufika hadi kidato cha nne, ingeweza kutoa mchango wa maana kwa nchi na hata kwa familia wanazotoka.

Ndio, tuanze na kuimarisha elimu ya msingi. Wakati fulani nilitembelea Shule ya Msingi Nduli mkoani Iringa. Ni umbali wa nusu saa kwa gari kutoka Iringa Mjini. Nduli iko Isimani. Pale niliwakuta watoto 120 wa darasa la kwanza wakiwa wamebanana katika darasa moja na mwalimu ni mmoja.

Hakika, madarasa kama hayo yako mengi katika nchi yetu. Watoto wetu hawa baadhi yao watakuja kuwa viongozi wa kesho wa taifa hili , hawastahili kuandaliwa katika mazingira ya namna hii.
Ebu tujiulize; hivi ni nini maana ya sisi kwenda shule na kushindwa kuwasaidia maelfu kwa maelfu ya watoto wa nchi hii kupata elimu bora ya msingi katika mazingira bora?

Ndio, tumekuwa wepesi sana wa kusahau tulikotoka. Wepesi sana wa kuwasahau tuliowaacha nyuma tulikotoka. Tuna wajibu wa kuuchukua. Kuukataa wajibu huo ni kuisaliti nchi yetu tuliyozaliwa. Ni aibu.

Mtanzania Profesa Joseph Mbele alipata kuchangia mada hii ya elimu niliyoianzisha mtandaoni. Profesa Mbele anaandika; “Hii inasikitisha, na ndio hali halisi sehemu nyingi za Tanzania. Wananchi hawatilii maanani taabu hii na serikali haitilii maanani. Nawalaumu wananchi, na nailaumu serikali”.

Hapo Iringa kuna baa nyingi zenye viti na meza nzuri, au makochi mazuri, watu wanataka hali hiyo. Hakuna mteja atakayeridhika iwapo meza na viti vilivyoko baa vitahamishiwa shuleni, na wanywaji wakae sakafuni au wanywe wakiwa wamesimama. Haikubaliki. Walevi wanastahili kukaa kwenye meza na viti, lakini watoto wakae chini.

Sherehe haziishi hapo Iringa, kama ilivyo katika nchi nzima. Michango ya sherehe ni mamilioni, na kreti za bia hazihesabiki. Lakini hakuna anayewazia kuchangia madawati, vitabu, au kalamu na daftari, kwenye hiyo shule. Mashindano ya urembo yanafanyika hapo Iringa, kama ilivyo katika sehemu zingine nchini, na watu wanatoa pesa nyingi kuhudhuria mashindano hayo. Hakuna anayewazia kutoa hela kama hizo kuchangia hiyo shule.

Kuna wakati tulisikia kwamba watu kadhaa wamechanga Sh200 milioni kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi. Moyo huu ungeelekezwa kwenye michango ya shule, shule zote nchini zingekuwa na hali nzuri. Hata hapo Iringa, ukipita mchango wa kampeni ya uchaguzi, mamilioni yatachangwa

Miaka kadhaa iliyopita, pia tulisikia kuwa CCM imeagiza magari 200 kwa ajili ya uchaguzi. Pesa hizi zingetosha kuiweka shule ya Nduli katika hali bora kwa kila namna, na ingetosha kuziboresha shule nyingi katika mikoa mbali mbali.

Vigogo wanapovinjari humo mikoani wanakuwa na misafaraya magari mengi. Gharama yake ni kubwa sana na ingetosha kuiboresha hii shule ya Nduli na shule nyingi nchini.

Ningeweza kuendelea kuandika, kuthibitisha kwamba hali ngumu ya hii shule ya Nduli na shule nyingi nchini, inasababishwa na kuendekezwa na wananchi na serikali.

Fedheha iliyopo Tanzania ni kuwa wafadhili kutoka Ulaya na Marekani wakishaona hali ya hizi shule zetu, wanajituma kuchangia na kuboresha hali. Watu wa Ulaya na Marekani wengi wako Tanzania wakifanya shughuli hizo. Wanachangisha hela huku kwao, pamoja na matatizo ya uchumi yalivyo, ili walete misaada kwenye shule zetu huko Tanzania.

Sisi wenyewe tunaendelea na bia, sherehe, na makamuzi mengine. Na viongozi wetu wanaona heshima kuwa wageni rasmi wakati misaada kutoka ughaibuni inapoteremshwa nchini. Na viongozi hao wanakuja kwenye shughuli hizo wakiwa na mashangingi ya bei kubwa, wakati wanaotoa misaada huku ughaibuni aghalabu hawana uwezo wa kununua mashangingi ya aina hiyo.” Anaandikia Profesa Joseph Mbele. Naam. Mjadala huu haujafungwa.

0788 111 765 /0658 111 765
mjengwamaggid@ gmail.com,
http://mjengwa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment