WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, July 5, 2012

Miaka 20 Ya Vyama Vingi; Upinzani Bado Ni Sawa Na Uadui! ( Makala Yangu Raia Mwema)



Na Maggid Mjengwa,

MIAKA 20 iliyopita, yaani Julai 2, 1992, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya kuruhusu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Miaka 20 imetimu, tumepiga hatua, lakini, mpaka hii leo, bado upinzani kwa wengine unatafsiriwa kama ni uadui, na wakati mwingine ni uhaini.

Na katika Tanzania yetu,  wenye fikra za kukipinga chama tawala, CCM na Serikali wamekuwa wakitengwa na hata kupewa majina mabaya. Nimeshawahi kumsikia mtu akiambiwa;

“ Alaa, unaongea na Lipinzani hilo!” Kana kwamba aliyeitwa ‘ Lipinzani’ hakuwa Mtanzania na binadamu kama wengine.
Hakika, katika kujadili hili la Katiba mpya, tuna kila sababu ya kuipitia historia yetu. Maana, naamini, kuwa historia ni mwalimu mzuri.

Itakumbukwa, katikati ya vuguvugu lile la mageuzi ya kisiasa miaka ya 90 mwanzoni, Watanzania zikatufikia habari; kuwa Oscar Kambona, aliyekosana na Nyerere na aliyekimbila uhamishoni Uingereza, alikuwa njiani kurudi nyumbani. Ujio wa Oscar Kambona ukawa gumzo la mjini na nje ya jiji. Kuna waliojiandaa kwenda uwanjani kumpokea.

Usiku mmoja ikasikika sauti ya Augustine Mrema redioni. Sauti ya Waziri wa Mambo ya Ndani. Mrema alitamka, kuwa kama Kambona angekanyaga mguu wake Dar es Salaam, basi, angekamatwa kujibu mashtaka ya uhaini.

Ni hofu ile ile ya serikali hata wakati huo. Hofu ya kuimarika kwa fikra za upinzani na kukua kwa upinzani. Mrema akatumika au akajituma kuwatisha na kuwakatisha tamaa Watanzania. Kambona alikanyaga Dar es Salaam, hakuwa na mashtaka ya kujibu. Ulikuwa ’ mkwara’ tu, kama wanavyosema mitaani.
Na Mrema, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliifanya kweli kazi ya kuwa ’ Mbwa wa Serikali’. Alibweka kweli kweli

Nakumbuka usiku mmoja mwanzoni mwa miaka ya 1990 nilimsikia Mrema akizungumza redioni kutishia maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF). Maandamano yale yalikuwa yahitimishwe kwa mkutano viwanja vya Mnazi Mmoja. Mwenyekiti wa CUF, James Mapalala, ndiye alikuwa aongoze maandamano hayo na kuhutubia.

Mrema akaaunguruma redioni usiku ule. Alishushamkwaramzito. Kuwa maandamano hayo si halali na yangekutana na nguvu za dola. Kesho yake, CUF waliingia mitaani. Ndiyo, Ungangari wa CUF ulianza siku nyingi.

Pale Mnazi mmoja FFU wakamwagwa, na farasi wao pia. Virungu vilitembea. James Mapalala, Mwenyekiti wa CUF, hakuonekana. Kukawa na taarifa, kuwa anatafutwa na Polisi.
Dar es Salaam ilikuwa ndogo wakati huo, lakini James Mapalala hakupatikana. Taarifa zinaashiria kuwa James Mapalala alikuwa amejificha kwenye moja ya makazi ya rafiki yake, balozi wa nchi moja ya Kimagharibi. Ni balozi gani huyo? Na nini hasa kilitokea miaka 20 iliyopita?

James Mapalala yungali hai. Huu ni wakati kwa waandishi vijana kuwatafuta wazee veterani wa harakati za mageuzi ya kisiasa hapa nchini. Wazee kama akina James Mapalala.

Hawa ni watu muhimu sana watakaotusaidia kupokea simulizi zao. Kisha ziwekwe kwenye maandishi, na iwe kumbukumbu za kihistoria. Ni historia yetu, tusiionee aibu. Ni urithi tutakaowaachia wajukuu zetu ili nao waweze kujifunza. Waweze kujitambua na kujenga mioyo ya uzalendo.

Nimepata kuandika, kuwa tumedhamiria kuifanyia marekebisho makubwa Katiba yetu. Tufanye hivyo tukiwa na dhamira njema na mapenzi kwa nchi yetu. Nimepata kuandika, kuwa katika hili la Katiba tujiulize; Je, Katiba yetu ya sasa, na kwa wakati uliopo, inakidhi matakwa ya shabaha na malengo yetu kama Taifa? Jibu langu ni HAPANA.

Na katika hili hatuna sababu za kugombania fito ilihali nyumba tunayojenga ni moja na ni yetu sote. Ieleweke, kuwa huko nyuma, madai ya Watanzania kupata Katiba mpya yamekuwa ni madai ya haki, muhimu na ya kihistoria. 

Tumewasikia hata wanaojidanganya, wakiandika, kuwa madai hayo yalitokana na ‘ Njama za Mabeberu!’. Hizi ni propaganda za miaka ya 70, zimepitwa na wakati.

Ni busara kutambua, kuwa wakati umebadilika. Mtanzania wa mwaka 1977 si Mtanzania wa mwaka 2011. Hoja hii ya Katiba si kama inzi anayetua na kuruka. Hoja ya Katiba kwa sasa inaongozwa na kundi kubwa la vijana wanaotaka mabadiliko. Hawa si inzi wanaotua na kuruka, ni siafu wanaokuja kwa kuongezeka idadi yao.

Na harakati za Watanzania kutaka marekebisho ya Katiba zina muda mrefu. Hizi si harakati mpya. Si harakati za chama au kikundi kidogo cha ’wapinzani’ wasioitakia mema nchi hii. Siku zote, yamekuwa ni madai ya msingi ya Watanzania, bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kidini, rangi na makabila.

Kama ni shauri mahakamani, basi, lilishafunguliwa zamani. Kinachofanyika sasa ni mwendelezo wa shauri. Si wengi, miongoni mwa vijana wa sasa, wenye kumbukumbu ya ukweli huu. 

Tayari mwaka 1991 vuguvugu la kudai vyama vingi na Katiba mpya lilikwishakuanza. Wakati huo madai makubwa yalikuwa mawili; vyama vingi na Marekebisho ya Katiba. Kuna mnaokumbuka ’ KAMAKA’- Kamati ya Marekebisho ya Katiba iliyoundwa na wanaharakati. Ikumbukwe, kuwa hayo yalikuwa ni madai ya Watanzania ndani ya mfumo wa chama kimoja.

Chifu Abdallah Fundikira aliongoza Kamati iliyoundwa, si na Serikali, bali wanaharakati, kuratibu mchakato wa kudai vyama vingi na Katiba mpya.

Hata wakati huo, Mzee Ali Hassan Mwinyi, kama Rais, aliweka ‘ mkwara’, kuwa madai hayo yasiendeshwe na watu au makundi ya watu bila kibali cha Serikali. Presha ya madai ilipoongezeka, tunakumbuka, kuwa Mzee Mwinyi aliweza kusoma alama za nyakati. 

Alizungumza pale Chuo Kikuu Mlimani na kuweka bayana dhamira ya Serikali ya kuunda ‘ Tume ya Nyalali’ . Tume hiyo ilizunguka nchi nzima kuwauliza Watanzania kama wanataka kuendelea na Chama kimoja au Vyama vingi.

Itakumbukwa, Chifu Fundikira alipata kutamka; kuwa huko ni kupoteza muda na fedha za wananchi. Itakumbukwa pia, Mabere Marando alikuwa Katibu wa Kamati ile ya wanaharakati ya kuratibu mchakato wa madai ya kuwapo na vyama vingi na marekebisho ya Katiba.

Marando alipata kutamka na kunukuliwa na Daily News, April, 12, 1991; “ We have a bad political system because our Constitution embraces political discrimination. What we want is that all of us should shout out that our Constitution is bad.” ( Mabere Marando, Daily News, April 12, 1991)
Tafsiri; “ Tuna mfumo mbaya wa kisiasa kwa sababu Katiba yetu ina ubaguzi wa kisiasa. Tunachotaka, ni sote, tupige kelele, kwamba katiba yetu ni mbaya.”)

Marando aliyasema hayo katika Semina ya kwanza ya Kamati ya kuratibu mchakato wa madai ya vyama vingi na Katiba mpya iliyoongozwa na Chifu Fundikira. Semina hiyo ilihudhuriwa na watu wapatao 800 kwa mujibu wa taarifa ya Daily News la April 12, 1991.

Na akina Chifu Fundikira waliandamwa sana na Serikali na chama tawala. Kwa mujibu wa Daily News la April 26, 1991, Mbunge wa Shinyanga, Paulo Makolo alimshambulia Fundikira kwa kusema kuwa , katika hilo la kuwa na vyama vingi na katiba mpya , Chifu Fundikira hakuwakilisha mawazo ya Wasukuma na Wanyamwezi wenzake.

This is not a Wanyamwezi and Wasukuma movement. It is the selfish interests of Fundikira and his ten colleagues. Our people are not after parties. They want food, water, education and health care.” ( Paulo Makolo, MP, Shinyanga, Daily News, April 26, 1991).

Mwenyezi Mungu umrehemu Chifu Abdalah Fundikira na wote wengine waliosimama kidete kuipigania nchi yetu.

No comments:

Post a Comment