WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, May 2, 2012

Hotuba Ya JK Tanga Na Furaha Ya Rais; Tafsiri Yangu




Ndugu zangu,

Mwaka huu nilipata kumfundisha mwanahabari kijana namna ya kufungua blogu. Nikamwelekeza kwa kutumia mfano, namna ya kuweka picha kwenye blogu yake mpya niliyomsaidia kujifunza namna ya kuifungua. Nikachagua picha ya mwanasiasa kijana wa CCM, nikaiweka kwenye blogu yake.

Nilipomaliza, akaniomba haraka sana nimfundishe namna ya kuondoa picha kwenye blogu yake. Hakutaka kabisa picha hiyo ya mwanasiasa kijana wa CCM ikae kwa muda mrefu kwenye blogu yake. Akanitamkia; kwa kweli sitaki kabisa kuwaona hawa jamaa kwenye blogu yangu.

Kiukweli, vijana wengi kwa sasa  wanaichukia CCM, na labda zaidi, wanauchukia ufisadi, na wanawachukia viongozi mafisadi na  ambao wanaamini wanalelewa na wanalindwa na CCM. Ndio maana ya vijana wengi leo kuchukia chochote kile kinachohusu CCM, ikiwamo rangi ya kijani.

Jana usiku nilisikiliza kipindi maalum TBC1 kilichorusha hotuba ya JK ya Mei Mosi aliyoitoa Tanga.
Tafsiri yangu;

Hakika, ni moja ya hotuba bora za JK alizopata kuwahutubia Watanzania.
 Ni yenye kutoa matumaini kwa wengi na yenye kuwasuta wanafiki wachache walio ndani ya chama chake. JK akiendelea kwa staili ile, basi, anaweza kuanza kuibadili mitazamo ya wengi juu yake, mitazamo ambayo kwa sasa mingi ni hasi.

Na JK akatamka, kuwa yale ya Dodoma  ( Bungeni) hayakumsikitisha wala kumfadhaisha, badala yake yamemfurahisha. Yumkini JK anajihisi kuanza kuutua mzigo. Lakini, furaha yake yaweza kuwa ya muda mfupi kama asipokwenda, kwa vitendo, mbali zaidi na kushiriki kazi ya kweli ya kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye hali ya sasa ikiwamo kudhalilishwa hata kwa kuhongwa pilau kwenye chaguzi kutokana na njaa zinazotokana na  viongozi na watendaji ' mapanya' wanaotafuna mali ya umma.

Nilimwona jana, JK anayejiweka mbali na ’ madudu’ yaliyoainishwa na CAG na yaliyowafanya baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM wachachamae Bungeni na hata kufikia hatua ya kuweka saini zao kushinikiza mawaziri wajiuzuru.
JK alichowaambia Watanzania jana ni kuwa yuko pamoja nao kwenye kilio chao cha ufisadi uliokubuhu  na unaofanywa na viongozi na watendaji waliopewa dhamana ya kulinda rasilimali za umma.

JK anasema- Kule kwenye halmashauri fedha zinatafunwa utadhani hazina mwenyewe! Ametumia lugha ya mtu wa kawaida na kwa kweli hicho ndicho ambacho umma umekifahamu kwa siku nyingi na Chadema ndio imeonekana kuwa mtetezi wao anayewasaidia kupambana na wezi wao. Hivyo basi, ni moja ya sababu ya kuongezeka kwa umaarufu wa Chadema na kupungua kwa kasi, umaarufu wa CCM. Maana, Chadema sasa ndio inaonekana kuwa ni kimbilio la wanyonge.

Kwa hotuba ile ya jana, JK ana fursa njema sasa ya kujiwekea legacy. Yale ya kukumbukwa nayo hata baada ya kuondoka madarakani; kusimama upande wa umma na kushiriki kwa vitendo kuwaandama viongozi na watendaji waliojigeuza miungu watu na huku wakishiriki wizi wa mali ya umma.  Na wengi wao wamo ndani ya CCM, au wanalindwa na CCM, Chama tawala.

Maana, 
wahenga  walinena; kila jambo lina dalili. Na nimepata kuandika, kuwa Afrika mvua hainyeshi ghafla, huanza na  mawingu kujikusanya. Ndio maana ya umuhimu wa kusoma alama za nyakati. Na kwenye nyumba panya huanza na shimo moja. Na mashimo ya panya yakiongezeka, basi, mwenye nyumba huwa na  kazi ngumu kupambana na panya hao.


Na huko nyuma nimepata kuandika, kuwa kuna wachache ndani ya CCM ambao Chama wamekigeuza kuwa ’ Shimo la Panya’- watoke wakatafune mali ya wananchi, kisha wakimbilie shimoni kwa maana ya kwenye chama. Na shimoni ndiko kwenye ’ kulindana’. Na hii ndio sababu ya msingi ya kupungua umaarufu kwa chama hicho tawala miongoni mwa Watanzania na hususan kundi kubwa la vijana.

Maana, ni ukweli, wengi wanaotuhumiwa kushiriki  ufisadi wamo ndani ya Chama tawala . Ni  wenye  mahusiano mazuri au kama inavyosemwa siku hizi, ni ’ marafiki’ wa CCM. Naam , hivi ni vijipanya tu  ni vyenye  ’vijishimo vyao’  ndani ya CCM. Si tumepata kusikia ikitamkwa; ” Ukitaka biashara yako ikunyokee, njoo CCM!”

JK wa sasa anaweza kuweka historia kwa kuongoza kazi ya kuondokana na ubaguzi wa kisiasa katika nchi yetu.  Ubaguzi huu wa mathalan, ’ Hawa ni wenzetu’ na ’ Wale ni maadui zetu’ umejengeka katika misingi ya kulindana katika maovu.  Wenye kuendekeza ubaguzi huu  ndio wenye kugombania fito wakati tunajenga nyumba moja.  

Jeffrey Sachs ni Mwanauchumi maarufu na ambaye JK amepata kukutana na kuongea naye kwenye Ikulu yake. Profesa Jeffrey Sachs ana mfano hai wa Poland.  Katika kuwashauri  kuinuka kiuchumi WaPoland wale , Profesa Sachs aliwaambia; ” Political power must be shared”.  Kwamba kuna umuhimu wa vyama kuwa na utayari wa kugawana madaraka ya uongozi wa kisiasa.

Ndio, Fundi Umeme yule Lech Walensa wa chama cha wafanyakazi na aliyeanzisha vuguvugu la mapinduzi ya kujikomboa kutoka Ukomunisti nchini Poland aliambiwa na Profesa Jeffrey Sachs; ”  Chama chako cha Solidarity kiwe radhi kuunda Serikali ya Mseto na Chama Cha Kikomunisti”. Na ikawa hivyo, kimoja kikatoa Waziri Mkuu na kingine Rais.  Kukawepo utulivu wa kisiasa. Poland ikaanza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi. Ndio, hakuna uchumi unaokua bila uwepo wa utulivu wa kisiasa.

Maana tunakumbuka siku ile JK alipotangaza mpango wa kiuchumi wa miaka mitano kule Dodoma, JK alitamka;  " Bila Utawala Bora , bila kuwa na demokrasia, bila kuheshimu Haki za Kibinadamu,  mafanikio ya kiuchumi hayatawezekana."

Rais  hakupigiwa makofi  ya nguvu. Ndio, wengi wa viongozi waliokuwa wakimsikiliza JK kwenye ukumbi ule wa Saint Gasper pale Dodoma ni Wana-CCM. Bila shaka kuna waliokuwa wakifikiria Ukuu wa Wilaya wao na Ukuu wao wa Mkoa. Walifikiria nyadhifa  zao. Mambo ya kupanua demokrasia ikiwamo uwepo wa  vyama vingi  kwao ina tafsiri ya kutishia vibarua vyao!

Nimepata kuandika;  kama kwenye nyumba yako umeingiliwa na panya wanaotafuna  vyakula na hata akiba yako ya nafaka, basi, mwenye nyumba una mawili ya kufanya; kusalimu amri na kuwaacha panya hao watafune mpaka nguo unazovaa au kuchukua hatua ya kupambana na panya hao.  Na kama panya ni wengi dawa ni kuitafuta sumu ya panya.

 Na nchi ni hivyo hivyo, swali ni hili; tunafanyanye , pale panya wachache,  kwa kutumia chama cha siasa kama shimo la kujifichia tunawaona  wakitafuna  mali za  wananchi usiku na mchana?

 Jibu; KATIBA MPYA ndio ’Sumu ya panya ’ tunayoihitaji  sasa kupambana na panya wachache wanaoitafuna nchi yetu. Panya hawa wakijua kuwa kuna Jaji wa Mahakama ambaye hakuchaguliwa na Rais wa chama chao bali kaidhinishwa na Bunge la wananchi, basi, wataogopa hata kuiba kalamu za ofisini.  Ndio, mengine yote nje ya kukaa chini kama taifa na kuandaa Katiba Mpya itakayotokana na wananchi ni  sawa na kutwanga maji kwenye kinu. 


Maggid Mjengwa,

Habari  kwa Hisani ya Mjengwa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment