WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, January 9, 2013

Warioba: Marufuku kuripoti maoni ya makundi maalum



Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetamka rasmi kuwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano yake na makundi maalum, vikiwamo vyama vya siasa, inayoendelea kwa lengo la kukusanya maoni ya Katiba Mpya.

Kwa kauli hiyo ya Tume hiyo, sasa itategemea huruma na hisani ya makundi, ambayo yatakuwa tayari ‘kuwatafunia’ na ‘kuwalisha’ wanahabari mambo yaliyojiri, badala ya wao wenyewe kuyapata moja kwa moja na kwa uhalisia wake kutoka ndani ya mikutano hiyo.


Kauli ya kuwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano hiyo, ilitolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kuanza mkutano kati ya tume yake na Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD).

Jaji Warioba alitoa kauli hiyo alipoulizwa na NIPASHE kama waandishi wa habari wangeruhusiwa kuingia ukumbini kusikiliza maoni ya UMD.

Alijibu kwa kifupi kwamba waandishi wa habari hawaruhusiwi kuhudhuria siyo tu katika mkutano huo juzi, bali katika mikutano yote kati ya Tume na makundi yote.

“Hamuwezi kuingia ukumbini (kwenye mkutano) kusikiliza maoni yanayotolewa. Siyo tu tuliwazuia jana (juzi), bali hata leo (jana). Pia na siku nyingine hamtaruhusiwa kushiriki,” alisema Jaji Warioba.

Mikutano kati ya Tume na makundi hayo ilianza juzi katika ofisi za Tume hiyo na katika kumbi tofauti za jengo la Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Katika ofisi za Tume, mikutano hiyo inaongozwa na Jaji Warioba pamoja na mjumbe wa Tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu.

Katika kumbi za jengo la Karimjee, baadhi ya mikutano inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Augustino Ramadhan na maofisa wengine wa Tume hiyo.

Katika mikutano yote hiyo, baadhi ya maofisa wa Tume, wamekuwa wakiwazuia waandishi wa habari kuhudhuria.

KAULI YA WARIOBA INAKINZANA

Kauli ya jana ya Warioba inakinzana na ile aliyoitoa juzi aliposena kwamba, waandishi wa habari walizuiwa kuhudhuria mkutano wa kutoa maoni kati ya Tume yake na Chama Cha Wananchi (CUF), kutokana na ukumbi uliotumika kufanya mkutano huo kuwa finyu.

Pia ilikinzana na ile iliyotolewa na Naibu Katibu wa Tume hiyo, Casmir Kyuki, aliyoitoa kwa waandishi wa habari katika viwanja vya Karimjee juzi kwamba, ni utaratibu wa Tume kwamba, wanapokutana na makundi hayo, hawafanyi mikutano ya wazi.

“Na hawa (vyama vya siasa) waliitwa na Tume kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa baadhi ya mambo. Utaratibu wake unatoa fursa kwa wajumbe wa Tume kuuliza maswali, kwani kuna baadhi ya mambo, ambayo wamekutana nayo wananchi waliyoyasemea,” alisema Kyuki.

Alisema awali, walipanga wasikutane na makundi hayo, kwa kuwa walitarajia kuwa wangekutana nayo katika mikutano waliyoifanya na wananchi mmoja mmoja, lakini wakaona kuwa uamuzi huo ungewafanya wakose kupata maoni muhimu, hivyo wakaamua kukutana nao.

 Kyuki alisema hawaamini kama kuwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano hiyo kunawanyima haki wafuasi wa vyama hivyo kupata maoni yanayowasilishwa na vyama vyao kwa Tume kwa kuwa vyama hivyo tayari vimekwishatoa misimamo yao siku nyingi kabla ya jana.

Hata hivyo, wakati Tume hiyo ikiwazuia waandishi wa habari kuhudhuria mikutano kati yake na makundi hayo, ilipoanza kazi yake mwaka jana, ilisimama na kuviomba vyombo vya habari kuisaidia kutoa taarifa kwa umma.

Katika mikutano yote ya Tume hiyo iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, mikoani na visiwani Zanzibar, vyombo vya habari havikuwahi kuzuiwa kuhudhuria.

Kipindi hicho wananchi mmoja mmoja walipokuwa wakitoa maoni yao kwa Tume kuhusu Katiba Mpya.

Hata hivyo, ugumu umeanza kujitokeza kwa sasa kwa makundi maalum.

WAANDISHI WALIPOANZA KUZUIWA
Kabla ya kauli hiyo ya Jaji Warioba kutolewa rasmi jana, waandishi wa habari walianza kuzuiwa kuhudhuria mikutano hiyo tangu juzi na baadhi ya watu waliojitambulisha kuwa ni waratibu wa mikutano kati ya Tume na makundi hayo.

Baadhi ya watu hao wamekuwa wakiwaambia wanahabari kuwa wamepewa maagizo hayo na Katibu wa Tume.

Hata hivyo, mwaka jana Jaji Warioba aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kutofika katika mikutano kati ya Tume yake na wananchi wanapokuwa wanatoa maoni yao kwa kuwa watawanyima uhuru wa kuzungumza.

Lakini kipindi hicho Tume haikuwahi kutamka kwamba, waandishi wa habari hawaruhusiwi kuhudhuria mikutano hiyo.

ATHARI ZA KUZUIWA WAANDISHI
Kuanzia juzi baadhi ya wawakilishi wa makundi maalum wanaokwenda kutoa maoni kwa Tume wamekuwa waoga kuzungumza na waandishi wa habari wanapomaliza mikutano yao na Tume.
Hatua hiyo imekuwa ikitafsiriwa kama ni “kufungwa midomo”.

ULINZI WAIMARISHWA KUWAZUIA WAANDISHI
Licha ya vyama vya siasa kuanza kutoa maoni yao kuanzia juzi, zipo taarifa kwamba, watumishi wa wizara, taasisi na mashirika ya umma, jana walianza kutoa maoni yao, huku ulinzi wa maofisa wa Tume ukiwa umeimarishwa ili kuhakikisha hakuna mwandishi wa habari yeyote anayefika katika kumbi wanapofanyia mikutano.

MIKUTANO YAFANYIKA KWA SIRI

Mikutano kati ya Tume na ujumbe wa vyama hivyo, kuanzia juzi imekuwa ikifanyika kwa siri tofauti na utaratibu uliokuwa ukitumiwa na Tume hiyo awali wa kuendesha mikutano ya kukusanya maoni ya mwananchi mmoja mmoja kwa njia ya wazi.

Hatua hiyo imekuwa ikizua maswali na manung’uniko lukuki kutoka kwa wananchi.

Kitendo hicho, ambacho kimekuwa kikishutumiwa na wengi, kinawafanya waandishi wa habari kulazimika kusubiri nje ya kumbi hizo huruma na hisani ya kupata kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa kilichojiri kwenye mikutano yao na Tume.

DK. BANA AMSHANGAA WARIOBA 

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema hakuna sababu kwa Tume hiyo kuzuia vyombo vya habari kuhudhuria mikutano hiyo.

Alihoji kuwa ni kitu gani kinachofichwa wakati makundi maalum yanapokwenda kutoa maoni tofauti na ilivyokuwa wakati wananchi wa kawaida wa mijini na vijijini walipotoa maoni yao na waandishi wa habari wakaruhusiwa kushiriki.

“Mheshimiwa Warioba na wenzake sijui wameshikwa na kitu gani mpaka kufikia hatua ya kuvizuia vyombo vya habari kushiriki katika mikutano hiyo. Kwani hivi sasa ni mazingira ya uwazi,” alisema Dk. Bana.

Alisema kama utaratibu wa kuzuia vyombo vya habari na kuwapo usiri ukiendelea, kuna hatari ya kupata rasimu ya katiba, ambayo haikutarajiwa na wananchi wengi kwa kuwa inaweza 'kuchakachuliwa' kisirisiri.

Alitaka vyama vya siasa vinavyotoa maoni yao kuweka wazi mfumo uliotumika katika kupata mawazo ya wanachama wao ili kuhakikisha kwamba, nao wameshiriki na hawakuburuzwa na kusemewa na viongozi wao waliofika katika Tume.

DK. BISIMBA: NI HATUA YA KUMINYA DEMOKRASIA
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen-Kijo Bisimba, alisema kitendo cha waandishi wa habari kuzuiwa kinaminya demokrasia na uhuru wa kupata taarifa.

Alisema hakuna sababu yoyote ya msingi inayomfanya Jaji Warioba kuzuia vyombo vya habari kushiriki katika kusikiliza na kutoa taarifa juu ya maoni yanayotolewa na makundi maalum katika jamii.

Akizungumza na NIPASHE juzi, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alilaani kitendo cha vyombo vya habari kuzuiwa nje wakati wao walipokaribishwa na Tume kwa ajili ya kutoa maoni yao.

NLD YAKATAA WAJUMBE WA TUME
Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema kuwa chama chake jana kilipata fursa ya kukutana na Tume na kuieleza kuwa wanachokifanya hakipaswi kuelezwa kuwa ni kutafuta katiba mpya, bali kuboresha katiba ya sasa.

Alisema jambo lingine alisema alilaumu kitendo cha Rais kuwateua baadhi ya watu katika Tume hiyo, kama vile Jaji Warioba, wakati ndiyo walioshiriki kutengeneza katiba ya sasa inayolalamikiwa kuwa ni mbovu.

Kwanini wasiweke wengine? Tume hiyo ilitakiwa ipatikane kwenye mkutano wa taifa. Wanawaongopea,” alisema Dk. Makaidi.

Alisema alishauri katiba mpya iimarishe utawala wa mikoa ili iwe na mamlaka ya kujiamulia mambo, iunde Baraza la Dini la Taifa ili waumini wajadili mambo yao, itamke idadi ya wizara, mikoa iongozwe na mawaziri, imnyime Rais uwezo wa kuteua wabunge badala yake raia wapewe uwezo wa kuamua kupitia kura ya maoni, uchaguzi wa Rais uhojiwe mahakamani na iwepo tume huru ya uchaguzi.


CCK: KURA YA MAONI KWANZA KUHUSU MUUNGANO
Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda, alisema chama chake kilikutana na Tume hiyo na kuieleza kuwa kabla ya kupendekeza Muungano wa aina gani unaotakiwa, iitishwe kwanza kura ya maoni kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar waamue kama wanataka Muungano uliopo uendelee au la.

Alisema wanataka kura hiyo ipigwe kwa kuwa Muungano umekuwa ukilalamikiwa muda mrefu.
Pia alisema walipendekeza kuwapo uhuru wa vyombo vya habari, mabunge mawili; la wananchi na seneti, ambalo uwakilishi wake utakuwa na uwiano kila mkoa na litakalokuwa likilisimamia Bunge la Wananchi.

Alisema jambo lingine walilopendekeza ni kutolewa ruzuku kwa vyama vya siasa na kuundwa kwa taasisi maadili itakayokuwa na uwezo wa kumchunguza hata Rais anapoingia na kutoka madarakani.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment