Chadema jana kiliwasilisha mapendekezo kadhaa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba; mojawapo kikitaka kuwapo kwa mfumo wa shirikisho wa serikali tatu kwenye Katiba Mpya.
Katika mfumo huo, Chadema kinataka kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika na Zanzibar, ambazo kila moja itakuwa na mamlaka kamili ya Rais, Bunge na Mahakama, na kuwapo pia kwa Serikali Ndogo ya Muungano.
Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Chadema iliyokutana na Tume hiyo jana, Tundu Lissu, alisema katika mapendekezo waliyoyawasilisha kwa Tume, wanataka Rais wa Serikali ya Muungano achaguliwe na wabunge wa Bunge la Tanganyika.
Pia achaguliwe na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, magavana, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya sekretarieti yake kukutana na Tume hiyo jana.
Wajumbe wengine waliounda sekretarieti hiyo, ni Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai); Zitto Kabwe (Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara na Mbunge wa Kigoma Kaskazini) na John Mnyika (Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema na Mbunge wa Ubungo).
Wengine ni Said Issa Mohammed (Makamu Mwenyekiti Chadema Zanzibar); Hamad Mussa Yussuf (Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar); John Mrema (Mkurugenzi wa Halmashauri na Masuala ya Bunge Chadema) na Profesa Kulikoyela Kahigi (Mbunge wa Bukombe).
Lissu alisema katika mapendekezo yao, wanataka kuwapo kwa pande mbili za Muungano haki ya kujitoa kwenye Muungano kwa sharti kwamba, wanaotaka hivyo, wapige kura ya maoni.
Alisema pia wanataka yabaki mambo saba pekee, ikiwamo linalohusu ulinzi na usalama katika Serikali ya Muungano.
Lissu alisema wanataka Rais wa Muungano akae madarakani kwa miaka mitano ingawa anaweza kuongezewa muda, lakini kuwapo na utaratibu wa kupeana zamu za urais kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Alisema Rais huyo pia ndiye atakayekuwa na mamlaka ya kutangaza vita, lakini ataruhusiwa kufanya hivyo baada ya kupata kibali cha Bunge na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Katika mapendekezo yao mengine, alisema wanataka kinga ya mashtaka ya jinai dhidi ya Rais iondolewe, na pia kuwapo na udhibiti mkubwa wa mamlaka ya Rais.
Alisema wanataka kila atakayeteuliwa na Rais lazima aombe kazi husika kwenye tume huru za kitaalamu na athibitishwe na Bunge.
Lissu alisema pia wanataka serikali iwe na wizara zisizozidi 18 na zisizopungua 15 na pia Bunge liwe na wabunge 250 na liwapo Bunge la majimbo litakalokuwa na wabunge 50.
Pia alisema katika mapendekezo yao, wanataka kila raia aliyetimiza umri wa miaka 18 awe na haki kuchagua na kuchaguliwa, na kwamba, lile sharti la awali la kutaka anayetaka kugombea urais lazima atimize miaka 40, wanataka lisiwepo.
Alisema pia kuwapo na utaratibu wa kila raia mwenye haki ya kupiga kura apige kura awe ndani au nje ya nchi, au awe huru au amedhibitiwa na vyombo vya dola.
Lissu alisema pia wanataka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) isiteuliwe na Rais kama ilivyo sasa, badala yake wanataka iwe tume huru yenye wajumbe 25.
Alisema katika wajumbe wa tume, 15 wapendekezwe na vyama vyenye uwakilishi katika Bunge na kwamba, wajumbe wengine wa NEC watoke kwenye chama cha mawakili wa Tanganyika, taaluma, taasisi zisizokuwa za kiserikali, vyama siasa, visivyokuwa na uwakilishi bungeni.
Lissu alisema wajumbe hao wakipatikana, watatakiwa kupelekwa bungeni kuthibitishwa na Bunge na kwamba, Mwenyekiti na Makamu wake wa NEC watateuliwa na wajumbe wa tume.
Kuhusu umilikaji wa rasilimali, alisema wanataka Katiba Mpya itamke kwamba,maliasili ni mali ya wananchi na kwamba, kama wananchi hawatatoa ridhaa isichukuliwe.
Pia alisema pia wanataka malipo ya mrahaba yapelekwe kwenye maeneo yaliko madini ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wapate asilimia 40 walipe kodi na asilimia 60 ibaki serikalini.
Alisema katika mfumo wa utawala, wamependekeza utaratibu wa kuwapo kwa mikoa na wilaya uliorithiwa kutoka kwa wakoloni uondolewe, kwa madai kwamba, mikoa na wilaya zimetengwa kwa misingi ya kabila.
Lissu alisema badala ya mfumo huo, kuwapo na mfumo wa majimbo yasiyopungua 10, ambayo alisema yataondoa ukabila.
Alisema katika mapendekezo yao, badala ya mkoa, wanataka kuwapo Jimbo la Nyanza Magharibi litakalohusisha mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga.
Jimbo lingine alisema liwe la Nyanza Mashariki, ambalo litahusisha mikoa ya Mara, Mwanza na Simiyu; Jimbo la Ziwa Tanganyika (Kigoma, Katavi na Rukwa); Jimbo la Kati (Tabora, Dodoma na Singida); Jimbo la Kaskazini (Kilimanjaro, Arusha na Manyara) na Jimbo la Pwani Kaskazini (Tanga, sehemu ya Pwani na sehemu ya Morogoro).
Jimbo lingine, alisema ni la Mji Mkuu wa Dar es Salaam; Jimbo la Pwani Kusini (Mtwara, Lindi, Mafia, Rufiji na Ulanga) na Jimbo la Nyanda za Juu Kusini (Njombe, Mbeya na Ruvuma).
“Ukigawanya nchi namna hiyo, hakuna jimbo litakuwa na rasilimali zake,” alisema Lissu.
Alisema pia wamependekeza kwenye mfumo wa utawala, kusiwapo mtu atakayeshawishi kwa Rais ili ateuliwe.
Pia wamependekeza miji iongozwe na mameya wa kuchaguliwa na kwamba, Katiba Mpya itamke kwamba, Kiswahili ni lugha ya taifa na kitumike katika shughuli zote za kiserikali, na pia miswada na sheria zote viandikwe kwa Kiswahili.
Chanzo: Nipashe
Soma zaidi hapa kutoka Nipashe: Zanzibar Ni Kwetu
No comments:
Post a Comment