WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 11, 2014

"SERIKALI TATU KUIBUA UBAGUZI"

assumpter-Mshama_34a28.jpg

KAMATI za Bunge Maalumu la Katiba zimeanza kuwasilisha bungeni maoni yake, kuhusu mijadala ya sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba mpya, huku wengi wakikataa muundo wa serikali tatu, kwa kusema utaibua hisia za ubaguzi kwa wananchi wa taifa moja.

Miongoni mwa kamati zilizowasilisha maoni jana bungeni ni Kamati Namba Tano, ambayo Makamu Mwenyekiti wake, Assumpter Mshama, alisema muundo wa serikali tatu ukipita, utaibua hisia hizo, ambazo hazipati nafasi katika mfumo uliopo wa serikali mbili.

Assumpter alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyesema; “Nje ya Muungano, hakuna Wazanzibari, kuna wao Wapemba na sisi Waunguja…dhambi hii haitaacha kuitafuna Tanganyika ambayo ina makabila mengi.”

Mbali na ubaguzi, walio wengi katika kamati hiyo walielezea hatari nyingine ya muundo unaopendekezwa, utajenga mazingira ya kulisambaratisha Taifa.
“Sura ya 17 ya rasimu inathibitisha kitakachotokea endapo muundo unaopendekezwa utakubaliwa. Mojawapo ya mambo yanayozungumziwa na sura hii ni masuala ya kugawana rasilimali, kugawana watumishi wa umma, madeni na mambo mengine.
“Mambo haya badala ya kuwaleta karibu, inawatenganisha wananchi wa pande mbili za Muungano…kwa mnasaba huu, muundo wa serikali mbili ndio ulioafikiwa na wajumbe wengi kuwa unalifaa taifa letu kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama ya wananchi wa pande mbili,” alisema.
Kuhusu kero za Muungano zinazodaiwa kudumu kwa miaka 50 na kuwa kichocheo cha kupendekezwa kwa serikali tatu, walio wengi katika Kamati hiyo walisema changamoto hizo wanazitambua na jitihada zinafanyika kuzikabili.
“Walio wengi wanaamini kuwa muundo wa serikali tatu hautakuwa suluhisho badala yake utaibua changamoto nyingine nyingi. Mchakato huu ni fursa kubwa na ya pekee kuzishughulikia changamoto hizi kwa mapana yake. “Mapendekezo yaliyotolewa na walio wengi, yanalenga kuzipa jitihada hizi kinga za kikatiba na kisheria ili ufumbuzi wake uwe endelevu,” alisema Assumpter.
Kutokana na hoja hizo, Assumpter alisema walio wengi wanapendekeza katika Sura ya Sita, Ibara ya 60 (1), irekebishwe na kusomeka “Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa serikali mbili ambazo ni: “Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wajumbe wengi pia katika Kamati hiyo, wamependekeza kuwepo kwa viongozi wakuu wenye mamlaka ya utendaji katika Jamuhuri ya Muungano waliotajwa katika Ibara ndogo ya (3), ambao watawajibika kila mmoja wao katika kutekeleza madaraka waliyopewa kuhakikisha wanalinda, wanaimarisha na kudumisha Muungano.
Viongozi wakuu hao ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tanganyika kufufuliwa?
Kamati hiyo Namba Tano, walio wengi wamependekeza kabla ya Rasimu ya Katiba kupitisha muundo wa serikali tatu, ni lazima nchi inayoitwa Tanganyika iwepo kwanza na kupewa mamlaka yake, kisha iamue inataka Muungano wa aina gani.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mshama alisema rasimu ya Katiba inapendekeza muundo wa serikali tatu zitakazotokana na Muungano wa nchi mbili, lakini hivi sasa Tanganyika inayopendekezwa kama nchi mshirika haipo.
Alifafanua Tanganyika haipo kwa kuwa mamlaka, uendeshaji na masuala yake yote yalikwishakabidhiwa kikatiba na kisheria katika nchi inayoitwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1964.
“Hivyo kama kuna shirikisho linapendekezwa basi ni lazima kwanza nchi hiyo inayoitwa Tanganyika iwepo, iwe na Katiba yake na vyombo vyote vya utawala ili iweze kuwa na mamlaka ya kuamua kama inataka Muungano. “Muungano wenyewe wa aina gani na kama ni shirikisho, basi Tanganyika iamue kwa msingi wa kuyakubali masharti ya shirikisho linalopendekezwa. Hilo likifanyika Hati ya Makubaliano iliyopo na ambayo ndiyo inayotajwa na Rasimu ya Katiba, itabaki kuwa waraka wa kihistoria,” alisema Assumpter.
Kamati Namba 2
Mwenyekiti wa Kamati Namba Mbili, Dk Shamsi Vuai Nahodha, alisema katika ibara ya kwanza inayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe walikuwa na mjadala mkali kuhusu maana ya maneno Muungano na Shirikisho, ambayo ufafanuzi wake ulitolewa.
Alisema Muungano ni makubaliano ya zaidi ya nchi moja, kuunda dola moja yenye nguvu, ambapo majukumu ya msingi ya nchi hizo yanakabidhiwa kwenye Serikali ya Muungano.
Alisisitiza Muungano wa Tanzania ni makubaliano kati ya Tanganyika na Zanzibar, ambapo Tanganyika ilikabidhi madaraka yake yote kwa serikali ya Muungano na Zanzibar ilikasimu baadhi ya madaraka yake kwa serikali ya Muungano.
Kwa upande wa Shirikisho, Dk Nahodha alisema Shirikisho ni makubaliano ya nchi mbili au zaidi, zinazounda Serikali moja chini ya kiongozi mmoja, lakini kwa muktadha wa rasimu ya Katiba iliyopo, Shirikisho linalozungumziwa litakuwa na serikali tatu na Marais watatu.
Alisema baada ya ufafanuzi wa kina, wajumbe walifanya uamuzi katika Ibara ya Kwanza wajumbe wengi ambao hawakufikia theluthi mbili walipendekeza neno Shirikisho lifutwe kwa sababu tatu; Kwanza, hati ya makubaliano ya Muungano inazungumzia kuwepo kwa serikali mbili yaani serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Hata Rasimu ya Katiba katika Ibara 1 (3) inatambua hati ya Muungano kama msingi na mwendelezo wa makubaliano hayo,” alisema Nahodha.
Alisema sababu ya pili ni Hati hiyo ya Muungano mpaka sasa haijafutwa na wala haijabadilishwa na tatu, Shirikisho la Serikali tatu linalopendekezwa katika rasimu, litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa eneo la Bahari ya Hindi lenye rasilimali nyingi ambazo mataifa makubwa wanaziwania.
“Udhaifu huu utayapa mwanya mataifa hayo kuzirubuni nchi washirika zisichangie gharama za kuendesha serikali ya shirikisho hasa tukizingatia kuwa serikali ya Shirikisho haina vyanzo vya uhakika vya mapato na endapo jambo hili litatokea Shirikisho litadhoofika na hatimaye kuvunjika.”
Msingi wa Muungano
Akizungumzia Sura ya Sita, inayozungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano alisema wajumbe walijadili na kuchambua na kukubaliana kwamba Muundo wa Serikali Mbili, kama ulivyoanishwa katika hati ya Muungano, ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema hata hivyo baada ya kupiga kura kwa ajili ya kupata uamuzi, theluthi mbili ya upande wa Tanzania Bara haikupatikana. Alisema ingawa theluthi mbili haikupatikana, wajumbe wengi kutoka pande zote, walipendekeza kwamba Ibara hiyo ifanyiwe marekebisho.
Alisema kutokana na marekebisho hayo; Ibara ya 60 (1), itasomeka; “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa serikali mbili ambazo ni (a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano na (b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ibara ya 60 (2) sasa itasomeka kwamba “Shughuli za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitatekelezwa na kusimamiwa na (a) vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, (b) vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na (c) vyombo viwili vyenye mamlaka ya utoaji haki. Hoja kinzani Akisoma maoni kinzani, Dk Nahodha alisema katika mjadala huo baadhi ya wajumbe walikuwa na mtazamo hasi hususani neno Shirikisho lilipotumika.
Kwa mujibu wa Nahodha, baadhi walisema wajumbe walio wengi walidhamiria kwa kiwango kikubwa kuleta marekebisho ama nakala ya rasimu yao ya siri ili kubadili kiini cha rasimu rasmi, ambayo kimsingi ni maoni na mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoundwa na Rais.

LIONS CLUB YAMTUNUKU JK MEDALI YA DHAHABU

D92A2779_cbaf2.jpg
Gavana wa shirika la Lions Club nchini bwana Wilson Ndesanjo akimvika Raisi JKmedali maalum ya uongozi  Bora na mahusiano mema wakati wa hafla fupi iliyofanyika ikulu Jijini Dar es salaam leo
D92A2810_0a8d8.jpg
Raisi JK akiwa katika Picha ya pamoja na viongozi wa Club y Lions waliofika Ikulu Jijini Dar es salaam leo kushiliki hafra ya kumtunuku Raisi medali maalum ya Uongozi bora na mahusiano mema.(Awadh Ibrahim)

source: mjengwa blog

Kafulila asisimua Bunge


Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, David Kafulila jana aligeuka shujaa bungeni na kubebwa juujuu na wajumbe wenzake kutoka kundi la walio wachache baada ya 'kusambaratisha' hoja za wajumbe wanaopinga Serikali tatu.

Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanua hoja kutoka kundi la walio wachache katika Kamati Namba Tano.

Miongoni mwa hoja ambazo alizijibu na kushangiliwa na wajumbe, ni juu ya gharama za Serikali tatu, kuwa zitavunja Muungano, kwamba Serikali ya Muungano itakosa mapato, hoja ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere na uhalali wa takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema hoja kuwa Serikali tatu ni kuvunja Muungano si za kweli, akisema ni propaganda zilezile ambazo CCM ilizitumia mwaka 1992 kutembea nchi nzima kupinga mfumo wa vyama vingi.

"Wakati ule CCM ilitembea nchi nzima huku wakionyesha video kuwa vyama vya upinzani vitaleta vita, lakini leo miaka 20 baada ya kukubali mfumo wa vyama vingi hakuna vita vilivyoletwa na upinzani," alisema Kafulila. Alisema haiwezekani tume zote ambazo zinaundwa na Serikali zipendekeze serikali tatu na kila wakati serikali iliyopo madarakani ikatae.

"Hoja ya serikali tatu siyo hoja ya Warioba, tume zote zilizowahi kuchunguza muundo ya Muungano zote zilipendekeza serikali tatu," alisema na kuongeza: "Ofisi ya Rais ilipendekeza serikali tatu, ofisi ya Waziri Mkuu ilipendekeza serikali tatu, inatuwia vigumu ndani ya muda mfupi, vyombo hivi vibadilike na kutaka serikali mbili."

Alisema wanaotaka serikali tatu wanataka kwa namna ambayo inaimarisha Muungano, tofauti na maoni ya walio wengi kuwa serikali ya Muungano itakuwa legelege kwa kuwa itakosa nguvu za kiuchumi.

"Ni kweli inawezekana vyanzo vya mapato vilivyopendekezwa havitoshi kuendesha Bunge, lakini ndiyo sababu tupo hapa, haiwezekani ripoti ya Tume iwe imekamilika pande zote," alisema na kuongeza:
"Wamependekeza badala ya kutegemea vyanzo vya washirika, tumependekeza kodi ya bandari ambayo ni karibu Sh3.6 trilioni inaweza kuwa ni kodi ya Serikali ya Muungano. Kodi hiyo pekee inatosha kuendesha wizara zote ambazo gharama yake si zaidi ya Sh3 trilioni."

"Kuna hoja hapa, haiwezekani kuwa fedha za bandari zote ziwe zinachangia Muungano kwani ni fedha za Tanganyika, lakini Muungano wowote ni lazima kukubali nchi kubwa kuchangia zaidi."

Kafulila ambaye hata baada ya kumaliza muda wake wajumbe walipiga kelele wakitaka aendelee, alisema kwa Serikali ya Muungano kupata mapato hayo tu, itakuwa haina haja ya kusubiri fedha za nchi washirika na pia itakuwa na uwezo wa kuchangia fedha kwa nchi washirika.

"Haiwezekani Watanganyika wakubali kubeba gharama kubwa ya serikali mbili badala ya gharama ndogo za serikali tatu na hii ndiyo inawapa hofu Wazanzibari kudhani kuna kitu kinachofichwa," alisema. Kuhusu hoja ya kutumia maneno ya Nyerere kupinga Muungano wa serikali tatu, alisema Mwalimu hakuwa nabii, alitazama mambo kwa wakati ule na alikuwa akibadilika kutokana na wakati.

chanzo Mwananchi

Thursday, April 10, 2014

Wabunge tangulizeni utaifa katika kujadili sura za katiba

Katuni
Wajumbe  wa Bunge Maalum la Katiba wanatarajia kuingia katika hatua nyingine muhimu kuanzia leo. Ni hatua ya kuwasilishwa na kisha kuanza kujadiliwa kwa sura za kwanza na sita za rasimu ya Katiba Mpya.
Baadhi ya wajumbe wameanza kuingiwa hofu, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Vyama. Wanaamini kwamba hatua hii itakuwa ngumu kutokana na malumbano makali yanayotarajiwa kuibuka miongoni mwao, hasa wakati wa kuzungumzia vifungu vinavyohusiana na muundo wa muungano.

Sisi tunawatakia kheri wajumbe, tukiamini kwamba pamoja na kuwapo kwa hofu ya kuzuka kwa malumbano hayo, bado hatua hii itamalizika salama na mwishowe shughuli za kuendelea kupitia rasimu zitaendelea na kutimiza lengo la kuwapo kwa Bunge hilo.

NIPASHE tunatambua msingi wa kuwapo kwa hofu hii ya kuibuka kwa malumbano.

Ni kutokana na ukweli kuwa jambo hili haliepukiki. Kila anayefuatilia kwa karibu mchakato huu wa kuundwa kwa katiba mpya anatambua kwamba hakuna namna ya kupitishwa kirahisi kwa sura hizo mbili za rasimu ya katiba, hasa kwa kuzingatia kuwa wajumbe wana mitazamo tofauti juu ya masuala mengi yakiwamo ya idadi ya serikali katika muundo wa muungano.

Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, NIPASHE tunaona kuwa ni vizuri wajumbe wa Bunge hili maalum wakatanguliza maslahi ya taifa dhidi ya kitu kingine chochote wakati wakiingia katika hatua hii.

Kwa kufanya hivyo, ndipo watakapotimiza lengo; ambalo ni kupitisha rasimu ambayo mwishowe itapelekwa kwa wananchi ili ipigiwe kura ya ndiyo au hapana.

Aidha, ni imani yetu kuwa wajumbe wote wa bunge hili wataifanya kazi waliyotumwa na Watanzania kwa umakini mkubwa ili hatimaye kuwa na rasimu itakayoungwa mkono na Watanzania walio wengi.

Kwa kuzingatia matumaini makubwa waliyo nayo Watanzania juu ya kupata katiba mpya, sisi tunaona kwamba ipo haja kwa wajumbe wote kutambua kuwa wanapaswa kuwa makini zaidi kwani safari ya kuelekea mafanikio itaendelezwa leo wakati watakapoanza kupitia sura hizo mbili zinazotajwa kuwa miongoni mwa maeneo nyeti ya rasimu.

Kama ikitokea wajumbe wakateleza kwa namna yoyote ile na mwishowe kutanguliza malumbano yasiyo na tija na kukosa mwisho mzuri, ni wazi kuwa mchakato mzima utakuwa shakani. Na gharama za kukwama kwa mchakato huo zitakuwa kubwa kwa Watanzania.

Mathalan, tunajua kuwa hakuna chochote chenye manufaa kwa taifa kitafanyika ndani ya Bunge hilo ikiwa wajumbe wataamua kutanguliza itikadi za vyama vyao dhidi ya maslahi ya Tanzania.
Taifa litakabiliwa na janga kubwa ikiwa wajumbe watapuuzia umuhimu wa kujenga hoja zao pasi na kujali mustakabali mwema wa nchi yao.
Hatari hii iko wazi. Kwamba, wajumbe wanapoamua kujenga hoja zao kwa kuzingatia utashi binafsi na maslahi ya vyama au makundi yao badala ya taifa, wanaweza kukosa uungwaji mkono wa kutosha kuhusiana na kile watakachokipigania. Mwishowe, theluthi mbili ya kura zinazohitajika ili kupitisha vifungu husika itakosekana.

Hivyo, tunawakumbusha wajumbe wote wa Bunge la Katiba kuwa Watanzania wengi hawapendi kuona mchakato mzima ukikwama kwa sababu ya malumbano yasiyokuwa na hoja zenye mashiko.

Tunakumbushia yote haya huku tukitambua kuwa si rahisi kwa kila upande, hasa ule unaopingana juu ya idadi ya serikali katika muundo wa muungano wataridhishwa na kila jambo. Bali, hekima, busara na uvumiliu ndivyo vitakavyowekwa mbele na kila mmoja kwa manufaa ya taifa.

Kila mjumbe atambue kuwa ili kufikia mwafaka, kuna baadhi ya mambo wanayoyataka sana yawemo kwenye rasimu ya katiba mpya yanaweza kukosa nafasi.
Hivyo, ni wajibu wao wakaendelea kushawishi wengine kwa hoja madhubuti na pia kupima uzito wa hoja mbadala kabla ya kutoa misimamo yao.
Hakika, kama wajumbe watakuwa makini katika hatua hii ya kuwasilishwa rasmi kwa sura za kwanza na pili za rasimu ya katiba, ni wazi kuwa watawatendea haki Watanzania.
Wataendelea kuwapa matumaini juu ya kutimia kwa ndoto za kuwa na katiba mpya kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho. Mungu ibariki Tanzania.
 
CHANZO: NIPASHE

Wasomi: Tunataka serikali moja

 
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samia Suluhu Hassan (kushoto), akipokea nakala ya kijarida cha wanataaluma 100 cha kutafuta Katiba Bora Tanzania kutoka kwa Mwandishi wake, Profesa Teddy Malyamkono, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya EUSARP kwenye ofisi za Bunge mjini Dodoma jana.(Pichan na Khalfan Said)
Wanataaluma wa Taasisi ya Utafiti ya Vyuo Vikuu vya Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAURP) wamekabidhi kitabu kinachoitwa Katiba Bora Tanzania kwa ajili ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba huku wakipendekeza muundo wa serikali moja.
Kitabu hicho kilikabidhiwa jana mjini hapa kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Hassan Suluhu na wanataaluma hao, Profesa Teddy Maliyamkono, Profesa Nehemiah Ossoro na Profesa Bonnaventure Rutinwa.

 Akizungumza kabla ya kukabidhi kitabu hicho, Profesa Maliyamkono ambaye ni Mkurugenzi wa ESAURP, alisema miaka 50 inatosha kutoka katika serikali mbili kwenda moja na siyo serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema ingawa uchaguzi wa Tume hiyo ni kuwa na nchi yenye serikali tatu, lakini kuna matatizo kadhaa makubwa katika muundo huo.

Alisema ni muhimu kwa Tanzania kuwa na muundo wa serikali ambao utakidhi mahitaji yake,“Haya ni pamoja na tatizo kubwa la kukosekana kwa ulinganifu kati ya nchi hizi mbili na mchanganyo wa sekta ya uchumi Zanzibar unaosababisha matatizo ya kifedha wa serikali ya kitaifa na mchango wake wa kifedha kwa serikali ya Muungano,”

alisema Profesa Maliyamkono Akizungumzia muundo wa serikali tatu, Profesa Osoro ambaye ni mchumi aliybobea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema katika utafiti wao, walibaini kuwa kupungua kwa gharama ya kuendesha serikali ya shirikisho inayopendekezwa itakuwa asilimia zaidi ya 97 ya gharama za  kuendesha muungano wenye serikali mbili.

Alisema punguzo hilo dogo katika gharama linatokana na kupunguza mambo ya Muungano kutoka 22 hadi saba , haiashirii kupungua kwa gharama za kuendesha serikali ya shirikisho inayopendekezwa kwa theluthi mbili.

 Alisema mambo saba ya Muungano yaliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kubaki katika serikali ya Shirikisho ni yale ambayo yana matumizi makubwa, kama vile ulinzi na usalama na mambo ya nje.

“Hii inatokana na ukweli kwamba mambo haya saba ya Muungano ni vipengele vikubwa vya matumizi…utafiti huu unaonyesha kwamba tofauti katika gharama za kuendesha ama Muungano wa serikali mbili au tatu si kubwa sana,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika Muungano wa serikali tatu, nchi mbili huru (Tanganyika na Zanzibar) kila moja itahitaji fedha za ziada kwa ajili ya matumizi yake.

Kuhusu gharama kuendesha mfumo wa Shirikisho uliopendekezwa, alisema Tanzania ni nchi kubwa na tajiri kwa madini na rasilimali nyingine za asili tofauti na Zanzibar ambayo ni nchi ndogo na ina idadi ya watu wasiopungua milioni na rasilimali zake ni chache.

“Kwa ufupi, Zanzibar mbali na utalii ni dhaifu sana kiuchumi…kwa Tanzania kuwa tajiri katika maliasili na utalii na idadi ya watu, inaweza kubeba gharama za kuendesha Muungano uliopo,” alisema

Alisema hilo linaweza kuwa ni tatizo kwa sababu Zanzibar inaweza kushindwa kuwasilisha mchango wake kama ilivyokubaliwa na pande zote mbili na Tanzania Bara pia itakataa kutoa msaada wowote wa ziada.

“Jambo hili linaweza kuwa na chanzo cha migogoro na misuguano kati ya nchi hizi mbili ambayo inaweza kuwa migumu kutatuliwa kisiasa…inaweza hata kusababisha kuvunjika kwa Muungano,” alisema

Alisema kwa kiasi fulani gharama za kuendesha mfumo wa serikali tatu inaweza kuwa kubwa ikilinganishwa na gharama yote ya kuendesha Muungano uliopo.

Naye Profesa Rutinwa, ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kwamba wanaotaka serikali tatu msukumo wao unatokana na mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ambayo imetamka kwamba Zanzibar ni nchi.

Hata hivyo, alisema hoja hizo hazina nguvu kwa sababu siyo mara ya kwanza  hoja kama hiyo kutolewa kwa kuwa kabla ya hapo, Katiba hiyo ilikuwa ikionyesha kwamba Zanzibar ni nchi.

Alitoa mfano kwamba, Katiba ya 2003 ina vifungu viwili cha 9 na 22 ambavyo vinaonyesha kwamba vinataja Zanzibar ni nchi na ni Taifa.

Alisema kwamba kwa upande wao suala la muundo wa serikali wanaliacha kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ili waweze kuliamua.

Akizungumza baada ya kupokea nakala hizo, Suluhu aliwashukuru wanataaluma hao kwa kujitolea kuandika kitabu hicho ambacho kitakuwa msaada mkubwa kwa wajumbe wa bunge hilo kwa ajili ya kutengeneza katiba yenye maslahi kwa Watanzania wote.

Alisema kwa sababu kanuni zinaruhusu kuwaita wataalamu kwa ajili ya kutoa ushauri, bunge hilo halitasita kuwaita wakati wowote watakapowahitaji.
 
CHANZO: NIPASHE

BERNAD MEMBE AMUWAKILISHA JK KUPOKEA TUZO NCHINI MAREKANI

wawa_4ab1a.jpg
Wageni kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo Watanzania waliohudhuria katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington
lady_4d937.jpg
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe, akimsikiliza mwendesha shughuli Lady Kate Atabalong Ndi, Kamishna Masuala ya Afrika wa Gavana wa jimbo la Maryland nchini marekani kabla ya  kupokea  Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa Jumatano, Aprili 9, 2014. Kushoto ni Naibu Spika Mhe Job Ndugai ambaye yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani, ambapo alialikwa kuhudhuria hafla hiyo. Nyuma yake ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Liberata Mulamula.
 

membe_e9a82.jpg
wenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Balozi wa Nigeria nchini Marekani Profesa Adebowele Adufye, akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe Tuzo la Kiongozi MAfrika kwa mwaka 2013 anayopokea kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C.
pamoja_7a123.jpg


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe katika picha ya pamoja na meza kuu baada ya kupokea   Tuzo la Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi Katika Maendeleo ya Bara la Afrika kwa mwaka 2013 kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika  sherehe ya kutunuku Tuzo hiyo kwenye Hoteli ya St. Regis mjini Washington, D.C., usiku wa , usiku wa jana  (Awadh Ibrahim)

source: mjengwa blog

Katiba Mpya: Nimeitafakari Sana Njia Ya Kikwete...

1_ecfa4.jpg

Katiba Mpya: Nimeitafakari Sana Njia Ya Kikwete...
Ndugu zangu,
Naziona ishara za kuendelea kwa mvumo mbaya wa upepo wa kisiasa na hususan inapohusu hoja ya Muungano na muundo wa Serikali.
Mjadala unaoendelea sasa ni kama vile umefunikwa kwa chandarua kisicho na kinga ya wadudu wenye madhara kama mbu.
Tunakoelekea si kuzuri. Msimamo wangu uko wazi, kuwa tunahitaji muundo wa Serikali Tatu ili tuimarishe Muungano wetu. Kwamba tunahitaji uwepo wa Tanganyika kama nchi.
Lakini, nahofia katika tofauti hizi za mitazamo, kuna wenye kuamini katika Serikali Tatu lakini bila kuwa na nia njema kwa nchi. Na kuna wenye kuamini hivyo wakiwa na dhamira njema pia. Hivyo hivyo kwa wenye kuamini katika Serikali Mbili.
Hivyo, nimeipitia mara kadhaa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa alipokuwa akifungua Bunge Maalum la Katiba. Nimejitahidi kuitafuta mantiki kwa alichokizungumza Rais wa Nchi. Naamini Jakaya Kikwete aliongea kile alichokiamini moyoni mwake. Kikwete alionyesha hofu juu ya Serikali Tatu ingawa aliweka wazi kuwa maamuzi ya mwisho ni ya Wabunge wenyewe. Ni haki ya Kikwete kama mwanadamu kuelezea hisia zake.
Lakini , Jakaya Kikwete si kama Watanzania wengine. Ni Rais wa Nchi. Nikifikiri leo, naamini ilikuwa sahihi kwa Kikwete kukisema alichokisema, hata kama hakifanani na misimamo kama ya kwangu.
Maana, nikiwasikiliza ndugu zetu wa Zanzibar , hasa wenye kuupinga Muungano katika hali iliyopo, na jinsi wanavyojadili, kwa kweli natishikia pia. Na hakika, kwa kuufuatilia mvumo wa upepo wa kisiasa unaoendelea sasa, Jakaya Kikwete alitusaidia kuyaweka wazi mawazo yake binafsi. Maana, ingawa Serikali Tatu na Tanganyika inahitajika, lakini, huu si wakati wake. Ni jambo la kusubiri lije tutakapokuwa tayari kama watu tulioungana; Visiwani na Bara. Na tuanze sasa kufanya jitihada za kuyatafuta maridhiano juu ya kwa nini haya ya kubadilli mfumo wa Serikali kwenda Serikali Tatu wakati wake haujafika.
Maana, kuendelea kujadili Serikali Tatu sasa ni kuzidi kuipeleka nchi yetu tunayoipenda kwenye mgawanyiko na mpasuko mkubwa. Ni busara nionavyo, kuwa Wabunge wetu kule Dodoma watambue kuwa rasimu ya Jaji Warioba, ukiacha muundo wa Muungano na mfumo wa Serikali , ina mengi sana ya muhimu ili kututoa hapa tulipo na kuwasaidia wananchi.
Waitafute busara ya kulisubirisha hili la Muuundo wa Muungano unaopendekezwa na Rasimu ya Warioba na hata muundo wa Serikali. Tubaki na Serikali Mbili na tuboreshe kinachoweza kuboreshwa.
Maana, si kila unachokigawa maana yake kuna kinachobaki. Kugawa pia kuna maana ya kumaliza pia.
Na mengine tuyafanyao katika wakati usio sahihi huzaa kutokuaminiana.
Na kwa mwanadamu pale mtaji wa imani unapomalizika, kinachobakia ni kumaliziana.
Usimwone nyani ana makovu ukadhani ni simba aliyemjeruhi. Nyani huishi kwa kumwogopa zaidi nyani mwenziwe.
Kugawanyika kwa shari ni kutawanya mitaji ya kuaminiana.
Na kitachobaki ni kuumizana, kwa kugombani kiduchu chunguni kilichogandiana...
Ni wakati sasa wa kutanguliza busara na hekima zitakazotunusuru na mpasuko mkubwa zaidi wa kijamii.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Maggid,
Iringa.