WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, July 7, 2015

Siku saba za urais ndani ya CCM



Dar/Dodoma. Ni wiki ngumu kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ndivyo unavyoweza kusema kwani chama hicho kinachotawala kitafanya vikao vyake vya juu vitakavyohitimishwa kwa kumpata mgombea wake wa urais.
Mchakamchaka utaanza na kikao cha Kamati ya Maadili keshokutwa kukutana. Tayari CCM imetangaza kuwa itatumia vigezo 13 ilivyojiwekea kuwachambua wagombea 38 waliochukua na kurejesha fomu ili kupata majina ya wachache watakaopigiwa kura na mkutano wake mkuu.
Awali, kulikuwa na watangazania 42 waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM, lakini wanne kati yao hawakurejesha fomu. Kamati Kuu itakayokutana Alhamisi itakuwa na kazi ya kuwachuja hadi kubakia wasiozidi matano yatakayopigiwa kura Ijumaa ijayo katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kubaki matatu.
Katibu wa Baraza la Ushauri wa Wazee wa CCM, Pius Msekwa juzi alilieleza gazeti hili kuwa mbali na sifa hizo, suala jingine litakalotizamwa ni iwapo wagombea hao walikiuka kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wote wa mchakato.
Majina matatu yatakayopitishwa katika kikao cha NEC ndiyo yatapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM utakaokaa Julai 11 na 12 na kupata mwakilishi mmoja wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Uzoefu unaonyesha kuwa chama hicho huzingatia mambo mengi katika kufanya uteuzi, ikiwa ni pamoja na kutafuta mtu atakayeondoa makundi yaliyoundwa wakati wa uteuzi wa mgombea urais.
Baadhi ya mambo yanayotajwa kuwa yatakuwa karata muhimu katika mchujo huo ni suala la Muungano, jinsia, eneo la kijiografia, rekodi ya mtia nia na kukubalika kwa kada hasa katika kipindi hiki ambacho upinzani umeimarika. Hofu inayoonekana kukikumba chama hicho ni ya kumpata mgombea mwenye sifa na anayekubalika na atakayeweza kukabiliana vyema na yule atakayesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kwamba hana mgombea anayemuunga mkono kinaonyesha jinsi mchujo huo utakavyokuwa mgumu.
Kauli ya Takukuru
Kutokana na unyeti wa wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah amesema vijana wake wako Dodoma na kuwatahadharisha wagombea wote kuzingatia sheria.
“Nawashauri wagombea wote wazingatie Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Kupambana na Rushwa, wafanye mambo kistaarabu na ambaye atakwenda kinyume, sheria itachukua mkondo wake,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema jeshi hilo limejiandaa vizuri kwa ugeni huo mkubwa.
“Natoa onyo kwa mtu yeyote mwenye nia ovu au kutaka kufanya kitendo chochote cha kuhatarisha usalama, atashughulikiwa kwa nguvu zote za kisheria,” alisema Misime.
Aliwataka wajumbe wa vikao hivyo, wageni na wananchi kutambua kuwa usalama unaanza kwa kila mmoja wao, hivyo wakiona jambo lolote linaloashiria uhalifu au si la kawaida, watoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Wasiwasi wa kukosa vyumba
Huku zikiwapo taarifa za hoteli zote kujaa mapema, mmoja wa wagombea Boniface Ndengo, alisema,
“Mimi nataka niwepo huko (Dodoma) kuanzia Jumanne jioni, nitajaribu kufanya mpango wa chumba lakini nimesikia vyumba vimejaa, sijui kama nitapata nafasi,” alisema.
Alisema hataki kubeba watu wengi, bali ataongozana na watu wasiozidi watatu na amepata habari kuwa wagombea wote wataalikwa kwenye mkutano mkuu.
Taarifa zilisema kuwa CCM imechukua hoteli zaidi ya 300 na hakuna wajumbe watakaochangia chumba kwa kulala wawili kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kauli ya wasomi
Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema katika uteuzi huo, ni vyema CCM ikamteua mwanachama anayekubalika na ambaye atamudu hali ya upinzani iliyopo sasa.
“Upinzani wa sasa siyo sawa na wa miaka mitano uliopita, wateue mtu atakayepata kura za pande zote kwa maana ya kura ndani ya chama na nje ya chama,” alisema Mbunda.
Alitolea mfano wa kile kilichotokea nchini Kenya wakati wa Kanu wakati chama hicho kiliposhinikiza mgombea fulani apitishwe wakati hakuwa anakubalika.
“Wasishinikize mtu fulani apite. Lazima wazingatie hayo ili kusije tokea mpasuko,” alisema na kuongeza kuwa binadamu wapenda hisia zao zizingatiwe.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete alisema CCM haikuwa na utaratibu mzuri tangu mchakato wa kuchukua fomu za kuwania urais ulipoanza.
“CCM lazima iwe na utaratibu mzuri wa kumchagua mtu au watu wachache watakaowania nafasi hiyo. Sasa tumeona kila mtu tu anajitokeza kuchukua fomu ya kuwania urais. Huo siyo utaratibu mzuri,” alisema Profesa Mbwete.
Alisema kutokana na hilo, inakuwa vigumu hata kutoa maoni juu mchakato wake wa kumteua mgombea urais.
Imeandikwa na Noor Shija na Sauwa (Dodoma), Fidelis Butahe na Suzan Mwillo (Dar).
source: mwananchi

No comments:

Post a Comment