WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, July 14, 2014

Rasimu ya Katiba; Hivi Watanzania tulitaka nini?

KATIKA wakati huu, Nauona  umuhimu wa kukumbushana swali hili nililopata kuliuliza. Maana, kwa mwanadamu usipojua unataka nini, basi, usishangazwe na matokeo ya ulichokifanyia kazi. Chaweza kuwa chochote kile.
Na swali hili la mfumo wa Serikali si mwanzo wa mwisho wa matatizo yetu yajayo kama taifa, bali ni mwisho wa mwanzo wa tulichodhani kuwa ni kutatua matatizo yetu ya muungano.
Tunakoelekea si kuzuri, maana, tumeamua kuacha kutumia busara na hekima na badala yake tunatanguliza ushabiki wa vyama na hata makundi na watu tunaowapenda. Yako wapi mapenzi kwa nchi tuliyozaliwa?
Maana, tulidhani ni mabadiliko makubwa yamefanyika katika nchi yetu pale ulipozinduliwa kwa kishindo mchakato wa kupata Katiba Mpya. Wengi wameanza kukata tamaa.
Tulidhani yangelikuwa  mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika tangu mwaka 1977. Ni  pale ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo wa 1977 yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa chama tawala na hata mfumo wa uongozi wa Serikali.
Katika  dunia hii, mabadiliko ya kijamii hupelekea mabadiliko ya kisiasa. Na WanaShosholojia  wanasema, kuwa sababu mbili zenye kupelekea mabadiliko hayo; sababu za ndani ya jamii husika (endogenous) na sababu za nje ya jamii (exogenous).
Kwa upande wetu, tunaona kuwa, sababu za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma kwenye kufikia hatua hii ya kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.
Na kwa jamii yetu kwa upana wake, ingelikuwa na  sababu za msingi  za kuyafurahia mabadiliko haya, maana, ni sawa na mwanadamu aliyepewa kikombe chenye nusu ujazo wa maziwa.  Utafahamu kama amefurahia au amechukizwa kwa namna  atakavyochagua kukielezea kikombe kile; anayekiona ni ’ kikombe nusu cha maziwa’  anaonyesha kutoridhika, na anayekiona ni  ’ kikombe kilichobaki  nusu tu kujaa’ huyo amekifurahia na anaonyesha matumaini kuwa iko siku kitajaa. Inahusu kuwa na matarajio chanya (Optimism) na kuwa na matarajio hasi (Pessimism)
Na hakika, Rais Jakaya Kikwete ameonyesha tangu mwanzo, dhamira yake ya kutuletea mabadiliko kama taifa.  Na Wajumbe wa Tume yaKatiba walifanya  kazi  njema iliyotufikisha kwenye hatua ya kuwepo kwa Rasimu ya kwanza ya Katiba na hata ya Pili. 
Nimepata kuandika, kuwa  katika dunia ya sasa, hakuna anayeweza kuyazuia mabadiliko yanayotokana na msukumo wa ndani ya jamii- Kule Urusi ya zamani,  Mikhael  Gorbachev alipoanzisha mageuzi  makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi watu hawakuamini walichokiona. Gorbachev aliuona wakati uliobadilika.  Mabadiliko yale makubwa ya kimfumo kule Urusi yalipata majina mawili; Perestroika  na Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya na Glasnot ni uwazi .
Kabla ya mageuzi yale  makubwa, Urusi  ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana kwa  uwazi.  Jamii ilijawa hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha. Kulikuwa na  usiri mkubwa. Lakini, ndani ya kufichwa huko, kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa. Gorbachev,  daima atakumbukwa kwa  ’ Kuvunja Ukimya’ na kuifanya Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana sasa.
Na hakika,  ‘ Kuzaliwa  kwa  Katiba Mpya’  katika nchi ingelipaswa iwe ni  sawa na ’ Taifa kujivua gamba’.  Maana, kujivua gamba huku kama taifa kunapaswa kuendane na kuanza kubadili mifumo yetu ya kifikra. Tuanze sasa kufikiri juu ya malengo ya taifa, kwa maana ya ndoto za taifa letu badala ya kutanguliza sana malengo ya vyama vyetu au zaidi malengo binafsi ya vyeo na mamlaka.
Nchi yetu ni kama nyumba kongwe.  Tuendelee kwa umoja wetu kuifanya kazi ya  kuikarabati upya nyumba yetu. Ipate mwonekano mpya. Kuikarabati  upya nyumba kongwe huweza pia kupelekea kuibomoa nyumba yenyewe.  Kutakuwa na fito na  vipande vya matofali vya kurudishia. Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndio,   fito na matofali mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima yatupwe, basi. Na hapo utakuwa umeikarabati upya nyumba yako.
Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine  kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa.  Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu.
Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye kuambukiza kwa haraka.
Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni  nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi  au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini.  Na imani ya wananchi kwa taifa na viongozi wao ni shina la matumaini  yao. Inakuwaje basi mwananchi  anapokosa imani na taifa na hata kwa kiongozi?  Katiba yetu iwe chachu ya kurudisha mioyo ya uzalendo kwa taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania.
www.raiamwema.co.tz: maggid mjengwa

No comments:

Post a Comment