Prof. Muhongo, Waziri Tanzania - Nishati na Madin
i
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema mwaka huu lazima alifumue Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kulisuka upya ili kukidhi mahitaji ya umeme.
Pia alisema Serikali, haitakubali kupandisha bei za umeme hadi hapo mapato na matumizi ya shirika hilo
yatakapofanyiwa ukaguzi na kujiridhisha.
Profesa Muhongo, alitoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam juzi, wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV mjini Dar es Salaam juzi.
Alisema msimamo wa Serikali, hadi sasa ni kwamba bei ya umeme haitapanda.
“EWURA na TANESCO, wamefuata taratibu zao za kubadilisha bei, lakini nimewaeleza na narudia kusisitiza chochote watakachojadili labda waje na bei ya kushusha umeme…Serikali haikubali bei ya kupandisha umeme huo ndio msimamo haubadiliki.
“Bei haitapanda, nimewaambia TANESCO kwamba endapo wanataka kupandisha bei ni lazima tukae chini na wao tuangalie matumizi yao ya fedha wanazozikusanya, sasa ikiwa kama matumizi yao ni makubwa hayaendani na hali halisi cha kwanza ni kufumua hilo shirika la TANESCO, nashukuru Watanzania walitoa maoni yao kuhusu muundo wa shirika wanalolitaka sasa yamekusanywa na wiki hii tutaletewa wizarani.
“Ujumbe wa mwaka wa 2013, ni lazima tufumue TANESCO tujenge upya ambayo itakidhi mahitaji yetu ya leo ya umeme, tunaotaka leo hii ni ule ambao utahakikisha uchumi wetu unakua kwa kasi zaidi, huwa unakua kwa asilimia 6.7, lakini tukitaka kupunguza umaskini ni lazima ukue kwa asilimia 8 hadi 10. Tukitaka ukue TANESCO ya sasa hivi haikidhi, lazima tuifumue huenda tutakuwa na kampuni moja mbili au tatu, nawahakikishia lazima tuwe na shirika na muundo mpya, inatupatia umeme wa uhakika, unaotabirika wa kuendesha uchumi wetu.
“Lakini pia mgawo wa umeme haupo na hautakuwapo, ndiyo maana sikubaliani na mawazo ya TANESCO na EWURA ya kupandisha umeme, kwa sababu fedha ambazo zinatumika kufua na kusafirisha umeme sasa hivi, ni fedha ambazo zinatokana na kodi za Watanzania.
“Fedha hazitoki TANESCO, wala EWURA hivyo hakuna sababu ya msingi mtu ambaye anazalisha umeme kwa kutumia hela yake alafu umpandishie bei, pia suala la mgawo halipo na nimewaeleza kwamba umeme wetu ambao tunautumia kwa wingi sasa hivi unatokana na gesi asilia, ni kati ya asilimia 40 mpaka 70, unategemea ni wakati upi tunachukua hizo takwimu, kwa hiyo umeme wetu mwingi hautokani na maji, kwa hiyo kina cha maji kishuke chini kiasi gani umeme wetu unatokana na gesi.
“Tunapaswa tutambue, miundombinu ya kuzalisha na kusambaza umeme imechoka, mashirika mawili yaliyoitengeneza TANESCO yetu hii yalikuja kwa pamoja mwaka 1930. Kwa hiyo tangu enzi ya ukoloni, miundombinu hii haijabadilishwa ndio maana ikitokea hitilafu Ilala, jiji zima linaweza kukosa umeme.
“Kinachofanyika sasa, ni kujaribu kuifanya iwe ya kisasa, kwa mfano katika hayo matengenezo inatokea kwamba umeme inabidi uzimwe sehemu fulani ndipo watu wanasema ni mgawo hapana sio mgawo... Watanzania, tunapaswa kuamua kama tunataka miundombinu yetu iboreshwe na wakati wa kuboreshwa lazima umeme uzimwe au tunataka kubaki na miundombinu ambayo mingine imekuwapo enzi ya ukoloni? Ni afadhali tuvumilie umeme uwe unazimwa ili tuboreshe miundombinu yetu,” alisema.
Soma zaidi
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment