Ndimara “Ndi” Tegambwage
MTWARA hawajasema wanataka wapeleke vikapu, vidumu na makopo wawekewe gesi.
Hapana!
Wanasema wanataka kuona utajiri wa gesi ukionekana kwenye nyuso zao; Kwenye miili yao - kwenye afya zao na akili zao. Basi. Ni jukumu la Serikali kuweka utaratibu wa kutekeleza hilo.
1. Kuna kitu kinaitwa kauli ya serikali juu ya maandamano ya wananchi wa Mtwara ya tarehe 27 Desemba kupinga gesi asilia iliyogunduliwa huko “kuondoshwa tu kwa mabomba kupelekwa Dar es Salaam, bila mafao kwao.”
2. Serikali imekuja na utetezi wa kisiasa kwa njia ya shairi:
“…Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani mwetu. Tusikubali kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio cha raslimali zilipo kwenye wilaya zetu. Tusikubali kuvunjavunja wilaya zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye tarafa zetu. Tusikubali kuvunjavunja tarafa zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye kata zetu. Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu."
Ni utetezi uliotarajiwa kutoka serikalini - hakuna uliobora zaidi kwao kuliko huu.
3. Bali shairi hili haliwezi kupigiwa makofi kwa kuwa ni serikali yenyewe ambayo imeshindwa kutumia fursa zilizopo kujenga hoja na kuhabarisha wananchi. Watawala na viongozi wengine wako mbioni kuiba na kufuja kila kinachofika machoni mwao; na wanafanya hivyo kwa usiri na wazi na kwa jeuri isiyomithilika.
4. Bali hoja kwamba kahawa, tumbaku, mahindi ya sehemu moja yanalisha sehemu nyingine ni mufilisi. Serikali haina chake kuhusu mazao haya. Serikali hailimi. Inajiingiza kuharibu ushirika (kama ilivyofanya); ivuruge nguvu ya ushirika iliyokuwa mhimili mmojawapo wa kudai haki kwa wakulima na wazalishaji wengine. Ni kuingilia kwa serikali katika biashara ya mazao ya wananchi ambako kunasababaisha hata mazao kushindikana kuuzwa kwa kuwa serikali katika eneo husika, inaweka vikwazo (Angalia: Kahawa - Bukoba - Kagera; Pamba - Mwanza na Shinyanga; Karafuu - Zanzibar; Korosho - Mtwara na Lindi). Katika hili, hoja ya waziri haina mashiko.
5. Tunajadili extractive products (na hata mbuga za wanyama) ambazo ni za wote na siyo biashara ya mtu mmojammoja. Hilo halinabudi kueleweka. Lakini maandamano ya Mtwara yana kitu cha nyongeza. Watawala wamezoea kuvungavunga - ni ubabaishaji wa kipuuzi sana kila siku kuwaambia watu wenye akili zao kuwa dhahabu imetuingizia kiasi fulani lakini fedha imenunua dawa za hospitali, imejenga barabara, imejenga chuo kikuu.
6. Wenye akili wanasema: Mapato yote ya almasi yataingia katika ujenzi wa barabara. Inasimamiwa hivyo na inakuwa hivyo. Mapato yote ya dhahabu yataingia kwenye elimu. Inasimamiwa hivyo na kuwa hivyo. Mapato ya tanzanite yataingia kwenye afya. Inasimamiwa hivyo na inakuwa hivyo. Upuuzi wa "kapu la bibi" katika mambo ya kifedha - ambamo mchukuaji ni mmoja na asiyeheshimu maadili wala uwajibikaji - hauwezi kuleta tija wala kushawishi yeyote kuamini serikali. Ni wezi tu, kila mmoja atasema.
7. Maandamano ya Mtwara yanapaza sauti za walioondolewa kwenye makazi yao sehemu zote yaliko machimbo ya madini nchini. Walitupwa nje kama takataka. Waliobahatika wakapewa mahema na wakristo; wameishi humo mpaka yakawa marapurapu - mpaka leo hawajafidiwa. Ambao hawakubahatika waliishia kulala nje wakifumbatwa na baribi, umande, mbu (usiku), na jua kali, upepo na mvua (mchana). Hesabu: wangapi wamekufa wangali wakilakana? Wameshuhudia watawala wakiingia migodini, wakishangiliwa na hata wakitoka na “vifurushi” bila hata kuwapungia mkono; huku wawekezaji wakipiga mbinja! Mtwara wameona hayo yaweza kutokea kwao katikati ya utajiri wa gesi.
8. Leo serikali inafumuka huko na taarifa inayosema yanayofahamika - the most obvious. Hakuna jipya. Tunafundisha waandishi kutafuta kitu kipya katika hoja "zinazoonekana kuchoka" kwa kuandikwa mara nyingi. Lakini kabla ya kutafuta, tunawauliza: Nani amechoka? Wanaoandika au hoja zenyewe. Mara nyingi, kama siyo zote, hoja hazichoki. Wanaochoka ni watu.
Wanachoka kwa kuwa butu, kutojali, kuishiwa maarifa, kukosa vyanzo vya fikra mpya; kupauka kwa kutonyunyizia mbongo kwa elimu na maarifa mapya, na mengine mengi. Lakini hoja, kila kukicha, katika kila mazingira tofauti - kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni - zinapata mnyumbuliko na kutoa mwanya kwa kitu kipya. Serikali haija kipya.
9. Kinachoitwa taarifa ya serikali hakioneshi kutambua kilio cha waandamanaji. Ama ni mchoko, mazoea ya ubabe wa watawala au upungufu mkuu wa uwezo wa kufikiri. Taarifa inalaani tu. Inaishia kusukuma mzigo kwa vyama vya upinzani. Huu nao ni upweke kiakili.
10. Mtwara hawajasema wanataka wapeleke vikapu, vidumu na makopo wawekewe gesi. Hapana! Wanasema wanataka kuona utajiri wa gesi ukionekana kwenye nyuso zao; kwenye miili yao - kwenye afya zao na akili zao. Basi. Ni jukumu la serikali kuweka utaratibu wa kutekeleza hilo.
11. Kwa serikali kusema maandamano hayajawahi kutokea Bukoba, Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Arusha na kwingineko ambako kuna raslimali ni matusi kwa wakazi wa maeneo hayo - ni kama kusema "wanajua kuumia kimyakimya!" Ni matusi.
12. Hakuna cha visingizio vya vyama vya siasa kuandaa maandamano. Kama wameandaa ina maana mazingira yameshawishi hivyo. Hilo lisingekuwapo wasingeandamana wala kufikiria kufanya hivyo.
13. Nani anasema Mtwara hakuwezi kutoka fikra bora? Nani? Sasa imetokea. Wanaikumbusha serikali kwamba imekuwa ikitumikia matajiri wa nje kuvuna raslimali za taifa na kuwaacha wananchi kufa; na kufa wakiwa masikini wa kupindukia. Gesi imekuwa kipenyo cha kupitishia ujumbe ambao umekuwa ukitolewa bila watawala kujali.
ndimara
Ndimara Tegambwage
Information and Media Consultant
P.O. Box 71775, Dar es Salaam
Tel: 255 (0)713614872
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment