WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, September 19, 2013

JK: Tutakabiliana na wauza ‘unga’ kwa nguvu zote;

jk_dawa_3bea9.jpg

Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya, Watanzania wawili Agnes Masongange na mwenzake, Melisa Edward jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North Gauteng katika kesi ya dawa ya kukamatwa na dawa hizo

Rais Kikwete alisema Serikali yake itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni kinyume na sheria za nchi.

Alisema hayo juzi usiku alipokutana na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani..."Serikali yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa dawa za kulevya na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja sheria za nchi yetu."

Masogange na Melisa walikamatwa Julai 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.

Aidha, amesema hayo siku chache baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).

Pia, Agosti 31, mwaka huu, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki 'Golota' na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa wakituhumiwa kubeba dawa za kulevya.

Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.

"Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu hatukutetei kamwe," alisema.
Masogange, Melisa wakwama dhamana

Masogange na mwenzake Melisa jana walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya North Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa zinazodaiwa kutumika kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama tik).

Taarifa kutoka Mahakama hiyo zinaeleza kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao itasikilizwa tena Novemba mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi Novemba.

Awahoji akina Masogange Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini kuwahoji Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini alisema hawakumpa ushirikiano.

Kamanda huyo alisema imebainika kuwa mzigo walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana na madai hayo, Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao kuendelea kusikilizwa nchini baada ya yeye (Nzowa) kushauriana na Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Afrika Kusini.

Alisema, inawezekana watuhumiwa wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.

Chanzo:Mwananchi

MATOKEO KAMILI LIGI KUU Tanzania

1111 1e313
YANGA 1 - 1 Prisons,
SIMBA 6 - 0 Mgambo
Kagera 2 - 1 JKT Oljoro (HM)

Azam 1 - 1 Ashanti
Coastal 1 - 1 Rhino
Mtibwa 0 - 0 MBEYA City
Ruvu Shooting 1 vs 0 JKT Ruvu. Chanzo: Shaffihdauda

YANGA SC ILIVYOKAMATWA NA WAJELAJELA SOKOINE LEO


0_800d3.jpg
Kiungo wa Yanga SC, Haruna Niyonzima akiwatoka mabeki wa Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Timu hizo zilitoka 1-1
 
source: mjengwa blog

Monday, September 16, 2013

Serikali imeshindwa kudhibiti uhalifu wa tindikali nchini?


Padri Mwang’amba (aliye tumbo wazi) akizungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
Matukio ya kumwagiwa tindikali yameendelea kukithiri huku Serikali ikiendelea kutoa ahadi za kudhibiti bila mafanikio.  Hivi karibuni baada ya raia wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali Zanzibar, Serikali iliweka mikakati mikali ya kudhibiti matumizi ya kemikali hiyo, lakini bado matukio hayo yameendelea kuwepo.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba ni mwendelezo wa uhalifu huo ambao Serikali imeshindwa kabisa kuudhibiti.

Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea, Padri Mwang’amba anasema alikuwa nje ya duka linalotoa huduma za mawasiliano ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege Wilaya ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.

Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na Serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.

Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo.

Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.

Tukio hilo linafuatia tukio la Agosti 7, mwaka huu ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar na vijana wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa.Waingereza hao walisafirishwa siku tatu baadaye kurudi kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu.

Utetezi wa Serikali
Siku tano baada ya tukio la Waingereza hao kumwagiwa tindikali, Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi iliwataka wananchi kuisaidia kuwafichua na kutoa ushahidi wa uhalifu huo kwani ni vigumu kuwabaini wahusika.

Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Eliezer Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.

“Mkemia Mkuu, Polisi hawawezi kubaini matukio haya bila ushirikiano wa wananchi kwani Tanzania ni nchi kubwa na ina watu zaidi ya milioni 45. Watu wanaingiza tindikali lakini wapo ambao wanatumia tindikali hiyo kwa matumizi haramu,” alisema IGP Mwema.

Amesema tindikali inaweza kutolewa kwa ajili ya shughuli za viwandani, maabara na usafirishaji na kwamba watu wanapotaka kuitumia kwa ajili ya kufanya uovu wanaweza kugundulika kupitia kwa taarifa zitakazotolewa na wananchi, kwa sababu wanakuwa wamezungukwa na jamii ya watu mbalimbali.

Matukio mengine
Tukio lingine lililoshtua ni lile la bilionea Said Mohamed Saad ambaye ni mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, kumwagiwa tindikali mwanzoni mwa mwezi Agosti.

Said anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini na inaelezwa kuathirika vibaya usoni, mikononi na kifuani.
Alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu akiwa kwenye moja ya maduka yake katika Jengo la Msasani Mall, Dar es Salaam.

Taarifa za siku ya tukio zilibainisha kuwa Said alikuwa akizungumza na mfanyakazi wake muda wa saa moja jioni ndipo akatokea kijana mrefu, mwembamba ambaye alimmwagia kimiminika kinachosadikiwa kuwa ni tindikali.

Ilibainishwa kwamba mfanyakazi huyo wa Said, Hassan Ahmad naye alijeruhiwa kidogo katika purukushani hiyo lakini alipopelekwa Hospitali ya Ami Wellness Centre, alitibiwa na kuruhusiwa huku bosi wake akipelekwa Afrika Kusini usiku huohuo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura anasema matukio ya kutumia pikipiki yanaonyesha kupangwa hivyo inakuwa vigumu kuwabaini wahalifu mapema. 

Tukio hilo linafanana na lile lililotokea Septemba 8, mwaka huu ambapo mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema wa Mburahati jijini Dar es Salaam, alimwagiwa kemikali hiyo na watu waliokuwa kwenye pikipiki ya matairi matatu.

Msema maarufu kama Mnyalu amelihusisha tukio hilo lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi ambapo yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) kulitumia kuegesha magari yake.

Akizungumza kwa shida katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa anakiri kuwa mstari wa mbele kupinga eneo hilo kutumiwa kinyume na sheria.

“Awali vijana wasio na ajira waliomba eneo hilo ili walitumie kwa mradi wa kuegesha magari, wakaandika barua, lakini Serikali ya mtaa ikakataa ikisema hilo ni eneo la kazi. Hiyo ilikuwa mwezi Oktoba mwaka jana, ilipofika Novemva, tukaona malori yanaegeshwa pale. Tulipofuatilia tukaambiwa ni mwenyekiti wa mtaa ameruhusu,” anasema na kuongeza:

“Tukajiorodhesha wana mtaa tukafika kama watu 60 na mimi nikawa mwenyekiti wao, tukapeleka barua yetu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye aliipeleka kwa ofisa wa mipango miji.”
Ameongeza kuwa ofisi ya mipango miji ya Kinondoni ilisema hilo ni eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari hivyo ikaagizwa kuwa magari hayo yaondolewe. 

“Kampuni iliyopewa tenda ya kuondoa yale magari ilifanya kazi bila kutoa notisi, ndipo yule mwenye magari akaenda kulalamika kwa mkuu wa mkoa. Malalamiko yakafika kwa Mkurugenzi ambaye aliagiza kampuni hiyo irejeshe hayo magari ili utaratibu ufuatwe,” alisema.  Aliendelea kusema kuwa yule mfanyabiashara aliendelea kukaidi kwa kuongeza magari mengine kwenye uwanja huo hadi yalipokuja kuondolewa kwa nguvu.

Msema alisema wakati mvutano huo ukiendelea, aliwahi kukutana na mlinzi wa mfanyabiashara huyo ambaye alimtahadharisha kuwa harakati zake hizo zitamponza kwani anafuatiliwa.

“Mimi sikukata tamaa kwani lile ni eneo la umma kwa nini mtu ang’ang’anie? Lakini watu wengi walinitahadharisha kuwa yule jamaa ananifuatilia, ndiyo maana siku ile ya tukio kuna bajaji kumbe ilikuwa inanifuatilia kwa muda mrefu,” anasema.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mburahati, Tungaraza amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo huku akimtaka mwandishi afike ofisini kwake kwanza.  Matukio  hayo yameanza muda mrefu na wakati mwingine yamehusishwa na chuki za kisiasa.

Baadhi ya wananchi wanashauri Serikali kuwa imara na tindikali hasa katika chaguzi zijazo, kwani tindikali ni rahisi kuibeba.

source: mwananchi

Mbowe, Lipumba, Mbatia wambana JK

mbowe 23301

Mshikamano wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya Bunge na sasa vyama hivyo vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

Jana wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) walikutana na waandishi wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Walisema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru walichokiita "utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi" hivyo wanaitaka Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika mchakato huo.

Akitoa tamko la pamoja kwa niaba ya viongozi wenzake, Profesa Lipumba alisema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.

"Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona ila aurejeshe bungeni,"alisema Lipumba na kuongeza:

"Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko."

Mwenyekiti huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya watu, hivyo mchakato huo haupaswi kuhodhiwa na chama kimoja, badala yake unapaswa kuwa shirikishi na jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa Katiba katika msingi wa maridhiano.

Kuna madai kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.

Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.

Itakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.

Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.

Mbowe na MbatiaKwa upande wake, Mbowe alisema: "Amani itavurugwa kama mchakato wa Katiba Mpya utahodhiwa na chama kimoja cha siasa, ikiwa hivyo sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani ni lazima haki iwepo."

Alisema fursa ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na watu wachache ndani ya CCM, na kwamba wapinzani watatumia kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea, ili washiriki katika kuidai Katiba iliyotokana na mawazo yao.

Mbowe alisema wapinzani hawatarudi nyuma na hawatakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa Katiba ya sasa.

"Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika katika kitabu chake kwamba, 'kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa makini'. Amani itaharibiwa na wale wenye dola, sio vyama vya upinzani" alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Mbatia alisema: "CCM ndio nini... Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo. CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubaki."

"CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu wanakosea, katika taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao. Katiba Mpya ni tendo la maridhiano na kisiasa sio kisheria, sisi tuna tofauti, lakini tumeziweka pembeni."

Mbatia alimtaka Rais Kikwete kusimamia kikamilifu mchakato wa Katiba ili historia isije ikamhukumu. "Yeye ndio ameanzisha mchakato huu wa kupata Katiba Mpya, aweke masilahi ya taifa mbele sio masilahi ya chama chake cha siasa, CCM haiwezi kuwa juu ya dola na Serikali, asisaini marekebisho ya Katiba yaliyofanyika bungeni,"alisema Mbatia na kuongeza: "Mkono wa Rais usilitumbukize taifa la Tanzania katika machafuko, kwanza hagombei tena urais wala uongozi ndani ya chama chake, sasa anamwogopa nani."

Vyama hivyo pia vimetangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa ni 'hujuma dhidi ya upatikaji wa Katiba Mpya'.

Mikutano hiyo itaanzia Septemba 21 mwaka huu, katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na baadaye viongozi hao watakutana na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.

Makundi mengine ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.

:CHANZO MWANANCHI.

Sunday, September 15, 2013

Padre Mwang’amba ahamishiwa Muhimbili, Rais Dk Shein ampa pole

Picture
Mmoja wa ndugu wa Padre Mwang'amba akimueleza Rais Dk Shein, hisia zake kwa uchungu akitaka zilichukuliwe hatua za kisheria na kukomeshwa vitendo hivyo.
Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Machuwi, Anselmo Mwang’amba kumwagiwa tindikali katika duka la mawasiliano ya intaneti la Sunshine, Mlandege mjini Unguja, gazeti moja linaripoti kudokezwa kuwa kabla ya tukio hilo, kiongozi huyo alitishiwa kuuawa na watu, ambapo mpaka sasa si yeye wala polisi waliokuwa tayari kuwataja.

Kwa mujibu wa baadhi ya watu walio karibu na kiongozi huyo, Padre Mwang’amba alitishiwa kifo zaidi ya miezi minne iliyopita lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Gazeti hilo linasema liliwasiliana na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa, kujua ukweli wa jambo hilo lakini aligoma kuthibitisha kwa kusema kuwa hana uwezo wa kulizungumzia huku akilitaka gazeti hilo liwasiliane na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Saidi Mwema, ambaye hata hivyo simu zake ziliita bila kupokewa.

Alisema kuwa msemaji mkuu wa masuala ya polisi ni IGP Mwema, huku akibainisha kuwa yeye anao uwezo wa kuzungumzia hali ya majeruhi huyo.

Padri Mwang’amba kwa sasa amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwang’amba ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Malezi kwa Vijana kilichopo Cheju wilaya ya Kati Unguja kinachomilikiwa na kanisa Katoliki, alifikishwa katika hospitali hiyo jana saa 3:00 asubuhi baada ya 
kusafirishwa kwa ndege ndogo ya Kampuni ya Coastal kutoka Zanzibar.

Alipofikishwa hospitalini hapo, Padri huyo alipokelewa katika kitengo cha dharura ambapo alipatiwa huduma katika kitengo hicho ikiwa ni pamoja na kufanyiwa vipimo mbalimbali kabla ya kuhamishiwa wodi namba 10 Kibasila.

Mara baada ya kuhamishiwa wodini, waandishi wa habari walitaka kumuona na kuzungumza naye, hata hivyo Padri Mwang’amba hakutaka kuzungumza kwa kile alichoeleza hana maelezo zaidi ya yale aliyozungumza baada ya kushambuliwa: “Sina cha kuzungumza zaidi, naendelea vizuri kama mnavyoniona, nilichosema ni kile kile alichozungumza na mmeona katika magazeti,” alisema.

Muuguzi Mkuu katika jengo la Kibasila, Rutgard Rutabingwa alisema, “tumempokea mgonjwa wetu yuko katika hali nzuri, maendeleo yake yanaridhisha,” alisema.

Padri wa Kanisa Katoliki Minara Miwili lililopo eneo la Mji Mkongwe, Asenga Thomas ambaye ameambatana na Mwang’amba kutoka Zanzibar alisema maendeleo ya padri huyo ni mazuri na kwamba hata maumivu aliyokuwa anayasikia juzi baada ya tukio yamepungua: “Ukiangalia hali ilivyokuwa baada ya tukio na leo (jana) utaona kuna tofauti kubwa, maumivu yamepungua, ndio maana hata usingizi amepata,” alisema.

Alisema Mwang’amba alishambuliwa juzi na watu wasiofahamika wakati akitoka katika duka  linalotoa huduma za mawasiliano ya intaneti: “Alitoka nje baada ya kupigiwa simu na kijana wake mmoja, ghafla ndio alimwagiwa tindikali…inavyoonekana waliokusudia kufanya tendo hili walikuwa wanamfuatilia na walifahamu hiyo ni sehemu anayokwenda sana, ndio wakamvamia na kumjeruhi hivyo,” alisema.

Alisema inasikitisha kuona hali ya Zanzibar imegeuka hivyo watu wanashambuliana na kujeruhi wengine bila sababu za msingi, hali inayotishia amani na usalama wa wananchi wanaoishi visiwani humo.

Daktari Abdalla Haidari wa hospitali ya Mnazi Mmoja amesema juzi kwamba Padri Mwang’amba amejeruhiwa usoni na kifuani kwa maji ambayo baada ya kuyafanyia uchunguzi wamebaini kuwa ni tindikali.
Picture
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza Padre Mwang'amba jana hospitalini Zanzibar, kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam.

Tukio hili limekuja baada ya mwezi uliopita walimu wawili wa kujitolea, raia wa Uingereza walijeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali katika maeneo ya mji Mkongwe, Shangani ambao ni Kate Gee (18) na Kristie Trup (18) walivamiwa na kujeruhiwa saa 1:00 usiku wakati wakienda kupata chakula cha usiku. Walikimbizwa Uingereza kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa muda katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Saalam.

Matukio mengine ya kushambuliwa ni pamoja la Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shekhe Fadhil Sulaiman Soraga aliyemwagiwa tindikali Novemba 6 mwaka jana, Sheha wa Shehia ya Tomondo, wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Omar Said aliyemwagiwa tindikali Mei 23 mwaka huu.

Pia Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa risasi na kujeruhiwa Desemba 26 mwaka jana na Padri Evaristus Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi  wakati akienda kanisani.

Kabla ya Padri Mwang’amba kupelekwa Dar es Salaam,  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein jana asubuhi alimtembelea hospitalini Mnazi Mmoja alikolazwa na kutoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitahidi kuimarisha uchunguzi wa  matukio ya watu kumwagiwa tindikali ili wahusika wapelekwe kwenye vyombo vya sheria.

“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee... ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisisitiza Dk Shein.

Amekieleza kitendo hicho kuwa ni cha kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa amesikitishwa na kitendo hicho na kumpa pole Padri Mwang’amba na kumuomba Mwenzi Mungu ampe nafuu haraka apone ili endelee kuitumikia jamii.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo nje ya Wodi alipolazwa Padri huyo, Dk. Shein aliwataka waumini hao kuwa na subira wakati Serikali ikichukua hatua kukabiliana na kitendo hicho.

“Ni jambo la kusikitisha kumfikisha binadamu wenzako katika hali kama hii ya majonzi. Hakuna anayetaka haya. Tuwe wastahamilivu Serikali tunachukua hatua,”aliwaambia waumini hao.  

Akizungumzia hali yake, Padri Mwang’amba alimueleza Rais kuwa ni nzuri na anaona vizuri lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua sehemu za machoni.

“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi,” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake hakuathirika sana. 

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mohamed Saleh Jidawi akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk Jamala Adam Taibu amesema alipofikishwa katika hospitali hiyo Padri Mwang’amba alipatiwa huduma zote muhimu za matibabu zinazostahiki. 

Kuhusu majeraha aliyopata, Dk Jidawi alieleza kuwa kwa ujumla asilimia 30 ya mwili wa Padri Mwang’amba umeathirika na kidogo sehemu za macho.

Kwa upande wa Wakristo kisiwani Zanzibar wamesikitishwa na tukio la kumwagiwa kwa tindikali kwa Padri Mwang'amba wakati akitoka katika duka la intaneti la Sunshine la Mlandege.
Baadhi ya wakristo waliohojiwa ikiwemo wa kanisa la Machuwi ambalo Mwang'amba alifanya kazi kwa miaka mingi, walisema sasa maisha ya jamii ya wakristo Zanzibar yapo mashakani.

Modesta Nkala wa kijiji cha Kitumba Wilaya ya kati ambaye husali katika kanisa la Machuwi alisema amesikitishwa na tukio hilo ambalo walengwa wake wakuu wanaonekana watu wa jamii ya Wakristo.
“Tuliposikia taarifa za tukio hili tulikusanyika na kulia sana kwa sababu Padri Mwang'amba  tulifanya kazi naye kwa miaka mingi katika kanisa la Machuwi wilaya ya kati Unguja akiwa mtumishi wa mungu muaminifu,” alisema.

Padri Mwanga'mba alihamishiwa katika kituo cha kulea na kutunza vijana kilichopo Cheju ambacho kinaendeshwa na kanisa Katoliki mjini hapa.

Muumini mwingine wa kanisa la Machuwi, Bulabo Pascal alisema baadhi ya watu wanaonekana kuelekeza visasi vyao kwa Wakristo bila ya sababu za msingi ikiwa ni hujuma na ukatili usiokubalika.

“Tunaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufutilia kwa karibu matukio ya vitendo vya hujuma vya watu kumwagiwa tindikali,”alisema.

Mpiga picha wa kujitegemea Martin Kabemba alisema matukio ya watu kumwagiwa tindikali hivi sasa yanaonekana ya kawaida  huku jambo la kushangaza hakuna mtu anayekamatwa.

Kiongozi wa kanisa katoliki Zanzibar, Askofu Augustino Shao alisema amesikitishwa na tukio hilo ambalo linaonesha vitisho kwa Wakristo waliopo Zanzibar.

Shao ambaye yupo nje ya Zanzibar alisema tukio la kumwagiwa kwa tindikali kwa Padri Mwang'amba lengo lake ni kudhoofisha juhudi za Wakristo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mapema Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alielezea masikitiko yake kwa matukio ya vitendo vya watu kushambuliwa kwa tindikali ambayo vimeelekezwa kwa jamii moja tu na watu wenye itikadi moja.
Alisema lengo la Serikali ya umoja wa kitaifa ni kujenga mazingira ya  utulivu wa kisiasa, na vitendo vya vurugu na watu kumwagiwa tindikali vinakwenda kinyume na malengo hayo.

Padri wa kanisa katoliki Minara miwili liliopo eneo la Mji Mkongwe, Asenga Thomas ambaye alikuwa akishughulikia safari ya Padri Mwang’amba kwenda hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema amejeruhiwa vibaya sehemu za uso na kulazimikwa kusafirishwa.

Aidha alisema kanisa linatarajia kutoa tamko rasmi kuhusiana na tukio la kumwagiwa kwa tindikali kwa padri Mwang’amba.

Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Yussuf Ilembo alisema hadi sasa Jeshi la Polisi halijakamata mtu yeyote kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi zaidi unaendelea.

---via hTanzaniaDaima na HabariLeo
 

Simba yaua, Yanga yashikwa

Beki wa Yanga Nadir Haroub Cannavaro akiwania mpira na mshambuliaji wa Mbeya City kwenye uwanja

Simba imekata mzizi wa fitina kwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0, huku mabingwa watetezi Yanga, Azam wakilazimisha sare ugenini dhidi Mbeya City na Kagera Sugar.

Kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Betram Mwombeki waliingia wakitokea benchi na kuifungia Simba mabao hayo mawili muhimu katika kipindi cha pili. Mabingwa watetezi Yanga, waliokolewa na bao la Didier Kavumbagu wakilazimisha sare 1-1 na Mbeya City waliopanda daraja msimu huu.

JKT Ruvu imeendelea kung’ang’ania kileleni baada ya kuichapa Ashanti United kwa bao 1-0 na kuweka rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo.

MBEYA
Mechi hiyo ilitawaliwa na vurugu na vituko vingi kabla ya kuanza kwake baada ya basi lililobeba wachezaji wa Yanga kushambuliwa kwa mawe, chupa za maji, bia na mashabiki wa Mbeya City wakati likiingia uwanjani na kusababisha kuvunja kioo cha dirisha la dereva.

Dakika chache kabla ya mechi kuanza meneja wa Uwanja wa Sokoine, Modest Mwaluka aliokota mayai matatu katikati ya uwanja.

Mwigane Yahya ndiye aliamsha shangwe za mashabiki wa Mbeya baada ya kuifungia Mbeya City bao la kuongoza katika dakika 49 akiunganisha krosi ya Mazanda.

Baada ya bao hilo Yanga, iliwapumzisha Nizar na Bahanuzi na kuwaingiza Oscar na Jerry Tegete mabadiliko yaliyozaa matunda kwani dakika ya 71 walisawazisha bao hilo kupitia Kavumbagu akimalizia krosi ya Tegete.

Dar es Salaam
Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden aliwapumzisha Said Khamis, Twaha Ibrahimu na kuwaingiza Henry Joseph na Betram Mwombeki ili kuimarisha safu ya kiungo iliyoonekana kuzidiwa nguvu na vijana wa Mtibwa.

Mabadiliko hayo yalizaa faida katika dakika ya 67, pale Joseph Shindika alipoipatia Simba bao la kuongoza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Amri Kiemba.

Dakika ya 90, Mwombeki aliwainua mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la pili akimalizia vizuri pasi ya Ramadhani Singano ambaye kabla aligongeana vyema na Joseph.

Safari ya Ashanti United kurudi ilipotoka imezidi kushika kasi baada ya jana kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Ruvu, goli pekee la Amos Mgisa.
Azam wameendelea na mwendo wa kusuasua baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Mshambuliaji Temi Felix aliwainua mashabiki wa Kagera Sugar,ambapo kiungo Hamisi Mcha aliisawazishia Azam. Katika michezo mingine Tanga, Coastal Union ilitoka sare 0-0 na Prisonsi.

Arusha wenyeji Oljoro JKT walilazimishwa sare 1 -1 na Rhino Rangers, wageni Rhino walipata bao la kuongoza kupitia Saad Kipanga kabla ya Amiry Omary kuisawazishia Oljoro katika dakika 27.

Vilevile Ruvu Shooting ilichapa Mgambo JKT kwa bao 1-0 shukrani k wa bao Elias Maguli.

Imeandaliwa na Vicky Kimaro, Jessica Nangawe (Dar), Msafiri Sanjito (Kibaha), William Paul (Kagera), Mosses Mashalla (Arusha), Doris Maliyaga (Mbeya) Salim
Mohamed (Tanga).

source: Mwananchi

Young Africans imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City;

kavu_kichwa_a987b.jpg

Young Africans imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji timu ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliochezwa jioni ya leo katika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Young Africans wakati wakiingia uwanjani washabiki wa Mbeya City walilirushia mawe na chupa za bia bus la wachezaji hali iliyopelekea kuvunja kioo cha upande wa kulia mwa dereva na kumjeruhi dereva Maulid Kiula aliyekua akiliendesha gari hilo.
Mara baada ya tukio hilo viongozi wa timu ya Yanga walichukua jukumu la kuwatuliza wachezaji na kuendelea kuwapa morali ambapo walituliza munkari wa kujeruhiwa na kuingia ndani kujiandaa na mchezo wenyewe.
Dakika za mwanzo Said Bahanuzi na Didier walishindwa kuzitumia nafasi za wazi na kiujumla hali ya mchezo ilikua sawa kwa timu zote huku washabiki wakikosa radha ya mchezo kutokana na ubovu wa uwanja.
Mbeya City walifanya mashambulizi langoni mwa timu ya Yanga lakini umakini wa walinzi na mlinda mlango Ally Mustapha 'Barthez' ulikuwa kikwazo kwa washambuliaji hao kuziona nyavu za watoto wa Jangwani.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Mbeya City 0 - 0 Young Africans.
Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji kufanya shambulizi langoni wa timu ya Yanga na dakika ya 46 ya mchezo waliweza kujipatia bao la kwanza kupitia kwa mshambuliaji Paul Nonga kwa kichwa aliyeukwamisha mpira wavuni kwa kichwa.
Kocha wa Yanga alifanya mabadiliko ya kuwaingiza Jerson Tegete na Oscar Joshua waliongia kuchukua nafasi za Said Bahanuzi na Nizar Khalfani ambao waliongeza nguvu na kubadili hali ya mchezo.
Dakika ya 60 Didier Kavumbagu aliipiatia Yanga bao la kusawazisha kufuatia golikipa wa Mbeya City kuuchezea mpira na Didier kuukwamisha wavuni lakini katika haliya ajabu mwamuzi alilikataa bao hilo.
Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao la kusawazisha dakika ya 71 kwa kifua akimalizia mpira uliopigwa na mlinzi Mbuyu Twite na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni bila ajizi.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Young Africans 1 - 1 Mbeya City
Mara baada ya mchezo wakati timu ikielekea hotelini washabiki wa timu ya Mbeya City wameendelea kuzirushia mawe gari zilizokuwa katika msafara huo ambapo wamevunja vioo vya bus kubwa tena na gari ndogo kioo cha nyuma chote.

source: mjengwa blog