WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, February 19, 2012

Uchambuzi Wa Habari: Dk Mwakyembe Naye Amwaga Sumu!



Ndugu zangu,

Kwenye vyombo vya habari kumekuwa na taarifa zinazochanganya  juu ya kinachomsibu Dk. Mwakyembe.

Na kama utangulizi ufuatao nitauzungumza kama hotuba fupi mbele ya watu wanaojiandaa kwa mlo wa kusheherekea harusi, basi, nina imani, zaidi ya nusu ya wageni waalikwa watainuka kwenye meza zao na kukiacha chakula.

Maana nitaanza kwa kusema;

Mabibi na Mabwana,

Wakati tukijiandaa kwa  mlo ulio mbele yenu ningependa kuwaeleza mafupi juu ya sumu na jinsi sumu inavyoweza kuingia kwenye mwili wako na hatimaye kukudhuru. Na bila shaka wote mnajua kuwa sumu inaua.

Ni hivi; unaweza kuwekewa sumu. Usipoiona na ukaiacha, basi, utakuwa umepona.  Ndio, kama kuna sumu imewekwa usiichukue. Kwa mantiki hiyo hiyo, jiadhari, unaweza ukashikishwa sumu.  Kuwa makini na wanaokupa mikono ya heri, mingine ni mikono ya kifo. Yumkini anayekupa  mkono amevaa glovu yenye sumu.

Ndugu yangu, unaweza pia   ukagusishwa sumu.  Kuwa makini na unayecheza nae muziki baada ya mlo huu. Kumbatio la muziki tulivu laweza kugeuka kuwa ni kumbatio la kifo.

Sumu inaweza  pia kukuingia  mwilini kwa kulishwa.  Uwe makini na anayekulisha kipande cha keki ya harusi. Na kama waweza kulishwa sumu hivyo hivyo waweza ’ kujilisha’ mwenyewe sumu. Chunga sana na anayekupa kipande cha nyama choma. Ukakipokea na hatimaye kukitia mdomoni.

Kama ilivyo kwa kulishwa na kujilisha sumu. Yawezekana pia sumu ikaingia mwilini mwako kwa kunyweshwa au kujinywisha.  Chunga sana na unayekaa karibu naye. Jichunge mwenyewe pia. Ukinywa vodka nyingi ni sawa na ’ kujinywisha’ mwenyewe sumu.

Sumu yaweza pia kukuingia mwilini kwa kumwagiwa. Kaa mbali sana na atakayefungua champeini isije kilichomo kikawa ni sumu.  Na wengine hamfahamu, kuwa   sumu yaweza  pia kukuingia kwa kupuliziwa.  Sahani yako ya chakula yaweza kuwa imepuliziwa sumu…

Ndugu zangu,

kuna njia nyingi sana za sumu kuingia mwilini mwako. Nisiwachoshe, tuendelee na  mlo wetu wa harusi!

Naam. Habari kubwa katika siku mbili hizi ni kadhia ya Dr. Mwakyembe na madai ya  sumu kuingizwa mwilini mwake na wabaya wake. Na kama mlivyoona hapo juu, bado haijawa wazi kama Mwakyembe kalishwa, kawekewa, kanyweshwa au kagusishwa sumu. 
Jitihada za Jeshi la Polisi juzi kutaka kutuambia WaTanzania ukweli juu ya kadhia hii zinaonekana kugonga mwamba  kwa kupingwa vikali na Mwakyembe mwenyewe. Tumesoma kwenye magazeti ya leo.

Nani anaongopa?

Bila shaka, habari hii imekuwa ikiwavutia wengi kwa vile kiu ya jamii ni kutaka kujua ukweli mzima. Jamii inataka kujua; nani anasema kweli na nani anaongopa. Vita inayopiganwa sasa imebaki kuwa ni vita ya maneno kwenye vyombo vya habari.

Kila upande unadai una ushahidi na unachosema lakini ushahidi huo hauwekwi hadharani ukaonekana.  Wanahabari nao wameonekana kusukumwa zaidi na upepo wa vita na kuandika yale ambayo wanadhani yatauza magazeti.  Kimsingi media inaweza ikamaliza vita hii kwa kuwauliza wahusika maswali sahihi na magumu yatakayotokana na  maelezo wanayotoa wahusika

Mfano, DCI Manumba anasema; ” Ukweli kuhusu  kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu , tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya ambayo nayo imewasiliana na  hospitali aliyokuwa amelazwa  Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha  kuwa hakuna sumu  katika maradhi yanayomsibu Mwakyembe.”- ( Mwananchi, Jumamosi, Februari 18, 2012)

Naam, kama DCI Manumba anadai wamethibitishiwa na Wizara ya Afya iliyofanya mawasiliano na hospitali anayotibiwa Dr . Mwayembe nchini India  kwamba Dr Mwakyembe hakukutwa na sumu mwilini ni kwanini wanahabari wasifike Wizara ya Afya kuthibitishiwa juu ya kile ambacho Manumba anadai kuthibitishiwa. Maana, haiyumkini kuthibitishiwa huku kukawa ni kwa mdomo tu.
Na Dk. Mwakyembe anaposema; ” Ripoti inatamka wazi kuwa  kuna kitu kwenye bone marrow ( ndani ya ute wa mifupa) kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua.” ( Mwananchi,  Februari 19, 2012.)

Kwa wanahabari kazi hapa ingekuwa kumbana Mwakyembe  awasaidie kupata maelezo ya ziada kutoka kwa mabingwa hao wa India ili iwasaidie ku-establish, bila mashaka, juu ya dhana ya sumu katika kinachomsibu Mwakyembe.

Vinginevyo, taarifa ya jana ya Dr Mwakyembe inatoa tafsiri pia ya mtu aliyejeruhiwa na aliyeamua ’kumwaga sumu’ hadharani. Taarifa ile ya Mwakyembe imeonyesha jinsi  watendaji wetu wakuu Serikalini na hata kwenye chama tawala wasivyoaminiana. 

Tumeona jinsi Mwakyembe alivyorusha makombora makali dhidi ya jeshi la polisi na kutoa tuhuma nzito ya jinsi  jeshi hilo linavyotenda hujuma . Kwa mtu wa kawaida atajiuliza; kama Mwakyembe Waziri na kada wa CCM analia kuchezewa faulo, je,  hali itakuwaje kwa mtu wa kawaida na kama ni mwanachama wa chama cha upinzani?

Swali lingine; kama baadhi ya mawaziri wa JK kwenye baraza moja wanaonyesha hadharani kuwa hawaaminiani wanamsaidiaje Rais wa nchi? Na je, Mwakyembe au Sitta wakihamishimiwa wizara ya Mambo ya Ndani  watafanyaje kazi na akina Manumba na Said Mwema? Na kuna wengi wanaomtarajia JK kufanya  mabadiliko makubwa  ya Baraza la Mawaziri kwa vile hawaridhishwi na utendaji wa Baraza lililopo.

Na haya yote tunayoyashuhudia  ni ’ maradhi ya taifa’  ya tangu uhuru kwa vile tumekuwa na Katiba yenye mapungufu makubwa na kwa sasa isiyokidhi mahitaji ya wakati uliopo. Tunamshukuru Rais wa nchi kwa kuonyesha dhamira ya kutuanzishia mchakato utakaopelekea kupata Katiba Mpya kwa Taifa la Kisasa.

Katiba ya sasa inaruhusu ’ ubaguzi wa kisiasa’. Inawatenga Watanzania wengine katika ushiriki wa uongozi na ujenzi wa nchi.  Na dhambi ya ubaguzi ndio inayotutafuna sasa hadi tukafikia hata viongozi watendaji wa juu ndani ya chama tawala  kukosa kuaminiana.
Ndio, Watanzania walio wengi  ’ hawajalishwa sumu’, isipokuwa, kwa miaka mingi Watanzania wamekuwa ’ wakibwigizwa ugoro’ uliowafanya wasinzie  kama watu waliopigwa  sindano ya ganzi.

Wengi  sasa , na hususan vijana, wanakataa mchana wa jua kali kubwigizwa ugoro na walio kwenye mamlaka. Wamebumbuluka. Wameanza kusoma katikati ya mistari. Ndio, wameamka na wana kiu ya kuiona Tanzania mpya na inayostawi. 

Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
Jumapili, Februari 19, 2012.

Habari kwa hisani ya Mjengwa Blog

No comments:

Post a Comment