Ndugu zangu,
Kwenye gazeti la Mwananchi jana Jumapili kulikuwa na habari ukurasa wa tano inayosema; “Mufuruki: Itikadi za kisiaa zinakwamisha wananchi”. ( Mwananchi Jumapili, Februari 5, 2012)
Habari hiyo ilinivutia sana na ikawa ya kwanza kwangu kuisoma. Mwandishi Exuper Kachenje anaripoti, kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maafisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini Bw. Ali Mafuruki ametaja kuwa itikadi za kisiasa ni vikwazo vikubwa vilivyowanyima na vinavyoendelea kuwanyima wafanyabiashara wazalendo nafasi wakiachwa nyuma na kuwapendelea wageni wanaoshikilia uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa.
Ali Mufuruki anasema; ” Vikwazo vikubwa kuliko vyote ambavyo mpaka leo vipo ni vile vilivyotokana na itikadi ya kisiasa ambavyo siyo tu ilimnyima nafasi mfanyabiashara mzalendo, bali pia iliwapendelea zaidi wasio wazalendo.”- Ali Mufuruki.
Mufuruki anazidi kubainisha, kuwa kwa muda mrefu Watanzania wengi wenye uwezo wa kufanya biashara kubwa walikimbilia kufanya kazi za kuajiriwa Serikalini, kwenye shughuli za za siasa huku wasio na uwezo wa kupata ajira wakihangaika na biashara ndogondogo na kuiacha sekta ya biashara kubwa kwenye mikono ya watu wenye asili ya kiasia.
Bwana Mufuruki akazidi kuwa mkweli na kusema, kuwa waasisi wa Uhuru wetu walitilia mkazo zaidi udhibiti wa nguvu ya utawala wa kisiasa bila kujali nafasi ya wananchi wao katika kudhibiti nguvu za uchumi. Hilo, kwa mujibu wa Mufuruki, ndilo lililowaacha wenye uwezo zaidi kudhibiti nguvu za uchumi wa nchi kwa miaka mingi ijayo.
Mtazamo wangu;
Bwana Ali Mufuruki amekuja na hoja ya kizalendo, nzito na muhimu sana kwa nchi yetu kwa sasa. Watanzania tumekuwa kama wagonjwa wa muda mrefu ambao, waganga mbali mbali tuliowapata wameshindwa kutwambia chanzo cha maradhi yetu. Hivyo basi, wameishia kujaribisha tiba , moja baada ya nyingine, bila mafanikio. Watanzania bado ni wagonjwa kiuchumi.
Bwana Ali Mufuruki amekuja na hoja ya kizalendo, nzito na muhimu sana kwa nchi yetu kwa sasa. Watanzania tumekuwa kama wagonjwa wa muda mrefu ambao, waganga mbali mbali tuliowapata wameshindwa kutwambia chanzo cha maradhi yetu. Hivyo basi, wameishia kujaribisha tiba , moja baada ya nyingine, bila mafanikio. Watanzania bado ni wagonjwa kiuchumi.
Ali Mufuruki ametusaidia kujua chanzo cha maradhi yetu. Na yuko sahihi kabisa. Alichokisema Mufuruki mara kadhaa nimekiita kuwa ni ubaguzi wa kisiasa. Nchi yetu inasumbuliwa na ’maradhi ya ubaguzi wa kisiasa’. CCM , kama ilivyokuwa kwa TANU, bado inaamini katika udhibiti wa nguvu za kisiasa.
Kuna mifano kadhaa ya Watanzania wazalendo waliofilisika kibiashara kwa ’ dhambi ya kuwaunga mkono wapinzani’. Tuna mifano kadhaa ya wafanyabiashara Watanzania wenye asili ya kiasia ambao biashara zao zinashamiri kwa vile walichagua tangu enzi, kuwa wafadhili wa TANU na baadae CCM ambayo ina hamu ya kuendelea kudhibiti nguvu za kisiasa badala ya kuandaa mazingira ya wananchi wake wadhibiti uchumi wao.
Wakati CCM ikitimiza miaka 35, hoja ya Ali Mufuruki waichukulie kama changamoto. Maana, zama za udhibiti wa nguvu za kisiasa zimepita. Kwenye pluralism kuna ustawi . Kwenye ' Chama Kushika Hatamu' kuna kudumaa. Huwezi leo kuendelea na udhibiti wa nguvu za kisiasa kama wananchi wako hawana udhibiti wa nguvu za kiuchumi na badala yake udhibiti huo huko mikononi mwa wananchi wako wachache wenye asili ya kiasia au wageni wanaoitwa wawekezaji.
Na huu si wakati tena wa kuwa na wanasiasa wenye kutoa hadharani, kauli kama; ” Anayetaka biashara yake imwendeee vizuri aje CCM!”
Tubadilike ili tusonge mbele kiuchumi , na tuzidi kuwa Wamoja kama taifa.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
Jumatatu, Februari 6, 2012
Habari kwa Hisani ya Mjengwa Blog
No comments:
Post a Comment