WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, January 31, 2013

DKT.SHEIN AZINDUA MAADHIMISHO KUZALIWA CCM



Makamu Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akivishwa Skaf na Mtoto Chipukizi Pili Hassan Suluhu mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Makao Makuu ya CCM Kisiwa Ndui kwa ajili ya Kufanya Uzinduzi wa Sherehe za Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa CCM,ambapo Kilele chake kitafanyika Huko Kigoma Tanzania Bara.


Makamu Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akitoa Hotuba katika Uzinduzi wa Sherehe za Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa CCM, Makao makuu ya Chama hicho Kisiwa Ndui Zanzibar. Kushoto yake ni Naibu katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai na kulia yake ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama Borafya Silima Juma.
Naibu katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai akitoa hotuba ya Kumkaribisha Makamo Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein  katika Uzinduzi wa Sherehe za Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa CCM, Makao makuu ya Chama hicho Kisiwa Ndui Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein  akikabidhiwa Vifaa mbalimbali vya Mchezo wa Mpira wa Miguu kwa ajili ya Mashindano maalum ya Ligi ya Timu za CCM Itakayo anza kutimua vumbi hapo kesho Kiwanja cha Amani ikiwa ni Shamra shamra za Sherehe ya kutimia Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa CCM, Makao makuu ya Chama hicho Kisiwa Ndui Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa CCM ambae pia ni Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein  kulia akimkabidhi Mipira na Vifaa mbalimbali vya Michezo Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo Mkoa wa Mjini  Ali Othman Said kwa ajili ya Ligi ya Timu za CCM Itakayo anza kutimua vumbi hapo kesho Kiwanja cha Amani ikiwa ni Shamra shamra za Sherehe ya kutimia Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa CCM, Makao makuu ya Chama hicho Kisiwa Ndui Zanzibar.
Vijana wa CCM wakiimba Wimbo Maalum wa Kuzaliwa kwa Chama CCM katika Uzinduzi wa Sherehe za Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa Chama hicho, kwenye Makao makuu ya Chama  Kisiwa Ndui Zanzibar.
Vijana wa CCM wakiimba Wimbo Maalum wa Kuzaliwa kwa Chama CCM katika Uzinduzi wa Sherehe za Miaka 36 ya Kuzaliwa kwa Chama hicho, Makao makuu ya Chama  Kisiwa Ndui Zanzibar. (PICHA NA YUSSUF SIMAI -MAELEZO ZANZIBAR).

DR.MIGIRO MKUU MPYA CHUO KIKUU HURIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Dkt. Asha Rose Migiro kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Taarifa iliyotolewa Dare Es Salaam na kutiwa saini leo, Jumatano, Januari 30, 2013 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza Alhamisi ya Januari 17, mwaka huu wa 2013.


Mheshimiwa Asha Rose Migiro ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Katibu wa NEC wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Aidha, Dkt. Migiro amepata kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania. 
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
30 Januari, 2013

NENO LA LEO: MWAKA NI KAMA ELFU KUMI YA BONGO, UKIICHENJI INAPUKUTIKA!




8 68dc3

Ndugu zangu,
Leo ni mwisho wa mwezi  wa mwaka mpya. Na mwaka  ulivyo ni kama noti ya shilingi elfu kumi ya Bongo. Ukiichenji tu, utashangaa inavyopukutika!
Ukae sasa ukijua, kuwa kesho ndio Februari Mosi. Hivyo, mwaka mpya wa 2013, kama ilivyo kwa noti elfu kumi, ndio tutakuwa tumeuchenji. Subiri sasa uone siku, wiki na miezi inavyopukitika. Fumba na kufumbua utasikia tumeshaingia Juni tinaelekea Bajeti ya Serikali ya Julai, na ukitoka hapo utafikiri mwaka unateremsha milima ya Kitonga.
Inatukumbusha nini?


Umuhimu wa kupanga mambo yetu. Inahusu muda na matumizi ya muda. Na mwanadamu usipokuwa makini na muda, itakuwa sawa na kisa kile cha mzazi aliyeulizwa na wanawe; " Mbona nguo za Krismasi hatujanunuliwa?"

Mzazi akawajibu wanawe; " Jamani, Krismasi ya mwaka huu imekuja ghafla sana!"
Kana kwamba hakujua, kuwa kwenye kalenda ya mwaka tarehe ya Krismasi imeshawekwa, Desemba 25!
Ndio, Afrika mvua hainyeshi ghafla, huwa kuna dalili zake. Na katika maisha, mambo mengi hayaji ghafla, bali hutuka tukiwa hatujajiandaa. Jiandae na mwaka unaoanza kupukutika kuanzia kesho, kama noti ya shilingi elfu kumi. Kila la kheri.
Maggid Mjengwa,
Iringa.

Kikwete: Fujo za dini ni biashara inayolipa


NA MWANDISHI WETU

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa mtindo wa kufanya fujo na kusambabisha uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha dini nchini, ni biashara inayolipa sana na ndiyo maana wakereketwa wa kufanya fujo hizo hawaishi.

Aidha, Rais Kikwete amesema ni jambo la kushangaza mno kuwa zipo jitihada kubwa za kutumia dini kuinyumbisha nchi kwa sababu ya kisingizio kwamba Tanzania imekuwa na amani kwa muda mrefu sana.Hata hivyo, amesema Serikali yake haitayumba wala kusita kupambana ipasavyo na wafanya fujo za kidini kwa sababu kama kuna jambo moja linaloweza kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania, ni fujo za kidini na kuwa jambo hilo linahitaji kuchukuliwa maamuzi na hatua za busara.Rais Kikwete alizungumzia fujo za kidini alipowasilisha utetezi wa kuvutia na maelezo ya kina kuhusu Ripoti ya Mchakato wa Nchi za Afrika Kujithamini Zenyewe katika Nyanja za Demokrasia, Utawala Bora na Uchumi (APRM) iliyowasilishwa kwa wakuu wa nchi wanachama wa APRM kwenye mkutano uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia usiku wa Januari 26, mwaka huu.Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema Rais Kikwete aliwaambia wakuu wenzake wa nchi kwenye mkutano huo ambako Ripoti za APRM za Tanzania na Zambia ziliwasilishwa kuwa: “Nakaribisha kwa mikono miwili pendekezo la APRM kuwa serikali isimamie kwa uangalifu tofauti za kidini nchini. Kama mnavyojua, Tanzania imekuwa na amani na utulivu kwa sababu tumekuwa na bahati kutokuwa na ugomvi wa kikabila, kidini ama yale ya kutokana na rangi za watu. Hali hii inatokana na ukweli kuwa tumetunga na kuwa na sera zisizokuwa za kibaguzi kwa wananchi wetu kwa misingi ya kabila, dini, rangi ama sehemu anakotoka Mtanzania. Ni sera nzuri na tutazidumisha.”Aliongeza: “Uzuri kuhusu dini katika Tanzania ni kwamba tunaamini na kudumisha uhuru wa kuabudu kwa kila mtu. Serikali haina dini. Lakini tunajua fika kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na wanasiasa na viongozi wa dini wenye malengo ya kuchochea fujo za kidini. Hatutayumba wala kusita kupambana ipasavyo na watu wa namna hiyo. Pale ambako uchochezi wa kidini unafikia kiwango cha kuhatarisha amani ya nchi ama uvunjifu wa amani na sheria, dola ina haki ya kuingilia kati.”Rais Kikwete pia alitumia muda mwingi kuelezea jinsi Serikali ya Tanzania inavyoheshimu na kudumisha haki za binadamu na pia alisema amefurahishwa kuwa Ripoti ya APRM imeelezea hatua ambazo Tanzania imekuwa ikichukua kustawisha na kuendeleza haki za binadamu katika miaka 50 ya uhuru wake.Alitoa mifano ya jinsi Tanzania inavyodumisha haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa kipengele cha kulinda haki za wananchi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1994.
CHANZO: NIPASHE

Ipo siku, uhuru wa fikra utawang’oa madikteta





DK. Mahathiri Mohammed alikuwa Waziri Mkuu wa Malaysia kwa miaka 22. Hata hivyo, haikuwa ni kazi nyepesi kwake kufikia nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi nchini humo, alipitia mitihani mingi na mikubwa.
Nitaieleza kidogo. Mahathir alikuwa muumini mkubwa wa usawa wa kiuchumi kati ya watu wenye asili ya China na wenyeji wa Malaysia wanaoitwa malays.
Wenyeji walikuwa wanaishi maisha magumu ya ufukara uliokithiri. Alichaguliwa kuwa mbunge katika Bunge la nchi hiyo, mwaka 1964 na akaamua kuwa sauti ya wanyonge wa Malaysia ndani ya Bunge na nje ya Bunge.
Mwaka 1968 aliandika makala kwenye gazeti moja la nchi hiyo na kusema ‘malaysia imevimba hasira za wengi na anahisi patatokea vurugu dhidi ya wachina’.
Wachina ndiyo waliokuwa wakishikilia uchumi wa Malaysia. Akaonya chama chake na serikali kuchukua hatua haraka bila kuchelewa. Hawakusikia. Akaitwa kwenye vikao vya chama chake cha UMNO ajieleze, akafukuzwa uanachama.
Mwaka mmoja baadaye yakatokea maafa makubwa nchini humo, zaidi ya watu 153 waliuawa jijini Kuala Lumpur. Mauaji hayo yanaitwa “matukio ya Mei 13, 1969”.
Hata hivyo, matukio hayo ya Mei yalibadili kabisa mwelekeo wa uchumi wa Malaysia. Mahathir alirudishwa kwenye chama mwaka 1974, akagombea tena ubunge, akashinda, akawa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Elimu, kisha Waziri wa Viwanda na Biashara (wizara yenye hadhi kuliko zote nchini humo). Mahathir Mohamad alichukua madaraka ya Uwaziri Mkuu wa Malaysia Julai 16, 1981, miaka 12 tangu afukuzwe uanachama wa chama chake kwa kusimamia yale anayoyaamini.
Historia itamwandika Mahathiri kama kiongozi pekee katika sura ya dunia aliyeweza kufuta umasikini wa nchi yake katika kipindi cha miongo miwili. Mwaka 1976 wakati anashika madaraka ya unaibu waziri mkuu, Malaysia ilikuwa na watu masikini asilimia 56 ya watu wake wote. Wakati anaondoka madarakani mwaka 2003, asilimia tatu tu ya watu wa Malaysia ndio walikuwa masikini. Rekodi hii haijawahi kufikiwa na nchi yoyote duniani.
Mahathiri alifanikiwa kuzungumza kama mwananchi wa kawaida, kiongozi wa kitaifa na mpinzani wa serikali na chama chake kwa wakati mmoja. Ni watu wachache sana wenye talanta ya namna hii na mara zote hupata misukosuko mingi, lakini hatimaye hushinda mitihani hiyo iwapo misukosuko hiyo haitamaliza maisha yao.
Mama Indira Gandhi aliyekuwa Waziri Mkuu wa India alipata misukosuko mingi, mingine aliishinda. Mingine ilimwangusha kwa muda na hatimaye maadui zake walimuua.
Naelewa kwamba mauaji ya Indira Gandhi yalisababishwa na chuki za watu wa kabila la sikhs nchini humo kutokana na ‘operation BlueStar’, hata hivyo vita ya mwaka 1971 na hali ya hatari aliyotangaza mwishoni mwa miaka ya sabini ilimfanya ajenge maadui wengi sana. Hata hivyo, kuna masuala kadhaa ya kujifunza kutoka katika maisha ya kihistoria ya mama huyu.
Baada ya baba yake Mzee Nehru kufariki na miaka michache baadaye wazee wa chama cha Congress kuamua kumteua Indira kuongoza chama chao, walitaraji kuwa watamtumia mwanamama huyu kufanya mambo yao watakavyo, akiwa hana msimamo wake au mwono wake wa India anayoiongoza.
Walikosea kumsoma. Indira aliungana na viongozi vijana wa chama cha Congress kufanya mabadiliko makubwa yenye mrengo wa kushoto dhidi ya mawazo ya wazee kama Morarji Desai aliyekuwa Waziri wa Fedha na mwenye mrengo wa kibepari katika kuendesha uchumi wa India.
Wakati Indira Gandhi na vijana walioitwa ‘young turks’ walikuwa wanasimamia misingi ya asili ya uanzishwaji wa chama chaCongress, msingi wa mabadiliko makubwa ya kijamii (‘prime instrument of social change’), wazee ambao waliitwa kwa kiingereza ‘syndicate of bosses’ walitaka kuendelea na hali ilivyo ambapo wenye nacho wanaendelea kufaidi matunda ya uchumi na watu masikini wanaendelea kuwa katika dimbwi la ufukara. Indira alichukua uamuzi wa kutaifisha benki zote na njia kuu za uchumi.
Wazee hawa wakamfukuza uanachama wa chama cha Congress. Indira Gandhi alianzisha chama kipya The Congress Requisitionistsambayo baadaye ilikuja kujulikana kama The Congress (I) ambapo watu waliita I kuwa inasimama kwa Indira!
Aliwashinda, akaendelea kuwa Waziri Mkuu wa nchi yake, akashindwa uchaguzi wa mwaka 1977.
Waliomshinda wakamkata na kumfunga jela hali iliyoleta taharuki nchi nzima, serikali mpya ikapoteza umaarufu kabisa kwani ajenda yao ilikuwa moja tu ‘chuki dhidi ya Indira’ na hawakuwa na ajenda ya kuijenga India. Mwaka 1979 chama cha Congress kilirudi madarakani. Indira aliuawa mwaka 1984 Oktoba, akiwa Waziri Mkuu wa India.
Tofauti ya Indira Gandhi na Mahathir ni kwamba Mahathir aliishi kuona mabadiliko makubwa aliyoyafanya kwa ajili ya nchi yake. Mama Indira hakuweza kuona lakini uamuzi wake wa miaka ya sabini kuhusu kilimo na maendeleo ya viwanda ndio umeipandisha India leo kuwa moja ya taifa lenye uchumi imara duniani.
Kwa nini leo nimeandika kuhusu watu hawa? Wasomaji wangu watakuwa wanahisia zao ambazo siwezi kuzizuia. Ujumbe wangu ni mwembamba sana kwamba mitihani kwenye siasa ni suala la kawaida.
Nchi yetu na vyama vyetu vya siasa vinapita kwenye vipindi vigumu sana. Hata hivyo, wachambuzi wetu wa masuala ya kisiasa hawayaweki haya mapito kwenye muktadha wa historia ama ya nchi yetu au ya mataifa mengine.
Vyama na nchi yetu imekuwa na vimekuwa ni mahala ambapo mawazo tofauti, maono tofauti na mitindo tofauti ya kufanya siasa au kuongoza imekuwa ni uadui na usaliti. Ni aghalabu sana kuona mtu ana mawazo tofauti bila kuonekana ametumiwa au amenunuliwa.
Mwanasiasa akisema jambo kinyume cha mawazo ya wenzake kwenye chama chake siku zote anaonekana ni mwanasiasa mkorofi na mipango inasukwa kumshughulikia mwanasiasa huyo.
Mwananchi akitoa mawazo tofauti na mawazo ya watawala anaonekana anatumika na watu wasiotajwa hata siku moja. Kiongozi wa kitaifa akionya kuhusu masuala fulani fulani ya nchi, atashambuliwa kwa kuonekana ni mbinafsi au anatafuta umaarufu. Hata kama mambo hayo hayo aliyoyasema yanakuja kusemwa baadaye na watu hao hao.
Nimesema hapo mwanzo, kwamba Mahathir Mohammad aliweza kuunganisha majukumu ya mwananchi wa kawaida, kiongozi wa kitaifa na mpinzani wa serikali kwa wakati mmoja. Mazingira ya kisiasa ya mwaka 1969 nchini Malaysia ndio yaliyopo hivi sasa nchini.
Mwanasiasa anayejaribu au kuthubutu kuwa mwanasiasa huru mwenye maono yake na mwenye uhuru wa kuweka mawazo hayo waziwazi, haishi kushambuliwa na kuitwa kila aina ya majina.
Mazingira ya ‘zidumu fikra za Mwenyekiti’ bado hayajaisha katika nchi yetu. Inafikia wakati hata kumpinga Rais wa nchi ni amani zaidi kuliko kumpinga kiongozi wa chama chako cha siasa, hii ni kwa vyama vyote.
Ukisoma maoni ya watu kuhusu suala la ‘matukio ya Mtwara Desemba 27, 2012’ utaona namna ambavyo taifa na uongozi vina uvundo wa uongozi mbovu na kuendeleza tabia ya ‘kutafuta mchawi’.
Mara moja viongozi walianza kusema watu wanatafuta umaarufu. Hata ndani ya vyama vya siasa ilionekana hivyo hata kama misimamo ya vyama hivyo ni dhahiri kabisa kuhusu suala la rasilimali za taifa.
Watu wa Mtwara walihitaji sauti ya kuwalinda, watawala wakaanza kushambulia sauti hizo kwa madai ya kipuuzi kabisa kama vile ‘kutafuta umaarufu’ ‘kununuliwa na wawekezaji’ nk ilihali wenye mamlaka wanasema ‘vurugu za Mtwara  zitakimbiza wawekezaji’.
Nani anayetumika na wawekezaji katika hali hiyo. Ndani ya vyama vya siasa nako kauli hizo hizo za watawala zinanunulika kwa maneno ya ubinafsi, kiherehere, kutafuta umaarufu, badala ya kutumia fursa za viongozi wenye kubobea kwenye masuala hayo kuongoza kuweka sawa ajenda ya wananchi.
Koffi Olomide amewahi kuimba ‘Lokuta eyaka na ascenseur, kasi verite eyei na escalier mpe ekomi’ ambayo ina maana ‘uongo hutumia lifti kupanda gorofa; ukweli hutumia ngazi lakini utafika tu. Ukiona uwezo wa viongozi wetu kufanyia kazi habari za uongo au hata wenyewe kutengeneza uongo, utajiuliza sana ubora wa uamuzi wao kuhusu nchi yetu. Viongozi wanasahu kuwa uongo huwafikia haraka sana kabla ya ukweli na hivyo wanapofanya uamuzi kutokana na uongo, ukweli ukifika inakuwa ‘too late’.
Naamini Ali Kiba au MwanaFA wataimba ‘ukweli hautengenezwi bali hutafutwa’.
Mahathir alifukuzwa uanachama wa UMNO kwa kosa moja kubwa sana, mawazo yake huru. Indira Gandhi alifanyiwa hujuma na wazee wa chama chake kwa kosa moja kubwa sana, mawazo yake huru. Wote walishinda na kuongoza nchi zao. Walivuka mitihani mikubwa.
Wakati mwingine ni vema kuwapa maadui zako watakacho na wewe kubakia ‘mwananchi, mwanasiasa wa kitaifa na mpinzani wa ‘status quo’.
source: Raia mwema Zitto Kabwe

SMZ yashtuka idadi ya watu kuongezeka kwa kasi



Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar , Balozi Seif Ali Iddy 


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewasisitiza Wazanzibari kutumia uzazi wa mpango ili kupunguza idadi ya watu ambayo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku katika visiwa vya Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga Mkutano wa 10 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Sensa ya 2002, Zanzibar ilikuwa na watu wapatao 980,000 na katika Sensa iliyofanywa mwaka jana 2012, ambapo ni miaka kumi baadaye, Zanzibar imekuwa na idadi ya watu 1,303,560 jambo ambalo Baloazi Seif alisema Serikali inapaswa kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wananchi wake.
“Mheshimiwa Spika ongezeko ni watu 323,560. Hili ni ongezeko kubwa sana. Hatuna budi sasa tufanye maarifa ya kupunguza kasi ya kuzaliana ili watoto wetu tuwalee vizuri zaidi,” alisema Balozi Seif mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Balozi Seif alisema idadi hiyo ya watu iliyoongezeka Zanzibar, Serikali haina budi kuwa na mipango madhubuti ya kudhibiti ongezeko la kasi la idadi hiyo ya watu na hivyo kushauri kuongeza bidii katika kufanya kazi na kuzalisha kwa wingi bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya watu wake ndani na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi.
Alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar jumla ya miradi 53 ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa yenye thamani ya wastani wa Sh97 bilioni katika sekta ya elimu, maji safi na salama, afya, kilimo, uvuvi na miundombinu ya habari, mawasiliano na barabara.
“Hii ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo nchi yetu imepiga katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati viongozi katika ngazi zote na wananchi wote kwa kushirikiana katika kufanikisha sherehe zetu hizi adimu ambazo zilifana sana,” alisema.
Akizungumzia suala la sheria zinazotungwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa nia ya kuwatumikia wananchi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasihi watekelezaji wa sheria hizo wazisimamie na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa ipasavyo bila ya kumuonea haya au aibu mtu yeyote atakayezikiuka sheria hizo.

source: Mwananchi
.

Siri mgogoro wa gesi yafichuka


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari kwenye makazi yake mkoani  Dodoma jana kuhusu hatua zilizochukuliwa kudhibiti vurugu za gesi mkoa wa Mtwara.Kulia ni waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi.Picha na Fidelis Felix 
Na Habel Chidawali, Dodoma na Abdallah Bakari, Mtwara 

MOJA ya mambo yaliyoamsha hisia za wakazi wa Mkoa wa Mtwara hadi kushinikiza kwa vurugu wakitaka gesi isitoke mkoani humo, ni taarifa kuwa nishati hiyo ingepelekwa wilayani Bagamoyo, nyumbani kwa Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema jana nyumbani kwake mjini Dodoma kuwa, mbali na imani hiyo, amebaini pia kuwa mpasuko ndani ya CCM mkoani Mtwara na harakati za kisiasa ni sababu nyingine iliyochochea mgogoro huo.

Pinda alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro huo ambao ulisababisha vifo vya watu wanne huku wengine wakijeruhiwa vibaya na uharibifu mkubwa wa mali zikiwamo nyumba za wabunge kuchomwa moto na namna alivyofanikiwa kuuzima.

Waziri Mkuu alifanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara, Januari 25 na 26 mwaka huu na kufanikiwa kuzima mgogoro huo baada ya kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya wadau wa gesi mkoani humo.
“Sasa hili nililitolea ufafanuzi kwa kukanusha kuwa siyo kweli kwamba gesi inakwenda Bagamoyo. Lakini pia baada ya kukaa nao nilibaini kuwa hata viongozi wenyewe wa CCM hawako pamoja,” alisema Pinda na kuongeza:

“Pamoja na hayo nikachukua maelezo kuhusu matatizo yao mengine na nikawaahidi kwamba nitayafikisha katika mamlaka husika ili waweze kuona namna ya kufanya.”

Madai kwamba gesi hiyo inapelekwa Bagamoyo yalikuwa moja ya ujumbe mkuu uliokuwa umeandikwa kwenye baadhi ya mabango wakati wa maandamano ya Desemba 27 mwaka jana yaliyofanyika Mtwara Mjini, yakiratibiwa na baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani.

Pinda alisema viongozi wa kisiasa mkoani Mtwara wakiwamo wabunge, wameonekana kuwa na mpasuko unaosababisha uchochezi kwa makundi ya watu.

Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya Waziri Mkuu, Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Alhaji Masoud Mbengula alikiri chama hicho kumeguka na akataja sababu kuwa ni makundi yaliyotokana na uchaguzi wa ndani uliofanyika mwaka jana.

“Tusiwe wanafiki, ni kweli kuna makundi ndani ya chama… wabunge hawako pamoja na ndiyo hali iliyotufikisha hapa… suala hili lipo wazi kabisa,” alisema Alhaji Mbengula.

Kamati ya Spika hatihati
Akizungumzia Kamati ya Bunge iliyotarajiwa kuundwa na Spika kwenda Mtwara kwa ajili ya kuwasikiliza wananchi wa huko, Pinda alisema hawezi kuingilia mhimili huo wa Dola isipokuwa atatoa taarifa bungeni na kama Spika ataona wabunge wameelewa, basi ataamua lolote.

“Nitakuwa na nafasi ya kuzungumzia jambo hili ndani ya Bunge na Spika akiona wabunge wamenielewa bila shaka atasitisha lakini akiona bado inafaa ataamua yeye,” alisema.

Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari jana, kiongozi huyo alifanya mazungumzo na Mawaziri wanaotoka Mkoa wa Mtwara ambao ni George Mkuchika (Utawala Bora) na Hawa Ghasia (Tamisemi) pamoja na wawekezaji wa kutoka China ambayo alisema yalilenga kuwapa halihalisi ya huko.

Nchimbi afunguka
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema vurugu hizo zimefikia mwisho na Serikali haitavumilia tena machafuko ya aina hiyo.

Dk Nchimbi alisema timu ya wataalamu ipo Mtwara kuweka mambo sawa na kusema Serikali itatimiza majukumu yake pasi na shaka yoyote na kusisitiza kuwa haiwezi kukubali Tanzania ikawa vipande.
Alisema Serikali inafanya tathmini kujua hali ilivyo Mtwara na ikibidi itasitisha shughuli zote za kisiasa mkoani humo.
Mtwara wampinga
Wakazi wa Mkoa wa Mtwara wamegawanyika baada ya ziara ya Waziri Mkuu baada ya baadhi yao kupinga mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi asilia kwa bomba kwenda Dar es Salaam.

Katika ziara yake, Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya manufaa yatakayopatikana mkoani Mtwara kutokana na uzalishaji wa nishati hiyo kiasi cha kumshangilia na kumpigia makofi.

Shura ya Maimamu Mtwara imesema jana kwamba haijaridhishwa na majibu iliyoyaita mepesi ya Waziri Mkuu katika hoja nzito na kwamba bado Serikali haijaupatia suluhu mgogoro huo.

“Baada ya kutoka pale tulifanya kikao kupitia maelezo ya Waziri Mkuu, kuna maeneo hatujaridhika … amezungumzia ‘powerplant’ (mtambo wa kufua umeme) kama mtambo wa kusafisha gesi, ndiyo aliousema utajengwa Madimba… lakini sisi tunahitaji ‘powerplant’, mashine za kufua umeme pamoja na hiyo ya kuchakata gesi iwe Mtwara… katika eneo hilo hatujaridhika,” Msemaji wa Shura hiyo, Sheikh Abubakar Mbuki alisema na kuongeza:

“Waziri Mkuu asituambie tu gharama za kutandaza nyaya ni kubwa kuliko bomba la gesi akaishia hapo. Atuambie gharama hizo ni kiasi gani badala ya kusema ni gharama kubwa… mbona gharama za bomba zipo wazi, kwa nini hizi za nyaya hazisemwi?”

Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Katani Katani alisema “Sijaelewa kabisa… nashangaa watu wanashangilia wakati madai yetu ya msingi hayajapata ufumbuzi… dai letu la kwanza lilikuwa viwanda vya kuchakata gesi vijengwe Mtwara, hilo limepatiwa ufumbuzi, la pili lilikuwa mitambo ya kufua umeme Megawati 600 ijengwe Mtwara.”

“Hili hajalipatia ufumbuzi, tunachokataa sisi wana Mtwara ni kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, tunataka mashine zinazojengwa Kinyerezi zihamishiwe Mtwara… kutuambia kupeleka umeme Dar es Salaam kwa njia ya nyaya ni gharama kubwa hilo sikubaliani.”

Alisema kutokana na kutopatikana kwa ufumbuzi wa dai hilo moja, bado wananchi wa Mtwara wataendelea kupinga mradi huo.

Akizungumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake juzi, Pinda alisema gesi ghafi haitasafirishwa kwa bomba kwenda Dar es Salaam na badala yake usindikaji utafanyika Mtwara.

“Wataalamu wanasema gesi haiwezi kwa namna yeyote ile kusafirishwa kama ilivyo, lazima ibadilishwe kuwa hewa au barafu… kiwanda cha kusafisha gesi kitajengwa Madimba, gesi yote itakayotoka Mnazi Bay itasafishwa hapo na masalia yote yatabaki huku ili kuvutia viwanda vya mbolea na vingine vinavyotumia malighafi hizo,” alisema Pinda na kuongeza:

“Kama tungekuwa tunasafirisha gesi ghafi basi hata kiwanda cha Dangote kisingejengwa hapa… gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme… tusaidieni wenzetu kuliokoa Taifa na tatizo la umeme.”
source: mwananchi