WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, July 28, 2014

Wajumbe Tume ya Warioba wafunguka


Wazungumzaji wakuu kwenye mdahalo wa Rasimu ya Katiba mpya uliopewa jina la �Nani anakwamisha kupatikana Katiba mpya,� Prof. Ibrahim Lipumba (kushoto), Stephen Wasira (katikati) na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni Mwanasheria, Tundu Lissu (kulia), wakiwa mbele ya hadhira kwenye ukumbi ulikofanyika mdahalo huo, jijini Dar es Salaam jana.

Baada ya kejeli, shutuma na udhalilishaji uliofanywa dhidi yao, wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ‘wamekikaanga’ Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukionya kisithubutu kubadili rasimu yenye maoni halisi ya wananchi.

Wajumbe wa tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, Humphrey Polepole na Awadhi, wametoa angalizo hilo wakati wa mdahalo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam kuhusu Katiba Mpya.

Wengine waliokuwa wazungumzaji katika mdahalo huo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano ya Umma), Stephen Wasira, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Kwa kipindi cha zaidi ya siku 60 la Bunge Maalum la Katiba linaloongozwa na Samuel Sitta, wajumbe wake hususani waliotokana na CCM, waliikejeli tume hiyo na kusema miongoni mwa wajumbe wake, hawana nia njema kwa nchi.

Karipio la Polepole na Awadhi linatokana na kuwapo mzozo unaohusishwa na pendekezo la kuwapo kwa muundo wa serikali tatu ambao unapingwa na CCM.Ingawa walipata muda mfupi katika mdahalo wa jana ulioandaliwa kupitia kipindi cha ‘Tanzania tunayoitaka,’ Polepole na  Awadhi, waliionya CCM kutoichakachua rasimu halisi huku wakiwaasa Watanzania kufuatilia mchakato huo kwa makini.

AWADHI
Awadhi, alisema tume ya Jaji Warioba ilikusanya maoni ya wananchi katika wilaya 143, ikifanya mikutano  12 kwa kila wilaya ya Tanzania Bara na 22 huko Zanzibar, hivyo kufanya jumla yake kuwa 1,700.

 Pia, alisema kulikuwa na mabaraza ya katiba 177 na kwamba asasi za kiraia 614 ziliunda mabaraza ambapo kwa ujumla wake, yalifanikisha kupatikana kwa rasimu halisi, hivyo akahoji, “iweje misingi yake ipinduliwe na kiundwe kitu kipya kwa watu 612?”

Hoja hiyo ilikuwa ni kujibu kauli tofauti zilizotolewa na Wasira ambaye alitumia takwimu kadhaa kuikosoa tume ya Warioba na kuhalalisha mabadiliko yanayofanywa na Bunge Maalum la Katiba.

Hata hivyo, Awadhi alipingana na Wasira kwa maelezo kuwa tume ya Warioba haikufikia kuandaa rasimu kupitia takwimu pekee.
“Tume ilichukua sampuli ya maoni, sasa kama wao (CCM) wanasema waliotaka serikali tatu ni wachache, wewe unapitisha serikali mbili kwa takwimu zipi?” alihoji.

Alisema, wajumbe wa iliyokuwa tume ya Jaji Warioba, wana haki ya kuendelea kuuzungumzia mchakato huo, licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuwakejeli na kumtaka Jaji Warioba ‘afunge mdomo.’

HOFU
Awadhi alisema ipo hatari kubwa kwa taifa ikiwa rasimu halisi ‘itachakachuliwa na kuruhusu kuwapo kwa serikali mbili. 
“Serikali mbili ina mambo mengi ambayo rasimu inayojadiliwa haina,” alisema na kutaja miongoni mwa hayo kuwa ni haki za adhi, serikali za mitaa na rasilimali za umma, kwa kadri ilivyowasilishwa na wananchi.

“Maoni ya wananchi yaliyogusia haki hizo na nyingine yalizungumzwa kwa misingi mikuu ambayo huwezi kwenda kudai kupitia rasimu hii (iliyochakachuliwa,” alisema.

WENGI NA WACHACHE:
Awadhi, alisema hoja dhana ya ‘walio wengi’ na      `wachache’ ni matokeo ya mifumo mikongwe na Katiba ya sasa inayolalamikiwa, na kwamba kutumia (mifumo mikongwe) izalishe Katiba Mpya italiingiza taifa kwenye matatizo.

POLEPOLE: HATUKUWA NA MISIMAMO YA KISIASA
Naye Polepole, alisema wajumbe wa tume ya jaji Warioba, hawakuongozwa na misimamo ya kisiasa, bali maoni ya wananchi.
Hata hivyo, alisema kuna mambo mengi hayamo kwenye rasimu na hayakujitokeza, hali inayowaumiza mioyo, na kwamba mengine yalitajwa kwenye mdahalo huo. 

“Si vema na haki kinachoendelea sasa hivi ingawa Katiba Mpya ni mchakato wa kisheria na siasa, lakini hiyo haina maana kwamba umilikiwe na vyama vya siasa,” alisema.

Alisema Katiba Mpya inahitaji kujenga muafaka, kufikia maridhiano, kuweka nidhamu kwenye mjadala, ushiriki makini unaozingatia uhuru wa wajumbe, mambo aliyosema hayajaonekana hadi sasa.

Alisema mchakato huo ukiachwa kwa vyama vya siasa kwa kudhani wana dhamana ya kuleta Katiba Mpya, hakutalitendea haki taifa hili.

PINDA: VIONGOZI WA DINI WAOMBEENI UKAWA
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaomba viongozi wa dini nchini kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili warudi bungeni kumaliza mchakato wa katiba.

Alitoa ombi hilo wakati wa ibada maalumu ya kumsimika Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ruvuma, Amoni Mwenda, kwenye kanisa hilo Usharika wa Songea, ambako mamia ya waumini pamoja na viongozi, wakiwamo maaskofu, mawaziri na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu walihudhuria.
CHANZO: NIPASHE

Wednesday, July 23, 2014

KHAMIS KIIZA ‘DIEGO’ APIGWA CHINI YANGA SC, OKWI KUENDELEA KUWIKA!

KLABU ya Yanga imembwaga mshambuliaji wake Mganda, Khamis Kiiza ‘Diego wa Kampala’ baada ya kusajiliwa kwa Wabrazil wawili, Andrey Coutinho na Geilson Santos Santana `Jaja`.Baada ya Jaja kusaini mkataba wa miaka miwili jana makao makuu ya klabu ya Yanga, kulikuwa na utata ni mchezaji gani atapigwa chini kati ya Kiiza na Emmanuel Anord Okwi.Awali ujio wa Jaja ulielezwa kuwaweka kitimoto Kiiza na Okwi, huku mmojawapo akitakiwa kutolewa kafara.
Taarifa za uhakika ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba kocha Maximo amependekeza kuachwa kwa Kiiza kutokana na ripoti iliyoachwa na Hans Van Der Pluijm.

Mzigo huo uliofuatwa chini ya kapeti unasema kuwa Pluijm katika ripoti yake aliyowasilisha kwa viongozi baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, alisema ili Emmanuel Okwi acheze Yanga sc, lazima Kiiza aondolewe.

Kwa kuzingatia mapendekezo hayo, Maximo amefuata ushauri huo na sasa Kiiza rasmi anaondoka Jangwani.

Katika hatua nyingine, imeelezwa na chanzo cha uhakika kuwa Maximo amewabana viongozi wa Yanga akiwataka wajenge uwanja wa mazoezi wa Kaunda ili kuepukana na adhaa anayoipata.

Maximo amewakazia na amesema hakuna jinsi, lazima uwanja huo ujengwe muda huu.

Pia amewataka viongozi kuboresha vyumba vya jengo la Jangwani ili wachezaji wote waishe pale.

Taarifa zinasema, Maximo amesema haiwezekani timu kukaa saa mbili kwenye foleni inapoelekea uwanjani na kurudi kambini.

Kwa mazingira hayo anataka wachezaji wake wakae makao makuu ya Yanga, mitaa ya Twiga na Jangwani, halafu uwanja  wa Kaunda ujengwe.

Mbrazil, Marcio Maximo anafahamika kwa kuwa na msimamo mkali katika mambo yake.

chanzo: matukiotz.com

LOGA AULA MKATABA I YA MWAKA MMOJA SIMBA SC, ATAMBA KUTWAA UBINGWA MSIMU UJAO!

KAMA ilivyotegemewa na kushauriwa na watu wengi, uongozi wa klabu ya Simba chini ya rais Evans Aveva umemsainisha mkataba wa mwaka mmoja kocha mkuu wa klabu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Loga amesaini mkataba huo leo makau makuu ya klabu ya Simba, mtaa wa Msimbazi, Kariokoo jijini Dar es salaam na kueleza kuwa kikosi chake kitakuwa bora  msimu ujao, huku lengo kubwa likiwa ni kutwaa ubingwa.
Kitendo cha kupewa kandarasi ya mwaka mmoja kimemfurahisa Logarusic  na kuahidi mambo mazuri kwa mashabiki na wanachama wa Simba katika mikikimikiki ya ligi kuu msimuawa 2014/2015 unaotarajia kuanza septemba 20 mwaka huu.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange `Kaburu` ndiye aliongoza zoezi la kumsainisha Loga kandarasi hiyo.
Kaburu alieleza kuwa uongozi umeamua kumpa majukumu kocha huyo na msalaba uliopo mbele yake ni kuhakikisha Simba inarudisha heshima kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu bara.
Kwa upande wa kocha msaidizi, Suleiman Abdallah Matola `Veron`, Kaburu alisema kocha huyo tayari alishasaini mkataba wa miaka miwili tangu mwezi desema mwaka jana, hivyo hakuna mabadiliko.
Awali kulikuwa na taarifa za uongozi wa Simba kumtimua Loga, lakini uongozi umeamua kumbakisha kwa kueleza kuwa wameridhishwa na utendaji wa kazi yake.
Kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya alijiunga na Simba desemba mwaka jana na mechi ya kwanza kuiongozo Simba ilikuwa ile ya Nani Mtani Jembe ambapo alishinda mabao 3-2.
Hata hivyo alipoanza kushiriki ligi kuu mzunguka wa pili baada ya kurithi mikoba ya Abdallah Kibadeni, Loga alimaliza msimu kwa kushika nafasi ya nne.
Mcroatia huyo anasifika kwa kuwa na msimamo mkali hasa suala la nidhamu kwa wachezaji.
Mara kadhaa wachezaji walidai kocha huyo ni mkali mno na kuna wakati anashindwa kuwatetea badala yake anawakalipia.

Lakini kwa tamadauni za wachezaji wa Tanzania, nidhamu ya mpira ni ndogo na kocha anayewasimamia sana anaonekana kuwa mbaya.

chanzo: matukiotz.com

Tuesday, July 22, 2014

JK AFUNGUA BARABARA YA PERAMIHO-MBINGA 78KM


Barabara ya Peramiho -Mbinga yenye urefu wa Kilometa 78 iliyofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa pamoja na Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wa Serikali wakivuta utepe kuashiria ufunguzi wa barabara ya Peramiho-Mbinga yenye urefu wa Kilometa 78.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wa kwanza kulia akizungumza na Waziri wa Ujenzi Dkt.John Magufuli kabla ya uzinduzi wa barabara ya Peramiho-Mbinga 78km .Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu. (FRIDAY SIMBAYA)

source: mjengwa blog

Monday, July 14, 2014

Rasimu ya Katiba; Hivi Watanzania tulitaka nini?

KATIKA wakati huu, Nauona  umuhimu wa kukumbushana swali hili nililopata kuliuliza. Maana, kwa mwanadamu usipojua unataka nini, basi, usishangazwe na matokeo ya ulichokifanyia kazi. Chaweza kuwa chochote kile.
Na swali hili la mfumo wa Serikali si mwanzo wa mwisho wa matatizo yetu yajayo kama taifa, bali ni mwisho wa mwanzo wa tulichodhani kuwa ni kutatua matatizo yetu ya muungano.
Tunakoelekea si kuzuri, maana, tumeamua kuacha kutumia busara na hekima na badala yake tunatanguliza ushabiki wa vyama na hata makundi na watu tunaowapenda. Yako wapi mapenzi kwa nchi tuliyozaliwa?
Maana, tulidhani ni mabadiliko makubwa yamefanyika katika nchi yetu pale ulipozinduliwa kwa kishindo mchakato wa kupata Katiba Mpya. Wengi wameanza kukata tamaa.
Tulidhani yangelikuwa  mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika tangu mwaka 1977. Ni  pale ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo wa 1977 yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa chama tawala na hata mfumo wa uongozi wa Serikali.
Katika  dunia hii, mabadiliko ya kijamii hupelekea mabadiliko ya kisiasa. Na WanaShosholojia  wanasema, kuwa sababu mbili zenye kupelekea mabadiliko hayo; sababu za ndani ya jamii husika (endogenous) na sababu za nje ya jamii (exogenous).
Kwa upande wetu, tunaona kuwa, sababu za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma kwenye kufikia hatua hii ya kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.
Na kwa jamii yetu kwa upana wake, ingelikuwa na  sababu za msingi  za kuyafurahia mabadiliko haya, maana, ni sawa na mwanadamu aliyepewa kikombe chenye nusu ujazo wa maziwa.  Utafahamu kama amefurahia au amechukizwa kwa namna  atakavyochagua kukielezea kikombe kile; anayekiona ni ’ kikombe nusu cha maziwa’  anaonyesha kutoridhika, na anayekiona ni  ’ kikombe kilichobaki  nusu tu kujaa’ huyo amekifurahia na anaonyesha matumaini kuwa iko siku kitajaa. Inahusu kuwa na matarajio chanya (Optimism) na kuwa na matarajio hasi (Pessimism)
Na hakika, Rais Jakaya Kikwete ameonyesha tangu mwanzo, dhamira yake ya kutuletea mabadiliko kama taifa.  Na Wajumbe wa Tume yaKatiba walifanya  kazi  njema iliyotufikisha kwenye hatua ya kuwepo kwa Rasimu ya kwanza ya Katiba na hata ya Pili. 
Nimepata kuandika, kuwa  katika dunia ya sasa, hakuna anayeweza kuyazuia mabadiliko yanayotokana na msukumo wa ndani ya jamii- Kule Urusi ya zamani,  Mikhael  Gorbachev alipoanzisha mageuzi  makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi watu hawakuamini walichokiona. Gorbachev aliuona wakati uliobadilika.  Mabadiliko yale makubwa ya kimfumo kule Urusi yalipata majina mawili; Perestroika  na Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya na Glasnot ni uwazi .
Kabla ya mageuzi yale  makubwa, Urusi  ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana kwa  uwazi.  Jamii ilijawa hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha. Kulikuwa na  usiri mkubwa. Lakini, ndani ya kufichwa huko, kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa. Gorbachev,  daima atakumbukwa kwa  ’ Kuvunja Ukimya’ na kuifanya Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana sasa.
Na hakika,  ‘ Kuzaliwa  kwa  Katiba Mpya’  katika nchi ingelipaswa iwe ni  sawa na ’ Taifa kujivua gamba’.  Maana, kujivua gamba huku kama taifa kunapaswa kuendane na kuanza kubadili mifumo yetu ya kifikra. Tuanze sasa kufikiri juu ya malengo ya taifa, kwa maana ya ndoto za taifa letu badala ya kutanguliza sana malengo ya vyama vyetu au zaidi malengo binafsi ya vyeo na mamlaka.
Nchi yetu ni kama nyumba kongwe.  Tuendelee kwa umoja wetu kuifanya kazi ya  kuikarabati upya nyumba yetu. Ipate mwonekano mpya. Kuikarabati  upya nyumba kongwe huweza pia kupelekea kuibomoa nyumba yenyewe.  Kutakuwa na fito na  vipande vya matofali vya kurudishia. Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndio,   fito na matofali mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima yatupwe, basi. Na hapo utakuwa umeikarabati upya nyumba yako.
Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine  kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa.  Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu.
Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye kuambukiza kwa haraka.
Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa zetu. Hii ni  nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi  au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini.  Na imani ya wananchi kwa taifa na viongozi wao ni shina la matumaini  yao. Inakuwaje basi mwananchi  anapokosa imani na taifa na hata kwa kiongozi?  Katiba yetu iwe chachu ya kurudisha mioyo ya uzalendo kwa taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania.
www.raiamwema.co.tz: maggid mjengwa

K: UKAWA WAMENIWEKA NJIAPANDA

kikwete_6b75d.jpg
Mbeya/Moshi. Rais Jakaya Kikwete amesema msimamo wa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umemweka njiapanda sawa na Watanzania wengine wanaoshangaa.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipohutubia waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) waliokusanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo nchini. (MWANANCHI)(FS)


“Kwa sasa matumaini pekee ya Ukawa kurejea bungeni ni mazungumzo yanayoendelea, yanayovihusisha vyama vinne vikubwa nchini chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,” alisema Rais Kikwete.

Kauli ya Rais Kikwete ni ya pili kwa kiongozi wa juu kuwazungumzia Ukawa kuiweka Serikali njiapanda baada ya ile ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa Juni 26 mkoani Tanga.

Pinda alisema hatima ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea uamuzi wa wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni. Alikuwa akizungumza na mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa.

Awali Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Barnabas Mtokambali akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais alimwomba kuingilia kati kuhakikisha Bunge la Katiba linatimiza matakwa yaliyokusudiwa.

Askofu Mtokambali alimsihi Rais kukwamua mgogoro uliopo kwa kuhakikisha wajumbe wa Bunge la Katiba wanaungana na kutekeleza matakwa ya sheria, kanuni ya kupata Katiba Mapya.

Akijibu, Rais Kikwete alisema masikitiko ya Askofu huyo na Watanzania wengine ni sawa na masikitiko yake na kwamba rai yake ni kuwasihi wajumbe hao wajipange kurejea kwenye mkutano ujao wa Bunge la Katiba.

Hata hivyo, alifafanua kwamba hatua pekee ambayo inatoa mwanga wa kuleta suluhu ni ile aliyoichukua msajili wa vyama vya siasa nchini kuwaita viongozi wakuu wa vyama vya CUF, Chadema, CCM na NCCR-Mageuzi hivi karibuni ambako viongozi hao wameonyesha ukomavu katika mazungumzo mazuri na yenye mwelekeo wa matumaini.

“Nampongeza msajili wa vyama vya siasa kwa hekima aliyoitumia kwa kuanzisha mazungumzo hayo na nawashukuru sana viongozi wa vyama vya siasa husika kwa kujadili kwa busara yenye mwelekeo wa kutatua tatizo hilo,” alisema.

Alisema vyama vinavyoshiriki kwenye mazungumzo hayo ndiyo vikubwa nchini na kwa vyovyote vile mambo yatakwenda vizuri hata hivyo alifafanua kuwa mazungumzo ya aina hiyo pia yanatarajiwa kuwashirikisha wadau wengine.

Nawaomba maaskofu, masheikh, wachungaji, maimamu, manabii kuwaombea wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba Mpya warudi bungeni Agosti 5 kukamilisha kazi ndani ya siku 60 nilizowaongezea bila kuomba nyingine tena,’’ alisema.

source: mjengwa blog