WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, February 5, 2015

Mawaziri wajibikeni si kusubiri kutishwa


Katuni.
Katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma mawaziri wameendelea kukamiwa na wabunge kutokana na utendaji wao ambao unatiliwa shaka.
 
Kikubwa ni malalamiko kuhusu wizara zao na kushindikana kutekelezwa kwa majukumu mbalimbali hali inayoathiri uwezo wa serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
 
Kwa mfano, Waziri wa Maliasi na Utalii, Lazaro Nyalandu, alikamiwa vilivyo na wabunge akidaiwa kuzembea kutangaza katika gazeti la serikali tozo mpya ya hoteli za kitalii katika hifadhi za taifa, hivyo kusababisha serikali kukosa mapato ya Sh. bilioni 80. 
 
Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2014, iliyowasilishwa bungeni ilisema kuwa Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), inapoteza Sh. bilioni mbili kila mwezi kupitia tozo mpya kwa mfumo wa ‘fixed rate’ badala ya mfumo wa zamani ‘Concession rate’ katika kipindi cha kuanzia Septemba mwaka jana mpaka hivi sasa.
 
Kamati hiyo pia ilisema Septemba 12, mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wamiliki wa hoteli zilizoko katika Hifadhi za Taifa dhidi ya Tanapa kupinga shirika hilo kuanza kutoza tozo mpya kwa mfumo wa fixed rate badala ya Concession rate.
 
Bunge pia lilielezwa kuwa hukumu hiyo iliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa tangazo katika gazeti la serikali kuhusu kuanza kutumika kwa tozo mpya, lakini ni takriban miezi minne sasa tangu kutolewa kwa hukumu hiyo tangazo hilo halijatolewa.
 
Bunge pia lilielezwa kuwa ni kwa msingi huo Tanapa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zinaendelea kupoteza mapato yanayofikia Sh. bilioni mbili kila mwezi, huku serikali ikilia kila siku haina fedha za kutimiza majukumu yake mbalimbali.
 
Ingawa hasara ya Sh. bilioni 80 ambayo serikali imepata inakokotolewa kuanzia mwaka 2011 kesi hiyo ilipofunguliwa hadi Septemba 2014, hata Kamati ya Bunge ilipoitaka Wizara ya Maliasili na Utalii iwe imeshatoa tangazo hilo hadi kufikia Januari 28, mwaka huu, bado imeendelea kuvuta miguu.
 
Mashambulizi mengine yalielekezwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwamba alisaidia mwekezaji mmoja jijini Dar es salaam kupata kiwanja, lakini halipi kodi ya Sh. bilioni 3 kwa Manispaa ya Kinondoni. 
 
Ingawa kwa desturi mwaka wa uchaguzi wabunge huwa wakali zaidi dhidi ya serikali, na kwa kweli mawaziri wengi huwa majeruhi kama ambavyo ilishuhudiwa kwenye mkutano wa Bunge wa 17 na 18 mwaka jana mwishoni kuhusiana na kashfa ya Tegeta ESCROW, mawaziri wengi wamekuwa ni kikwazo kikubwa kwa serikali kutekeleza majukumu yake.
 
Tunajua ni jukumu la Bunge kikatiba kuisimamia serikali. Ni kweli pia kwamba Bunge likilala na serikali pia hulala, lakini utaratibu huu wa mawaziri kusubiri kukaliwa kooni na wabunge ndipo watekeleze majukumu yao hakika hauwezi kuiponja nchi.
 
Tunakumbuka jinsi sakata la Tokomeza lilivyoleta mtafaruku bungeni mwaka juzi, hatimaye likaondoka na mawaziri wanne; ndivyo pia ilivyokuwa mwaka 2012 juu ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2009/10 pamoja na kashfa nyingine ziliwafanya wabunge wawang’ang’anie mawaziri sita, lakini wakaondolewa watano.
 
Pamoja na siasa zote zinazoweza kuwa zinachangia ukali wa wabunge dhidi ya serikali au waziri mmoja mmoja, hasa inapotiliwa maanani kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi ambao kila mwanasiasa anatupa karata yake kwa ajili ya kujipanga kwa uchaguzi baadaye mwaka huu, mwenendo wa mawaziri wengi kusubiri kushurutishwa ndipo wafanye kazi, kwa kweli unapaswa kubadilika.
 
Kwa wastani tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani kila baada ya miaka miwili na ushei hivi imekuwa inabadilisha mawaziri. Kila wanapobadilishwa kwa hakika ni baada ya wabunge kuwa mbogo. 
 
Kila wakati wabunge wanapowakamia mawaziri ambao wamekuwa ni tatizo katika utendaji wanaungana kwa pamoja, wa chama tawala na kambi ya upinzani. Hali hii ingawa inatajwa kama moja ya mafanikio ya Bunge katika kuisimamia serikali, bado siyo siha njema ya kiutendaji kwa upande wa serikali.
 
Ni dhahiri mawaziri wanajua wajibu wao, wanajua kuwa wako serikalini na kazi yao kubwa ni kuhakikisha serikali inatekeleza majukumu yake, kila wizara kwa sehemu yake. Ni jambo la fedheha kwamba baadhi ya mawaziri wanaona fahari kuwa viti vya mstari mbele bungeni, lakini kwa kweli utendaji wao ukiwa hauakisi hata chembe hadhi na heshima waliopewa na taifa kukalia viti hivyo.
 
Uzembe huo ambao umesababisha mabadiliko ya mawaziri kila baada ya miaka miwili hivi, umesababisha hata kasi ya utendaji na usimamiaji wa shughuli za serikali ndani ya wizara kuwa ndogo. Kila waziri mpya anayeingia kwenye wizara anachukua muda kuwa na kasi ya kutenda kwa kuwa ni lazima ajifunze baadhi ya mambo. Busara ya kawaida inaelekeza kujifunza kwanza kuhusu mazingira mapya kabla ya kuanza kuleta mabadiliko chanya.
 
Ni rai yetu leo kwamba wakati sasa umefika kwa mawaziri kutambua wajibu wao na wasisubiri wabunge wawe wakali ndipo wawajibike kulingana na majukumu waliokabidhiwa na rais. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment