Hakuna kitu kibaya katika maendeleo ya jamii yetu kama siasa ikitumika vibaya katika maumuzi mbalimbali; Siasa ni safi sana usipoijua haitakusumbua, lakini ukiijua na ukiendekeza kwa misingi tu ya siasa inaweza kukupa ugonjwa wa moyo na itakupa shida; kwa mtazamo mwingine siasa kwa nchi zetu ambazo tunaziita dunia ya tatu mara nyingi zinarudisha maendeleo nyuma katika kivuli cha unafiki wakati wanasiasa wakivaa ngozi ya kondoo wakati kwa ujumla wao ni chui wa ubinafsi;
Mtihani mkubwa ambao unawakabili sana wananchi wanatakiwa kweli wajue wanasiasa ni nani pamoja na mapenzi ya vyama vyao; kwa maneno mengine wananchi wanatakiwa kuelewa kuwa Siasa ni matokeo ya wanasiasa, wakiwa wenye hekima na waliojaa busara siasa ni nzuri sana, lakini wakiwa wale ambao wanatafuta umaarufu siasa inakuwa haina tija kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa jumla. Kwa hiyo siasa hubaki kuwa ni porojo za kujinufaisha kwa kikundi Fulani cha watu, na maamuzi yao daima yanalenga sana katika unafiki na sio ukweli wa maendeleo; Maamuzi yao yanaendelea kuwa “sisi na wao” au “hiki ni chetu wao hawana haki
Unajua mwanasiasa wa kweli ni Yule ambaye atamwambia mwananchi ukweli hata kama anajua kwa kufanya hivyo utapoteza umarufu wake, lakini mwisho wa siku mwananchi atafaidika na maamuzi hayo kwa vizazi vijavyo;
Nionavyo mimi wanasiasa wetu wengi wamebaki na mtazamo unaolenga sana katika kuwafanya wao waweze kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali:
Hebu angalia wabunge wengi na kampeni zao je utetezi wao ni wa maendeleo endelevu au inaishia kumfurahisha mwananchi kwa kipindi Fulani? Na ukiangalia sana utetezi wao mwisho una kuwa na majuto makubwa “ Maafa ya Jagwani mfano, furaha ya wananchi kuishi kwenye bonde hilo ambalo sio salama imeleta matokea gani kwa taifa na wananchi kwa ujumla?furaha yao imedumu kwa kipindi kifupi sana tumejionea wenyewe;
Sasa lipi bora umwambie mwananchi ukweli ajue na akasirike na akija kugundua kuwa ushauri wako ulikuwa mwiba kwake lakini umemletea amani na maendeleo endelevu, kwani haitaji tena kutafuta pesa kujenga nyumba nyingine, na kwa kweli kwa msimamo wako wa ukweli na unaofikiria miaka 100 mbele wananchi na vizazi vyao watakushukuru kwa maisha yao yote?
Nawauliza wanasiasa wetu, kweli wanakuwa na washuri wakuwashauri nini wanatakiwa kuzungumza ili wanachokiongee kiwe na tija kwa muda mrefu? Au wamezoea tu kuropoka kupata cheap popularity? Hebu liangalie sakata la kupanda kwa bei ya ferry kigamboni nini kinaendelea ni siasa au malumbano? Ni ufanisi au uwakilishi? Ni tija au kutafuta umaaurufu? Ongezeko la nauli linahitajika kwa sasa kulingana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na kushuka kwa shilingi au hakuna haja ya kupandisha?
Wanasiasa wanasahau kuwa siasa inatakiwa kuwa ni sehemu ya uongozi ambao unatakiwa utawaliwe na maadili ya kusimamia ukweli; siasa zetu na wanasiasa wetu wanatabia ya kufanya maamuzi ya pamoja, lakini tukumbuke falsafa ya maamuzi ya wengi ni kuwa “kila mtu miongoni mwao anapoiteza uwezo wake wa kufikiri sahihi na anaanza kufikiri kulingana na fikra za mwenzake na tatizo ni hili kama Yule mwenye ushawishi mkubwa atakuwa na mawazoa mgando basi itakuwa tatizo kwa wote”
Wanasiasa wanatakiwa wakumbuke yafuatayo;
· Kufanya vitu muhimu na vikubwa ni ngumu sana kwa wanansiasa na hata kutoa maelekezo ya mambo muhimu ni ngumu pia kwa ajili ya ufanisi, kwani mawazo mazuri na mazito mara nyingi yanaanza na mengi yataishia kugusa maisha ya watu kwa wakati uliopo na sio kwa faida ya baadae.
· Kadiri ambavyo wanafanya na kutekeleza wajibu wao bila kuogopa ndani ya jamii ni ukweli kuwa hata jamii itaendelea kuwahitaji na kamwe haitatamani wanasiasa hao waondoke madarakani;
wanasiasa tunaomba yafuatayo toka kwenu Chonde:
· Mtufungulie njia za maendeleo kwa kuwa wakweli;
· Tunawaomba mfanye kazi kwa umakinifu fikra zenu ziwe daima katika kuboresha maisha ya wananchi kwa utaratibu ambao utazingatia sheria zilizopo, uwezo wa kujiendesha sisi wenyewe kiuchumi ili kuboresha huduma kwa kuwatumia washauri wa ndani.
· Kuondoa woga wa kuthubutu kimaamuzi na kujua maendeleo maana yake ni nini? Tumefikaje hapa na sasa tufanye nini? Hebu angalia matatizo mengi ambayo Taifa limepitia ambayo imesababishwa na misimamo ya wanasiasa wake?
· je wanasiasa wameshajaribu kujiuliza kuwa kwanini tupo katika hali hii na tufanye nini kuibadilisha. Mmeshawahi kutoa changamoto kwa wananchi katika sehemu husika je tutayafikiaje maisha bora? Tupende au tusipende kamwe maisha bora hatyatapatikana kwa njia za mkato.
Katika mambo mengi ambayo wananchi wanayafurahia ni yale ambayo wananchi wanaambia kuwa tutaendelea bila kazi ngumu, mtatembea bure bila kulipa nauli hapo itakuwa shangwe; kwa kweli tatizo letu tunafurahia mambo ambayo yameshatengenezwa hata Marekani imeendelea kwa kujituma na kazi ngumu na wananchi wake kuambiwa ukweli;
Tutake tusitake msingi bora wa maendeleo lazima tuhakikishe kuwa wananchi wanashiriki kikamilifu katika kila hatua ya kujenga nchi na kuleta mabadiliko ambayo yanatokana na mikono yao wenyewe.
Kama taifa ili tuweze kusonga mbele Kimaendeleo kauli ya Baba Wa Taifa bado ina nguvu kwamba maendeleo yetu yatategemea sana “ Siasa safi iliyojaa uadilifu na sio unafiki; Watu ambao nasi lazima tujitume sisi wenyewe na kuondoa dhana ya kusubiri tufanyiwe kila kitu eti na wanasiasa; na uongozi ambao hauogopi kuondolewa madarakani kwa kumwambia mwananchi ukweli kwa ajili ya maendeleo yake na kizazi chake hapo baadae;
Huu ni muda wa kushirikiana wote tulete maendeleo ya nchi kwa haraka hebu tusimame na tufanye maamuzi ya kutufanya tuendelee kwa haraka kwa nyenzo zetu
Kamwe wanasiasa tusiwape nafasi ya kuendelea kutugawa sisi wananchi katika matabaka mawili;
- Tabaka la uadui miongoni mwetu sisi wenyewe
- kuendelea kututumia sisi
kama nyenzo/ngazi ya kujinufaisha na kufanikisha maisha binafsi?yao
No comments:
Post a Comment