WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 14, 2013

Ya Kenya na Rais wa nchi anapotoa machozi hadharani



MWAKA 2010 vyombo vya habari vya dunia vilimwonyesha Rais Hamid Karzai wa Afghanstan akitoa machozi hadharani.

Ni pale alipotamka kwa uchungu akielezea hali ya nchi hiyo kukosa amani; “ Watoto wangu watakwenda kuishi uhamishoni kwenye nchi za kigeni?…,” akaanza kububujikwa machozi.

Rais Karzai  alizungumza na kutoa  machozi kutokana na kuona hali halisi ya nchi yake. Kwamba kuendelea kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe na kukosekana kwa amani kutasababisha hata watoto wake mwenyewe ( Rais) kukimbilia uhamishoni. Jambo hilo lilimuuma sana. Tuna cha kujifunza.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliomalizika hivi karibuni, na kwa kurejea Uchaguzi wetu Mkuu uliopita na matokeo yake, tunaona, kuwa na Watanzania nao, kupitia Katiba mpya ijayo,  wanataka mabadiliko ya kimsingi. Hii si kiu ya chama cha siasa, ni kiu ya Watanzania kwa ujumla wao. Vyama vya siasa vina wajibu wa kusaidia kufanikisha kukidhi kiu hii ya wananchi.

Kwa chama tawala, kuruhusu kuanzishwa kwa mchakato wa kupata Katiba mpya si tendo la kuwafanyia ’hisani´wapinzani wa kisiasa, bali, ni wajibu wa kisiasa kwa maslahi ya nchi na kuna maslahi ya kisiasa hata kwa chama tawala.

Idadi ya Watanzania  wanaoonyesha kuchoshwa na hali iliyopo inaongezeka. Wanataka ijengwe misingi imara zaidi ya demokrasia. Wanataka haki zaidi za kidemokrasia na hivyo kuweza kupiga hatua zaidi za maendeleo ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu na nchi yao kwa ujumla.

Ni dhahiri, Katiba mpya inaweza kuwa nyenzo ya kutufikisha tunakotaka kwenda. Ikumbukwe, kuwa hata kabla ya Uchaguzi Mkuu wetu uliopita, tulimsikia Jaji Mkuu ( mstaafu) Augustino Ramadhani akitamka; kuwa Katiba ni waraka unaoishi ( a living document ). Kwamba inaweza kubadilika ili kukidhi  mahitaji ya wakati husika.

Ndiyo, wakati umefika. Na hata pale aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya,  Raila Odinga alipotua Mwanza mwaka 2010 aliweka wazi, kuwa Katiba ni jambo la wananchi. Inapofika wakati wananchi wanapohitaji marekebisho ya Katiba, ni vema jambo hilo likafanyika. Wao Kenya wamesubiri kwa miaka 47. Na sasa wameamua kuondokana na Katiba iliyotokana na mkoloni.

Ndiyo,  Katiba tuliyo nayo Tanzania ya tangu mwaka 1977, kwa macho, si ya wasomi wetu tu, hata watu wa kawaida, imeonekana haikidhi matakwa ya wakati uliopo. Ndiyo msingi wa hoja ya kuja kwa Katiba mpya.

Maana, katika nchi zetu, Katiba zimetokana na Katiba za mkoloni. Vifungu vingi vya Katiba vimekuwa ni kama kazi ya kunakiri na kupachika ( copy and paste) kutoka Katiba ya mkoloni. Kwa Wakoloni waliotawala nchi zetu, Katiba ilikuwa na maana moja kubwa; wachache kuandaa utaratibu wa kuwatawala walio wengi.

Waafrika tulio huru kutoka minyororo ya wakoloni, tunapaswa sasa kuandaa Katiba za kutuwezesha kujitawala, si kikundi kidogo cha Waafrika wenzetu kututawala. Ni makosa kuiacha kazi hiyo kufanywa na kikundi kidogo cha watu katika nchi, kwa maana ya chama cha siasa.

Hivyo, ni za kupongezwa, juhudi za Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete katika kuhakikisha Katiba mpya inapatikana kabla ya 2015.
Na hakika, kwa kutanguliza ubinafsi wetu, tunawaandalia watoto na wajukuu wetu, mazingira magumu ya kuishi kwa amani katika nchi yao. Katiba mpya ijayo, iwe ni kwa Tanzania ya leo, kesho na keshokutwa.  Ni urithi wa maana na wa kistaarabu tutakaowaachia watoto na wajukuu zetu. Na mathalan, Tume Huru ya Uchaguzi, ni DHAMANA ya kipekee ya amani na utulivu tutakayowaachia Watanzania wa vizazi vijavyo.

Maana, katika nchi zetu hizi,  mara nyingi  watu huanza kuhasimiana kutokana na kukosa imani  na wenye kuhesabu kura; na hasa Tume ya Uchaguzi.

Tujifunze pia kutoka kwa wenzetu. Kwa mfano, wenzetu kule Marekani katiba yao ina zaidi ya miaka 200,000. Kubadili kipengele tu katika katiba ya Marekani inaweza kuwa ni mchakato wa miaka 10. Hakuna hata Rais wa Marekani anayeweza kuichezea Katiba ya Marekani kwa maslahi yake, anaweza kuishia gerezani anayejaribu kufanya hivyo. Wamarekani wale hata wakimweka ‘mwendawazimu’ Ikulu wanajua namna ya kumdhibiti kikatiba.

Ni tofauti na sisi. Mwanafalsafa Charles Montesque aliyeasisi nadharia ya mihimili mitatu ya dola alikuwa na maana pia ya kumpunguzia Rais nguvu nyingi.

Wakati huo huo alitaka kuongeza nguvu kwa Bunge na Mahakama. Katika nchi zetu hizi, unapozungumzia kuliongezea nguvu Bunge na Mahakama, ina maana pia ya kutoa tafsiri ya kuipunguzia nguvu Serikali na kwa maana hiyo kumpunguzia nguvu Rais.

Leo tunatumia muda mwingi kujadili nani atateuliwa kuwa waziri kwenye baraza jipya. Kesho tutajadili nani atateuliwa kuwa mkuu wa mkoa. Keshokutwa tutajadili nani atakuwa mkuu wa wilaya. Tunajadili vyeo na watakaoshika vyeo hivyo. Ndivyo tulivyo. Hatujadili namna tutakavyowaumba wateule hao wawajibike kwa wananchi.

Na tujadili yale yenye maslahi mapana kwa nchi yetu, leo, kesho na keshokutwa. Nahitimisha.

source: Raia Mwema:  Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment