WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 14, 2013

TAMKO LA VIONGOZI WA KIISLAM JUU YA HALI YA UVUNJIFU WA AMANI NA UCHOCHEZI WA KIDINI NCHINI

JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM (T)
TAMKO LA VIONGOZI WA KIISLAM JUU YA HALI YA UVUNJIFU WA AMANI NA UCHOCHEZI WA KIDINI NCHINI
 
LILILOSOMWA KATIKA HOTELI YA LAMADA 09/03/2013
--
Sisi viongozi kutoka katika Jumuiya na Taasisi mbalimbali za Kiislamu nchini tumelazimika kukutana kutafakari na kujadili kwa kina hali ya uvunjifu wa amani na kuzorota kwa mahusiano ya kidini hapa nchini. Katika siku za karibuni tumeshuhudia hali ya uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali nchini mwetu. Na pia tumeshuhudia matamko mbali mbali kutoka kwa Viongozi wa Serikali, Viongozi wa dini na Asasi za kiraia kulaani na kuonya juu ya hatari inayoikabili nchi yetu.

 Pamoja na kuwa kumekuwepo na matukio mengi ya uvunjifu wa amani nchini kama kadhia ya mabucha ya nguruwe mwaka 1993, mauaji ya Waislamu katika Msikiti wa Mwembechai mwaka 1998, mauaji ya raia katika mikutano ya kisiasa, kutekwa na kuuawa kwa waandishi wa habari na matukio mengine mengi, lakini matukio ya hivi karibuni ya kushambuliwa viongozi wa dini yaliyotokea Zanzibar na vurugu za kidini mkoani Geita yamelitikisa Taifa. 

Ndugu wananchi na wanahabari, baada ya kukaa na kutafakari mwenendo wa matukio ya uvunjifu wa amani nchini na kutafakari baadhi ya kauli na matamko yanayotolewa na baadhi ya Viongozi wa Serikali, Jumuiya za Kidini na Asasi za kiraia tumeona tuseme yafuatayo: 

Mosi, Kumekuwepo na matukio kadhaa ya kusikitisha katika jamii, ya baadhi ya watu kushambuliwa, kujeruhiwa na hata wengine kuuawa. Jambo la kusikitisha sana ni kuwa baadhi ya kauli na matamko ya baadhi ya viongozi wa Serikali na Viongozi wa dini yanamuelekeo wa kukuza tatizo zaidi la mfarakano wa kidini kuliko kuleta maelewano miongoni mwa Wanadini mbalimbali, hasa Waislamu na Wakristo. 

Hatudhani kama kauli hizi zina nia njema. Imekuwa ni kawaida kila anaposhambuliwa au kuuawa Padri baadhi ya Viongozi wa Serikali, na wale wa Kikristo, vyombo vya habari, baadhi ya Asasi na taasisi za kiraia wamekuwa wakiwanyooshea vidole na kuelekeza lawama zao kwa jamii ya Waislamu kuwa wao ndiyo wahusika wa vurugu na mauaji ya viongozi wa kidini hata kabla ya uchunguzi kufanyika na kujulikana mhusika. 

Imekuwa ni jambo jepesi kuwanyooshea vidole Waislam pasina kuwa na ushahidi, hata pale matukio kama ya kushambulia na kuua ambayo yana hitaji uchunguzi wa kina, bila hata kusubiri uchunguzi wa vyombo vya usalama na Jeshi la Polisi, tayari Waislam wanalaumiwa. Hizi tuhuma za holela dhidi ya Waislam ndizo zinazopandikiza chuki kati ya Waislam na Wakiristo. 

Waislam wanahisi kuwa wao ni muhanga (victims) wa uvunjifu wa amani. Shutuma hizi za holela zisizokuwa na ushahidi zinawafanya Waislam wahisi kuwa hawatendewi haki, wananyanyaswa na kufanywa daraja la pili. Mathalani, 

(1) Chanzo cha mauaji yaliyofanywa na polisi Mwembechai mwaka 1998, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam wa wakati huo aliwalaumu waislam kuwa wanawakashifu wakristo. Bila hata kufanya uchunguzi haraharaka akawaomba radhi Wakristo na kuamuru polisi kufanya uvamizi na mauaji hayo ya Waislam. 

(2) Wakati mwingine serikali imekuwa ikitoa kauli za waziwazi za kuwahamasisha Wakristo wawaone Watanzania ambao ni Waislamu kuwa ni maadui zao na maadui wa taifa lao. Januari 2001, Waziri Mkuu wa wakati huo alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari kuwa Serikal, inazo taarifa kuwa kundi la magaidi waliopata mafunzo nchi za nje limerejea nchini na magaidi hao wanapanga kuilipua hospitali ya Muhimbili. Kufuatia kauli hiyo watu watatu waliokuwa watumishi wa Muhimbili ambao ni Waislamu akiwemo Profesa wa Micro-Biology walitiwa mbaroni na kuwekwa mahabusu. Japo baadaye waliachiwa kwani hawakuwa na hatia yoyote, lakini chuki dhidi ya waislam ilikuwa ishapandikizwa. 

(3) Tarehe 24 Agosti 2001 Waislamu walifanya maandamano kupinga kufungwa kwa Khamisi Dibagula kwa kusema Yesu si Mungu. Serikali kupitia jeshi la polisi likawatangazia wananchi wote kuwa Waislamu wamepanga kuyalipua makanisa siku ya Jumapili ya tarehe 2 Septemba 2001. Na Serikali ikawahakikishia Wakristo kuwa itaweka maaskari wa kuwalinda na hiyo shari ya Waislamu. Uzushi huu uliwachochea Wakristo wawachukie Waislamu na hivyo waunge mkono hatua za serikali za kuwakamata na kuwaadhibu. Hivi Waislam wajihisi vipi kwa tuhuma kama hizo zisizokuwa na ushahidi? Ni wazi mwenendo huu unawatia wasi wasi Waislam kuwa kuna agenda ya siri dhidi yao. Pili, Waislam kama Wanadamu wengine wanapenda kuishi kwa amani na utulivu. 

Hakuna binadamu anayependa kusemwa vibaya, kuishi kwa hofu na ukosefu wa amani. Mwenendo wa kuwalaumu waislam kuwa wanavunja amani si jambo la kuvumilia kwani linajenga mfarakano miongoni mwa Waislam na Wakristo. Ifike mahali basi serikali na viongozi wa Wakristo wawe na uadilifu, pale inapofanywa jinai basi sheria ichukue mkondo wake pale inapothibitika kuwa jinai imetendeka na mhusika kufikishwa mbele ya sheria; na siyo tu kukimbilia kutoa hukumu kabla ya uthibitisho wa kimahakama. Na pale Juma anapofanya jinai basi isemwe ni Juma na si Uislam. Mathalani; Hivi karibuni baada ya kuuawa kwa Padri Evarius Mushi huko Unguja tukio ambalo lilifuatia baada ya tukio jingine la kupigwa risasi na kujeruhiwa, kiongozi mwingine wa Kanisa, Padri Ambros Mkenda pia huko Unguja, Serikali kupitia Waziri wa mambo ya ndani ilitoa kauli kuwa ni matokeo ya kazi za ugaidi, huku baadhi ya vyombo vya habari vikitoa mwelekeo wa lawama kwa waislam na kuyahusisha mauaji hayo na Al-Shabaab, Al-Qaeda, Boko Haram na vikundi vingine vya Kiislam vinavyohusishwa na ugaidi. Serikali imetoa tamko hili bila hata kufanya uchunguzi kujua sababu za kuuawa kwa kiongozi huyo wa dini na hata bila kuwajua wauaji hao. Hii ni hatari kubwa sana. Kulikuwa na sababu gani kwa serikali kukimbilia kusema kuwa ni tukio la Kigaidi wakati haijafanya uchunguzi? Huku si kutoa mwelekeo wa majibu ya uchunguzi? Sasa tunaambiwa FBI wanafanya uchunguzi. Kwani kila mauaji yanayofanyika hapa nchini ni ugaidi? Inaonekana lengo ni kuwapaka tope Waislamu pamoja na dini yao. 

Lakini pia tunajiuliza, kwa nini serikali isubiri mpaka Padri auwawe halafu watoe kauli hiyo ambapo wangeliweza kuvidhibiti vikundi hivyo kabla hata huyo mtu hajauwawa, na kunusuru maisha yake ikiwa ilijua kuwa kuna magaidi? Wangelidhibitiwa hao wahalifu tusingelalamika, maana waislam tusingelituhumiwa. Viongozi wa Kikiristo pia wamekuwa wakitoa shutuma kuwa Padri Mushi ameuawa na waislam na kwamba mauaji hayo ni ya kidini. Kauli hizi za serikali na viongozi wa Wakristo ni hatari sana kwa amani ya nchi yetu.

 Kauli hizi zinachochea uhasama miongoni mwa Watanzania wakiamini kuwa kuna baadhi wanaandamwa kwa sababu ya dini yao.Ikumbukwe pia kuwa matukio ya kuuawa au kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini na wanadini si lazima yawe yamekusudiwa kidini. Mathalani;Gazeti la Rai la tarehe 7/11/2012 liliandika kwamba, mauaji yaProfesa Mwakyusa yalipangwa na kuratibiwa ndani ya shirika la watawa la Peramiho mkoani Ruvuma ambako inaelezwa ndimo walimo wahusika wakuu wa mauaji hayo kutokana na ugomvi wa umiliki wa mgodi wa dhahabu Lukarasi ulioko wilayani mbinga uliokuwa unamilikiwa na shirika la Benedikt la Peramiho.

 Taarifa hizo zilisema kwamba Profesa Mwakyusa alikuwa akihifadhi nyaraka za umiliki wa mgodi huo na yalikuwepo maagizo kutoka kwa mkubwa wa Shirika anayetajwa kwa jina la Fr. Lambert akiwaagiza Wakurugenzi walioteuliwa kusimamia hisa za shirika hilo kwenye mgodi huo kutofanya jambo lolote pasipo kumshirikisha Profesa Mwakyusa. Profesa Mwakyusa aliteuliwa na Buruda (father) Edmund na Buruda Aidani wote ikioneshwa wana hisa 2000 kwenye mgodi huo wa dhahabu. 

Tofauti za kimaslahi ndizo zilizosababisha kuuawa kwa Profesa Mwakyusa. Tukio lingine la uhalifu ni lile lililotokea katika Parokia ya Mikocheni Jimbo kuu la Dar es salaam mwaka jana Padri Audax Kaasa Paroko aliumia kwa kuvunjika mguu baada ya kuvamiwa na majambazi, nyumbani kwake (Mwananchi la 25/02/2013). 

Mwaka jana katika Jimbo la Iringa Mapadri wawili wa kanisa katoliki Paroko wa Isimani Padri Angelo Burged (60) na msaidizi wake Padri Herman Myalla (36) walishambuliwa na majambazi na kuumizwa vibaya kwa silaha zikiwamo risasi za moto na ambapo walinusurika kufa (Mwananchi la 25/02/2013). Kuuwawa na kujeruhiwa kwa viongozi wa dini zote nchini hakukuanza leo wala si kwa viongozi wa dini ya kikristo pekee. 

Hivi karibuni Mashekhe pia kujeruhiwa na kuuliwa, mbona Serikali haijasema kuwa huo ni mpango wa ugaidi? Imamu wa Msikiti wa Mwembetanga aliuwawa kwa kupigwa risasi na polisi Januari 26, 2001, na katibu wa muft wa Zanzibar alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana hapo Novemba 6, 2012. 

Pia Sheikh Ali Khamisi wa msikiti wa Mwakaje huko Unguja aliuawa kwa kupigwa mapanga akiwa shambani kwake Februari 22, 2013 lakini hakutajwa gaidi wala gaidi hajakamatwa. Serikali iwe makini isilichukulie jambo hili upande mmoja tu kuwa hayo ni mambo ya ugaidi na ugaidi huu ukaelekezwa kwa waislam, ni hatari. 

Hivi sasa vijana wa kiislam wanakamatwa na kutiwa ndani kwa tuhuma za uchochezi wa kidini na kusababisha kuuwawa kwa baadhi ya viongozi wa dini na wengine kujeruhiwa. Kamanda wa kanda maalum alisema hayo baada ya kuwa kuna vijana wa kiislam wanne wamekamatwa jijini Dare s Salaam katika juma lililopita. 

Vyombo vya dola vinapaswa kufanya shughuli zake kwa umakini katika kuyafuatilia kwa ukaribu matukio hayo ili isiwe chanzo cha kulitumbukiza Taifa letu katika vurugu za kidini. Kwa upande wetu tunaona huu ni wakati muafaka sasa kwa serikali na jamii mbali mbali kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo yaliyojitokeza ili kudumisha amani na utulivu badala ya kuleta propaganda na chuki dhidi ya jamii ya Waislam. 

VURUGU ZA KIDINI MKOANI GEITA
 Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vurugu zimesababishwa na maelekezo ya Maaskofu na Wachungaji kwa waumini wao kuchinja wanyama kwa ajili ya kitoweo na hata kuuza mitaani. Akizungumza na gazeti la mtazania la tarehe 11/02/2013, Mkuu wa wilaya ya Geita Manzie Mangochie alisema vurugu hizo zimekuwa zikichochewa na kituo kimoja cha redio mkoani Mwanza alisema kutokana na Mchungaji wa kanisa la FPCF kutumia vipaza sauti kutangaza kuwa lazima wachinje na nyama kusambazwa kwenye bucha zao. Alisema baada ya tamko hilo asubuhi yake Wakristo walichinja ng'ombe na mbuzi katika viwanja vya makanisa yao na kuisambaza katika bucha zilizopo soko la msufini. Ndipo waislam wakaitana kwenda kuzuia nyama hiyo isisambae kwenye soko la msufini na kununuliwa na waislamu wengine. Baada ya hapo ikatokea vurugu zilizopelekea kifo cha mchungaji na waislam sita kujeruhiwa vibaya. 

Tukio hilo pia lilisababisha uharibifu wa mali na baadhi ya watu kukamatwa. Cha kujiuliza ni kuwa hali hii imetoka wapi na chanzo chake ni nini? Miaka yote waislam wamekuwa ndio wachinjaji. Na hata pale viongozi wa serikali walipotoa maelekezo kuwa Serikali inatambua waislam ndio wanaopaswa kuchinjwa bado walitokea wachungaji na maaskofu kupinga. Je ujasiri huu wanautoa wapi? Mbona wachochezi hawa hawakamatwi? Sisi viongozi wa Jumuiya na Taasisi za kiislam tumesikitishwa sana na kauli ya Mhe. Waziri Mkuu kukataa kuwatoa waislam waliokamatwa katika tukio lile ili kujadili suluhisho la mgogoro, kwa madai ya kutokuwa na uwezo wa kuingilia suala hilo wakati wakristo walipompa sharti Mhe. Waziri wa mambo ya ndani alitekeleza mara moja kuwatoa wakristo wote waliokamatwa katika tukio lile. Hali hii inachochea chuki na hisia za kibaguzi miongoni mwa wananchi. 

MADAI YA WAISLAM Kumekuwa na juhudi za kupotosha ukweli juu ya madai ya Waislam hapa nchini. Lakini pia kuna juhudi kubwa zinazofanywa na baadhi ya Viongozi wa Serikali na wa dini kuwatoa Waislam kwenye madai yao ya msingi kwa propaganda za kuvuruga amani na utulivu. Madai makuu ya Waislam yasipotoshwe ni haya yafuatayo: 

• Serikali iweke na kutambua utaratibu wa kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi ambayo itaendeshwa na Waislamu wenyewe kama moja ya Mahakama za nchi. Mahakama za kadhi zitaendeshwa chini ya usimamizi wa Kadhi Mkuu na Naibu Kadhi Mkuu watakao chaguliwa na Waislamu kwa kuzingatia sifa za kielimu katika fani ya Sheria ya Kiislamu na kutambuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.Mashauri yote yanayohusu ndoa, talaka, mirathi, waqf, malezi ya watoto, hibba (zawadi), wosia, biashara, bima, benki kwa mujibu wa dini ya Kiislamu yasikilizwe katika Mahakama ya Kadhi alimradi mhusika/wahusika ni Waislamu. Waislam wanalidai hilo na wala si kosa la jinai na hamna ugaidi katika hilo. 

• Serikali itambue kuwepo kwa vyombo huru vinavyounganisha makundi mbalimbali ya wanadini husika na vyombo hivyo viwe na nafasi sawa katika uwakilishi wa masuala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa. Pia kuwe na utaratibu wa kutambua Jumuiya au Taasisi za kidini kwa nafasi sawa katika uwakilishi wa masuala ya kidini ndani ya Serikali. Au waumini wawe huru kuwa na taasisi itakayo wawakilisha katika masuala yao ya kitaifa. 

• Serikali ifute MoU kati ya Serikali na Taasisi za Kikristo na kuwafidia Waislam kiasi sawa cha fedha na fursa nyingine mbalimbali zilizokwenda katika Taasisi za Kikristo kupitia MoU.

 • Endapo MoU baina ya Serikali na Wakristo itaendelea, Serikali iwalipe fidia Waislam kwa kiasi sawa cha fedha na fursa yingine zilizokwenda katika Taasisi za Kikristo kupitia MoU pamoja na kuwekwa MoU baina ya serikali na Waislam. 

• Serikali ichukue hatua za haraka kutatua matatizo ya kudhulumiwa kwa wanafunzi Baraza la Mitihani (NECTA). Waislam walioneshea kidole hilo mwaka jana. Wanafunzi Waislam walipandishiwa viwango vya ufaulu wakafeli 70%. Viliporekebishwa wakafaulu kwa kiwango kikubwa zaidi ya hapo. 

Kama mwaka jana, mwaka huu Baraza la Mitihani lilipandisha tena viwango vya ufaulu kwa nchi nzima na kuleta janga hilo nchi nzima. Madai yetu ni yale yale kuwa serikali iuwajibishe uongozi wa Baraza la mitihani kwani unalipeleka Taifa letu mahala pabaya. 

HITIMISHO Ndugu wananchi na wanahabari, baada ya kukaa na kutafakari mwenendo wa matukio ya uvunjifu wa amani nchini na kutafakari baadhi ya kauli na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali, Jumuiya za Kidini na Asasi za kiraia tumeazimia yafuatayo. 

1. Sisi Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini tunaungana na wapenda amani wote kulaani kwa nguvu zote mauaji, manyanyaso na udhalilishaji wa aina yeyote unaowalenga viongozi wa dini. Mwenendo wa mauaji yenye kuwalenga viongozi wa dini yatalitumbukiza taifa letu kwenye janga kubwa iwapo hatua ya kurejesha amani haitachukuliwa. 

2.Tunawatahadharisha Viongozi wa Serikali na wa dini ya Kikristo kuwa makini katika kutoa kauli na matamko kuwashutumu Waislam kuhusika na mauaji bila ya kuwa na ushahidi kwani kauli hizo zinaweza kulitumbukiza Taifa kwenye machafuko ya kidini. 

3. Tunavitaka Vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uadilifu na uzalendo na kuepuka propaganda, chuki na uchochezi hasa inaporipoti matukio nyeti kama ya mauaji ili kuepusha Taifa letu kuingia katika vurugu za kidini na kuvuruga amani iliyopo nchini. 

4. Tunaiomba serikali kuacha kamata kamata dhidi ya Waislam kwa kisingizio cha uchochezi wa kidini. Vyombo vya dola vinatakiwa kufanya kazi zao kwa weledi, umakini na uadilifu katika kubaini wahalifu ili kuepusha kuwadhuru wasiohusika. 

5. Tunaunga mkono kauli ya Raisi Kikwete ya kuwepo kwa mjadala baina ya Wanadini mbalimbali ili kuzungumza na kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayochochea migogoro ya kidini hapa nchini. 

6. Kimsingi katika nchi hii hakuna mgogoro kati ya Waislam na Wakristo kwani tunaishi pamoja kwa kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii. Serikali inaweza kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani kutokana na kupuuza na kutoshughulikia madai ya msingi ya waislam. Madai hayo ni pamoja na tatizo la Baraza la Mitihani, Kuwepo kwa Mahakama ya kadhi, suala la Tanzania kujiunga na OIC na kuwepo kwa MoU kati ya Serikali na Kanisa nk. 

7.Tunawashukuru Waislamu wote kwa uvumilivu mkubwa mliouonesha katika kipindi hiki kigumu na kamata kamata ya Waislamu, kuadhibiwa na kuonywa kwa vyombo vya habari vya kiislam. (Radio Imaan na Gazeti la Annur). 

Tunawaomba kuendelea na Subra hiyo na kutochokozeka na kutotoka kwenye Agenda. Aidha tunawaomba Viongozi wote mliohudhuria kuwaomba Waumini wote kuzidisha dua na kumshitakia ALLAH (s.w) dhidi ya wale wote wanaokusudia mabaya dhidi ya dini yetu.
 
source: Haki Ngowi

No comments:

Post a Comment