Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Goefrey Nyange 'Kaburu'
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Goefrey Nyange
'Kaburu' pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope wametangaza
kujiuzulu nafasi zao ndani ya klabu hiyo kuanzia jana, imefahamika.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kaburu aliliambia gazeti hili kwamba
amefikia maamuzi hayo kutokana na wakati mgumu anaokumbana nao kwenye
klabu hiyo licha ya jitihada mbalimbali anazozifanya za kuhakikisha
Simba inasonga mbele.
Kaburu alisema anaamini kuwa baada ya kukaa pembeni, wanachama
wengine wenye uwezo wa kuongoza huenda wakapata mafanikio na kuifikisha
mbali klabu yao.
"Timu yetu ni ngumu sana kuiongoza, tunatukanwa... nimechoka," alisema Kaburu.
Awali, kabla ya Kaburu kufikia uamuzi mgumu wa kubwaga manyaga,
Kaburu alikiri kuona barua ya kujiuzulu kwa Hanspope na kueleza kwamba
ameiwasilisha kwa mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage kwa njia ya barua
pepe kwani hivi sasa (Rage) yuko nje ya nchi kwa matibabu.
Katika maelezo yake, Hanspoppe alisema ameamua kujiuzulu kufuatia
matokeo mabaya ya timu yao katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara na
pia kuondolewa kwao katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada
ya kupata kipigo cha jumla ya mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo de Libolo
ya Angola.
"Ni kweli nimejiuzulu nafasi zote nilizokuwa nashikilia ili tuwape
wengine nafasi," alisema Hanspope ambaye wiki iliyopita ndiye
aliyeongoza msafara wa Simba kwenda kuwavaa Libolo nchini Angola.
Hanspope alisema kuwa tayari ameshawasilisha barua yake ya
kujiuzulu kwa uongozi na anawatakia mafanikio Wanasimba wengine
watakaochukua nafasi zake.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, jana jioni alikiri kupokea barua za kujiuzulu kwa Kaburu na Hanspope.
Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu
ya Tanzania Bara wamekuwa wakishinikiza viongozi wao kuachia ngazi
kutokana na mfululizo wa sare na vipigo katika ligi kuu na pia
kuondolewa kwao mapema katika michuano ya Afrika.
Hata hivyo, Rage aliwahi kupuuza rai ya kutakiwa kujiuzulu kutoka
kwa baadhi ya wanachama kwa maelezo kwamba yeye siyo mchezaji wala kocha
na hivyo, wanaotakiwa kuhojiwa kufuatia matokeo yao mabaya ni watu wao
wa benchi la ufundi.
Aidha, uongozi wa Simba ulitangaza wiki iliyopita kupitia kwa
msemaji wao, Ezekile Kamwaga kuwa wataitisha mkutano mkuu wa dharura ili
kujadili mwenendo wa timu yao. Hata hivyo, Kamwaga hakusema ni lini
mkutano huo utafanyika.
Rage, Kaburu na viongozi wengine wa kuchaguliwa wa Simba waliingia
madarakani kwa ksihindo mwaka 2010 na kwa mujibu wa katiba ya klabu yao,
watamaliza muda wao wa kuongoza mwakani wakati utakapofanyika uchaguzi
mkuu mwingine.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment