MARA
kadhaa huwa nikifikiria baadhi ya riwaya na hekaya tulizosoma tukiwa
wadogo najiuliza iwapo walioziandika walijua wanatuandikia sisi au la,
lakini jibu nililolipata hadi sasa, na ambalo lina chembe chembe nyingi
zaidi za usahihi ni moja, nalo ni kwamba jamii nyingi duniani, na watu
wengi duniani, wamewahi kufanya mambo ya kipuuzi na ya kijuha kabla
yetu.
Hii inatufanya tukose sifa ya kuwa waanzilishi wa ujuha, kwani
walikwisha kutangulia wengine ambao matendo yao ndiyo yaliyozalisha
hekaya tulizosoma.
Baadhi ya hekaya hizo ziliibuliwa na matendo halisia ya watu
waliowahi kuishi huko zamani, lakini nyingine zilikuwa ni hadithi za
kubuni ingawaje zilitokana na matendo ya watu fulani katika jamii au
jamii nzima. Lengo la hadithi hizi huwa ni kutoa mafundisho na maonyo
kuhusu hasara za kufanya mambo ya hovyo na faida za kutenda mambo
yanayopasa.
Hekaya moja imenijia katika kumbukumbu zangu, ingawaje sikumbuki
iwapo ilitokana na Abou Nawas (Abunwasi, kama tulivyomjua sisi
Waswahili) au Esopo au mtu mwingine aliyeishi kale zaidi.
(Kwa wale wasiomjua Abou Nawas, huyu alikuwa msomi, mwanafalsa,
mshairi na mwanasayansi aliyeishi zama za Haroun al Rashid, Khalifa wa
Baghdad (miaka 786-809) enzi za mwamko mkuu wa Kiislamu na Kiarabu
katika fani nyingi za sayansi na utafiti. Naye Esopo alikuwa mtumwa
wa Uyunani aliyeishi miaka 600 kabla ya Yesu kuzaliwa).
Hadithi yenyewe ninayotaka kuieleza ni ile ya juha aliyekutwa
akikata tawi la mti huku amelikalia. Alikuwa anatafuta kuni. Mpita njia
mmoja aliyemuona alimtanabahisha kwamba angeanguka, lakini mtema kuni
akaendelea na shughuli yake bila kumjali mpita njia.
Mtema kuni alipofanikiwa kulikata lile tawi, naye akadondoka chini,
pu! Na kuchunika hapa na pale, lakini hakufa. Na bado akawa na nguvu
kuondoka pale chini ya mti na kuelekea mjini kumsaka yule bwana
aliyemuonya kwamba angedondoka.
Alipompata alimtaka amueleze ni vipi alijua kwamba angeanguka, na
kwa sababu alikuwa amedhihirisha kipaji chake cha utabiri, sasa ni
lazima amjulishe siku yake ya kufa itawadia lini. Sikumbuki ni vipi
walimaliza ugomvi wao huo, kwani kulikuwa na kutoelewana kwa aina yake.
Funzo tunalopata hapa, pamoja na kutuasa kwamba tusikate matawi
tuliyoyakalia, ni kwamba katika mazingira mengine unaweza
kujisababishia matatizo kwa kusema jambo lililo dhahiri ukiwaambia watu
wasio na upeo wa kulitambua au wasiotaka kusumbua akili zao kidogo
kulitafakari, au walio wavivu mno kulifikiria, au walio na shughuli
nyingi muhimu kwao kuliko hilo unalowaambia.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kuhusu kisa cha wanafunzi wa kidato cha NNE
kushindwa vibaya katika mitihani ya mwaka jana. Wapita njia wengi
wamekuwa wakiiambia serikali kwamba imekalia tawi inalolikata na
itaanguka, lakini serikali, kwa miaka mingi, imekuwa ikiendelea kutema
kuni bila kujali.
Ilipojali ni pale, katika awamu ya tatu, chini ya urais wa Benjamin
Mkapa, ilipochukua hatua ya kuiadhibu HakiElimu ambayo ilikuwa
ikiitanabahisha serikali kuhusu elimu ya hovyo iliyotolewa kwa watoto
wa taifa hili.
Tawi ililokalia serikali lilikwisha kukatika kitambo, na serikali
(pamoja na sisi sote) ilikwisha kuchubuka tangu zama, lakini ni safari
hii ndipo serikali imetambua kwamba imedondoka, na imekwenda mjini
kumtafuta yule aliyeitanabahisha. Sijui ni kwa nini inamtafuta huyu
bwana, lakini inawezekana serikali nayo inataka iambiwe siku yake ya
kufa, na ndiyo maana ikawafuata watema kuni walioionya.
Serikali imeunda tume ya kuitabiria mustakabali wake, na katika tume
hiyo imewaingiza aliyekuwa mkurugenzi wa HakiElimu wakati shirika hilo
likiadhibiwa kwa kuiambia serikali isikate tawi ililolikalia, na
mbunge mmoja ambaye naye siku za hivi karibuni alitaka kupeleka bungeni
hoja ya kuchunguza tabia ya serikali yetu ya kukata matawi
iliyoyakalia, lakini akapuuzwa na hoja yake ikatupiliwa mbali siku
chache kabla ya tawi kukatika na mti mzima kutikisika.
Masuala mengi ya kitaifa ni magumu, yana miingilio na mitokeo
lukuki, yamejificha na yanahitaji weledi mkubwa kuyang’amua na
kuyashughulikia kwa kiwango cha kuridhisha, na mara nyingi hukabidhiwa
kwa wataalamu wenye weledi wa kiwango cha juu kuyakabili.
Hakuna kilichojificha katika kuporomoka kwa viwango vya elimu nchini
humu; kila kitu kiko barabarani, ni sawa na kukalia tawi huku
ukilikata; hakuna sababu ya kuanza kuunda tume ya watu wale wale ambao
wamekuwa wakikuambia ukweli ulio wazi nawe ukiwapuuza, kuwabeza na
hata kuwaadhibu.
Binafsi, nilikuwa mwenyekiti wa bodi ya HakiElimu wakati ule na
nilifadhaishwa sana na mwenendo wa serikali, kwani sikuamini kwamba
wakuu wa serikali hawakujua kwamba walimu walikuwa dhaifu katika uwezo
wa kufundisha, kwamba walikuwa hawana vitabu na nyenzo nyingine za
kufundishia, kwamba walimu walikuwa hawalipwi stahili yao na kwamba
malipo yao yalikuwa yanacheleweshwa bila sababu, na kadhalika.
Sikuweza kuamini kwamba watu waliopewa majukumu (tena kwa kuyaomba
wenywe) ya kuendesha nchi walikuwa hawaoni matatizo yaliyo bayana kwa
kila mwanajamii, kwani sikuelewa dhana ya kipofu kumuongoza mwenye
macho. Leo wanashangaa, wanataharuki, wanababaika, wanaunda tume. Ili
iweje hasa?
Tumeamua kuifanya elimu iwe ni jambo la kila familia kufanya kadri
ya uwezo wake na uelewa wake wa maana ya elimu bora, na kwa maana hii
serikali ilikwisha kujitoa katika kuratibu elimu ya watoto wa nchi hii.
Kila mtu anajifanyia atakavyo. Basi, tusilalamike, na wala tusipoteze
fedha za kodi za watu wetu kuendesha tume zisizokuwa na tija.
Kwa mara nyingine tena, nasema kwamba tumepotea, na tumepotea vibaya
mno, na kwamba unapokuwa umepotea, nusura yako ya awali ni kutambua
kwamba umepotea. Hili bado hatujalitambua.
source: Raia Mwema: Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment