Ndugu Zangu,
Bwana Yesu alipotembelea mto
Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki, Simoni alikuwa ni miongoni
mwa wavuvi hao. Yesu akasema; " Simoni, acha kuvua samaki,nifuate ukawe
mvuvi wa watu.
Naam, watu wengi wanaangamia kwa
kukosa uelewa. Kwa kutojitambua. Wanahitaji ukombozi wa kifikra. Na siku
zote, haki uinua taifa, vivyo hivyo, dhulma huangamiza taifa. Na mahala
pasipo na haki, basi, hapo hapatukuwa na amani.
Oneni, maovu yametamalaki katika dunia tunamoishi. Siku zote, kujipendelea ndilo shina la maovu. Si tuna mifano hai.
Oneni, wale wenzetu waliokaa na
wakaamua kuuza nyumba za Serikali. Na Waziri mwenye dhamana alisimamia
utekelezaji wa dhulma ile kwa Watanzania, huku naye akiwa
ameshajikwapulia nyumba yake. Lililopelekea uamuzi wa hila na ghilba wa
kuuza nyumba za serikali ni ubinafsi na hulka ya baadhi ya viongozi
kutaka kujipendelea.
Karibu wote waliouziwa au kujiuzia
nyumba hizo za Serikali, nyumba za wananchi, tayari walikuwa na nyumba
kabla. Siku zote, hamu inakuwa ni jambo jema, endapo binadamu ataweza
kuitawala hamu/tamaa yake.Wanadamu tusipoitawala hamu yetu, tukaanza
kujipendelea, kuwasahau wengine, basi, hilo huwa ndio chimbuko la maovu.
Hupelekea kutoelewana baina ya
wanandugu, na hata kwa marafiki walioshibana. Hupelekea vurugu na
machafuko katika jamii. Tunazungumzia uwepo wa upendo, haki na usawa.
Dini nyingi zinazungumzia umuhimu wa upendo, haki na usawa katika jamii. Iwe ni Uislamu na Ukristo vivyo hivyo.
” Naapa kwa zama . Hakika binadamu
wote wamo katika hasara isipokuwa wale walioamini na wakafanya matendo
mema. Wakahusiana na haki na wakahusiana na subira” (Koran tukufu, Surat
ASWR) Biblia nayo inasema; kuwa Kaini alikuwa mtu wa kujipendelea mno,
akamwua nduguye. Mfalme Saulo alijipendelea mno, akamdhulumu Daudi. Yuda
alijipendelea mno, akakubali kumsaliti Yesu kwa Vipande thelathini vya
fedha. Hatimaye, akamsaliti Yesu.
Na ufufuko wa Bwana Yesu utukumbushe
jukumu letu la kupambana na maovu katika jamii. Utukumbushe jukumu la
kusaidia kazi ya kuwakomboa kifikra wanadamu wenzetu.
Kama Bwana Yesu alivyomkumbusha Simoni kwa kumwambia; ” Simoni, acha kuvua samaki. E nenda ukawe mvuvi wa watu.
Ni Neno la Leo.
Pasaka Njema.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam
0788 111 765
No comments:
Post a Comment